Rais Jakaya
Kikwete ameikataa taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera
kuhusu waathirika wa mafuriko na waliokosa makazi na kumpa siku moja
kukaa na timu yake kuandaa nyingine inayoendana na hali halisi ya janga
hilo. Eneo
la Dumila, Morogoro lilikumbwa na mafuriko makubwa na kusababisha
wakazi wake kupoteza makazi na mali huku mamia ya magari yakiwamo mabasi
yanayosafirisha abiria kukwama baada ya kubomoka kwa Daraja la Magole
linalounganisha Barabara ya Dar es Salaam na Dodoma.
Mvua hizo zilizonyesha kwenye Wilaya ya Kilosa, ndizo zilisababisha kufurika kwa Mto Mkundi unaopita kwenye eneo hilo.
Taarifa ya Bendera - Bendera
alitoa taarifa ya mafuriko kwa Rais Kikwete kwa niaba ya viongozi wa
mkoa, wakiwamo wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa taasisi
mbalimbali akisema wananchi 12,472 wamepoteza makazi. Alisema pia kuwa
nyumba 1,141 zilibomoka na 2,551 ziliingiliwa na maji huku kaya 2,759
zikiathiriwa na mafuriko. Bendera alisema misaada ya mahema na vyakula
imeanza kutolewa pamoja na dawa za kukabiliana milipuko ya magonjwa
endapo itatokea.
Alisema pia
kuwa tayari baadhi ya miundombinu imeanza kurejea kama kawaida huku
huduma za majisafi zikitolewa na magari ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ), Kikosi cha Zimamoto Morogoro na Kampuni ya China ya
High Quality Consulting and Development Solutions. Bendera alisema pia
kuwa jumla ya Sh53.7milioni zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa makazi
ya muda ya waathirika hao.
JK aikataa taarifa - Rais
Kikwete aliyekuwa akikatizakatiza taarifa hiyo ya Bendera kwa maswali
na ufafanuzi, alizikataa takwimu hizo akisema hazionyeshi uhalisia.
Akizungumza na wananchi wa eneo hilo wakiwamo waliokuwa kwenye kambi
iliyoko Sekondari ya Magole, Rais Kikwete aliwahakikishia upatikanaji wa
vyakula, dawa na majisafi na salama.
Pia
aliviagiza viwanda vya magodoro kuzisaidia haraka iwezekanavyo, familia
zilizoathirika na kuahidi kuwa Serikali italipa baadaye ili kuwaepusha
wakazi hao na hasa watoto na athari za kiafya.
Alisema kazi
ya ujenzi wa makazi ya muda itafanywa JWTZ na si makandarasi kuepusha
baadhi ya viongozi kujinufaisha kwa mafuriko hayo. Rais Kikwete
aliwataka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kuangalia uwezekano wa
kutoa magogo yaliyoziba katika makaravati na kuzibua mifereji ili
kuruhusu maji kupita kwa urahisi.
Akizungumzia
ripoti hiyo Rais Kikwete alisema: “Mmeshindwa kufafanua watu
walioathiriwa na mafuriko hayo ni wangapi na wanasaidiwa vipi hasa
katika mahitaji mbalimbali na muhimu ya kimsingi kama chakula.
“Taarifa
yenu inanitia shaka. Sasa ninawataka viongozi wa mkoa pamoja na Mkuu wa
Mkoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wote wa halmashauri kurudia upya
kumbukumbu zenu na kupata idadi kamili ya waathirika ili kujua namna ya
kuwasaidia. “Ninyi kama viongozi na mnashughulikia maisha ya watu,
mnatakiwa kuwa na kumbukumbu zenye usahihi wa majina na kama hamna
uhakika wa majina mnaomba vyakula kwa ajili ya nani? Misaada mingine kwa
wahisani ya nini?
“Tunataka
tujue wanasaidiwaje, kina mama ni wangapi na kina baba, watoto, tutoe
misaada kadri inavyostahiki. Sasa kwa takwimu hizi mnafahamu hawa watu
wako wapi? Tutawasaidiaje? Wameathirika kwa kiasi gani?.” Rais Kikwete
alisema kiongozi mzuri hupimwa wakati wa kipindi cha matukio na matatizo
au majanga yanapotokea. Aliwataka viongozi hao kujipanga kwa kuwatambua
watu walioathiriwa na mafuriko kwa kuwa na majina sahihi na idadi yao.
Miundombinu - Meneja
wa Tanroads Mkoa wa Morogoro, Injinia Doroth Mtenga alisema ofisi yake
itatumia kiasi cha Sh400 milioni kukamilisha matengenezo ya eneo la tuta
la Daraja la Magole katika Mto Mkundi lililozolewa na maji na
kusababisha mafuriko makubwa.
Fedha hizo
zitatumika kurekebishia makaravati na madaraja mengine madogo katika
eneo hilo kutoka Wami Dakawa hadi Daraja la Mkundi, Magole ambayo
huathiriwa mara kwa mara pindi mto huo unapojaa. Mtenga alisema kuwa
ujenzi huo unakusudiwa kukamilika ndani ya wiki ya kwanza ya Februari na
kama hali ya hewa itaendelea kuwa nzuri, ukarabati huo unatarajiwa
kuendelea na kukamilika taratibu na magari yataweza kupishana kama
ilivyokuwa awali.
Wakati hayo
yakifanyika, mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wameanza
kazi ya kurudishia nguzo na nyaya za umeme zilizoharibiwa na mafuriko
hayo huku wataalamu wa Kampuni ya Matrac Telecom, wakirekebisha Mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano kwenda Mkoa wa Dodoma ambao pia uliharibiwa.
Kaimu
Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifwani amekabidhi kwa
uongozi wa Mkoa wa Morogoro vifaa tiba, magodoro 100 na dawa mbalimbali
zenye thamani ya zaidi ya Sh80 milioni.
Chanzo - Mwananchi
No comments:
Post a Comment