TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Friday, November 15, 2013

MAZITO YAMKUTA MBUNGE LEMA ,JK ARUDISHA ZAWADI YA DHAHABU,VIWANJA VIBOVU SABA VYASIMAMISHWA LIGI KUU

Posted: 13 Nov 2013 12:10 AM PST
  • ALIKUWA KWENYE MATIBABU AFRIKA KUSINI
  • NCCR- MAGEUZI KUZUNGUMZIA MSIBA 
Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi, amefariki dunia jana alasiri nchini Afrika Kusini, katika Hospitali ya Milpark, Johannesburg.

Dkt. Mvungi ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi na Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UB), alipelekwa nchini humo baada ya kuvamiwa na kujeruhiwa usiku wa kuamkia Novemba 3 mwwaka huu akiwa nyumbani kwake, Kimbamba Msakuzi.
Chama cha NCCR-Mageuzi, kimethibitisha juu ya kifo hicho na kuongeza kuwa, taarifa kamili zitatolewa leo Makao Makuu ya chama yaliyopo Ilala, kuanzia saa tatu asubuhi.
Mtoa habari hizo ndani ya chama ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema marehemu Dkt. Mvungi alikuwa kiongozi mkubwa ndani ya chama na ametumia fursa hiyo kukifanya chama hicho kiwe na wanachama wengi.
Dkt. Mvungi baada ya kujeruhiwa kwa mapanga, alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Tumbi, iliyopo Kibaha, mkoani Pwani na baadaye kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kitengo cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).
Kutokana na hali yake kutoimarika vizuri akiwa hospitalini hapo, Novemba 7 mwaka huu, Dkt. Mvungi alisafirishwa kwa ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Flightlink, kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi hadi mauti yalipomkuta wakati madaktari wakiendelea kuokoa maisha yake.
Msemaji wa Kitengo cha Taasisi ya Mifupa (MOI), Bw. Jumaa Almas, alisema walilazimika kumsafirisha Dkt. Mvungi kutokana na afya yake kutoimarika vizuri.
Dkt. Mvungi alipata majeraha makubwa kichwani ambapio katika msafara wake, aliongozana na Daktari Bingwa wa Upasuaji Ubongo na Mishipa ya Fahamu Dkt. Clement Mugisha na Muuguzi, Bi. Juliana Moshi.
Juzi Jeshi la Polisi nchini kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, alisema watu tisa ambao walihusika kumpiga, kumjeruhi na kuiba vitu mbalimbali vya marehemu Dkt. Mvungi, tayari wamekamatwa.
Dkt. Nchimbi alisema watu hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kwa nyakati tofauti ambapo awali walikamatwa sita na juzi kufikia tisa.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, ambaye alikuwepo katika mkutano huo, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Msigwa Mpopela (30), Shabago Magozi na Hamadi Ally, jina maarufu 'Hatibu'.
Wengine ni Zakaria Raphael (dereva wa bodaboda), Mmanda Saluwa, Juma Hamisi, Longisho Semeriko (muuza ugolo), Paul Jeirosi na mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Kilimimazoka, ambao wote ni wakazi wa Dar es Salaam
"Watuhumiwa hawa walikutwa na mapanga, kigoda ambavyo vimethibitika kuwa vilitumika katika tukio hilo, pia walikutwa na simu ya mkononi mali ya Dkt. Mvungi," alisema.
Kamishna Kova alisema, katika mahojiano ya awali na watuhumiwa, walikiri kuhusika na tukio hilo na ushahidi umekamilika kwa asilimia 80.
"Watuhumiwa wote wamekiri kosa hivyo tunakamilisha upelelezi ili wafikishwe mahakamani mara moja," alisema.
Marehemu Dkt. Mvungi, aliwahi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi



Posted: 13 Nov 2013 12:16 AM PST

  •  ACHAFULIWA MTANDAONI, AITUHUMU UVCCM TAIFA
Queen Lema, Arusha na Mariam Mziwanda, Dar
  Katika hali isiyo ya kawaida, Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema, ameutuhumu uongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Taifa kwa mada ya kusambaza picha zinazoonesha akiingiliwa kinyume na maumbile katika mitandao ya kijamii.

