TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Wednesday, July 3, 2013

•Msafara wa Rais Obama magari 33, Dar yazizima



Posted: 01 Jul 2013 10:29 PM PDT

•Ulinzi wake washangaza wengi, barabara zafungwa

•Ammwagia sifa Rais Kikwete, kumaliza ziara yake leo

Mapokezi ya Rais Barack Obama wa Marekani alipowasili jijini Dar es Salaam jana. Rais Obama yuko katika ziara ya siku mbili nchini. 


Na Waandishi Wetu

MAELFU ya wakazi wa Dar es Salaam, jana wamejitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Rais wa Marekani, Bw. Barack Obama ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku mbili, akitokea nchini Afrika Kusini ambako alifanya ziara ya siku mbili.

Katika ziara hiyo, Rais Obama ameongozana na mkewe Mama Michelle, watoto wao Maria (10), Sasha (7) na ujumbe wake.

Rais Obama aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, saa 8:30 na ndege yake aina ya Air Force One. Alipokelewa na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete, mkewe Mama Salma, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Baada ya ukaribisho huo, alikagua gwaride maalumu ambalo liliandaliwa kwa ajili yake, kupigiwa mizinga 21 na kuangalia ngoma za asili zilizokuwa zikitumbuiza uwanjani hapo.

Ngoma hizo zilimvutia Rais Obama ambaye alihamasika kuzicheza akionekana mwenye furaha.

Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyekuwa wa kwanza kuondoka uwanjani hapo kwenda Ikulu, baadaye kufuata Rais Obama ambaye alitumia gari maalumu aina ya Codillac One.

Msafara wa Rais Obama ambao ulikuwa na magari 33, uliondoka uwanjani hapo kwenda Ikulu, saa 9:15 alasiri. Baada ya kuwasili Ikulu, alifanya mazungumzo ya faragha na Rais Kikwete na baadaye kuzungumza na waandishi wa habari.

Rais Obama azungumza

Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Rais Obama alisema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo muhimu na kusisitiza kuwa, Tanzania ina uwezo mkubwa wa kukuza uchumi wake.

“Ziara yangu imelenga kuboresha taasisi zilizopo nchini pamoja na kuchochea ushirikiano katika programu mbalimbali, nchi yangu ipo tayari kuisaidia Tanzania katika sekta ya nishati na umeme.

“Pia ziara yangu imelenga kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha biashara, kutokomeza ugonjwa wa malaria na vifo vya watoto...naipongeza Serikali ya Rais Kikwete kwa kusaidia kuimarisha usalama huko Darfur, Sudan,” alisema.

Rais Obama pia alimpongeza Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein na kusisitiza kuwa, Serikali ya Marekani itazidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala ya usalama kwa ajili ya faida ya kizazi kijacho.

Alipoulizwa na mwandishi, Bw. Peter Ambikile juu ya Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) wa Marekani umeifanyia nini Tanzania, Rais Obama alisema nchi yake imesaidia kupunguza ugonjwa wa malaria na mpango huo umekuwa na mafanikio makubwa.

Aliongeza kuwa, Marekani pia inalenga kuiwezesha Afrika katika masuala ya umeme na kuiwezesha kuzalisha chakula cha kutosha.

Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema MCC imekuwa na msaada mkubwa kwa Tanzania ambapo malengo yaliyopo ni kuongeza usambazaji wa huduma na upatikanaji wake jijini Dar es Salaam pamoja na umeme vijijini.

Alisema Serikali ya Marekani imefanya mambo mengi kwa Tanzania kama kupunguza vifo vya watoto, maambukizo ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Katika ziara hiyo, Rais Obama alipata fursa ya kupanda mti ambao utabaki kuwa kumbukumbu kwa Tanzania.

Ulinzi mkali

Kuanzia asubuhi, maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam yalikuwa shwari ambapo askari wa Jeshi la Polisi wakiwa na magari, waliimarisha ulinzi wakiwa na silaha za moto pamoja na mbwa.

Katika uwanja wa ndege, makachero wa Marekani na Tanzania, walishirikiana kuweka ulinzi katika maeneo yote yanayozunguka uwanja huo na barabara zilizotumiwa na viongozi hao.

Mapokezi yake yatikisa

Mamia ya wananchi walikusanyika katika barabara aliyopita Rais Obama kwenda Ikulu wengi wao wakiacha shughuli zao na kutoka maofisini ili kuangalia msafara wa kiongozi huyo ambaye alikuwa akisubiriwa kwa hamu.

Awali askari wa Vikosi vya Upelelezi vya Marekani (FBI), walijikuta katika wakati mgumu baada ya kushindwa kutambua barabara ambayo angepita Rais Obama akitokea uwanja wa ndege kutokana na ukosefu wa vibao vinavyoonesha majina ya barabara.

Akizungumza na gazeti hili, Ofisa wa polisi ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema, kutokana na hali hiyo Serikali ililazimika kuweka vibao katika barabra ya Sokoine Drive na Gerezani.

Wanasiasa watoa maoni

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw. January Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, mkoani Tanga, alisema ujio wa Rais Obama ni fursa nzuri kwa Tanzania katika kuimarisha demokrasia, uchumi na kuchochea uwekezaji endelevu katika sekta za nishati, miundombinu, viwanda, kilimo.

“Ziara ya kiongozi huyu ambaye ni rais wa 44 nchini Marekani, itasaidia kuhamasisha wawekezaji wajitokeze kwa wingi katika sekta mbalimbali nchini...hakuna cha ajabu kwa Taifa kubwa kama hili kushirikiana na Tanzania,” alisema Bw. Makamba.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema ujio wa kiongozi huyo unaweza kuwa na faida ya kukuza uchumi kama misaada inayotolewa na nchi hiyo itafanyiwa kazi kwa vitendo.

“Tunatambua jinsi Taifa hili linavyoisaidia Tanzania kupitia mipango mbalimbali ila nchi yetu inakabiliwa na tatizo la kushindwa kujipanga ili kufikia malengo... tunapaswa kuondokana na hali hii ili kukuza uchumi.

“Kimsingi ujio wa Rais Obama hauwezi kubadilisha maisha ya Mtanzania au jambo lolote, sisi tunapaswa kufanya kazi kwa bidii na kujipanga kwa kutumia rasilimali tulizonazo,” alisema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), kilichopo mkoani Mwanza, Profesa Mwesiga Baregu, alisema ziara hiyo inaweza kuwa na faida kwa Tanzania kama wenyeji wake wamejipanga kumweleza mahitaji yao.

“Kwa mtazamo wangu naona Rais Obama amekaribishwa nchini hivyo ujio wake unaweza kuwa na faida kama waliomkaribisha watakuwa wamejipanga kwa hoja nzuri, Sitarajii kama tutawapa nafasi kubwa katika suala la usalama au nishati badala yake tuangalie mbali zaidi ili kuimarisha mambo yetu,” alisema.

Maoni ya wananchi

Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam walioshiriki katika mapokezi hayo, walisema wamefurahishwa na ujio wa kiongozi huyo ambao ni neema kwa Tanzania hasa kwa kukuza uchumi wake.

Bw. Dadi Nahinga, alisema yeye binafsi amefurahi kumuona Rais Obama akiwa nchini kwani siku zote alikuwa akimuona katika televisheni akimfananisha na kiongozi shupavu mwenye msimamo na mapenzi makubwa kwa Tanzania.

Naye Bw. Heri Mahonyo, alisema alitegemea kumuona Rais Obama akiwa kwenye gari la wazi akiwapungia mikono wananchi ambao wamejitokeza kwa wingi kushuhudia msafara wake.

“Enzi ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kiongozi anapokuja nchini alikuwa akitumia gari la wazi ili kupungia mikono watu waliojipanga barabarani tofauti na sasa,” alisema.

Kwa upande wake, Bw. Godfrey Ndyanabo alisema ujio wa Rais Obama una manufaa makubwa kwa Tanzania kwani anaamini mikataba ambayo ataisaini, italeta tija kwa Taifa.

Alisema Watanzania wanapaswa kuendeleza uzalendo wao kwani kitendo cha kujitokeza na kumlaki kiongozi huyo ni utamaduni tuliojengewa na waasisi wa Taifa hili.

Bw. Saidi Maganga, mkazi wa Kariakoo, alisema ziara hiyo ni fursa nzuri kwa Tanzania kujitangaza kimataifa na vivutio vya utalii vilivyopo katika mikoa mbalimbali
 nchini.
Mkazi mwingine, Bi. Irene Mkumbusho anayeishi Mbagala, alisema Rais Obama ameonesha mapenzi yake kwa Tanzania kwani nchi nyingi za Afrika zinamuhitaji hivyo anaamini ujio wake utachochea maendeleo ya sekta mbalimbali.
Alisema pamoja na ziara hiyo kuwa na manufaa kwa Tanzania, wakazi wa jiji hilo wamepata usumbufu mkubwa ambapo barabara nyingi zimefungwa hivyo wamelazimika kutembea kwa miguu.
Bw. Cyprian Basenga alisema, Serikali ikiamua inaweza kuboresha usafi wa mazingira kama ilivyofanya katika ziara ya Rais Obama hivyo aliomba utaratibu huo uendelee.
Alisema pamoja na ujio wa Rais Obama kusababisha usumbufu kwa wananchi, una faida kubwa kitaifa na kimataifa kutokana na uwekezaji wake katika sekta ya umeme kupitia mradi mkubwa ambao utawanufaisha wananchi wengi.
Aliwataka wananchi kuachana na fikra potofu kuwa Rais Obama amekuja Tanzania kwa masilahi binafsi hivyo umefika wakati wa kuachana na mawazo hayo bali ugeni huo ni neema kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo.
Aliongeza kuwa Watanzania wanapaswa kutumia fursa hiyo ili kuuliza ugeni huo nchi yao inatumia njia gani kupandisha uchumi wao ili mbinu hizo ziweze kutumika nchini.
Bw. Iddy Fundi mkazi wa Mbagala, alisema ujio wa Rais Obama, umekwamisha shughuli nyingi za maendeleo ambapo wananchi wengi wametembea kwa miguu katika umbali mrefu
Alisema wafanyabiashara wengi wamelazimika kufunga biashara zao ili kupisha mapokezi ya kiongozi huyo na kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri ya kuimarisha ulinzi wa maeneo mbalimbali.
Kwa upande wao, wafanyabiashara katika Soko la Kariakoo, walisema ziara ya kiongozi huyo imekwamisha biashara zao kutokana na wateja kushindwa kufika sokoni.
Walisema pamoja na hasara waliyoipata, wamefurahishwa na ujio wa Rais Obama ambaye amelifanya jiji hilo kuwa katika hali ya usafi na ulinzi kuimarishwa hivyo kupunguza vibaka ambao walikuwa kero kwa wateja wao na wananchi wengine.
“Kwa kweli mitaro ni misafi, hatukutegemea kama kuna siku ingeboreshwa na kuacha kutoa harufu...tunaomba mpango huu uendelee ili tuweze kujiepusha na maradhi,” walisema.
Wakati huo huo, mfanyabiashara wa nguo sokoni hapo, ameulalamikia uongozi wa jiji kwa kuwatuma askari wawanyang’anye bidhaa zao kwa sababu ya kufanya biashara kandokando ya Barabara ya Uhuru.
“Mimi naona ujio wa Obama hauna manufaa yoyote kwa sisi watu wa chini badala yake imetuongezea umaskini kwa kuchukuliwa bidhaa zetu ambazo zinatuingizia kipato cha kuhudumia familia, kulipia kodi ya nyumba na kufanyia mambo mengine,” alisema.
Bw. Alimas Issa, ambaye ni mfanyabiashara wa Bagamoyo, aliitupia lawama Serikali na kudai haijatoa elimu ya kutosha juu ya ujio wa kiongozi huyo.
Mwananchi apigwa
Saa chache kabla Rais Obama hajawasili nchini, mkazi wa Dar es Salaam ambaye jina lake halikufahamika mara moja, alijikuta akipata kipigo kutoka kwa askari polisi katika eneo la Posta ya Zamani baada ya kumkashifu kiongozi huyo.
Baada ya kipigo hicho, kijana huyo alichukuliwa hadi Kituo cha Polisi Kati kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Watoto wazaliwa MNH
Jumla ya watoto tisa wamezaliwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), usiku wa kuamkia jana, siku ambayo Rais Obama na ujumbe wake aliwasili nchini.
Akizungumza na gazeti hili, Ofisa Habari wa Hospitali hiyo, Bw. Aminiel Algaesha, alisema kati ya watoto hao wanne wa kike na watano wa kiume.
Alisema watoto hao pamoja na mama zao wanaendelea vizuri ambapo hadi jana mchana wameruhusiwa kurudi majumbani.
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi wamelalamikia mwendo kasi wa msafara wa Rais Obama hivyo kukosa fursa ya kumuona.
Wananchi hao waliokuwa wamejipanga barabarani na kuongeza kuwa, kiu yao ilikuwa kumuona kiongozi huyo lakini ndoto hiyo imekuwa tofauti na walivyotarajia.
Bw. Hassan Hamza, mkazi wa Kivukoni, alisema amesimama barabarani tangu saa nne asubuhi lakini alishindwa kumuona kiongozi huyo kutokana na mwendo kasi wa msafara wake.
“Mimi nilijua angepita katika gari la wazi akitupungia mikono badala yake tukashuhudia mabenzi yake myeusi yakipita kwa kasi, hata kama kilichozuia ni sababu za kiusalama...bado angeweza kutupungia mikono,” alisema.
Aliongeza kuwa, “Si kweli kwamba tuliokaa barabarani hatuna kazi za kufanya bali ni utashi wetu tukitaka kumuona kiongozi huyu ndiyo uliotufanya tukae muda mrefu barabarani”.
Katika hatua nyingine, baadhi wa wananchi walionekana wakitoka katika ofisi zao na kujipanga kwenye Barabara ya Sokoine ili kushuhudia msafara wa kiongozi huyo.
Maofisa usalama waliokuwa katika barabara hiyo, waliimarisha ulinzi kwenye eneo hilo wengine wakiwaondoa watu waliosimama katika milango, madirisha ya ofisi zao ili wajipange barabarani.
Ziara ya Rais Obama imelenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara na nchi za Afrika. Kiongozi huyo pia ametembelea Senegal ambapo ujio wake Tanzania, ndiyo unahitimisha ziara yake barani Afrika.
Jana usiku Rais Obama aliandaliwa dhifa ya kitaifa na mwenyeji wake Rais Kikwete ambapo leo, atatembelea mitambo ya kuzalisha umeme ya Symbion iliyopo, Ubungo na kuhitimisha ziara yake ya siku mbili saa sita mchana katika uwanja wa ndege.
Posted: 02 Jul 2013 02:00 AM PDT

