Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
23/3/2015. Dar es
salaam.
Tanzania inatarajiwa
kuwa mwenyeji wa mkutano wa wawekezaji (Round Table Investment Forum) na Marais
wa nchi 5 za ukanda wa Afrika Mashariki utakaofanyika jijini Dar es salaam
kuanzia Machi 25 hadi 26 mwaka huu.
Akitoa taarifa ya
mkutano huo Mkuu wa wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Saidi Meck Sadiki amesema kuwa Marais hao Paul Kagame wa Rwanda,
Pierre Nkurunzinza wa Burundi, Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya
na Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo watahudhuria mkutano huo
wakiwa wameambatana na jumla ya
wawekezaji 350.
Amesema Tanzania kwa
mara nyingine imepata heshima ya kuandaa mkutano huo na kufafanua kuwa wawekezaji hao wamekwisha anza kuwasili jijini Dar es salaam kuanzia Machi 22 , Machi huku marais nchi hizo
wakitarajiwa kuwasili jijini humo kuanzia Machi 24,2015.
Amesema wakiwa nchini
Tanzania Marais hao watashiriki kwenye mkutano wa wawekezaji utakaofanyika ukumbi
wa Mikutano wa Kimataifa Mwalimu J.K.Nyerere kuanzia Machi 23 hadi 26,
watatembelea bandari ya Dar es salaam ili kuona namna nchi za Ukanda wa Afrika
Mashariki zinavyoshirikiana katika masuala ya ushuru wa forodha na usafirishaji
wa bidhaa mbalimbali.
Amebainisha kuwa kabla
ya kuaondoka nchini Tanzania Machi 26,
2015 Marais hao pia watatembelea miundombinu ya reli inayotumika kusafirisha
mizigo nchi za maziwa makuu kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika
usafirishaji wa bidhaa mbalimbali baina ya nchi zao.
KUHUSU MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA JIJINI DAR ES
SALAAM.
Aidha, kuhusu mvua zinzoendelea kunyesha katika jiji la Dar es salaam na kusababisha madhara, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
salaam Saidi Meck Sadiki amewataka wananchi kuzingatia agizo la kuhama
mabondeni na maeneo mengine hatarishi ili waepuka maafa kufuatia watu 7
kupoteza maisha kutokana na kutokana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha.
Akifafanua kuhusu
matukio hayo Mhe. Sadiki amesema maeneo yaliyokumbwa na mafuriko hayo na kupata maafa hayo ni bonde la Mto Msimbazi
na eneo la Buguruni kwa Myamani.
Amesema kuwa maeneo
yaliyokumbwa na mafuriko hayo yameonekana kuwa
na wingi wa takataka ngumu na wingi wa mifuko ya plastiki iliyotupwa na wakazi hao hali iliyochangia
kuziba mifereji inayopeleka maji katika bonde la mto Msimbazi na maji hayo
kuhamia kwenye makazi ya watu.
Ameeleza kuwa kazi ya
uokoaji , kumwaga dawa kwenye maji yaliyotuama ili kuzuia athari ya magonjwa ya
milipuko, kuzibua mifereji na kukusanya taka katika maeneo hayo inaendelea ili
kuruhusu maji kupita kwa urahisi na kuwataka
wakazi hao kuepuka kutupa taka ngumu zinazoziba mifereji ya maji.
Amesema Serikali
inasubiri taarifa kutoka kwa viongozi wa Serikali za Mitaa kwa maeneo ambayo
wakazi wake wanaishi kihalali ili waweze kupatiwa misaada ya kibinadamu.
Kwa upande wake
Kamishina wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Suleiman Kova
amethibitisha vifo vya watu hao 7 waliopoteza maisha kutokana na maeneo yao
kukumbwa na mafuriko pamoja na athari ya Umeme.
Akitoa ufafanuzi wa
vifo hivyo amesema kuwa watu 5 wamepoteza maisha kwa kusombwa na maji na
wengine 2 wamepoteza maisha kutokana na ajali iliyosababishwa na Lori moja
kugonga Transfoma ya umeme eneo la Buguruni Mnyamani.
Kamishna Kova amesema
tayari Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na
Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) wameunda kikosi kazi cha uokoaji.
Ametoa wito kwa
madereva wa magari ya mizigo, mgari binafsi na yale ya abiria kuepuka kupita
katika maeneo yaliyojaa maji ili kuepuka ajali na vifo vinavyoweza kuzuilika.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam akitoa taarifa ya mkutano
wa wawekezaji (Round Table Investment Forum) na wakuu wa nchi 5 za ukanda wa
Afrika Mashariki utakaofanyika jijini Dar es salaam kuanzia Machi 25 hadi 26 mwaka huu.
Kamishina wa Polisi wa
Kanda Maalum ya Dar es salaam Suleiman Kova akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na
usalama katika jiji la Dar es salaam na vifo vya watu 7 waliopoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua
kubwa zinazoendelea kunyesha katika jiji
la Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment