Maelezo
Dar es Salaam
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella
Mukangara ameungana na mamia ya Watanzania katika kuaga mwili wa aliyekuwa
Mchezaji wa Klabu ya Simba Partick Mafisango aliyefariki katika ajali ya gari
usiku wa kuamkia juzi katika eneo la chang’ombe Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa misa ya kuaga mwili wa Marehemu
iliyofanyika katika viwanja vya Sigara, Dk. Mukangara alisema Serikali imepokea
kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mchezaji huyo kwani msiba huo ni pigo kubwa kwa
wanajumuiya wa klabu ya Simba, familia na taifa kwa ujumla.
Dk. Mukangara alisema Mafisango atakumbukwa na wengi kwa kuwa
alikuwa ni kijana wa mfano wa kuigwa na aliyejitolea kwa hali na mali katika
kuisaidia klabu yake ya Simba katika michuano mbalimbali ya kitaifa na ile ya
kimataifa.
“Mafisango alikuwa ni kijana maalum kwani alivuka mipaka na
kuja nchini kuichezea Simba, na historia
yake inaonyesha kuwa aliichezea TP Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo,
APR ya Rwanda, pia alikuwa Nahodha wa Timu ya Taifa ya Rwanda, na alichezea klabu
ya Azamu ya Jijini Dar es Salaam”.
Aidha Dk. Mukangara aliwataka wapenzi, mashabiki, wananchama
na Viongozi wa Simba kutokata tamaa kutokana na msiba huo na badala yake klabu
hiyo iendelee na nafasi yake ya ushindi katika michuano mbalimbali
inayowakabili.
Waziri Mukangara pia alivitaka vyama vya michezo nchini kuwa
na mipango endelevu ili kupata vijana wengi zaidi ili kuendeleza tasnia ya
michezo nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden
Rage alisema Uongozi wa Klabu hiyo umepokea kwa masikitiko taarifa za msiba wa
Mafisango kwani mchezaji huyo alikuwa mcheshi na aliyependwa na kila mtu
klabuni hapo.
Rage alisema tukio la kifo cha Mchezaji huyo litakumbukwa kwa
miaka mingi ijayo kwani kwa mara ya kwanza klabu hiyo kupata msiba wa mchezaji ilikuwa
ni mwaka 1978, ambapo Simba iliondokewa na aliyekuwa mchezaji wake Hussein
Tindwa.
Aidha Rage alisema kuwa klabu hiyo imeamua kutoitumia milele
jezi namba 30 aliyokuwa akitumia Marehemu Mafisango, ikiwa ni hatua ya kuenzi
mchango wa mchezaji wakati akiitumikia klabu hiyo.
Kwa mujibu wa Rage alisema katika michuano ya Ligi ya
Tanzania Bara iliyomalizika hivi karibuni, mchezaji huyo alifunga magoli 11,
hatua iliyomfanya kuwa mchezaji aliyeongoza
kwa idadi ya magoli iliyofungwa na wachezaji wa nafasi ya Kiungo kuliko
wote katika ligi hiyo.
Naye Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, Celestine Musigwa alisema
kifo cha mchezaji si pigo kwa klabu ya Simba
pekee bali pia kwa wapenda mpira wa miguu, kwani Mafisango alikuwa ni
mmoja wa wachezaji hodari vijana katika medali ya mchezo wa soka nchini.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Angetile Osiah alisema shirikisho hilo limeshtushwa na taarifa za kifo cha
mchezaji huyo, kwani kifo chake ni pigo kwa familia nzima ya wapenzi na
mashabiki wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.
Wakati huohuo,mwili wa Maehemu Patrick Mafisango unatarajiwa
kusafirishwa leo (jana) nchini kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ambapo ndipo
alipozaliwa marehemu kwa ajili ya shughuli za mazishi.
Afisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema msafara wa
wachezaji na Viongozi wa Simba unarajia kuongozwa na Joseph Itang’are na mwili
wa Marehemu unatajia kusafirishwa kwa ndege katika uwanja wa Kimataifa
wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment