Na Mwandishi Wetu
MWIMBAJI nguli wa muziki wa Injili barani Afrika, Rebecca Malope ambaye ni raia wa Afrika Kusini anatarajia kuongeza nguvu katika Tamasha la Krismasi linalotarajia kufanyika Desemba 25 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama muimbaji huyo atakuwa jukwaa moja na wenzake Sarah K wa Kenya na Ephraim Sekeleti wa Zambia ambao watafikisha shukrani za Watanzania baada ya kufanya uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu, uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Msama alisema Kamati yake inaendelea na mchakato wa kufanikisha tamasha hilo ambalo ni muendelezo wa Tamasha la Amani lililofanyika Oktoba 4 uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Aidha Msama alisema Watanzania walichukilie tamasha hilo kama sehemu ya kurudisha shukrani kwa Mungu baada ya kutupitisha katika kipindi kigumu cha uchaguzi Mkuu ambao ulifanyika kwa amani na utulivu ingawa kulikuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani.
Msama alisema waimbaji wa Tanzania watakaosindikiza tamasha hilo ni pamoja na Rose Muhando, Upendo Nkone, Joshua Mlelwa, Kwaya ya Wakorintho wapili huku kamati ikiendelea na mchakato wa kufanikisha tamasha hilo.
“Tumejipanga vilivyo na tamasha la Krismasi, hivyo tujiandae kupiga goti la kumrudishia Mungu Shukrani baada ya uchaguzi Mkuu ambao ulikuwa na mguso wa aina yake kutoka kwa vijana walioonesha kutaka maendeleo kutoka kwa serikali,” alisema Msama.
Naye mjumbe wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha hilo, Khamis Pembe aliwahakikishia Watanzania watakaohudhuria tamasha hilo ulinzi wa uhakika kupiia Jeshi la Polisi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment