- LIPUMBA ASEMA MBOWE AMEDHALILISHWA BUNGENI
Rachel Balama na Darlin Said
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), tukio la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuondolewa bungeni mjini Dodoma kwa agizo la Naibu Spika, Bw. Job Ndugai, lilipangwa na Serikali ili kuhakikisha Muswada wa sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba mwaka 2013, unapitishwa bungeni ili kulinda masilahi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi CHADEMA, Bw. John Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.Alisema Serikali ilipanga kupitisha muswada huo bungeni ndio maana hata Bw. Mbowe kama Kiongozi wa Upinzani bungeni, aliposimama kutaka kuzungumza, hakupewa nafasi hiyo badala yake alitakiwa akae na alipokataa Bw. Ndugai aliagiza atolewa nje jambo ambalo hawakuliunga mkono.
Aliongeza kuwa, Serikali inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wabunge wa CCM wanakuwa wengi katika Bunge la Katiba ili kupitisha mambo wanayoyataka."Kilichopitishwa bungeni na wabunge wa CCM ni kibaya kuliko ilivyokuwa awali...wameharibu zaidi, CHADEMA imepinga kwa masilahi ya makundi mengine ya kijamii ili yaweze kupata uwakilishi katika bunge hilo," alisema.
Bw. Mnyika alisema CHADEMA walipendekeza Bunge la Katiba lipunguze uwakilishi wa chama kimoja ambapo katika kipengele cha wajumbe 166 wanaoteuliwa na rais, iongozwe na kufikia wajumbe 359 lakini Serikali imekataa."Lengo letu ni kutoa nafasi kwa makundi mengine ya kijamii kama wakulima, wafanyabiashara, wafanyakazi na taasisi nyinginezo kutoa wawakilishi wao kwenye bunge hili," alisema.
Alisema upande wa Zanzibar, hakukuwa na wawakilishi waliotoa maoni yao juu ya nafasi ya Zanzibar katika bunge hilo na kilichosemwa na Serikali ni uongo."Serikali baada ya kushindwa kuchakachua Mabaraza ya Katiba, sasa imeona njia pekee ya kufanya hivyo ni kuhakikisha kwenye Bunge la Katiba wabunge wa CCM wanakuwa wengi," alisema.
Akizungumzia uamuzi wa Bw. Ndugai kumtoa nje Bw. Mbowe, alisema Naibu Spika amevunja kanuni ya 76 ya Bunge kwani hana nguvu ya kuita askari ambapo kwa mujibu wa kanuni ya 20, alitakiwa kuhairisha shughuli za Bunge."Ndugai amefanya kosa la kuwaingiza watu wasiohusika bungeni na kuruhusu vitendo vya uhalifu vitokee ili kupitisha muswada walioutaka na kulinda masilahi ya chama kimoja.
"Sekretarieti ya CHADEMA itakutana kesho (leo) ili kujadili kwa undani suala hili na kulishughulikia, pia tutatumia nguvu ya umma (wananchi) kuhakikisha katiba haivurugwi, tutakutana na vyama vingine vya upinzani," alisema.Alisema chama hicho hakioni sababu ya kuharakisha katiba badala yake kama wanataka katiba hiyo itumike katika Uchaguzi Mkuu 2015 ni vyema ikaandaliwa ya mpito.
Aliongeza kuwea, katika Bunge lijalo Sheria ya Kura za Maoniambayo itajadiliwa ni ya hatari zaidi kuliko Bunge la Katiba na isipofanyiwa marekebisho, itazusha mgogoro mkubwa zaidi.Katika hatua nyingine, Chama cha Wananchi (CUF), kimepinga kitendo cha askari wa Bunge, kumtoa nje Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Bw. Freeman Mbowe, baada ya kuzuiwa kuzungumza.
Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.Alisema kitendo cha Naibu Spika wa Bunge, Bw. Job Ndugai, kuwaagiza askari wa Bunge wamtoe nje Bw. Mbowe, hakiwezi kukubalika, bali ni unyanyasaji na udhalilishaji mkubwa.
"Ni kitendo cha aibu na hakikupaswa kufanywa na Naibu Spika (Ndugai), CUF tunajiuliza angesimama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kutaka kuzungumza angemnyima?" alihoji.Alisema Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mwaka 2013, ulikuwa na utata mkubwa kwani Serikali imeubadili kwa kuondoa maoni muhimu ya wadau ambapo Wazanzibari hawakushirikishwa ipasavyo.
"CUF tunataka muswada huu urejeshwe kwa wananchi ili ujadiliwe upya, mbali ya Mbunge wa Singida Mashariki (Tundu Lissu- (CHADEMA) na Naibu Katibu Mkuu wa CUF upande wa Zanzibar (Hamadi Masoud), kuthibitisha kuwa Zanzibar haikushirikishwa, wabunge wetu hawana taarifa kama wananchi wao walishirikishwa.
"Kuupitisha muswada huu ni njama za wazi za Serikali na kiti cha Spika kutelekeza maoni ya wananchi na kuyapatia kipaumbele ya CCM, hivyo kuondoa uhalali wa Bunge na kiti cha Spika katika kusimamia mchakato wa kutafuta Katiba Mpya," alisema.Katika hatua nyingine, Prof. Lipumba muswada huo unampa Rais Jakaya Kikwete, mamlaka ya kuteua watu anaowataka kuwa wajumbe wa Bunge la kutunga sheria.
Aliongeza kuwa, hivi sasa kila taasisi itapaswa kuteua majina tisa na kumpa Rais ambaye atateua jina moja au asiteue kabisa,CCM na Serikali wanajua hujuma wanazofanya katika mchakato huu ili kupata katiba wanayoitaka wao si wananchi," alisema.Alisema upo umuhimu wa wananchi kuunga mkono msimamo wa wabunge wa upinzani na kudai kuwa, watendaji wa Serikali wakiwemo Mawaziri na Naibu Spika, wanamhujumu Rais Kikwete asifanikishe mchakatato wakupata Katiba Mpya.
Alisema muswada wa kwanza wa Mabadiliko ya Katiba ulikuwa mbovu ambapo Rais Kikwete alilazimika kuzungumza na wapinzani ili kuurekebishaWakati huo huo, CUF imedai kusikitishwa na kitendo cha kupigwa na kutupwa nje ya lango la Bunge Mbunge wa Mbeya Mjini, Bw. Joseph Mbilinyi (CHADEMA), na kuvuliwa hijab kwa Mbunge wa Viti Maalum, Bi. Mozza Abeid (CUF) na kudai huo ni udhalilisha usiokubalika.
No comments:
Post a Comment