MNAMO Mei
2012, gazeti la Rai
Mwema lilichapisha mahojiano maalum na Sophia Simba ambayo yalikuwa na
kichwa cha habari ‘Si kweli kwamba sipendwi na wanaume – Sophia Simba’.
ili kuweza kumfahamu mwanamama huyo ambaye Jumamosi
Machi 11, 2017 ilikuwa siku mbaya kwake baada ya kutimuliwa ndani ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) kwa makosa ya kinidhamu.
Wakati mahojiano
hayo yakifanyika, Sophia alikuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala
Bora – ndiyo inayoshughulikia pia masuala nyeti ya nchi), na pia alikuwa
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Endelea na
mahojiano hayo, ambapo pamoja na mambo mengine, alizungumzia masuala ya
uhusiano wake wa kimapenzi…
Raia Mwema: Wasomaji wetu wangependa kukufahamu kwa
sababu mengi yamekuwa yakisemwa na
yakinong’onwa hususan kuhusu elimu yako; labda kwa vile hawaifahamu
vizuri. Unaweza kutupa CV yako kwa kifupi?
Mama Sophia Simba: Asante kwa kunipa
nafasi hii adimu. Nimefurahi kwamba
umeweza kufika ofisini kwangu na kuweza kuongea na mimi. Nashukuru
kwamba umeona upo umuhimu wa watu kunijua mimi Sophia ni nani hasa.
Ni kweli
maneno mengi yamekuwa yakisemwa ambayo hayapendezi, lakini nitafanyaje? Kwa hiyo, kwa kifupi sana ningependa
nikufahamishe labda pengine kwa kupitia
wewe watu watanifahamu.
Mimi
naitwa Sophia Simba. Ni Sophia Mathew Simba. Nyambi ni jina langu la nyumbani.
Wazaramo wana majina yao ya ukoo, kwa hiyo mimi ni Nyambi na mdogo wangu
alipewa jina lingine. Nilipokuwa mdogo baba yangu akasema huyu ni Nyambi.
Kwa kifupi
sana, mimi ni mtoto wa mfanyabiashara. Baba yangu alitokea Kisarawe, kijiji
kinachoitwa Sungwi. Baba yangu alisoma Minaki. Alipomaliza Minaki alirudi hapa
Dar es salaam. Baba yangu aliwahi kufanya kazi mpaka ya uvuvi. Aliacha shule kutokana na umbali kutoka
kijijini kwake Sungwi kwenda Minaki.
Watoto
waliokuwa wakitoka bara walikuwa wanasoma boarding, lakini watoto wa Kisarawe
wenyewe walikuwa wanatakiwa watembee umbali mrefu. Kwa hiyo, kutokana na hiyo
alifikia mahali haikuwezekana.
Baba yangu
mwanzoni alikuwa Mwislamu. Alikuwa
anaitwa Omari Simba. Kutokana na kusoma pale Minaki, aliamua kubadilisha dini.
Baba yangu alibatizwa katika Kanisa la St. Albans – hili la hapa mjini. Na baada ya hapo baba
yangu aliondoka akaenda Morogoro kufanya shughuli za biashara.
Kule
alikutana na mama yangu, mwanamke wa Kiluguru ambaye naye historia yake alikuwa
Sister wa Roman Catholic. Kwa hiyo walikutana na wakaoana.
Katika
maisha yetu yote tumeishi kama Wakristu wa Roman Catholic. Mpaka leo mimi ni
Mroman Catholic ingawaje kila mtu ananipa dini ambayo anaitaka. Kwa hiyo, mimi
ni mmoja wa watoto tisa. Mimi ni wa pili.
Raia Mwema: Makazi yenu hasa yalikuwa wapi?
Mama Sophia Simba: Makazi yetu yalikuwa
Dar es salaam na Morogoro. Dar es Salaam tuliishi Bungoni, Ilala. Lakini tukiwa
wadogo kabisa baba yangu alijenga nyumba yake ya kwanza kabisa Morogoro, Kwa
Kingu.
Alifanikiwa
sana kwa shughuli za baa. Mimi ni mtoto ambaye nimesomeshwa kwa pesa za pombe.
Baba yangu alikuwa na baa inayoitwa Uzaramo Bar, Morogoro lakini pia alikuwa na
baa inayoitwa Simba Bar. Kwa hiyo, mimi kufungua vizibo vya bia najua.
Nikiwa
bado mdogo nilikuwa nauza mishikaki. Siku zote nyumba yetu ilikuwa upande baa,
upande tunaishi sisi. Kwa hiyo, baba yangu aliendelea na shughuli za baa muda
mrefu.
Raia Mwema: Ulianza shule wapi?
Mama Sophia Simba: Mimi nilianza
shule Morogoro katika shule inayoitwa
Kilakala, baada ya hapo nikapelekwa
shule ya boarding inayoitwa Ilonga Middle School, Kilosa. Baada ya hapo
nikasoma Forest Hill Secondary School. Sisi ndiyo waanzilishi wake.
Ule mwaka
ambao wanafunzi wengi tuliambiwa hatukuchaguliwa tuliunganishwa darasa la saba na la nane. Kwa
hiyo sisi tulimalizia darasa la nane. Huo ulikuwa mwaka 1965. Shule nyingi (za binafsi) zilianzishwa mwaka
huo. Shule za Kibohehe, Forest Hill, Mzizima na Kinondoni, zote zilianza wakati
huo.
Baada ya
pale nikaenda Kibosho Secondary School. Kwa bahati mbaya baba akafariki, wakati
huo nikiwa nafanya kazi NDC. Kabla hajafariki, baba alitaka sana nifanye
shughuli za biashara, niendeleze biashara ya familia.
Baada ya
kumaliza shule nilichaguliwa nikasomee ualimu lakini sikwenda, na badala yake nikapata kazi NDC. Hapo NDC
nilianza kazi 1971 hadi mwaka 1979.
Baada ya
hapo nikaingia Lonrho Group of Companies baada ya kuacha kazi NDC. Kutoka pale
nikaanza kazi Metal Engineering Industries Development Association (MEIDA)
ambayo ilianzishwa na Waswedish. Nikiwa hapo nikaamua kwenda kusoma. Nilianza
mafunzo ya Certificate of law mwaka 1985. Nilipenda sana kusomea sheria.
Mwaka 1987
nilianza kusomea shahada ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na
nikahitimu mwaka 1992 au 1993. Kuna mwaka hapo katikati chuo kilifungwa kwa
sababu ya kuwapo mgomo.
Baada ya
kuhitimu Chuo Kikuu nikarudi kufanya kazi Metal Industries; kwani wakati nasoma
walikuwa wamenipatia likizo isiyokuwa na malipo. Baada ya kurudi walinipandisha
cheo kuwa legal and administrative officer; kwani kabla ya kwenda chuo kikuu
cheo changu kilikuwa administrative officer tu.
Wakati
niko NDC nilikuwa katibu wa tawi la UWT la NDC na Mama Anna Mkapa alikuwa
mwenyekiti wetu, tulifanya mambo mengi mazuri.
Nilipokuwa
MEIDA niliomba pia kuwa diwani wa viti maalumu. Kulikuwa na uchaguzi mwaka 1993
au 1994. Nikawa diwani hadi 1995. Mwaka 1995 wakasema kuna viti maalumu vya
ubunge kwa akina mama. Mimi nikagombea vitu maalumu.
Mwaka huo
wa 1995 nilipata invitation ya kwenda Beijing, China kuhudhuria mkutano wa
wanawake duniani. Nikakataa, nikampa mwenzangu nikamwambia mimi siendi nitabaki
hapa kwa ajili ya kampeni za ubunge. Sikwenda mimi Beijing kwa sababu ya
kampeni hiyo. Kwa hiyo mwaka 1995
Nikashinda,
na hivyo nikaingia bungeni.