  Mbali ya uongozi huo, Bw. Lema pia alimtuhumu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Bw. Sadifa Juma Khamis, kwa kushiriki kumchafua hivyo amemtaka Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda, achukue hatua na kudai ushahidi wa jambo hilo upo hadharani.
  Bw. Lema aliyasema hayo Mjini Arusha jana alipokutana na waandishi wa habari ili kuzungumzia jambo hilo na kusisitiza kuwa, suala hilo limemsikitisha sana. “Ushahidi wa namba za simu zilizohusika kusambaza picha hizo upo, Khamis (Mwakilishi Jimbo la Donge, Zanzibar), anahusika na udhalilishaji uliofanywa na vijana wa UVCCM Taifa,” alisema Bw. Lema.
  Alisema picha hizo zimesambazwa katika mitandao ya kijamii na watumiaji wa simu za mkononi zikiwa na ujumbe unaodai Lema akilawitiwa na wanaume wenzake.Aliongeza kuwa, Oktoba 29 mwaka huu, mkewe aliyemtaja kwa jina la Bi. Neema Lema, alipata picha hizo zilizotumwa moja kwa moja katika simu yake zikiwa na ujumbe usemao “Hiyo ndiyo kazi anayoifanya mume wako”.
   Bw. Lema alisema, suala hilo halikuishia hapo kwani picha hizo zilitumwa kwa mama mkwe wake na kusababisha familia ya mke wake na wazazi wake kukosa amani “Mke wangu alitumiwa picha hizi katika mtandao wa WhatsApp na baadaye ilisambazwa zaidi hadi kwa wapigakura wangu jimboni na kudai ndiyo kazi inayofanywa na Mbunge wao,” alisema.
  Aliongeza kuwa, uchafu huo ulikuwa ukifanyika wakati akiwa bungeni Dodoma ambapo Bw. Khamis, alionekana akisambaza picha hizo kutoka kwenye kompyuta yake (mpakato), kuwapa wabunge jambo ambalo lilichangia amani ya bunge kuharibika siku hiyo.
 “Wakati picha hizi zikisambazwa, nilijulishwa suala hili na wabunge wanawake wa CCM, ilibidi niende kwa Spika ambaye alikiri picha hizo zimesababisha akose morali ya kuendesha vikao. “Pia nilizungumza na uongozi wa Bunge nikilalamikia kudhalilishwa kwa kutengenezewa picha zinazoonesha nikiingiliwa na wanaume wenzangu... Spika aliahidi kulishughulikia,” alisema Bw. Lema.
  Bw. Lema alisema, kutokana na picha hizo, bado hazimnyimi kinga ya kuendelea kusema ukweli juu ya jambo lolote badala yake ataendelea kupambana ili kuwatetea wanyonge.“Kamwe siwezi kuwatafuta waliotengeneza picha hizi na kuzisambaza kwenye mitandao na simu za watu bali atawasaidia viongozi wa UVCCM kuzisambaza kwenye Makanisa, Misikiti, mikutano ya hadhara ili kuwaonesha wananchi ukatili dhidi yake unavyozidi kushika kasi asiwe na sauti ndani ya nchi,” alisema.
  Wakati huo huo, Mke wa Mbunge huyo, Bi. Neema, alisema hicho ni kitu kidogo sana dhidi ya mumewe na waliofanya vitendo hivyo walilenga kuvunja ndo yake lakini haitatokea. Sadifa azungumza
  Akijibu tuhuma hizo akiwa njiani kwenda nchini Ethiopia, Bw. Khamis alisema jumuiya hiyo au yeye mwenyewe hawezi kutumia cheo chake kufanya vitendo hivyo.
  “Mimi na Mheshimiwa Lema wote ni wabunge, tofauti yetu ipo katika vyama na majimbo...tomefahamiana bungeni na wala simjui kwa undani, tuhuma dhidi yangu si za kweli kwani siwezi kufanya kitendo hicho ambacho si cha kibinadamu hata kama tuna tofauti za kisiasa.
 “Mimi ni Muislamu na dini yangu hairuhusu kufanya hivyo, binafsi sijui kutumia kompyuta na Mheshimiwa Lema analijua hilo...hivi sasa Ofisi ya Bunge imeanza kutoa mafunzo kwa wabunge wasiojua kutumia kompyuta, nami najifunza,” alisema.
  Alisema simu anazomiliki ni mbili, moja ni Nokia ya tochi na nyingine ya kichina yenye laini tatu na hajui kama simu hizo zina mitandao na hajawahi kujaribu.Bw. Khamis aliongeza kuwa, hulka yake hayupo karibu na makundi yanayoweza kumuingiza au kumshawishi afanye vitendo hivyo hivyo yupo tayari kukutana na Bw. Lema kwa amani ili wazungumze na kuwasaka waliofanya vitendo hivyo ambavyo si vya kistaarabu.
“Mheshimiwa Lema akinitafuta nitampa ushirikiano, ninachokijua mimi, mwenzangu ananitafutia umaarufu kwa sababu pamoja na vyeo nilivyonavyo bado sifahamiki sana.
  “Natumia cheo changu ndani ya UVCCM kuijenga jumuiya na CCM... kwanza namuomba radhi kwa sababu tayari ana imani potofu dhidi yangu, pili namshauri afanye utafiti,” alisema.
Alisema imani yake ni kwamba, tofauti zao kisiasa haziwezi kumshawishi afanye vitendo hivyo kwani ipo siku Bw. Lema anaweza kurudi CCM na kufanya naye kazi pamoja.
  Aliongeza kuwa, umefika wakati wa Bw. Lema kukumbuka kuwa, tofauti za kisiasa zilizopo ndani ya chama chao pia zinaweza kutumika kumchafua katika mitandao