 Na Darlin Said

VIJANA wameshauriwa kutotegemea ajira za kuajiriwa badala yake wajiajiri wenyewe kwa kujiunga katika vikundi vinavyotoa mikopo ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Thomas Tebaliwe wakati akisoma risala kwa wahitimu wa Chuo cha Eagle Wings.
Tebaliswe alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa.
Pia aliwashauri wahitimu hao kutumia elimu yao katika kujiajiri kwa kuchangamkia fursa zilizopo ili kuepuka kuwa tegemezi.
"Msitegemee kuajiriwa kwani kitendo cha kujiajiri wenyewe kwa kujiunga katika vikundi vinavyotoa mikopo ni njia mojawapo ya kujikwamua kiuchumi," alisema.
Katika mahafali hayo ambayo ni ya kwanza tangu kuanzishwa kwa chuo hicho zaidi ya wanafunzi 30 walihitimu mafunzo yao katika kozi mbalimbali.
Posted: 01 Jul 2013 10:33 PM PDT

UONGOZI wa Kampuni ya Reli nchini (TRL) umesitisha kutoa huduma ya usafiri wa treni kutokana na vichwa viwili kupata ajali iliyotokea jana asubuhi eneo la Kamata, Kariakoo, anaripoti Stella Aron.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na TRL kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Mhandisi Kipallo Kisamfu, alisema kichwa kimoja kiligongwa na roli la mizigo aina ya Fuso katika makutano ya barabara hiyo.
Katika ajali hiyo, dereva wa Fuso alifariki dunia papo hapo na utingo wake alinusurika.
Aliongeza kuwa, kichwa kingine kiligongwa na daladala aina ya Isuzu ambapo baadhi ya abiria wa basi hilo walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakiwemo askari wawili wa Kikosi cha Reli mmoja akiwa mahututi.
Aliongeza kuwa, kutokana na ajali hizo huduma za treni zilisimama kwa muda na kuwepo kwa mabadiliko ya ratiba yaliyochangiwa na ujio wa Rais Barack Obama wa Marekani.
Alisema uongozi wa TRL umetoa taarifa kwa wakazi wa jiji hilo juu ya kusitishwa huduma ya treni siku ya leo hadi kesho ambapo zitarejea kama kawaida.
Posted: 02 Jul 2013 01:52 AM PDT

 Na Andrew Ignas


UO N G O Z I w a U m o j a wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Tandika wilayani Temeke, Dar es Salaam umesema umechoshwa na mwenendo wa chama kutowapa kipaumbele baada ya uchaguzi.
Hayo yalisemwa juzi na Kamanda wa vijana wa UVCCM katika kata hiyo ambaye pia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Kisarawe, Zena Mgaya wakati wa kufunga Baraza Maalumu la Vijana Kata ya Tandika.
Baraza ambalo liliambatana uzinduzi wa mashina ya UVCCM Kilimani na Sateta ambayo yalizinduliwa na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Omari Matulanga.
"Hili lipo wazi, sasa nasema ni mwisho kama wanachukulia sisi ni kama watu tunawanadia sera zao ili wachukue nchi basi imefikia mwisho, tumechoshwa," alisema Zena Mgaya. 
Posted: 02 Jul 2013 01:40 AM PDT

 Fatuma Mshamu na Josephine Burton

MKAZ I wa Ki b a h a Kongowe aliyetambulika kwa jina la Albert Madeje (30) amefariki dunia baada ya kugongwa na gari wakati akivuka barabara.
Tukio hilo lilitokea Juni 30, mwaka huu majira ya saa tatu kamili usiku alipokuwa akivuka barabara ya Morogoro eneo la Mbezi Mwisho.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura alisema ajali hiyo ilihusisha gari namba aina ya BWM iliyokuwa ikiendeshwa na Herman Berege.
Kamanda huyo alisema, dereva huyo alikuwa akitokea Mbezi kwa Yusuph akielekea Kimara.
Alisema, alipofika maeneo hayo alimgonga mwenda kwa miguu huyo aliyekuwa akivuka barabara.
Katika ajali hiyo, Wambura alisema, Albert alifariki papo hapo.
"Baada ya kutokea ajali hiyo madereva wa bodaboda wa eneo hilo walijichukulia sheria mkononi na kumshambulia dereva huyo.
"Kwa kumpiga mawe, fimbo na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili na kuharibu gari lake kwa kulivunja vioo kwa mawe na kumpora mali alizokuwa nazo kwenye gari," alisema.
Hata hivyo, Kamanda huyo alisema maiti imehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala na dereva amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo hakuna aliyekamatwa na upelelezi unaendelea.
Posted: 01 Jul 2013 10:37 PM PDT
Kassim Mahege na 

Rehema Maigala 
MFALME Mswati III wa Swaziland amewataka Watanzania kubuni b i d h a a mb a l imb a l i ambazo zitakuwa na uwezo wa kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi. 
Rai hiyo aliitoa jana wakati akifungua maonesho ya Biashara ya Kimataifa katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam. 
Alisema, anaamini Tanzania inapenda kuwa miongoni mwa nchi tajiri duniani hivyo kuna kila sababu za kuongeza ubunifu zaidi katika uzalishaji wa bidhaa nchini.
"Maonesho haya yanatoa fursa kwa Watanzania kubuni biashara nyingine zaidi ili kufanya ushindani wa kibiashara duniani," alisema Mfalme Mswati.
Katika hatua nyingine, Mfalme huyo aliwataka vijana kuacha kubweteka badala yake wanatakiwa kupanga mipango ya baadaye kwa lengo la kunyanyua uchumi wa nchi.
Alisema, anaamini kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Swaziland utadumu ikiwa ni pamoja na kutangaza bidhaa kati ya nchi hizo mbili ukiwemo utamaduni.
Kwa upande wake Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati akimkaribisha Mfalme Mswati alisema, Tanzania inajivunia kuwa kisiwa cha amani ambayo Serikali itaendelea kuidumisha daima. 