Mwaka 1995
nilifanya mafunzo ya Post Graduate Diploma on Women Law kwenye Chuo Kikuu cha
Zimbabwe na mwaka 2005 nilifanya Masters
ya Community Economic kwenye Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Thesis yangu ilikuwa Women
and Economic Empowerment in Tanzania.
Mwaka 1972
mimi niliolewa. Mume wangu alikuwa ni mwanasheria wa Chama cha Ukombozi cha
Afrika Kusini cha ANC. Siku zile walikuwa wakiwaita wakimbizi, lakini wenyewe
walikuwa wanataka waitwe freedom fighters.
Mume wangu
aliruhusiwa pia kufanya kazi za uanasheria nchini. Kabla ya kufariki aliwahi
kufanya kazi pia benki. Alikuwa anaitwa Clifford Zex Senge. Wengi walikuwa
wanamwita kwa jina la Cliff. Wanasheria wengi wanamjua.
Kwa hiyo,
niliolewa na Cliff na nikazaa naye watoto wawili. Watoto hao walikwenda Afrika
Kusini kwa baba yao lakini sasa wote wamerudi. Maisha ya Afrika Kusini ni
magumu hayako that easy.
Kuna watu
wanasema mimi ni kituo cha polisi, wanaume wananikimbia. Nilisoma kwenye gazeti
(eti) wanaume hawanitaki. Lakini I was married.
Raia Mwema: Uliolewa na Msouth Afrika na kwa bahati
mbaya akafariki dunia. Lakini nasikia ulikuwa na mahusiano na ulionekana mwaka
1995 ukiwa na Kitwana Kondo, Meya wa zamani wa Dar es Salaam na mbunge wa
zamani wa Ilala. Uhusiano wako na yeye ulikuwa wa aina gani?
Mama Sophia Simba: Sawa, mimi nilikutana
na Mzee Kondo… Kwanza nakubali nilikuwa na mahusiano naye, na nimezaa naye
mtoto wa kiume. Nilikuwa na Mzee Kondo kutoka mwaka 1975. Nilikutana naye
wakati akigombea ubunge; mimi nikiwa kama mpiga debe wake. Kwa hiyo tulikutana
mwaka 1975 na tukaachana mwaka 1983.
Siyo kama
tulioana, hapana, alikuwa boyfriend. Yeye siku zote amekuwa na mke wake. Kwa
hiyo, nilizaa naye kweli mtoto mmoja na mpaka sasa hivi mimi namuheshimu Mzee
Kondo. Na baada ya hapo, mwaka 1983, ameshaoa mara mbili au mara tatu lakini
mimi bado namheshimu mpaka watu hawaelewi mahusiano yangu mimi na yeye yakoje.
Hata
tulipokwenda bungeni watu wengine walidhania ni mtu na mkewe, lakini mimi
sijaolewa na Kitwana Kondo. Namheshimu sana, ni baba wa mtoto wangu.
Raia Mwema: Sasa tuje kwenye nafasi yako ya uenyekiti wa UWT. Wewe katika miaka
yako hii mitano unataka UWT iwe ya namna gani baada ya kuvaa kofia iliyovaliwa
na wanawake wazito huko nyuma kama Bibi Titi Mohammed, Sophia Kawawa na Anna
Abdallah?
Mama Sophia Simba: Asante kwa swali hilo.
Kwanza nishukuru walionitangulia kwamba wamefanya kazi kubwa. Wao ni role
models ambao tulikuwa tukiwatizama na sisi kufanya kazi chini yao.
Nikiri
kwamba nimefanya kazi chini ya Mama Sophia. Alipokuwa mwenyekiti, mimi nilikuwa
katibu wa tawi. Mama Abdallah alipokuwa
mwenyekiti wa taifa, mimi nilikuwa mwenyekiti wa UWT tawi la kata ya Upanga
Magharibi. Kwa hiyo, hawa wote wamekuwa viongozi wangu na nimewaona walivyokuwa
wakifanya kazi.
Mimi
katika kipindi hiki cha miaka mitano nitaendeleza yale yote ambayo nimejifunza
kutoka kwao, lakini pamoja na hivyo; mambo yamebadilika. Itabidi na sisi UWT
tubadilike.
Ukumbuke
kwamba hapo nyuma mimi nilipoinga UWT nilikuwa mfanyakazi. Sasa hivi baada ya
matawi ya kazini ya chama kuvunjwa, kumekuwa na gap hapo. Wafanyakazi wengi wapo wapo tu. Wanawake wengi hawapo katika
chama, hawapo katika jumuiya, wapowapo tu.
Wapenzi
wengi wa CCM wako kama vile wa Simba na Yanga – hawana kadi, hawana nini. Kwa
hiyo, mimi mkakati wangu mmoja mkubwa ni kuhakikisha nawapata hawa akina mama.
Nitawafuata hukohuko waliko katika maeneo yao kuwahamasisha kuinga UWT.
Hadi sasa
tunaendelea vizuri. Tuna kitengo kizima kinachoelezea jinsi ya ku-capture na
kuwahamasisha akina mama na kuwaambia; na wewe pia unaweza kuwa mwanachama wa
UWT, unaweza kuwa mwanachama wa CCM, usikae tu bure hivi hivi.
Kwa
kufanya hivyo, UWT itakwenda na wakati. Tunawahitaji hawa young generation
twende nao tusiwaache nyuma. UWT isiwe jumuiya ya wazee na watu wazima tu.
UWT iwe ni
jumuiya ya wanawake vijana pia, kwa sababu naamini ukishirikiana na vijana kuna
mengi ambayo utaweza kujifunza. Tunaweza tukaifanya UWT ikawa hatua moja zaidi
kutoka hapa tulipo.
UWT
tumejipanga kuanzisha tawi la UWT makao makuu. Na lingine ambalo tumesema
tutafanya ni kuifanya UWT isiwe tegemezi kiasi hicho. UWT ina mali zake nyingi
ambazo zimekuwa dormant kwa muda mrefu. Kwa hiyo, tunataka tuzitumie ili tuweze
kwa kiasi fulani tujitegemee.
Hivi sasa
watendaji wote UWT wanategemea ruzuku kutoka CCM. Kwa hiyo, tunakipa mzigo mkubwa sana Chama
cha Mapinduzi. Lazima tuangalie ni jinsi gani tunaweza tukatumia raslimali tulizokuwa nazo, nadhani tutaipunguzia mzigo
CCM.
Kama
nilivyosema siku yangu ile ya kwanza, ni lazima twende na wakati. Nilitumia maneno: ‘UWT iende na dot com.’
Generation ni dot com, tusirudi nyuma.
Raia Mwema: Lakini baadhi ya watu wanasema kwamba
labda umeanza na gea ngumu kidogo baada ya Katibu Mkuu wako, Husna Mwilima kuwa
amewajibishwa na Baraza Kuu. Huoni kwamba kitendo hicho cha kumwondoa ni hatua
ngumu kwako?
Mama Sophia Simba: Kwanza nikiri kwamba si
jambo zuri kwamba katibu mkuu wangu imebidi Baraza Kuu limwondoe. Mimi binafsi
siyo kitu ambacho nilitarajia, kwa sababu mimi ndiye niliyemtafuta yeye na jina lake kulipeleka kwenye vikao vya chama
ili lipitishwe.
Kwa hiyo,
hiyo imeonyesha kwamba ni udhaifu kwa upande wangu. Nikiri kwamba sikulifanyia
kazi vizuri lile jina. Pengine nilikuwa sikujiandaa vizuri. Binadamu kufanya
makosa ni kawaida, na pale nilikosea.
Hata
hivyo, nilijitahidi sana kufanya naye kazi vizuri. Nimekaa naye kipindi cha
mwaka mmoja. Unapopewa madaraka inabidi kwanza ujifunze, kwa hiyo nilijitahidi
sana kuhakikisha kwamba katibu mkuu
huyu, ambaye mimi mwenyewe nilimtafuta, aweze ku-cope na ile ofisi.