Posted: 13 Nov 2013 12:25 AM PST

 Rais Jakaya Kikwete, amerudisha zawadi ya dhahabu safi gramu 227 aliyopewa na Kampuni ya Nyamigogo Grand Vezir Holdings ya mkoani Geita na kutaka itumike kuwasaidia watoto yatima, anaripoti Mwandishi Wetu
. Zawadi hiyo alikabidhiwa juzi katika sherehe ya uzinduzi wa Mgodi wa Uchenjuaj iDhahabu wa kampuni hiyo uliopo nje kidogo ya Mji mdogo wa Kharuma ambako ndiko Makao Makuu ya Wilaya Mpya  ya Nyang’hwale,mkoani humo.
  Dhahabu hiyo ina thamani ya sh. milioni 16 kwa bei ya sasa katika soko la dhahabu duniani ambapo baada ya kukabidhiwa, Rais Kikwete aliuliza; “Sasa nifanye nini na zawadi hii, naomba kuirudisha hii dhahabu muiuze popote, fedha ambayo itapatikana tutawapa watoto yatima,” alisema.
  Akizungumza na wananchi katika mgodi huo, Rais Kikwete aliupongeza uongozi wa mgodi na kusema umeongeza thamani ya dhahabu na ya maisha ya wananchi katika eneo hilo.Aliushauri uongozi wa mgodi huo, kufanya jitihada za kuboresha teknolojia inayotumika. “Mgodi huu ni mradi wa maana sana kwani umeongeza thamani ya dhahabu na kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hili, ubunifu huu unastahili pongezi.
  “Lazima tuboreshe teknolojia, ile inayotumika katika mgodi huu ni ya zamani kidogo, hii ni sawa na hadithi ya mtu mwenye chongo katika jamii ya vipofu watupu, yeye anaonekana kama mfalme,” alisema Rais Kikwete.
  Mgodi wa Nyamigogo ni wa marudio kwa maana ya kuzalisha dhahabu kutokana na mchanga ambao awali ulifukuliwa ili kutoa dhahabu na ulianzishwa mwaka 2011 ambapo hadi sasa, sh. bilioni 1.6 zimewekezwa katika uendelezaji wa mgodi huo.
  Katika risala ya uongozi wa mgodi huo, ilisema mgodi huo unazalisha kati ya gramu 500 na 600 kwa mwezi na umeajiri watu 45 wakiwemo wanawake 10.Tangu kuanzishwa kwake, umekuwa unaunga mkono shughuli za jamii inayouzunguka kwa kujenga zahanati na madarasa ya shule katika vijiji viwili.
  Rais Kikwete amezindua mgodi huo kama sehemu ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo akiwa katika ziara yake rasmi ya kikazi mkoani humo ambao ni miongoni mwa mikoa minne aliyoianzisha mwaka 2012.
  Ziara hiyo imemalizika jana kwa kupokea ripoti ya maendeleo ya Wilaya ya Nyang’hwale na kuhutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mji Mdogo wa Kharuma

Posted: 13 Nov 2013 12:29 AM PST
 Frank Monyo na Daniel Samson
  Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zuberi Samatabe, amewahimiza walimu wa shule za msingi kuwajengea wanafunzi utamaduni wa kujisomea vitabu ili kuongeza uelewa katika masomo yao.
Aliyasema hayo katika uzinduzi wa tovuti ya kufuatilia mgawo wa vitabu vya chenji ya Rada uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Lengo la tovuti hiyo ya www. pesptz.org ni kutoa taarifa kwa wadau wa elimu pamoja na wanafunzi juu ya vitabu vinavyosambazwa katika shule za msingi kwa kutumia chenji hiyo.
Alisema, Serikali ya Uingereza iliamuru fedha zilizotumika vibaya katika manunuzi ya Rada zirudishwe kwa Watanzania na zitumike katika manunuzi ya vitabu na madawati kwa shule za msingi.
"Fedha za chenji ya Rada sh. bilioni 72 zilizorudishwa ziliingizwa katika mpango wa manunuzi ya vitabu na madawati katika shule za msingi na asilimia 75 zimetumika katika manunuzi ya vitabu vya wanafunzi na vya mwongozo wa walimu kufundishia," alisema Samatabe.
  Kwa upande wake Meneja Takwimu wa Kampuni ya Data vision International, William Kihula alisema Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza (DFID) iliwapa jukumu la kutengeneza tovuti kufuatilia mgao wa vitabu vya chenji ya Rada, ili kuwezesha ushirikishwaji wa wadau wa elimu na wananchi katika kufuatilia usambazaji wa vitabu shuleni.
  Alisema hatua hii itawezesha serikali kuendelea kutembelea katika maeneo yake na kuwa na uendeshaji wa uwazi ndio maana wamejenga mfumo huu katika namna ambayo itaweza kutumika na wizara hata baada ya mradi huo wa mgawo wa vitabu vya chenji ya rada kuisha.
"Tovuti hiyo ndio pekee inayoweka mtandaoni majina yote ya shule za hapa nchini wilaya na mikoa iliyopo hii itatoa mwanga wa kuanzia katika ufuatiliaji wa maendeleo ya mwanafunzi mmoja mmoja," alisema Kihula.
  Aliongeza kuwa, kuwepo kwa jitihada za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuanza kutumia mfumo mpya wa kupima ufaulu wa wanafunzi kwa kuhusisha "Continous Assessment" kwa kuanza na shule za sekondari.
  "Katika hili Datavision tupo kwenye hatua za mwisho za kutengeneza mfumo wa teknolojia itakayowezesha kupatikana na kutunza taarifa za maendeleo ya mwanafunzi shuleni kwa wakati," alisema Kihula.
Posted: 13 Nov 2013 12:32 AM PST

 Penina Malundo na Maua Mashu
  Wafanyakazi wakiwemo vibarua zaidi ya 200 wa Kampuni ya STRABAG inayojenga barabara ya mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam wamegoma.

Mgomo huo ulianza jana jijini humo kwa madai ya kutaka kulipwa stahiki zao za zamani kabla ya kampuni hiyo kuingia mkataba na kampuni nyingine.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana na waandishi wa habari, wafanyakazi wa kampuni hiyo walisema kuwa, wameingia katika kampuni hiyo kwa sheria zote na wengi wao wameweza kufanya kazi zaidi ya mwaka mmoja, hivyo wanapaswa kulipwa madai yao kabla ya kuvunja mkataba na Kampuni ya STRABAG.
Walisema kuwa, mgogoro mkubwa uliibuka kati ya vibarua hao na kampuni iliyoingia mkataba na Strabag ijulikanayo kama Laba Constractors juu ya malipo watakayolipwa kuwa madogo tofauti na malipo ya Kampuni ya Strabag.
"Jumamosi tulikaa kikao na viongozi wa Laba Constractors wakatueleza kuwa kuanzia siku ya Jumatatu (juzi), malipo yetu yatakuwa chini yao, kwani wameingia mkataba na Kampuni ya Strabag kwa ajili ya kulipa wafanyakazi wake na vibarua, jambo la kushangaza sisi hatujapata taarifa yoyote kutoka kwa Strabag juu ya mkataba huo walioingia na Kampuni ya Laba Constractors," alisema mmoja wa vibarua hao ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Alisema kuwa, Kampuni ya Strabag ingefanya utaratibu maalumu wa kumaliza madai yote ya msingi kwa vibarua wake na hapo ndipo wangeweza kuanza kuingia mkataba na kampuni nyingine.
"Mpaka sasa hatujui hatma yetu, sisi tumekaa hapa toka saa 12 asubuhi na tutaendelea kukaa mpaka kieleweke hadi tupatiwe haki yetu, malipo yetu tupewe ndiyo kampuni nyingine ianze upya na sisi, kwani tumeshakaa zaidi ya mwaka mmoja, kisheria sisi tayari ni wafanyakazi halali," alisema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi katika Kampuni ya STRABAG (TAMICO), Abdullah Rukusa alisema kuwa, Kampuni ya Strabag ilikuwa inawalipa vibarua hao malipo ya sh. 12,500 kwa siku huku malipo ya posho yakiwa sh. 4,800 kwa saa za ziada.
Alisema kuwa, Kampuni ya Laba Contractors inataka kuwalipa vibarua hao kiasi cha sh.10,000 kwa siku hali itakayofanya kampuni hiyo kuwanyonya wafanyakazi hao pindi wanapoanza kazi saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Laba Contractors, Emanuel Mshana alisema kuwa, mkataba kati yao na Kampuni ya Strabag ulisainiwa Jumamosi iliyopita na kazi rasmi ilianza kufanyika juzi huku tayari akidai wamekutana na wafanyakazi hao kwa mazungumzo.
Alisema kuwa, vibarua 95 waliopewa na Kampuni ya Strabag kati yao 45 ndio walioanza kufanya kazi nao juzi na kampuni yao kuongeza vibarua 28 kwa siku, kwa ajili ya kufanya kazi.
Juhudi za kumtafuta Mkurugenzi wa Kampuni ya Strabag ziligonga mwamba baada ya kugoma kuzungumza na waandishi wa habari huku geti likizuiliwa na mawe makubwa ya barabaran
Posted: 13 Nov 2013 12:39 AM PST

 Na Grace Ndossa
   Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba (NHC), Nehemia Mchechu ametunukiwa tuzo ya uongozi bora pamoja na cheti kwa kutambua mchango wake mkubwa katika jamii na ndani ya shirika hilo.