Posted: 02 Jul 2013 02:09 AM PDT

 Na Kassim Mahege

WATANZANIA wameshauriwa kulipa kodi kwa wakati ili kuharakisha maendeleo ya taifa pamoja na kuepusha usumbufu wa foleni dhidi yao.
Akizungumza na gazeti hili jana kwenye maonyesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba jijini Dar es Salaam, Ofisa Mwandamizi kwa Elimu ya Walipakodi Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Msafiri Mbibo alisema hiyo ni mojawapo ya changamoto wanazokumbana nazo.
"Kuna malalamiko mengi ikiwemo suala la msongamano wa watu wengi wanaposubiri kipindi cha mwisho cha kulipa kodi, ambapo kunakuwa na msongamano wa watu wengi na kusababisha usumbufu kwao," alisema.
Alisema, ni vyema kutosubiri kipindi cha mwisho kulipa kodi kwani wakati huo watu wengi huwa wanalipia, hivyo kusababisha kero.
Akifafanua zaidi alisema, TRA kazi zake kubwa ni kukadiria kiasi cha kulipakodi, kukusanya kodi ikiwemo kuwasilisha makusanyo ya walipa kodi kwa Serikali.
Posted: 02 Jul 2013 02:33 AM PDT

 Na Rehema Maigala

WAAJIRI wenye viwanda nchini wametakiwa kujitokeza na kushiriki katika kazi ya kutoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa wanafunzi ili kuwaongezea ujuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katika maonyesho ya Biashara ya 37 ya Kimataifa, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Zebadiah Moshi alisema waajiri wasaidie kutoa mafunzo kwa wanafunzi katika kujifunza stadi zao kwa vitendo.

"Wanafunzi wanapata shida katika kipindi cha kujifunza kwa vitendo, kwani waajiri wengi wanakuwa hawatoi mwanya kwa wanafunzi kuingia katika viwanda kwa ajili ya kupata elimu ya vitendo," alisema Moshi.
Alisema kuwa, wafanyakazi wa viwandani wawe bega kwa bega katika utoaji wa elimu ili kufanikisha elimu kwa vijana.
Aidha, alisema wafanyakazi wanatakiwa kuingia madarasani kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanafunzi na kuwasiliana na walimu juu ya uandaaji wa mitaala na ufundishaji.

"Teknolojia ya sasa ni ile inayobadilika, hivyo ni vizuri wafanyakazi wa viwandani kushirikiana na vyuo vya ufundi katika utoaji wa elimu hasa kwa kile kipya ambacho kinachojitokeza katika ulimwengu huu," alisema Mosha.
Posted: 02 Jul 2013 02:27 AM PDT

 Na John Gagarini, Kibaha

MTU mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Abdul Ramadhan (35) amewatapeli baadhi ya wakazi wa Kwa Mathias wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani kwa kuwachimbisha kaburi kisha kutoweka.
Aidha, mtu huyo aliwaachia kaburi tupu bila kuzikwa marehemu kama alivyowaomba azike ndugu yake.
Tukio hilo lilitokea juzi kwenye mtaa huo baada ya mtu huyo kufika hapo na kuomba kusaidiwa kumzika mfanyakazi wake ambaye alidai kuwa hana uwezo wa kumsafirisha kwani kwao ni mbali.

Mbali ya kuwachimbisha kaburi wakazi hao pia alifanikiwa kuwaibia simu mbili pamoja na kamera moja na kuwaachia deni kwenye vyakula ambavyo vilitumiwa na wachimba kaburi huku kingine kikiwa kimeandaliwa bila ya kuliwa.
Akielezea mkasa huo Ustaadhi wa Masjid Kadiriya uliopo Kwa Mathias, Said Omary alisema kuwa, mtu huyo alifika msikitini hapo na kukutana na kiongozi kisha kuomba kuwa asaidiwe kuzikiwa mfanyakazi wake msikiti ukamkubalia na taratibu zikaanza kufanyika.
Omary alisema kuwa, baada ya kuelekezwa na mkuu wake alitakiwa ashughulikie suala hilo na kwenda na mtu huyo kwenye makaburi ya mambo akiwa na watu wengine watatu kwa ajili ya kuchimba kaburi kwa ajili ya kumsitiri marehemu.
"Tulikwenda makaburini na wachimbaji wakaanza kazi ya kuchimba kaburi akawaletea chai na maandazi 20 wakanywa wakaendelea na kazi yao, mimi akaniambia twende Hospitali ya Tumbi aliko marehemu kwa ajili ya kumwandaa," alisema Omary.

