TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Monday, May 14, 2012

Demokrasia ya Tanzania yapigiwa mfano duniani, na mtandao wa Gazeti la Majira


Posted: 11 May 2012 01:14 AM PDT

Wawekezaji wa madini wamponza mchimbaji
 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw.Diwani Athuman, alisema Bw. Magunila, alishambuliwa juzi mchana na kundi la wachimbaji wadogo wadogo katika machimbo ya dhahabu yaliyopo kijiji cha Mhandu kata ya Chela, wilayani Kahama.
Bw.Athuman alisema siku ya tukio hilo, Bw.Magunila alikuwa amefuatana na wawekezaji kutoka nje ya nchi na kwenda nao katika machimbo hayo bila kuwashirikisha, kitu walichomtuhumu anataka kuuza eneo hilo kwa maslahi yake binafsi, ndipo walipoanza kumshambulia kwa mawe na marungu.  
Akiongea kwa taabu na mwandishi wa habari hizi alikolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Bw. Magunila, alisema eneo hilo ni mali yao na Mkuu wa Wilaya Meja Matala kwa vile wameshalikatia leseni kutoka mwaka jana.

Bw.Magunila alisema eneo la machimbo ya dhahabu la Mhandu walishalikatia leseni ya majina mawili yeye na Meja Matala, ambapo wana viwanja sita.
Wachimbaji wadogo wadogo katika eneo hilo ambao hawakupenda majina yao yaandikwe gazetini waliwatuhumu Meja Matala na Magunila kutumia ujanja wa kulichukua eneo hilo bila wao kuwashirikisha.
Diwani wa Kata ya Chela Bw. Mibako Mabubu, alisema Bw.Magunila, alifanya kosa kwenda eneo hilo bila kushirikisha viongozi wa kata pamoja na kudai ana leseni ya viwanja sita.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Meja Matala alipoulizwa alikiri kuwepo kwa tukio hilo ila akasema hawezi akalizungumzia suala hilo kama Bw.Magunila.
Ofisa Madini Mkazi wa Wilaya ya Kahama Bw.Tuna Badoma, alipotakiwa kuthibitisha kuhusu leseni ya Bw.Magunila na Meja Matala alisema yeye si msemaji
Posted: 11 May 2012 01:07 AM PDT

Na Godfrey Ismaely, Dar es Salaam

IMEBAINISHWA kuwa demokrasia iliyopo Tanzania ni moja wapo ya chachu inayowafanya watu wengi zikiwemo nchi zilizoendelea duniani kutamani kuwa nayo, lakini inashindikana kutokana na mifumo yao ya kiutawala.
Mbali na hayo Watanzania wamehimizwa kuendelea kuilinda, kuheshimu na kuitumia vyema demokrasia hiyo katika kujadili ikiwemo kuibua mambo ambayo hayana uchochezi ili kuharakisha maendeleo yao.
Changamoto hiyo ilitolewa juzi na Waziri Mkuu mstaafu wa Rwanda Bw. Faustine Twagiramungu ambaye kwa sasa anaishi mjini Brussels nchini Ubeligiji wakati akichangia mada kwenye kipindi cha Straight Talk Afrika ambacho huwa kinarushwa na Sauti ya Amerika (VOA) kutoka mjini Washington DC nchini Marekani.

Hata hivyo sababu kuu iliyomsukuma Waziri huyo mstaafu kutamka hivyo ni kutokana na mada ambayo iliwasilishwa katika kipindi hicho ambayo iliangazia tija ambayo inaweza kupatikana kwa Bara la Afrika baada ya Wafaransa kufanya uamuzi wa kidemokrasia na kumuingiza madarakani Bw. Francois Hollande.
"Huwezi kumpima mtu kwa matendo yake ila uamuzi na siasa safi hususan demokrasia zenye mantiki kwa Afrika ndizo kimbilio na ufunguo wa maendeleo kwa Afrika;
"Nikiwa huku nilipo (Ubeligiji) nchi ambazo ninaweza kujivunia kuwa na demokrasia ya kweli si kwetu Rwanda... ni Tanzania na ninaamini iwapo wataitukuza (Watanzania) demokrasia hiyo ni fundisho pekee na mfano wa kuigwa katika Bara la Afrika na hata nje ya bara letu," alisema Bw. Twagiramungu.
Hata hivyo baadhi ya wachangiaji wa mada hiyo kutoka sehemu mbalimbali duniani walisema kuwa, nchi za Afrika ikiwemo Tanzania haziwezi kutegemea wahisani kuziendesha ila umefika wakati sasa rasilimali zinazowazunguka kutumika vyema kwa manufaa ya Waafrika.
"Kuchaguliwa kwa Rais mpya nchini Ufarasa kwetu (Afrika) si tija, haijalishi sera zake zinajikita katika Ujamaa au la!...tutakachofanya ni kuendelea kudumisha umoja na ushirikiano, lakini masuala ya uwajibikaji kwa manufaa ya nchi zetu yanatuhusu wenyewe," alisema mmoja wa wachangiaji wa mada hiyo kutoka nchini Nigeria.
Hata hivyo tafiti zinaonesha kuwa mbali na changamoto za hapa na pale demokrasia iliyopo Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kutokana na Watanzania wenyewe kuwa na maamuzi yao pekee bila kulazimishwa na watu ya kuwachagua ikiwemo kuwakataa viongozi ambao wanaona hawawajibiki ipasavyo.
Posted: 11 May 2012 01:01 AM PDT

Posted: 11 May 2012 12:59 AM PDT

Na Jovin Mihambi, Mwanza

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Evarist Ndikillo, amewataka wafanyabiashara nchini kuagiza bidhaa kutoka nchi za nje zenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa na vinavyoendana na uchumi wa nchi ili kila mwananchi aweze kumudu kuvinunua na vitumike kwa muda mrefu.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Bw. Saidi Amanzi, katika hotuba yake aliyoitoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, wakati wa ufunguzi wa duka la kuuza pikipiki na bidhaa zingine zinazotengenezwa na kampuni ya Honda ambalo limefunguliwa na Kampuni ya QM Quality Motors Limited lenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara nchini wamekuwa wakiingiza bidhaa mbalimbali ambazo hazina ubora na nyingi kutoka China.
Alisema kufunguliwa kwa duka hilo la kuuza pikipiki za Honda pamoja na bidhaa zingine ambazo ni jenereta, pampu za kusukumia maji, injini za kuendeshea mitumbwi limekuwa ni mkombozi kwa wananchi wa kanda ya Ziwa na mikoa mingine ya jirani.
Naye Meneja mauzo na Masoko wa kampuni ya QM Quality Motors Limited, Bw.Sudhir Borgaonkar, alisema bidhaa za kampuni yake ikiwemo pikipiki za Honda ambazo alisema zinauzwa bei nafuu ikilinganishwa na zile za kutoka China.
Posted: 11 May 2012 12:58 AM PDT

Diwani wa Kata Vijibweni Bw.Selemani Methew akimpa pole mzazi aliyejifungua watoto mapacha Bi.Robi Wambura katika Hospitali ya Vijibweni Wilaya Temeke, Dar es Salaam juzi, (Picha na Heri Shaaban)
Posted: 11 May 2012 12:52 AM PDT

Na Mwali Ibrahim

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Zimbabwe Rosemary Mugdza amesema kikosi chake kipo kamili kukabiliana na timu ya Taifa ya wanawake 'Twiga Star' katika mchezo wake wa kirafiki wa kimataifa utakaochezwa kesho katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, kocha huyo alisema, walikuwa wakisaka timu ya kucheza nayo ikiwa ni kwa ajili ya maandalizi yao na mechi ya Nigeria ambapo waliamua kuichagua Tanzania kutokana na uwezo mkubwa waliokuwa nao.
"Twiga ni timu nzuri na yenye uwezo na ndio maana tuliona ni timu ya kuchuana nayo tukiwa katika maandalizi ya mchezo wetu huo kwani tunaimani tutapata mazoezi ya kutosha," alisema.
Aliongeza kuwa kwa upande wa maandalizi wamejiandaa vya kutosha hivyo wanaimani kubwa ya kufanya vizuri katika mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri katika mchezo wao ujao.
Kwa upande wake Ofisa Habari wa Shirikisho la soka nchini (TFF) Bonifance Wambura akizungumza kwa niaba ya kocha wa Twiga, Boniface Mkwasa alisema hata kwa upande wao mchezo huo utakuwa ni mchezo mmoja wa kimataifa ambao ni kwa ajili ya mechi ya maandalizi ya kuivaa Ethiopia Mei 26, mjini Adis Ababa.
"Huu ni mchezo wa kwanza  wa kimataifa wa kirafiki kwa ajili ya kujiweka sawa kwani timu hii itacheza mchezo mwingine wa kirafiki Mei 20 ambapo kwa sasa tunatafuta timu ya kucheza nayo," alisema.
Alisema, timu hiyo ilikuwa mkoani Mwanza ikimalizia ziara yake ya kucheza michezo mbalimbali ya kujipima nguvu ambapo sambamba na mkoa huo pia walicheza mchezo mmoja mkoani Dodoma.
Wambura alisema, kwa upande wao wako tayari kukabiliana na timu hiyo kwani wanaijua vizuri walishawahi kuchuana nayo katika mashindano ya All African Games mwaka jana.
Alitaja viingilio katika mchezo huo kuwa  VIP A ni sh. 10,000, VIP B sh. 5,000 na viti vingine vikiwa ni sh. 1,000 ambapo wanaimani mashabiki watajitokeza kwa wingi kuisapoti timu hiyo..
Posted: 11 May 2012 12:47 AM PDT


Na Stella Aron

WANANCHI wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya zao bure ili kuzuia na kutibu magonjwa mbalimbali yanayoangamiza jamii kwa asilimia kubwa.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Agakhan Bi. Loveluck Mwasha, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya siku ya uuguzi duniani, ambayo huadhimishwa Mei 12, kila mwaka.
Alisema katika kusherehekea siku hiyo uongozi wa hospitali hiyo umeazimia kutoa huduma ya upimaji bure kwa magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu kesho katika ukumbi wa Mlimani City.
"Tumechagua magonjwa hayo kutokana na watu wengi kupoteza maisha kwa kutofahamu dalili za magonjwa hayo kwa kushindwa kupata huduma za matibabu, " alisema Bi.Mwasha.
Bi.Mwasha alisema siku hiyo watatoa ushauri mbalimbali kwa watu warefu au wafupi na wenye uzito mkubwa namna ya kupunguza uzito ili kuepukana na ugonjwa wa shinikizo la damu na magonjwa mengine nyemelezi.
Alisema wananchi watakaogundulika kuwa na magonjwa hayo watatakiwa kwenda kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kupata huduma zaidi, ambapo hivi sasa kuna idadi kubwa ya watu wanaougua magonjwa hayo lakini hawajitambui.
"Kwa wastani wa mwezi Agakhan tunapokea wagonjwa 50 wa kisukari ambao hupata tiba na kurejea majumbani mbali ya wale wanaolazwa," alisema Bi. Mwasha.
Muuguzi huyo alisema kabla ya kusherehekea siku hiyo uongozi wa hospitali hiyo jana ulitoa mafunzo kwa wauguzi wake namna ya kufuata maadili ya kazi na utoaji wa chanjo.
"Tumetoa mafunzo kwa wauguzi wetu ili waweze kukumbuka na kufuata maadili ya kazi zao na utoaji wa ushauri kwa jamii kufahamu umuhimu wa chanjo, " alisema.
Posted: 11 May 2012 12:46 AM PDT
Diwani wa kata ya kilosa wiliya ya Nyasa Bw. Issa Mustapha (kulia) akimuekeza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Bw.Said Mwambungu (wa tatu kulia) nama ilivyonusurika kuuawa na wananchi wa kata hiyo baada ya kuwakatalia kushiriki kuongoza zoezi la kutoa uchawi kwa watu waliotuhumiwa kuhusika na vitendo vya kishirikina katika eneo hilo, wengine ni wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo.Picha na kassian Nyandindi
Posted: 11 May 2012 12:31 AM PDT


Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya kupatikana na simu gerezani inayomkabili  aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT), Bw. Amatus Liyumba, kutokana na hakimu anayesikiliza kesi hiyo kutokuwepo mahakamani.
Wakili wa Serikali Bi.Elizabert Kaganda, alisema jana mbele ya hakimu Bi.Devota Kisoka, wakati kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo. Alisema Bw.Suwart Sanga anaumwa hivyo ameshindwa kufika mahakamani.
Kutokana na hali hiyo kesi hiyo imepangwa kuendelea kusikilizwa Julai 2, mwaka huu. Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa, Julai 27, mwaka jana, Bw.Liyumba akiwa mfungwa kwenye gereza la Ukonga anadaiwa kukutwa na kifaa kilichozuiliwa kisheria ambacho ni simu aina ya Nokia, rangi nyeusi yenye laini namba 0653004662 na IMEI 356273/04/276170/3.
Posted: 11 May 2012 12:29 AM PDT

Posted: 11 May 2012 12:27 AM PDT


Na Elizabeth Mayemba

KAMPUNI ya Simu za mikononi ya Airtel jana ilizindua awamu ya pili ya mpango kabambe wa mpira wa miguu nchini Airtel Rising, ambao nia yake ni kutafuta na kukuza vipaji vya mchezo huo kutoka ngazi ya chini kabisa mpaka ya taifa.
Michuano ya Airtel Rising Stars iliyozinduliwa na mchezaji wa zamani wa Manchester United Quinton Fortune, itaanza kutimua vumbi Mei 24 mwaka huu, kutoka mikoa sita, fomu za usajili zinapatikana kwenye makao makuu ya ofisi za Airtel Lindi,Mbeya,Arusha,Kinondoni, Ilala na Temeke.
Awamu ya kwanza ya mpango huu ilifanyika mwaka jana na kupata mafanikio makubwa, lengo likiwa ni kuvipika vipaji vinavyochipukia chini ya umri wa miaka 17, nafasi ya kuonyesha vipaji vyao kwa makocha waliobobea pia kupata nafasi ya kuendeleza vipaji vyao.
Akizungumza Dar es Salaam jana kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Sam Elangallor alisema, mafanikio ya mwaka jana yanaonesha mpira wa miguu una uwezo wa kuunganisha makabila mbalimbali na pia kuleta hamasa kwa jamii ya chini hadi taifa.
"Mwaka jana zaidi ya timu 11,000 Afrika zilijiandikisha kushiriki kwenye michuano hii kuanzia kwenye mtoano na kuchagua wachezaji ambao waliunda timu zilizoshiriki kwenye ngazi ya mkoa, ushiriki huu mkubwa ulituonesha ya kwamba tuko kwenye njia sahihi, na ndio maana tuna hamasa kubwa na awamu hii ya pili kwa mwaka huu," alisema Elangallor

Alisema kama ilivyokuwa kwa mwaka jana, mpango huu utaanzia ngazi ya mkoa na taifa na kufuatiwa na kliniki ya soka ya kimataifa chini ya wakufunzi kutoka klabu ya Manchester United ya Uingereza, kwa mwaka huu kutakuwa na mashindano ya siku nne ya timu bingwa kutoka kila nchi itakayoshiriki kushindania taji jipya la Airtel Rising Stars African Champion.
Kwa mwaka huu michuano hii imezinduliwa na mchezaji wa zamani wa Manchester United Quinton Fortune, mchezaji aliyesajiliwa na kocha Sir Alex Ferguson mwaka 1999 akitokea klabu ya Atletico Madrid wakati huo akiisaidia timu yake kushinda vikombe vitatu.

Raia huyo wa Afrika kusini aliweza kuzoea haraka mazingira wa Uingereza na kuweza kupata namba ya kudumu kwenye kikosi cha Ferguson kama winga wa kulia,kiungo wa kati na mshambuliaji, akiwa Man U Fortune aliiwezesha timu yake kushinda taji la FA mwaka 2003.

Posted: 11 May 2012 12:25 AM PDT

Mchezaji wa zamani wa Klabu ya Manchester United ya Uingereza Quinton Fortune, akipiga mpira kuashiria uzinduzi rasmi wa michuano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya Airtel Rising Stars. Uzinduzi huo ulifanyika jana,  kwenye Hoteli ya Sea Clif, jijini Dar es Salaam.(Na Mpigapicha Wetu)

Posted: 11 May 2012 12:22 AM PDT

Na Heri Shaaban

UONGOZI wa Kata Vijibweni iliyopo Kigamboni wamemuagiza Mganga Mkuu Zahanati ya Vijibweni, Bi.Rukia Msumi, kuagiza walinzi wa zahanati hiyo kuacha geti wazi ili wagonjwa waweze kuingia baada ya kutokea tukio la mjamzito kujifungulia getini.

