*Apata mapokezi ya kihistoria akitokea Marekani *Adai Tanzania hakuna utawala wa kidemokrasia *Wanafunzi 808 Dodoma wakihama chama hicho
Na Peter Mwenda MWENYEKITI
wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amewasili jana
akitokea nchini Marekani na kupata mapokezi ya kihistoria.
Wachambuzi
wa mambo ya siasa wanasema kuwa, kurejea kwa kiongozi huyo kutasaidia
kukinusuru chama hicho ambacho hivi sasa kimekubwa na jinamizi la
kuondokewa na wanachama wake.
Profesa Lipumba aliwasili katika
Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere saa 9:20 alasiri ambapo
viongozi mbalimbali wa chama hicho walijitokeza kumpokea wakiwemo
wabunge na wanachama wakiongozwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif
Shariff Hamad.
Baada ya kushuka kwenye ndege, Prof. Lipumba
alifanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa CUF katika chumba maalumu
cha mapumziko.
Baada ya kumaliza mazungumzo, Prof. Lipumba
alitoka nje na kuvalishwa shada la maua huku vigelegele na nderemo
zikitawala katika maeneo mbalimbali ya uwanja huo.
Eneo la uwaja
lilijaa wafuasi wa CUF waliokuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za
kumpongeza Prof. Lipumba kwa kuwa mwafrika pekee kuchaguliwa kwenye
kamati ya kuchunguza chanzo cha mdororo wa uchumi duniani.
Kutokana
na wingi wa watu walijitokeza kumpokea, Maofisa Usalama walimzuia Prof.
Lipumba na Maalim Seif, kuhutubia wananchi katika uwanja huo.
Maofisa
hao walishauri viongozi hao waondoke ndipo Prof. Lipumba aliamua
kuzungumza na waadishi wa habari na kusema kuwa, kazi anyoifanya nchini
Marekani angeweza kuifanya Tanzania kama mchumi aliyebobea lakini hapati
ushirikiano.
“Nipo tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali ya
Tanzania kuhusu masuala ya uchumi, hii itatokana na utawala na
demokrasia ambao kwa sasa haupo nchini Tanzania,” alisema.
Aliwashukuru Watanzania na wafuasi wa CUF kwa kujitokeza kumpokea na kudhihilisha kuwa, wananchi wana imani na chama hicho.
Kwa
upande wake, Shekhe Issa Ponda, akiongoza mashekhe wenzake 20 kutoka
misikiti mbalimbali jijini Dar es Salaam, alisema mchango wa Prof.
Lipumba ni heshima kubwa kwa Tanzania.
Ofisa Mawasiliano wa CUF,
Bw. Salium Biman, alisema chama hicho kitachukua dola mwaka 2015
kutokana na umati mkubwa wa watu waliojitokeza uwanjani wenye imani na
Prof. Lipumba.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar,
Bw. Ismail Jussa Ladhu, alisema umati uliojitokeza kumlaki Mwenyekiti
huyo ni salamu tosha kwa mbunge wa Wawi, Bw. Hamad Rashid Mohammed kuwa
chama hicho bado kina nguvu.
“CUF imeanza kazi rasmi ya kuimarisha chama ili 2015 tuchukue dola kwa kishindo,” alisema, Bw. Jussa.
Baada
ya kuzungumza na waandishi wa habari, Prof. Lipumba aliondoka na
msafari wa watu walifika kumpokea ukiongozwa na pikipiki, magari na
watembea kwa miguu hadi Uwanja wa Karume.
Awali mapokezi hayo
yaliingia dosari baada ya gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 854
AMN, lililokuwa limejaza wafuasi wa chama hicho, kupinduka na
kusababisha watu 10 kuumia.
Taarifa nyingine zinasema kuwa, gari
lingine ambalo lilikuwa likitokea Rufiji mkoani Pwani kupeleka wafuasi
wa chama hicho uwanjani hapo, lilimgonga mtembea kwa miguu na kufa papo
hapo.
Wakati huo huo, Mwandishi wetu kutoka Dodoma anaripoti
kuwa, zaidi ya wanafunzi 808 wa Vyuo Vikuu mkoani hapa ambao ni
wananchama wa CUF, wametoa tamko la kujitoa na kurudisha kadi kwa
uongozi wa chama hicho kwenye matawi ya vyuo vyao.
