Na: Elizabeth Michael
Suleiman Mbuguni
MSANII wa filamu nchini, Elizabeth Michael 'Lulu' jjuzi ameshindwa kutoa salamu za mwisho kwa msanii mwenzake katika tasnia hiyo, Steven Kanumba ambaye anadaiwa kabla ya kifo chake walikuwa pamoja nyumbani kwa marehemu Sinza Vatcan jijini Dar es Salaam.
Lulu ambaye anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Osterbay, Kinondoni jijini Dar es Salaam inadaiwa kwamba aliomba kwenda kutoa salamu za mwisho kwa msanii huyo nguli wa filamu ambaye alifariki Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam.
Hata hivyo msanii huyo alishindwa kutokea katika shughuli za kumuaga Kanumba, kutokana na habari zilizodai kwamba ni za kiusalama.
Juzi Kamanda wa Mkoa wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyela alinukuliwa katika vituo vya televisheni nchini akisema kwamba Lulu anashikiliwa katika cha Oysterbay, lakini kwa kuwa suala hilo lipo kisheria alikuwa anasubiri matokeo ya daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Kanumba.
"Ni kweli tunamshikilia Lulu, lakini hata hivyo hatuwezi kulizungumzia lolote kwa kuwa suala hili lipo kisheria na bado mwili wa marehemu unafanyiwa uchunguzi hospitalini," alisema Kenyela.
Hata hivyo katika shughuli za kuuga mwili wa Kanumba yaliyofanyika katika viwanja Leaders Klabu, Dar es Salaam maelfu waliojitokeza kutoa salamu za mwisho kwa nyota huyo wa filamu nchini walishindwa kufanya hivyo kutokana na wingi wa watu waliojitokeza.
Ilikuwa ni simanzi, majonzi na vilio katika viwanja hivyo baada ya mwili wa Kanumba kuwasili sehemu iliyotayarishwa, huku baadhi ya wanawake wakidondoka na kupoteza fahamu.
Hatua hiyo iliwafanya watoa huduma ya kwanza kutoka Msalaba Mwekundu kuwa na shughuli pevu ya kuwapeleka katika magari yao kwa ajili ya kuwahudumia.
Kutokana na tafrani hiyo MC alilazimika kutangaza kusitisha shughuli ya kumuaga Kanumba, kitu ambacho watu waliofika katika viwanja hivyo kuanza kupiga kelele za kutoridhishwa.
Hata hivyo kabla ya kutangaza kusitisha viongozi wa serikali walioongozwa na Makamu wa Rais, Mohamed Ghalib Bilal kupewa nafasi ya kuuga mwili huo pamoja na baadhi ya ndugu wa karibu.
Viongozi wengine waliopata nafasi ya kutoa salamu za mwisho kwa marehemu Kanumba, alikuwa mke wa Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete, Mke wa Makamu wa Rais Mama Bilal, Waziri Ardhi Anna Tibaiujka, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe.
Viongozi wengine ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Dkt. Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecky Sadiq, Mbunge wa Kinondoni Idd Azzan, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana na Meya wa Manispaa hiyo, Yusuf Mwenda.
No comments:
Post a Comment