Agizo hilo lilitolewa juzi wakati wa ziara ya kushtukiza iliyofanywa na diwani huyo, Bw. Suleiman Methew akiongozana na wenyeviti wake. Alikemea vikali kitendo cha walinzi kukataa kufungua milango hadi mjamzito akajifungulia nje.
Bw. Methew alimtaka mganga mkuu awaagize walinzi wa hospitali hiyo kuruhusu magari kuingia ndani wakati wote.

Bw.Methew alisema baada ya kupata malalamiko ya makosa  yanayofanywa na walinzi wa zahanati hiyo kwa muda mrefu yeye kama kiongozi amekerwa.
"Wananchi wangu kufanyiwa vitendo vya aina hii sijaridhika navyo, kuanzia leo naomba magari yote ya wagonjwa yaingie ndani kama vituo vingine vya afya wanavyofanya pindi wanapopokea wagonjwa," alisema Bw.Methew.
Alimtaka mganga huyo kusimamia suala hilo ili vitendo vya aina hiyo visijirudie.
Kwa upande wake Mganga Mkuu, Bi.Rukia Msumi, alisema taarifa hizo zilimfikia na alitoa onyo lakini kampuni hiyo ya ulinzi ilipuuzia.
Posted: 11 May 2012 12:20 AM PDT

Askari wa doria wakikagua pikipiki baada ya kuzikamata kwenye makutano ya Barabara za Bibi Titi Mohamed na Uhuru, Dar es Salaam jana. (Picha na Charles Lucas)
Posted: 11 May 2012 12:17 AM PDT

Na Queen Lema, Arusha 


WAFANYAKAZI wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha wamedai afya zao zipo hatarini kutokana na kukosa choo na kusababisha mazingira ya ofisi hiyo kutapakaa maji machafu.

Suala hilo limekuwa likilalamikiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kupatiwa ufumbuzi huku wafanyakazi hao wakiendelea kukumbwa na adha ya harufu mbaya.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa sharti la kutonukuliwa majina yao kwenye vyombo vya habari, walisema adha hiyo imekuwa ikiwakumba zaidi watumishi waliopo chini ya jengo hilo la ofisi ya mkuu wa wilaya.

Mmoja wa watumishi hao alisema watumishi waliopo ghorofa ya juu wamekuwa wakimwaga maji na kusababisha choo cha chini kuzagaa uchafu.

"Kama mnavyoona hii hali inatisha kwani ni muda mrefu choo hiki kimeziba wenzetu wakimwaga maji huko juu, uchafu wote unatoka," alisema mtumishi huyo.

Wafanyakazi hao kutoka idara mbalimbali za serikali katika jengo hilo, walidai kuwa wamekuwa wakipata shida kutokana na kukosa sehemu ya kujisaidia na kulazimika kwenda umbali mrefu kutafuta huduma hiyo ya choo.

Alidai taarifa ya ubovu wa choo hicho walitoa kwa viongozi akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Bw.Raymond Mushi, bila kupatiwa ufumbuzi. Kukosekana kwa huduma ya choo katika jengo hilo kumewakumba watumishi wa idara mbalimbali za Serikali.

Akizungumzia hali hiyo Katibu Tawala wa Wilaya, Bw. Emi Lyimo, alikiri kupata taarifa juu ya ubovu wa choo hicho, lakini alidai kuwa suala hilo lipo juu yake na tayari taarifa walishazifikisha ofisi kunakohusika.

Alisema hali ya ubovu wa choo hicho ni ya siku nyingi hata Mkuu wa Wilaya anaifahamu.

Kwa upande wa Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Bw. Everin Itanisa, alipoulizwa kuhusu ubovu wa choo katika jengo hilo alidai kuwa taarifa hizo anazo na kilichokwamisha ukarabati ni ukosefu wa fedha.