Wanafunzi hao
walidai kuwa, wamelazimika kujiondoa katika chama hicho kutokana na
kitendo cha viongozi wa ngazi ya juu kujali zaidi maslahi binafsi na
kukidumaza chama.
Tamko la kujitoa katika chama limetolewa na
Mwenyekiti wa Tawi la St. John Bw. Muhamed Abdullha kwa niaba ya
wanafunzi wezake katika kikao kifupi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa
mikutano chuoni hapo.
Bw. Abdullah alisema wanachama waliojitoa
ni wasomi wa elimu ya juu katika vyuo vyote mkoani haapa ambao
wamerudisha kadi za chama hicho na kila mmoja atachagua chama cha kwenda
ambacho kina mtazamo wa kuleta maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
“Uongozi
wa CUF kimsingi umetuchosha, hatujui unajali maslahi ya nani, inaonesha
wazi kuwa viongozi wachache wa juu wanalinda maslahi binafsi na ndiyo
maana chama hakikui.
“Kutokana na hali hiyo, wanafunzi ambao ni
wanachana wa CUF tumelazimika kurudisha kadi, kila mmoja atachagua cham
cha kwenda chenye mwelekeo wa kusaidia wananchi,” alisema.
Walisema
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Bw. Ismail Jussa Ladhu,
amekuwa akitumia madaraka yake vibaya na kukiuka katiba ya chama hicho
jambo ambalo limekuwa kilichangia kuwepo matakaba kati ya Tanzania Bara
na Zanzibar.
Katika tamko lao, wanafunzi hao walidai kuchoshwa na
tabia za viongozi wa chama kuingiza udini kwa kuwabagua Wakristo na
Waislamu na kujenga ukuta kati ya Wazanzibari na wenzao wa bara jambo
ambalo ni kinyume na katiba yao.
|
Posted: 11 Mar 2012 11:49 PM PDT
Maelfu
ya wanachama na wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) wakiwa wamejaa
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) kumpokea
Mwenyekiti wao Profesa Ibrahim Lipumba aliyewasili jana alasiri akitokea
Marekani, picha ndogo ni Profesa Lipumba na Katibu Mkuu wake, Maalim
Seif Sharif Hamad wakisalimia wananchi. (Picha na Peter Mwenda)
|
Posted: 11 Mar 2012 11:30 PM PDT
*Ataka mafisadi watoswe katika chaguzi za chama hicho Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WAZIRI
wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Samuel Sitta, amewapa mtihani
mzito wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Mwanza na mikoa
mingine nchini kuweka historia katika chaguzi mbalimbali ndani ya chama
hicho kwa kukisaficha chama na kuwatosa wagombea wanaotaka uongozi kwa
maslahi binafsi kwani wanachangia kukishushia hadhi chama hicho.
Alisema
kama mafisadi na makundi yao yatapewa nafasi za uongozi ndani ya chama,
watajuta kupoteza nafasi muhimu ambazo zinapaswa kufanyiwa mabadiliko
ya kihistoria na watakuwa wameshiriki kuisaliti CCM na kuiweka pabaya
chaguzi zijazo.
Bw. Sitta aliyasema hayo juzi katika mkutano wa
hadhara ambao ulihudhuriwa na maelfu ya wana CCM pamoja na waananchi
katika Uwanja wa Magomeni, uliopo Kata ya Kilumba, jijini Mwanza.
Alisema njia pekee ya kuinusuru CCM ni wanachama kuhakikisha wanachagua viongozi waadilifu kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa.
Aliongeza
kuwa, wananchi wengi bado wana imani na chama hicho lakini
wanalalamikia mwenendo wa baadhi ya viongozi hivyo uchaguzi wa mwaka huu
lazima uwe wa kihistoria.
“Hii ndio fursa ya kukinga’risha chama
chaetu, wana CCM tumieni uchaguzi huu kuchagua viongozi wanaopinga aina
zote za ubaguzi ukiwemo wa kipato, tuchague viongzoi wenye huruma na
wanaotetea wanyonge ambao ndio wengi.
“Tusipofanya hivyo na
kuwaachia wenye uchu na matajiri, tutakuwa hatujaitendea haki imani
yetu, itikadi yetu na misingi yetu, tuweke historia katika uchaguzi huu
kwa kuwaenzi waasisi wetu wa Taifa.
“Baba wa Taifa Mwalimu
Nyerere, alituachia msingi wa CCM kutetea wanyonge na huu umedhihirika,
tumekuwa wakombozi hadi nje ya nchi, ukombozi huo ndio aliomnfanya Mzee
wetu Karume kuwajengea maghorofa wanyonge hivyo lazima turudi katika
misingi hiyo,” alisema Bw. Sitta.
Bw. Sitta ambaye alialikwa na
Kamati ya Siasa Wilaya ya Ilemela na Kata ya Kirumba kuzindua kampeni za
kumnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, alisema CCM imekuwa ikilaumiwa na
Watanzania kwa kupoteza uelekeo, kushindwa kuendeleza sera na itikadi
iliyomo ndani ya katiba yake.
“Imani yetu rushwa ni adui wa haki,
sitapokea wala kutoa rushwa, huu ndio wakati wa kurudisha chama chetu
katika njia yake na kusafisha vumbi la kila aina ili CCM ing'ae mbele ya
jamii, tusipofanya hivyo, tutakua hatukitakii mema,” alisema.
Akimnadi
mgombea udiwani wa kata hiyo, Bw. Jackson Robert, maarufu kama
'Masamaki', Bw. Sitta alisema mgombea huyo anastahili kuchaguliwa
kutokana na uadilifu na msimamo wake thabiti katika kusimamia sera za
CCM.
Alisema ushindi alioupata wa asilimia 70 ndani ya chama hicho ni dalili ya ushindi wake katika uchaguzi huo.
Bw.
Robert atachuana wagombea wengine wa vyama mbalimbali huku mpinzani
wake mkuu akitarajiwa kutoka chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA).
|
Posted: 11 Mar 2012 11:28 PM PDT
Pamela Mollel na Queen Lema, Arusha
RAIS
mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa, leo anatarajia kuzindua
kampeni za mgombea ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, kwa
tiketi Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Sioi Sumari.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Katibu wa CCM mkoani hapa, Bi. Mary
Chatanda, alisema kampeni hizo zitahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa
chama hicho.
Alisema uzinduzi huo utakuwa tofauti na vyama vingine vya siasa ambavyo vinakodisha watu kutoka nje ya jimbo hilo.
“Tutazindua
kampeni kwa kishindo ili kuwapa wananchi fursa ya kuona jinsi
tulivyojipanga kushinda, kampeni zetu zitafunguliwa na Rais mstaafu, Bw.
Benjamin Mkapa na viongozi wengine wa kitaifa watakuwepo ila
tumeojipanga kupambana,” alisema Bi. Chatanda.
Katika hatua
nyingine, Bi. Chatanda alisema wananchi wanapaswa kutokubali kudanganywa
na aina yoyote ya propaganda kuhusu madai ya mgawanyiko wa wanachama
ndani ya CCM.
Alisema wanachama wote wapo katika kundi moja jambo
ambalo linawapa matumaini ya ushindi. Akizungumzia pingamizi lilowekwa
na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), dhidi ya mgombea wao,
Bi. Chatanda alisema pingamizi hilo limefutwa.
Bw. Sumari alikuwa amewekewa pingamizi na CHADEMA kwa madai kuwa hajawahi kukana uraia wa nje.
|
Posted: 11 Mar 2012 11:24 PM PDT
FEBRUARI
2009, Rais Jakaya Kikwete alimvua madaraka na kumfukuza kazi aliyekuwa
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera, Bw. Albert Mnali, kutokana na
kitendo cha kuwacharaza bakora walimu wa shule za msingi wilayani humo.
Hatua hiyo ilitokana na Bw. Mnali kufanya kitendo cha udhalilishaji kisichokubalika katika jamii na kuwavunja moyo walimu.
Bw.
Mnali aliamrisha polisi kuwacharaza viboko walimu ambao aliamini wao
ndio wamechangia wanafunzi wa shule za msingi wilayani humo kufeli
mitihani.
Tukiachana na hilo, wachambuzi wa mambo ya uchumi
wanasema ufadhili unaotolewa na wahisani kutoka mataifa mbalimbali
duniani una faida na madhara yake.
Mwishoni mwa wiki, gazeti moja
linalotoka kila siku liliandika habari inayosema “Mholanzi amchapa
vibao Mwalimu Mkuu”. Tukio hili lilitokea katika Shule ya Msingi Marera,
iliyopo Kata ya Rhotia, Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha.
