Mkaguzi
Msaidizi wa Polisi ambaye ni Polisi Tarafa wa Muklati Elibariki Kileo
akitoa taarifa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas wakati wa makabidhiano ya
kikosi kazi cha askari 15 watakaofanya kazi pamoja na wananchi wa Tarafa
ya Muklati wilayani Arumeru. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la
Polisi Arusha)
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)
Liberatus Sabas akitoa elimu ya Polisi Jamii kwa viongozi, vikundi vya
ulinzi shirikishi na wananchi wa Tarafa za Muklati na Enaboishu wilayani
Arumeru. Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Askari wa Jeshi
la Polisi pamoja na viongozi wa Tarafa za Muklati, Enaboishu, Poli,
Mbuguni Moshono na King’ori zilizopo katika wilaya ya Arumeru
wametakiwa kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kufanikisha
dhana nzima ya Ulinzi Shirikishi.
Akiongea
katika vikao tofauti vilivyofanyika mwishoni mwa wiki hii wakati wa
kusambaza askari 15 kwa kila Tarafa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema
ushirikiano huo utafanikiwa endapo tu askari Polisi watakuwa wanatumia
lugha nzuri na kufanya kazi kwa maadili huku viongozi wa Tarafa, Kata,
Mitaa au vijiji watakuwa tayari kuwapa ushirikiano.
“Kama
kutakuwa na ushirikiano wa dhati ambao utawezesha kufanya kazi kama
timu moja basi kutakuwa na kuelezana ukweli na hivyo kuondoa majungu
badala ya kila kundi kufanya kazi kwa kujitenga”. Alisema Kamanda Sabas.
Kamanda
Sabas alisema serikali wanayoitumikia ni moja hivyo ili kukidhi malengo
ya kuimarisha Ulinzi na Usalama katika maeneo yao makundi hayo
yanatakiwa kuungana na kufanya kazi kama familia moja hali ambayo
itasaidia kuongeza vikundi vya ulinzi shirikishi, kupata taarifa za
uhalifu na wahalifu na hatimaye kupunguza vitendo vya uhalifu kama si
kuutokomeza kabisa.
Alisema
siku zote wahalifu wanafanikiwa sehemu ambazo ni dhaifu na zile sehemu
ambazo zimeungana wanashindwa kupenya kwani uhalifu wowote ambao
unahusisha watu wa mbali unaanzia toka kwa mwenyeji hivyo kama kila
mwenyeji ataungana na wenzake kwa kuukataa uhalifu basi daima maeneo yao
yatakuwa salama.
Kamishna
huyo Msaidizi Mwandamizi wa Polisi pia aliwaomba wananchi hao
kujitokeza mahakamani pindi wanapotakiwa kutoa ushahidi hali ambayo
itasaidia kuwatia hatiani watuhumiwa watakaowakamata kinyume cha hapo
jamii itaendelea kuvivyooshea vidole jeshi la Polisi pamoja na Mahakama.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata ya Ngaramtoni iliyopo katika Tarafa ya
Muklati Bw. David Kimisi (CCM) alimpongeza Kamanda Sabas kwa hatua yake
ya kuamua kutembelea Tarafa zote za Mkoa huu kwa nia ya kutoa elimu ya
Polisi Jamii kwa viongozi, vikundi vya Ulinzi Shirikishi pamoja na
wananchi na pia hatua yake ya kusambaza askari hao 15 kila tarafa ili
waweze kutoa huduma karibu na jamii.
Diwani
huyo alisema katika Tarafa yake kuna ushirikiano mkubwa kati ya
Viongozi, wananchi ambao wanashirikiana vema na Mkaguzi wa Polisi wa
Tarafa hiyo Elibariki Kileo pamoja na askari wa Tarafa hiyo hali ambayo
imesaidia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa vitendo vya uhalifu na
wahalifu.
Alimalizia
kwa kusema maneno ya Kamanda Sabas yameongeza chachu ya kuimarisha
ulinzi katika eneo hilo huku viongozi na wananchi wa eneo hilo wakiwa na
mipango dhabiti ya kukikarabati kama si kujenga kituo cha Polisi
kingine ili kiweze kuhudumia idadi kubwa ya watu wa eneo hilo kwa
wakati mmoja.
No comments:
Post a Comment