  Tuzo hiyo ilikabidhiwa jana jijini Dar es Salaam na Rais wa Rotary Klabu ya Mzizima, Ambrose Nshala ambapo alieleza kuwa Mkurugenzi huyo amekuwa kiongozi bora na amethubutu kufanya kazi kwa ujasiri na kuonesha ndoto za kufika mbali.
  Alisema kuwa, Mkurugenzi huyo ni kijana mdogo, lakini ameonesha uthubutu wake katika kufanya kazi na mageuzi ndani ya shirika, hali ambayo imeonesha hatua kubwa kiuchumi na kazi anazofanya zitalifikisha mbali shirika.
  Alisema kuwa, Rotary klabu inathamini mchango wake na kutambua kazi aliyofanya kwa jamii kwani ni kubwa hivyo wametoa tuzo hiyo na cheti kwa ajili ya kuongeza hamasa kwa viongozi wengine kuiga mfano wa mkurugenzi huyo ili nchi iweze kupata maendeleo.
  Kwa upande wake, Mchechu alisema kuwa, tuzo hiyo itasaidia kuongeza hamasa zaidi katika kufanya kazi ili nchi iweze kupata maendeleo.
  Alisema kuwa, sera za Tanzania ni nzuri ila tatizo liko kwenye utekelezaji kwani viongozi wengi wanathamini maneno kuliko vitendo, hivyo ndiyo vinavyofanya mambo mengi kukwama.
  Pia alisema, sera nyingi hapa nchini nyingi huishia kwenye karatasi na nchi nyingi huiga sera za Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ndiyo maana zimepiga hatua
Posted: 13 Nov 2013 12:36 AM PST

 Na Mwandishi Wetu
  Imeelezwa kuwa kuanzishwa kwa kampuni huru za minara ya mawasiliano ya simu, kunaweza kupunguza gharama za uendeshaji kwa kampuni za simu za mkononi nchini, hivyo kuweza kusaidia kuleta ahueni kwa watumiaji wa simu hizo.

Kabla ya hapo kampuni zote za simu za mkononi nchini kila moja ililazimika kujenga mnara wake ambao unahitaji kiasi kikubwa cha uwekezaji ikiwa ni pamoja na matumizi ya jenereta, ulinzi na gharama nyingine za uendeshaji.
Hayo yalibainishwa jana na Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa Kampuni ya Helios Towers, Michael Magambo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
"Hapo ndipo kampuni huru za minara zinapoingia. Humiliki, husimamia na huendesha minara, inayoweza kutumiwa na kampuni nyingi za simu kwa wakati mmoja na pia hata matangazo ya Tv, redio na mawakala wa hali ya hewa," alisema.
  Alisema, matumizi ya mnara mmoja huondoa mzigo wa gharama za uwekezaji wa miondominu pamoja na shughuli nyingine kwenye eneo la mnara.
  Pia alisema, kampuni za simu zinapata nafasi ya kuelekeza nguvu zaidi katika eneo wanaloliweza zaidi kutoa huduma za sauti na 'data' kwa Watanzania.
 "Wengi hawaufahamu mchango wetu katika kupanua huduma za simu Tanzania na Afrika kwa ujumla. Helios Towers ni kampuni kubwa ya minara huru nchini, ikiwa imejenga zaidi ya minara 1,000 ya Tigo Tanzania mwaka 2010, kisha ikajenga minara mingine 250 na inatarajia kuongeza mingine 150 ifikapo Desemba mwaka huu," alisema Magambo.
  Aidha, alisema kwa miaka miwili iliyopita, maeneo ya Helios yanayotumiwa kwa pamoja na kampuni za simu ni asilimia 53 kwa sasa na ni asilimia 60 ya maeneo mapya kwa nchi nzima huku ikisubiri uthibitisho wa serikali wa kuchukua minara ya Vodacom Tanzania.
"Tumekuwa tukisikia wakosoaji wakidai kwamba, kampuni kama Helios hayana ushindani kwa kuwa yamekamata soko kubwa.
  "Hii si kweli. Uhakika ni kwamba Helios imekuwa chachu ya kuwapo kwa ushindani kwenye soko la huduma za simu, ikiruhusu wageni kuingia kwenye soko na kuwapa nafasi watoa huduma kupeleka vijijini bila wasiwasi.
  "Mwishowe ni walaji ndio hufaidika zaidi kwa kupunguziwa bei za simu na kuchagua mtandao wanaoutaka. Ukweli ni kwamba tunafungua zaidi soko," aliongeza Magambo.
  Hata hivyo, katika kupunguza changamoto za kupeleka huduma maeneo ya vijijini yasiyo na huduma za simu, awali Serikali ilitoa gari lijulikanalo kama Universal Communication Action Fund (UCAF) linalosaidia kupunguza gharama na kuwahamasisha watoa huduma kwenda kwenye soko la vijijini.
  Hatua hiyo ilitokana na Sheria ya Upatikanaji wa Mawasiliano ya mwaka 2006 yenye lengo la kukuza maendeleo ya kijamii na uchumi mijini na vijijini kupitia TEKNOHAMA.Mbali na hayo Kampuni ya Helios iko mbioni kuweka mitambo 27 chini ya UCAF
Posted: 13 Nov 2013 12:42 AM PST

 Na Mwandishi Wetu
  Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel Tanzania imeamua kupambana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini kwa kuzisaidia shule mbalimbali za sekondari kupata miundombinu ya kufundishia na vifaa vya kujifunzia.

  Pia kampuni hiyo kupitia mradi wake wa Shule Yetu imewanufaisha wanafunzi wa Shule ya Sekondari Chalinze iliyopo mkoani Pwani baada ya kukabidhi vitabu vya masomo ya sayansi vyenye thamani ya sh. milioni tano kwa shule hiyo.
  Akizungumza wakati wa kukabidhi vitabu hivyo, Meneja Masoko wa Airtel Kanda ya Kusini na Mkoa wa Morogoro, Aminata Keita alisema vitabu hivyo vitatumika katika kuongeza kiwango cha uelewa na kukuza ufaulu kwa wanafunzi wa shule hiyo ambao walikuwa na tatizo la uhaba wa vitabu.
  "Vitabu hivi...vitatumika kukuza ufaulu kwa wanafunzi maana wanafunzi wataweza kujisomea kwa urahisi na kufuatilia masomo kwa ukaribu zaidi," alisema Aminata.
  Aliongeza kuwa, msaada huo wa vitabu ni sehemu ya mpango mkakati wa kuzisaidia shule za kata zinazolalamikiwa kufanya vibaya katika mitihani yao ya kitaifa.
  "Tumetoa vitabu vya masomo ya sayansi tukijua kabisa wanafunzi wengi hushindwa masomo hayo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo upungufu wa zana za kujifunzia ila nina imani mradi huu wa Shule Yetu utaziwezesha shule za kata kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa," alisema Aminata.
  Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo, Emmanuel Kahabi alisema, upatikanaji wa vitabu utarahisisha kazi ya ufundishaji kwa wanafunzi na pia wanafunzi wataweza kuelewa kiurahisi maana zana za kufundishia zinapatikana
Posted: 13 Nov 2013 12:49 AM PST

Neema Ndugulile
  Timu ya Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) na kupewa onyo kali kwa timu yake ya U20 kutocheza mechi ya utangulizi walipocheza na Yanga.

  Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema pia Mbeya City wanatakiwa kulipa gharama za uharibifu, baada ya mashabiki wao kuvunja kioo cha basi la Yanga, baada ya gharama hizo kuthibitishwa na bodi hiyo.
  "Pia Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa mashabiki wake kushambulia basi la wachezaji wa Tanzania Prisons, baada ya mechi dhidi yao na kulipa gharama za uharibifu baada ya kuthibitishwa na Bodi ya Ligi," alisema Wambura.
  Alisema Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za mashabiki wake ilipocheza na Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani ambapo mwamuzi msaidizi, Hassan Zani alishambuliwa kwa mawe na kujeruhiwa mkononi na kichwani, tukio lililosababisha mchezo kusimama kwa dakika tatu.
  Wambura alisema beki wa Coastal Union, Hamad Khamis amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga kichwa kwa makusudi Kipre Tchetche wa Azam. "Kitendo hicho kilisababisha refa amtoe nje kwa kadi nyekundu, hivyo atakosa mechi tatu zinazofuata za timu yake.
  "Nayo Simba wamepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za mashabiki wake wakati wa mechi dhidi ya Kagera Sugar," alisema Wambura.
  Alisema adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa kanuni. Pia Bodi ya Ligi imeahirisha kufanya uamuzi wa mechi kati ya Stand United na Kanembwa JKT iliyochezwa Uwanja wa Kambarage, ili kukusanya taarifa zaidi. Mechi hiyo haikumalizika. Bodi ya Ligi itakutana tena Jumapili.
Posted: 13 Nov 2013 12:46 AM PST
Na Fatuma Rashid
  Bodi  ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board), imefungia viwanja saba vilivyokuwa vikitumiwa na timu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL), hadi vitakapofanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya mechi za mpira wa miguu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema uamuzi huo umefikiwa na TPL Board katika kikao chake cha kwanza kilichofanyika juzi ambapo pamoja na mambo mengine, kilipitia ripoti za mechi za VPL na FDL katika mzunguko wa kwanza.
  Alisema viwanja vilivyofungiwa na marekebisho yanayotakiwa kufanyika kwanza, ili viruhusiwe kutumika tena ni Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba (majukwaa yake yamechakaa, hivyo kuhatarisha usalama wa watazamaji) na Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga (vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo (dressing rooms) havina hadhi.
  Wambura alisema Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya (sehemu ya kuchezea-pitch ni mbovu), Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha (sehemu ya kuchezea ni mbovu), Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi (vyumba vya kubadilishia kutumika kwa ajili ya shule ya awali), Uwanja wa Majimaji mjini Songea (pitch ni mbovu) na Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro (pitch ni mbovu).
  Wambura ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, alisema klabu ambazo timu zake zinatumia viwanja hivyo zimeshataarifiwa rasmi juu ya uamuzi huo, ambapo ama vinatakiwa kuwasiliana na wamiliki wa viwanja hivyo, ili wafanye marekebisho au kutafuta viwanja vingine vya kuchezea mechi zao.
  Wakati huo huo, timu za Taifa za Future Taifa Stars na Taifa Stars zinacheza leo. Mechi hiyo ya kirafiki itafanyika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
  Mechi hiyo ni maalumu kwa Benchi la Ufundi la Taifa Stars linaloongozwa na Kim Poulsen, kuangalia wachezaji kumi kutoka Future Taifa Stars watakaoongezwa katika Taifa Stars, tayari kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa Novemba 19, mwaka huu jijini Arusha.
  Watazamaji 300 tu wataruhusiwa kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini jana. Miongoni mwa wachezaji wanaotarajia kuripoti ni kipa Ivo Mapunda wa Gor Mahia.
Posted: 13 Nov 2013 12:57 AM PST

Na Fatuma Rashid
  Kocha mpya wa timu ya Azam Fc anatarajiwa kutua katika kikosi hicho mapema, kabla ya wachezaji wa timu hiyo kurudi kambini.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Msemaji wa timu hiyo, Jaffer Iddi alisema wachezaji wote wamepewa likizo ya wiki mbili, hivyo uongozi upo katika mchakato wa kutafuta kocha atakayerithi mikoba ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mwingereza Stewart John Hall.
Msemaji huyo alisema kocha mpya atakapowasili, ndipo atakapojua ni mchezaji gani atataka aanze naye na yupi amalize naye, kwani yeye ndiye atakuwa akiufahamu uwezo wa wachezaji kuanzia mazoezini hadi katika mechi.
Akizungumzia katika mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza ya michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, Iddi alisema ilikuwa nzuri kuliko nyingine kwani wote walikuwa wazuri na walipigana kutafuta nafasi nzuri katika kumalizia mzunguko huo.
  Alisema timu yake kwa sasa ipo mapumziko na itarudi kambini baada ya wiki mbili, ili kujipanga zaidi kwa mzunguko wa pili wa ligi hiyo na michuano ya kimataifa.
  Aliongeza kuwa, katika mzunguko wa pili anaimani timu yake itakuwa vizuri zaidi kutokana na kuona pamoja na kupima uwezo wa kila timu shiriki za Ligi Kuu, ambazo uwezo wake wameshauona, hivyo anaona timu itajifunza kutokana na walichokiona katika mzunguko wa kwanza.
  Kocha Hall aliwaaga wachezaji na benchi la ufundi, mara tu baada ya mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Mbeya City uliomalizika kwa sare ya mabao 3-3 kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.  

No comments:

Post a Comment