Lakini
kukawa kuna matatizo ya… Kwanza huwezi kumfananisha huyo na akina Thecla
Mchauru, Kate Kamba, Dk Msimu ambao kiwango cha elimu yao kidogo ilikuwa zaidi.
Hata Halima Mamuya elimu yake iko juu zaidi ya huyu.
Huyu
alibebeshwa mzigo ambao hakustahili, tulifanya makosa. Tulimbebesha mzito
mkubwa wa kiutendaji. Pengine kisiasa kazi nyingine angeweza kuzifanya, lakini
kiutendaji… Kuna kazi za utendaji zina miiko yake ambayo kiwango cha elimu yake
ilikuwa kidogo kina matatizo.
Raia Mwema: Sawa kulikuwa na makosa, lakini wewe
ulimpataje pataje hadi akaukwaa ukatibu mkuu wa UWT?
Mama Sophia Simba: Huyu alikuwa mjumbe wa
Baraza Kuu la UWT, ndicho kitu kimoja ambacho kilinifanya nimteue. Nimekuwa
naye kwenye baraza tokea mwaka 2003. Mimi nimemjua Husna wakati nikigombea
ujumbe wa Baraza Kuu. Kwa hiyo, nilipokwenda Arusha yeye ndiye aliyenisaidia
kutafuta kura, siyo campaigner, lakini ndiyo
nilianza kumfahamu. Lakini nikamfahamu pia ndani ya vikao. Kwa hiyo
nilimjua kwa hivyo.
Na kwa
bahati mbaya sana, sikujaribu kuomba ushauri kwa mtu yeyote kutaka kujua habari
zake zaidi. Ndiyo maana nasema nakiri makosa. Hakuna mtu aliyenishawishi kuhusu yeye.
Raia Mwema: Eneo lile la Maria Hostel kulikuwa na
mpango wa kujenga jengo kubwa kuondoa hali ya utegemezi ya UWT ambayo umekwishaieleza. Je mpango huu
bado upo?
Mama Sophia Simba: Mpango wa
kuendeleza kiwanja cha mtaa wa Lindi cha
Maria Nyerere Hostel upo. Tumekuta mpaka na ramani zimeshachorwa, lakini sisi
kamati yetu ya utekelezaji tunataka tujiridhishe, tutumie utaalamu zaidi. Lile
jengo tulilolikuta pale linataka kujengwa lilikuwa haliendani na wakati.
Kwa hiyo,
tulichokuwa tukingojea kwanza ni kupata Baraza la Wadhamini kwa sababu lile
baraza la wadhamini lililopita la UWT, limemaliza muda wake. Sasa limepatikana
jipya. Majuzi walikuwa na kikao chao cha kwanza cha Baraza la Wadhamini.
Mwenyekiti wao ni Mzee Said El Maamry ambaye ni mwanasheria.
Tumelizindua
baraza letu na sasa tunachotaka ni kupata hati ya pale Maria Nyerere. Maria
Nyerere ilikuwa trusteeship ya Tanganyika Women, sasa hivi ni Tanzania Women.
Jina limeshabadilishwa, na sasa tunangojea hati mpya. Tukishapata hati tutaweza kuwekeza pale na kujenga kitu
kizuri.
Raia Mwema: Kitu kizuri namna gani, kwani mnataka
kujenga kitu gani?
Mama Sophia Simba: Tunataka tujenge office
blocks na apartments, na sisi wenyewe tutakuwa na floor moja kwa ajili ya ofisi
zetu. Tutakuwa na ukumbi wetu mkubwa wa mikutano, ni vitu kama hivyo.
Raia Mwema: Sasa hebu tuelezee kuhusu jengo jipya
lile ambalo lilikuwa makao makuu. Nini mnachotarajia kupata kutoka hapo kwa sababu
nalo lilileta minong’ono.
Mama Sophia Simba: Jengo jipya limekwisha,
linangojea kufunguliwa. Lakini kwa kifupi sana niseme kwamba jengo hilo jipya haliko chini ya
management ya UWT. Jengo jipya mkataba
uliosainiwa ulikuwa ni mkataba wa UWT kulipwa certain amout of money kwa mwaka,
hakuna percentage.
Mkataba
uliosainiwa haukuwa mzuri. Kwa hiyo, sisi UWT hatuna eneo lolote. Sisi tutakuwa
tunapata kodi ndogo tu. Kiwanja bado ni cha kwetu, lakini lile jengo wale tumeingia nao mkataba
wa miaka 33. Kwa hiyo they will run that thing kwa muda wa miaka 33. Sisi
tutapata pesa kidogo.
Naona aibu
hata kuzisema. Pesa tutakazozipata kwa mwaka hazisaidii hata kuwalipa mishahara
makatibu wetu wote wa jumuiya lakini ndiyo hivyo tumejifunza kutokana na
makosa.
Raia Mwema: Hivi hakuna namna ya kuweza kukutana na
waliowekeza mkajadiliana nao kurekebisha huo mkataba?
Mama Sophia Simba: Mkataba uliopo ni
binding, mkataba umeshaingiwa. Hiyo amount ambayo imefikiwa ni ambayo baada ya
kuzungumza nao wakaongeza. Lakini sisi tunasema
tumeshajua pale yeye anakodisha kwa kiasi gani, basi tunataka tumwambie,
basi, na sisi tuongezee kigogo, lakini hiyo ni subject ya mazungumzo ya sisi na
yeye.
Raia Mwema: Bunge linalokwisha kwa sasa lina wanawake wanaowakilisha majimbo 17. Je, mnao
mkakati wowote wa kuweza kuwasaidia wanawake kuwa na ushindani wa kutosha na
wanaume kwenye majimbo?
Mama Sophia Simba: UWT tayari
tumeshatengeneza mkakati wetu wa kuhakikisha
wanawake wengi zaidi wanajitokeza kugombea kwenye majimbo. Majimbo siyo
ya wanaume, majimbo ni yetu sote kwa hiyo kuna ziara tumeshajipanga. Tutazunguka nchi nzima
kuhakikisha wanawake wanajitokeza kugombea kwenye majimbo.
Tutahakikisha
wanakwenda kupiga kura na kuhamasisha wanawake kuipigia kura CCM. Kwa hiyo
tunakwenda kupiga ndege watatu kwa jiwe moja.
Naamini
itakapofika mwaka 2015 wanawake watakaokwenda kwenye majimbo watakuwa wengi
zaidi kwa sababu tumeshawawekea ukomo.
Wengine
wamekuwa wabunge wa vitu maalumu kwa miaka 15 na wengine hivi sasa wameshaingia
miaka 20, na bado hawajathubutu kugombea kwenye majimbo. Lakini kwa sasa
mkakati tulionao ni kuhakiksiha wanawake
wengi wanajitokeza.
Raia Mwema: Halmashuri Kuu ya CCM imekubaliana na
pendekezo la Baraza Kuu lako juu ya ukomo wa viti maalumu, lakini baadhi ya
wabunge waliopita wa muda mrefu ambao wanadhani mlikuwa nao, wanadai
mumewatosa. Hayo manung’uniko yao wewe unayajibuje?
Mama Sophia Simba: Nafurahi kupata nafasi
hii nijibu hilo. Suala la ukomo wa viti maalumu halikuanza na mimi. Suala la
ukomo wa vitu maalumu tumeanza kulizungumzia mwaka 1998 au 1999. Lakini kwa
sababu sisi wenyewe tuko mle mle kwenye baraza Kuu, likaminywa.
Likarudi
tena 2000 hadi 2005. Likazungumzwa
tukiwa Arusha, likazungumzwa tukiwa Moshi. Watu wanalipooza kwa sababu kila
binadamu tuna kitu kinaitwa choyo, unajifikiria wewe. Kwa hiyo, lile jambo ni
jambo la siku nyingi. Hao wote wanaolalamika wanalijua, wanaiongopea jamii.
Suala la
ukomo halikuletwa na Sophia Simba, suala la ukomo lililetwa na Baraza Kuu,
isipokuwa kwenda kwenye NEC ndiyo limepelekwa safari hii.
Tatizo ni
kwamba siku zile tulikuwa tunalizungumza kwenye Baraza Kuu lakini halitoki kwenda NEC. Hivi sasa
limekwenda kwenye NEC, na kwa bahati mbaya sana hao wanaolalamika wengine
wameshakuwa wabunge miaka 15, wengine miaka 10.
Baraza Kuu
lilisema kuwa nafasi za vitu maalumu ambazo ni za upendeleo, siyo wapendelewe
hao hao tu kila siku. Ziliwekwa ili kumuwezesha mwanamke aweze kupambana na
vile vigezo ambavyo tumesema vinatufanya wanawake tushindwe kuingia kwenye
majimbo nao kwa sababu ya kuwapo mfumo dume.
Tumesema
wanawake kwa sababu ya mfumo dume tuna aibu, hatuwezi kuongea kwenye majukwaa.
Kwa sababu ya mfumo dume wanatutukana (eti) tunaogopa lakini tunasema pia
kwamba mwanamke hana pesa za kwenda kwenye kampeni.
Sasa
Baraza Kuu linasema huyu mwanamke au mama baada ya miaka kumi amekaa bungeni
amekwenda kwenye mikutano, ana pesa anashindwa nini? Aende zake kwenye jimbo.
Hiyo ndiyo concept tuliyozungumza kwamba tayari
ile kazi ya upendeleo imeshafanya kazi. Imeshamtengeneza huyu mwanamke kuwa
mwanasiasa.
Sisi shida
yetu tunakata tuwe na wanawake wanasiasa wengi. Sasa hawa wanakuwa kama
selfish, wanaona wao. Kuna mwingine anathubutu anasema ‘he mimi kule kwangu nikitoka mimi, sina jimbo
kule. Lakini kama huna jimbo wewe ukitoka mwanamke mwingine atachukua nafasi
yako, kaa pembeni.
Kwa hiyo
mimi wananionea kusema kwamba nimewacha kwenye mataa. Na hao kwanza waliokaa
wanaosema kwamba nimewatosa, mimi UWT nimechaguliwa na wanawake wa Tanzania
yote.
Na
nimechaguliwa; hivyo siyo kazi yangu kulipa fadhila. Nimechaguliwa niwahudumie
wanawake wa Tanzania na kwa kufanya hivyo, kwa kuweka ukomo baada ya miaka kumi
tutaona majimbo mangapi wanawake watachukua.
Watajitokeza
tu, sisi wanawake tunapenda sana kusukumwa. Sasa nenda hapa, sasa nenda pale.
Mama Anna Abdallah aliweza mwaka 2005 kutusukuma. Aliniambia Sophia nenda Ilala,
wewe fulani nenda pale.
Isitoshe
siku hiyo kwenye Baraza Kuu ajenda ya kuwe na ukomo haikutoka kwenye kamati
yangu ya utekelezaji, ilitoka pale pale barazani.
Hilo ndilo
lililotokea kwa hiyo kina mama popote walipo naomba wasilichukulie hilo kama ni
langu binafsi isipokuwa hofu ya wale wanaotaka waendelee na wasiotaka wenzao
wengine wapata hizo nafasi ndiyo iliyofanya waende wakapeleke hadithi hizo.
Lakini
siku moja wataniona shujaa. Kwa suala hili kulipeleka kwenye NEC ilikuwa kazi kubwa, lakini imewezekana. Hata
hivyo, NEC imesema lisianze mwaka 2010, litaanza mwaka 2015. Mwaka 2015 ni
keshokutwa tu panapo na uhai. Kwa hiyo tutaona sura mpya zinaingia.
No comments:
Post a Comment