TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Friday, December 9, 2011

MASTAA WAANGUA VILIO KUTOKANA NA MSANII WA ZE COMEDY VENGU HALI YAKE KUENDENDELEA KUWA TETE



Na Joseph Shaluwa
WINGU zito limetanda kwa mastaa nchini wakionesha majonzi makubwa juu ya afya ya staa mwenye uzani wa juu Bongo, Joseph Shamba a.k.a Vengu (pichani) ambaye hali ya afya yake ni tete, kalamu ya Risasi Mchanganyiko inaandika kwa simanzi.

Vengu ambaye ni mchekeshaji wa Kundi la Orijino Komedi linalorusha michezo yake kupitia Kituo cha Runinga cha TBC1 cha jijini Dar es Salaam, kwa muda mrefu sasa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiendelea na matibabu huku ugonjwa unaomsumbua ukiwa siri.

Habari ambazo zimepatikana mpaka sasa, zinaeleza kwamba Vengu anasumbuliwa na maradhi ya kichwa bila kufafanua zaidi aina ya tatizo alilonalo kichwani.

Kwa nyakati tofauti, mastaa wameonesha vilio vyao juu ya staa mwenzao huyo kwa kile walichoeleza kuwa wanafichwa maradhi yanayomsumbua, lakini pia hawapati taarifa rasmi kutoka kwa watu wa karibu na msanii huyo ili nao waweze kuonesha undugu wao kama familia moja katika fani.

Mastaa waliopata fursa ya kuzungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, juzi Jumatatu na kutoa maoni yao ni Vincent Kigosi ‘Ray’, Ruth Suka ‘Mainda’, Maimartha Jesse, Aunt Ezekiel, Mhe. Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Ambwene Yesaya ‘AY’ na Jacqueline Wolper.
Ray, Mainda, Aunt na Wolper ni wasanii wa filamu, Maimartha ni mtangazaji, AY ni mwanamuziki wa Bongo Fleva wakati Sugu ni Mbunge wa Mbeya Mjini huku akiendeleza harakati zake katika muziki wa kizazi kipya.

RAY
“Kaka kwenye hili suala (la Vengu) fedha si tatizo, tatizo ni usiri wa kinachomsumbua ndugu yetu. Hata sisi wasanii wenzake tukiuliza, hatupewi ushirikiano mzuri.

“Kwa mfano ni juzi tu, nilimpigia Masanja (Emmanuel Mgaya) na kumuuliza kuhusu tatizo la Vengu, hakusema chochote zaidi ya kuniambia anaumwa tu. Ugonjwa unafichwa. Jambo lingine ni utaratibu wa kumuona, sisi wasanii nadhani tungepewa kipaumbele kwenda kumuona mwenzetu, maana ICU (Chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum) hawaruhusu watu kuingia hovyo.

“Hata hivyo, siamini kama Komedi wameshindwa kumsaidia kama anahitaji usaidizi. Unajua Vengu anafanya kazi TBC1, televisheni ambayo ipo chini ya serikali, nini kinashindikina?” alisema na kuongeza:
“Huu ni wakati wa wasanii wote nchini kushikamana. Kwa kufanya hivyo tutaonesha umoja wetu.”

AY
“Najua kwamba jamaa anaumwa, lakini sijapata details (maelezo) zaidi ya kusikia anaumwa kichwa. Inauma sana kwa kweli, unajua Vengu ni msanii mwenzetu na katika kipindi kama hiki anahitaji sana faraja yetu.

“Kiukweli bado sijaenda kumuona, lakini nitajipanga nikamuone. Kama kutakuwa na harambee ya kumsaidia, nipo tayari muda wowote kutoa kile nitakachojaliwa.”

MAIMARTHA
“Maradhi hayana hodi. Leo kwa Vengu kesho kwa mwingine. Mastaa tuoneshe mshikamano katika kumsaidia mwenzetu. Nilipata bahati ya kwenda kumuona Muhimbili siku kama sita zilizopita, hali yake ni mbaya...
“...maskini! Haongei...hajitambui. Tunapaswa kuchangishana tumsaidie. Sisi ndiyo ndugu zake. Nashukuru sana kwa kutukumbusha na ninawaomba mastaa wenzangu tumkumbuke jamani.”

SUGU
“Kiukweli sijapata nafasi ya kwenda kumuona, majukumu yamenibana sana, lakini najipanga niende. Kwa mara ya kwanza nilisoma taarifa za kuugua kwake kwenye gazeti, tena nilimuona Mhe. Rais (Dk. Jakaya Kikwete) naamini atakuwa amemsaidia.

“Unajua rais ndiyo kila kitu katika nchi, kwa hiyo kama alikwenda kumuona, nina imani ikiwa Vengu anahitaji msaada wowote, basi ni lazima atakuwa amepatiwa. Juzi tu, nimesoma kwenye gazeti, serikali imewapeleka watoto kama 20 hivi India kwa matibabu, naamini kwa Vengu ambaye ni msanii na ana mchango kwa taifa ni rahisi zaidi.

“Sema kuna tatizo la taarifa. Washkaji zake (Orijino Komedi) hawajajipanga vizuri kuhusu kutoa taarifa. Ukiachana na hao, kuna vyama vya wasanii, nadhani walipaswa kutoa maelekezo vizuri kwa wasanii badala ya kuona na kusikia kutoka kwenye vyombo vya habari.”

MAINDA
“Nilisoma kwenye gazeti, lakini kiukweli inaumiza sana. Kuna umuhimu wa Kundi la Orijino Komedi kutoa taarifa rasmi kwa wasanii, maana tupo gizani. Mimi nilisikia juujuu kuwa anaumwa, lakini nilipoona kwenye gazeti ndiyo nikashtuka. Sikujua kama yupo serious (amezidiwa) vile. Namuombea kwa Mungu ampe afya.”

WOLPER
“Ndiyo kwanza nasikia habari hizi kutoka kwako, nipo busy namuuguza mama yangu ambaye ni mgonjwa sana. Enhee... amelazwa wapi ili nikitoka hapa nikamuone?”
Risasi Mchanganyiko lilimtajia wodi na hospitali aliyolazwa ili akamtembelee kama alivyosema mwenyewe kwamba hana taarifa zozote!

AUNT
“Sikuwa najua chochote kuhusu Vengu, nilisoma tu gazetini. Kinachoonekana ni kwamba, haya mambo yanapelekwa kimyakimya sana. Sisi kama wasanii wenzake tuna haki ya kupata taarifa ya moja kwa moja juu ya afya ya mwenzetu lakini pia tuna wajibu wa kumsaidia.

“Wasanii hatuna umoja wa kweli, nashauri tuitane, tuketi na kujadiliana namna ya kumsaidia. Ni kweli Kibongobongo wasanii hatuna uwezo kivile wa kumsaidia kifedha, lakini kwa sababu tuna wadau wapenda burudani wanaweza kutupa support kama sisi tukianza. Wasanii tuamke, tushikamane tumsaidie mwenzetu.”

KALAMU YA RISASI
Hakuna jambo gumu linaloshindikana kwa Mungu, Vengu kwa sasa ni mgonjwa lakini kwa maombi yetu Watanzania, siku moja ataamka na kuendelea kutoa burudani kwa jamii. Tunamuombea kwa Mungu apone haraka– MHARIRI.

No comments:

Post a Comment