Mashuhuda
wa tukio hilo wanadai kuwa, raia wa Uholanzi, Bi. Marise Koch, ambaye
ndiye mfadhili wa shule hiyo kwa kukarabati majengo ya shule, ofisi,
nyumba ya walimu na kutoa kompyuta ndogo 'Laptop', alimdhalilisha
Mwalimu Mkuu Bw. Emmanuel Ginwe kwa kumpiga vibao mbele ya wanafunzi,
walimu wenzake.
Tukio hilo limeripotiwa katika Kituo cha Polisi
Karatu na kufunguliwa jalada namba KRT/RB/835/2012. Bi. Koch aliwakuta
walimu wa shule hiyo wakipanga ratiba ya shule na kuhoji kwanini
hawajaingia darasani.
Walimu hao walijibu tayari wanafunzi
wamepewa kazi za kufanya lakini majibu hayo hayakumridhisha. Aliamua
kwenda ofisini kwa Bw. Ginwe na kudai yeye anafadhili vitu vingi lakini
walimu hawafundishi, kuanza kukusanya kopyuta alizotoa kama msaada
shuleni hapo lakini Mwalimu Mkuu alimsihi asifanye hivyo.
Baada
ya Bi. Koch kuona anazuiwa, alimpiga Bw. Ginwe vibao na kuendelea
kuzikusanya kitendo ambacho kiliwashtua walimu na wanafunzi
walioshuhudia tukio hilo.
Sisi tunasema kuwa, tukio hili
halikubaliki kwani dhana ya ufadhili si kunyanyasa watu wanaopewa
misaada na kuingiza mambo yao katika mitaala ya elimu nchini.
Kimsingi,
kilichofanywa na Bi. Koch ni kosa kisheria hivyo tunaliomba Jeshi la
Polisi wilayani Karatu, lichukue hatua stahiki za kuhakikisha mfadhili
huyo anafikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Matatizo
yaliyopo katika sekta ya elimu na nyinginezo si kigezo cha kuwafanya
Watanzania wanyanyasike na kudhalilishwa ndani ya nchi yao. Tumechoka na
manyanyaso ya aina hii, tunataka sheria imuadhibu Bi. Koch kama
ilivyofanya kwa Bw. Mnari ambaye alifukuzwa kazi kwa kosa la
kudharirisha walimu.
Kama Serikali itashindwa kuchukua hatua
stahiki dhidi ya mfadhili huyu, upo uwezekano wa kukwamisha maendeleo ya
elimu shuleni hapo kutokana na ukweli kwamba, walimu katika shule
husika hawatakuwa na imani na serikali yao kwa sababu haijawali.
|
Posted: 11 Mar 2012 11:22 PM PDT
Na Pendo Mtibuche, Dodoma SERIKALI
mkoani Dodoma imesema suala la upandaji holela huduma za matibabu ya
afya chini ya mifuko ya afya ya jamii NHIF na CHF limekuwa likiathiri
utendaji wa mifuko hiyo.
Hali hiyo imedaiwa kutokana na wauzaji wa dawa na watoa huduma kubadilisha bei ya dawa wanavyotaka na kwa wakati wowote.
Hayo
yalielezwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt.Rehema
Nchimbi wakati akifungua kongamano la siku moja la wadau wa Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Dodoma.
Alisema, sekta hiyo ya afya
imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ambazo ambazo zimekuwa
kuongeza malalamiko mengi kuhusu ukosefu wa dawa katika vituo vingi vya
Serikali na hasa vilivyopo ndani ya Manispaa ya Dodoma na Halmashauri ya
Wilaya ya Kondoa.
Alisema, kutokana na suala hilo kuwa nyeti basi ipo haja ya Serikali kulitazama kwa makini suala hilo na kulitafutia ufumbuzi.
Mbali
na changamoto hiyo ya kupanda kwa bei ya matibabu, lakini pia Mkuu huyo
wa mkoa alibainisha kuwa pia kumekuwepo na vituo vya afya ambavyo
vina uhaba wa watoa huduma wenye sifa hasa vijijini, hivyo suala hilo
linasababisha utoaji huduma hafifu zisizokidhi kiwango kinachotakiwa kwa
wanachama.
Alisema, hali ya afya katika Mkoa wa Dodoma inahitaji
kufanyiwa tathimini ya uhakika ili kuona ni njia zipi zitakazoinua
mifuko hiyo miwili ya afya ya jamii yaani NHIF na CHF ili iweze kufanya
vizuri.
|
Posted: 11 Mar 2012 10:59 PM PDT
Na Mkwasi Issa, Pemba ZAIDI
ya miche 15,000 ya mikarafuu inatarajiwa kutolewa kwa wakulima kisiwani
Pemba katika kipindi cha mvua za msimu wa masika ambazo zinatarajiwa
kuanza kunyesha visiwani humo mwaka huu.
Ofisa
wa Mashamba ya Serikali kisiwani Pemba, Bi.Asha Saleh Mbarouk
aliyaeleza hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kuhusiana
na mikakati ya Serikali ya kuimarisha zao la karafuu katika msimu huu.
Alisema
kuwa, ni vema wakulima kuanza kuyatayarisha mashamba yao mapema kabla
ya mvua za masika hazijaanza ili kujiweka tayari kwa ajili ya kupanda
mikarafuu mipya.
Bi. Mbarouk alisema, kila mkulima anayehitaji
kupatiwa miche ya mikarafuu anatakiwa kujaza fomu ambazo zinapatikana
kwa maofisa wa kilimo kwa kila shehia, fomu amabazo zitamuwezesha
kupatiwa miche hiyo.
Aidha, alisema miche hiyo inapatikana vitalu
vilivyoko Weni katika Wilaya ya Wete, Kicha kwa wilaya ya Micheweni,
Kigope Wilaya ya Mkoani pamoja na Kitalu Wilaya ya Chake.
Hata
hivyo Ofisa huyo aliwataka wakulima kuwa tayari kwenda kuchukuwa na
kujaza fomu ambapo kwa sasa watendaji wa kilimo wameanza kukagua na
kupima mashamba operesheni ambayo kwa sasa inaendelea katika shehia ya
Mtambwe Kaskazini.
|
Posted: 11 Mar 2012 10:57 PM PDT
Na Theresia Victor, Dodoma MHANDISI
Deogratius Assey ambaye amejitokeza katika kinyang’anyiro cha kugombea
nafasi ya ubunge, Bunge la Afrika Mashariki (EAC) kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema tayari amerejesha fomu katika
ofisi ya chama hicho mkoani Dodoma kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo.
Akizumgumza
na Majira baada ya kurudisha fomu hiyo jana, Bw. Assey alisema,
alilazimika kuingia katika ushindani huo kwa ajili ya kutaka kutetea
maslahi ya vijana kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Bw. Assey
alisema, pamoja na kuwepo kwa sera za kuwepo kwa jumuiya hiyo lakini
bado haijapata mtu madhubuti ambaye yupo tayari kwa ajili ya kuwatetea
na kuwapiagania vijana kuingia katika ushindani wa ajira kupitia EAC.
Alisema,
alilazimika kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kwani alikuwa
hajiamini kuwa kama angeweza kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa
wananchi kwa kumuunga mkono kama ambavyo kwa sasa mambo yamekuwa mazuri
kwa kupata ushirikianao wa kutosha.
“Lakini cha kushangaza
nimeungwa mkono na wanacha wote wa Chadema na hata wale wasiyo kuwa
wanachama, hata hivyo wamenichangia hata gharama za kulipia fomu ambayo
ilikuwa inagharimu shilingi laki moja...lakini wamenichangia,”alisema
Bw.Assey.
Aliongeza kuwa, ikiwa atafanikiwa kuipata nafasi hiyo
atahakikisha kuwa vijana wanatetewa zaidi katika masuala ya ajira
tofauti na ilivyo sasa ambapo Watanzania bado hawajaweza kunufaika na
suala zima la ajira kwa vijana katika jumuiya.
Aidha, kwa upande
wake Katibu wa Mkoa wa Dodoma CHADEMA, Bw. Stivine Masawe alisema,
ameipokea fomu ya mgombea huyo na kusema kuwa haina makosa yoyote na
hivyo iko sawa na ataiwasilisha Makao Makuu ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo jijini Dar es Salaam.
Bw. Masawe alisema, kujitokeza
kwa Mhandisi Assey ambaye ni kijana na mwanachama hai katika chama hicho
ni fursa pekee kwa vijana kutatuliwa matatizo yao kama atapata nafasi
ya kuchukua nafasi hiyo ya ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
|
Posted: 11 Mar 2012 10:50 PM PDT
Kiungo
wa timu ya Simba, Patrick Mafisango (kulia) akijaribu kuwatoka mabeki
wa Toto African ya Mwanza wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.(Picha na Michael Machellah)
|
Posted: 11 Mar 2012 10:49 PM PDT
*Wadaiwa kumpiga mtoto, mechi yao yaingiza mil. 73/- Na Zahoro Mlanzi WACHEZAJI
wa Yanga Nurdin Bakari, Athuman Idd 'Chuji' na Jerryson Tegete,
wanadaiwa kumpiga mtoto anayeishi Mtaa wa Faru na Swahili, Kariakoo, Dar
es Salaam na kumsababishia maumivu. Tukio hilo lilitokea juzi
usiku baada ya mtoto huyo kuwazomea kutokana na kipigo cha bao 3-1 dhidi
ya Azam FC ambapo gari la Yanga lililokuwa limebeba wachezaji,
lilisimama na wachezaji hao kwenda kumpiga mtoto huyo ngumi na mateka.
Kwa
mujibu wa shuhuda aliyekuwepo eneo la tukio (jina tunalo), alisema “
Baada ya mtoto huyu kuwazomea, Chuji, Nurdin na Tegete walishuka kwenye
gari la kumuadhibu, walipomaliza kiu yao walirudi katika basi lao na
kuondoka,” alidai mtoa habari huyo. Alidai kuwa, walipokwenda kumuangalia mtoto huyo walimkuta katika hali mbaya huku mwili wake ukiwa na majeraha.
Vyanzo mbalimbali vya kuaminika vilidai kuwa, mtoto huyo alikimbizwa hospitali kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Alipotafutwa
kwa njia ya simu ili aweze kuzungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda Mkoa
wa Kipolisi Ilala, Saada Juma, alisema hana taarifa zozote kwani hadi
anaondoka ofisini juzi saa 1:30 usiku, hakuna mtu aliyetoa taarifa ya
tukio hilo.
“Leo (jana) Ma-OCD wangu walikuwa wakinipa taarifa za
mara kwa mara kuhusiana na tukio la kuwasili kwa Mwenyekiti wa Chama
cha Wananchi (CUF), Bw. Ibrahim Lipumba lakini taarifa za kupigwa mtoto
hadi akafariki dunia au kukamatwa kwa wachezaji wa Yanga hilo
sijalipata,” alisema Kamanda Juma.
“Kama lipo nadhani nitapata
taarifa ila kinachonishangaza, tutaanzaje kupaata taarifa za kifo kabla
ya kuumizwa mtoto husika kwani hizo ndio zingesaidia kupata majibu ya
uhakika kwa hicho unachonieleza lakini siwezi kusema uongo ila ukweli ni
kwamba sina taarifa na hilo,” alisema.
Majira halikuishia hapo
pia lilimtafuta Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llody Nchunga ambaye alisema
hana taarifa za wachezaji wake kufanya fujo, kukamatwa au kufa kwa mtoto
huyo.
“Sijui kama hilo tukio lina ukweli, ninachokiamini mimi ni
kwamba, wachezaji wote walirudi klabuni na leo (jana) asubuhi,
nilikwenda kuzungumza nao tukaamua kuwapa siku moja ya mapumziko hivyo
wamekwenda majumbani kwao,” alisema Nchunga.
Alisema kama tukio
hilo lilifanyika, labda ni baada ya kurudi klabuni na baadhi yao kutoka
tena kwenda mitaani kufanya fujo lakini walipotoka uwanjani, warurudi
klabuni.
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu timu hiyo, Kostadin
Papic atawachukulia hatua wachezaji wote waliomfanyia fujo mwamuzi
Israel Mujuni kutoka Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mechi
iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Papic alisema kitendo
kilichofanywa na wachezaji wake hakikuwa kizuri na utovu wa nidhamu
hivyo atahakikisha anawachukulia hatua. Wakati huo huo, mchezo kati ya Yanga na Azam umeingiza sh. milioni 72,731,000. Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari Dar es Salaam
na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface
Wambura, alisema watazamaji 19,339 walikata tiketi kushuhudia mechi
hiyo kwa kiingilio cha sh. 3,000 viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 viti
vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B wakati kwa VIP A
ilikuwa sh. 15,000.
|
No comments:
Post a Comment