Alisema, wakiwa njiani alimwambia kuwa anaomba simu yake ili awasiliane na ndugu zake kwani ya kwake imeisha chaji pia amtafutie mpigapicha kwa ajili ya tukio hilo kwa ajili ya kuwaonyesha ndugu juu ya mazishi hayo.
" Tu l i kwe n d a kwa mp i g a p i c h a wakakubaliana apige picha akasema kabla ya kwenda Tumbi wakachukue nyama na vitu vingine kwa ajili ya msiba huo na walipofika Maili Moja wakachukua nyama kilo 25," alisema Omary.
Aliongeza kuwa, wakati wameshapima nyama aliwaambia ngoja akanunue viungo vingine lakini hakurudi tena na kutoweka kusikojulikana huku kaburi likiwa limeshachimbwa na liko wazi hadi sasa.

Kwa upande wake mpigapicha Juma Said ambaye yeye aliibiwa kamera na simu alisema kuwa, walikubaliana apige picha 36 hadi 40 ambazo gharama yake ni sawa na sh. 36,000 au 40,000.
Alisema, wakati wako kwenye harakati ya kununua nyanya alimwachia begi likiwa na kamera na simu lakini aliporudi hakumkuta akiwa yeye na Ustaadhi na dereva wa teksi ambayo aliikodisha kwa shughuli za mazishi hayo.
"Alituacha mimi na ustaadhi tukiwa na nyama huku tukimsubiria hali ambayo ilitufanya tuingie matatani kwani wauzaji nyama ilibidi watubane ndipo tulipowaelewesha juu ya hali halisi ndiyo ikawa salama kwetu na kuondoka," alisema.
Watu waliokumbwa na hali hiyo walisema kuwa mbali ya kudanganya mambo yote hayo pia tapeli huyo aiagiza chakula sahani 20 kwenye hoteli lakini hakuonekana tena.

"Katika kufuatilia walibaini jina la mtu huyo, kwani siku moja kabla ya tukio hilo alilala kwenye nyumba ya kulala wageni ya Iwawa iliyopo Mtaa wa Kwa Mbonde jirani na hapo wakazi hao walitoa taarifa kwenye Kituo cha polisi Kwa Mathias juu ya tukio hilo," alidai mkazi mmoja.
Posted: 02 Jul 2013 03:27 AM PDT

 Na Heckton Chuwa, Moshi
MRAJIS wa vyama vya ushirika nchini, Dkt. Audax Rutabanzibwa, amesema kuwa serikali kupitia ofisi yake itahakikisha Benki ya Ushirika mkoani Kilimanjaro (KCBL) haifi na badala yake inaimarika ili kuinua ushirika na mkulima mmoja mmoja.
Dkt. Rutabanzibwa aliyasema hayo wakati akizungumza na wanachama wa chama kikuu cha ushirika mkoani humo (KNCU) wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika juzi mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
"Ni vyema benki hii ikaimarishwa na zingine zianzishwe sehemu mbalimbali hapa nchini, hizi na taasisi za kifedha zinazomgusa mkulima mmoja kwa mmoja kwa vile zinaanzishwa na wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya ushirika," alisema.


Alivishauri vyama vya msingi pamoja na KNCU kuhakikisha wanaitumia benki hiyo kwa kukopa fedha kwenye taasisi hiyo kwa vile faida itakayopatikana itarudi kwa wanachama wake kupitia gawio.
"Serikali kwa upande wetu tutafanya kila litalowezekana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo benki kuu, kuhakikisha benki hii inakua na kuimarika kwa vile inamgusa mkulima moja kwa moja na ushirika," alisema.
Aidha, Dkt. Rutabanzibwa alitahadharisha uuzwaji wa mali za kiwanda cha kukobolea kahawa kilichopo mjini Moshi cha TCCCo kwa lengo la kununua mitambo mipya ya kukobolea kahawa kutokana na iliyoko sasa hivi kuchakaa na hivyo kuathiri utendaji.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa KNCU, Bw. Maynard Swai, alisema kuwa chama hicho kikongwe barani Afrika tayari kimeilipa KCBL zaidi ya sh. milioni 150 ikiwa ni sehemu ya deni wanalodaiwa na benki hiyo.
"Ms imu wa 2 0 0 8 / 2 0 0 9 hatukupeleka malipo yoyote KCBL kutokana na mdororo wa kiuchumi ulioikumba dunia na kuiathiri KNCU kiasi cha kupata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 800," alisema.
Katika hatua nyingine, Bw. Swai amesema kuwa chama hicho kilikusanya kilo 1,444,250 za kahawa hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, yenye thamani ya shilingi bilioni 3.7 ambayo alisema ni asilimia 72.7 ya lengo lililowekwa la kukusanya kilo 2,000,000 za kahawa katika msimu wa 2012/2013.
Posted: 02 Jul 2013 03:09 AM PDT

 Na Yusuph Mussa, Lushoto

BAADHI ya madiwani wa Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Ta n g a w ame w a t a k a wakaguzi kuzipa usajili shule nne za msingi na mbili za sekondari kwa madai wananchi wamechangia nguvu zao kujenga shule hizo.
Miongoni mwa shule hizo ni pamoja na Shule ya Sekondari January Makamba iliyopo Kata ya Milingano katika Tarafa ya Mgwashi wilayani humo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki kwenye Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, Diwani wa Kata ya Milingano Ramadhan Hozza alisema wananchi wametumia nguvu zao kujenga Shule ya Sekondari January Makamba na ile ya Kwalei ukiwemo mfuko wa jimbo.
"Nia ya kujenga shule za msingi ni kupunguza umbali mrefu wa kutembea watoto wetu, hivyo tunaomba Serikali itoe usajili kwa shule nne za msingi.
"Pia kwa sekondari ya January Makamba na Kwalei, Shule ya Sekondari Mbelei iwe ya kidato cha tano na sita, kwani wananchi na mfuko wa jimbo umechangia shule hizo," alisema Hozza ambaye pia ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli January Makamba.


Diwani wa Kata ya Vuga, Ali Sechonge alisema umefika wakati kuacha kuongeza shule za sekondari na kujenga za ufundi, kwani kutawasaidia wanafunzi wanaoishia kidato cha nne kuweza kuwa na ujuzi na kujiajiri.
"Utitiri wa shule za sekondari ni mkubwa sana na nyingine zilijengwa kisiasa. Kama kuna uwezekano kuanzishwe shule za ufundi badala za sekondari, kwani watoto wanaomaliza kidato cha nne bado ni wadogo na hawana pa kwenda, hivyo shule za ufundi zitawasaidia kupata ujuzi," alisema Sechonge.
Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Bumbuli, Ramadhan Mkongo alisema halmashauri hiyo yenye kata 16 ina shule za sekondari 28 kati ya hizo nne ni binafsi.

Hata hivyo, kutokana na hali hiyo, aliwaomba madiwani wasiongeze shule nyingine za sekondari bali ziboreshwe zile zilizopo huku akisema Sekondari ya January Makamba itafunguliwa ikizingatia vigezo.
"Ni kweli mfuko wa jimbo pamoja na nguvu za wananchi zimetumika kujenga Shule ya Sekondari Janauary Makamba, na sisi tutapitia na kuwajulisha wakaguzi wa Kanda ya Kaskazini, lakini ni lazima tufuate utaratibu wa wizara, badala ya kujenga mpya tuboreshe zilizopo," alisema Mkongo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli, Beatrice Msomisi akijibu hoja za madiwani hao alisema Sekondari ya Mbelei kuwa ya kidato cha tano na sita alisema vigezo vya shule ya aina hiyo lazima ziwe na huduma muhimu kama maji kwa vile zitachukua wanafunzi kutoka pembe zote za nchi.
Akifunga baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bumbuli Amir Shehiza alisema ili kupanua uchumi wa halmashauri hiyo watajenga soko na stendi kwenye miji ya Soni na Bumbuli huku wakiboresha barabara zinazounganisha vijiji, kata, tarafa na wilaya jirani.

No comments:

Post a Comment