Alisema ukarabati wa choo hicho unahitaji gharama kiasi cha sh.milioni 12 na ofisi yake haikuwa na fedha isipokuwa wamepata nusu baada ya kuamua kuchangishana katika idara zote za ofisi.
Posted: 11 May 2012 12:14 AM PDT

Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Homes Expo, inayojishughulisha na makazi, Bw. Zenno Ngowi, akisoma taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), Dar es Salaam jana, kuhusu Maonesho ya Sekta ya Nyumba yatakayofanyika, Dar es Salaam, mwezi juni, mwaka huu. kushoto ni Mratibu wa Matukio wa taasisi hiyo Bw. Richard Mvula na Meneja Masoko Bi. Nice Chande. (Picha na Charles Lucas)
Posted: 11 May 2012 12:10 AM PDT

Darlin Said na Radhia Adam

KAMPUNI ya Mobile Ticketing LTD imezindua huduma mpya ya kukata tiketi za usafiri wa mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani inayojulikana kwa jina la "Tiketi popote" kwa kutumia simu za mikononi ambapo mteja atapata huduma ya tiketi popote alipo.

Huduma hiyo inategemewa kutumika kwa mikoa yote ya Tanzania ambapo kwa sasa huduma hiyo itaanza kutolewa katika mikoa ya Dar es Salaam,  Mwanza, Arusha, Tabora, Mtwara, Kilimanjaro, Lindi, Morogoro pamoja na nchi za jirani.
Huduma hiyo imeanza kutumika rasmi mara baada ya kuzinduliwa na kwa sasa inahusisha huduma za M-pesa, Airtel money pamoja na Easypesa.

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bw.Abert Muchuruza, alisema wameanzisha kampuni hiyo kwa lengo la kuondoa usumbufu wanaoupata wasafiri pindi wanapoenda kukata tiketi ikiwemo kuuziwa tiketi bandia, kuzidishiwa nauli na wapiga debe na kuuziwa tiketi za magari yasiyo safiri.
Huduma hiyo inatoa taarifa zote za mteja ikiwemo namba ya gari, namba ya siti pamoja na jina la gari atakalosafiri nalo abiria na ikitokea tatizo, msafiri anajulishwa.
Mbali na huduma ya tiketi kwa mabasi kampuni inatarajia kutoa huduma kwa vyombo vingine vya usafiri kama treni na meli.
Posted: 11 May 2012 12:08 AM PDT

Askari wa usalama Barabarani, akimuamuru dereva wa daladala namba T 225 BRD, kuegesha gari hilo kando ya barabara ya Azikiwe, Posta Dar es Salaam jana, baada ya kukiuka kanuni za usalama barabarani. (Picha na Charles Lucas)
Posted: 11 May 2012 12:04 AM PDT


Na Elizabeth Mayemmba

TIMU ya soka ya Simba imewasili salama jijini Khartoum, Sudan, jana usiku majira ya saa 5:49 ikitokea jijini Nairobi, nchini Kenya tayari kwa pambano lake la Kombe la Shirikisho (CAF) dhidi ya Al Ahly Shendi, ambapo walipokelewa na uongozi wa Chama cha Soka cha Sudan (SFA) lakini
Hata hivyo timu hiyo ilikiona cha moto kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoumbaada baada ya kutua kwa kuwekwa uwanjani hapo kuanzia saa sita usiku hadi saa saba na nusu usiku kwa kisingizio cha kumalizia taratibu za kiulinzi na kiusalama uwanjani hapo.

Kiongozi  wa SFA alipoulizwa kwanini wachezaji wanazidi kuwekwa uwanjani hapo wakati ni usiku wa manane , kiongozi huyo alijibu kwa mkato kuwa"Hata kwenu pia mlifanya hivihivi.”

Simba walitakiwa kuingia Sudan saa mbili usiku lakini walichelewa kufika kutokana na hitilafu iliyokuwepo katika ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) iliyopaswa iwachukue kutoka Nairobi.

Msafara huo wa Simba wa wachezaji 19 na viongozi wanane ulifikia katika Hoteli ya Shariqa lakini jana timu hiyo ilitakiwa kusafirishwa kwenda katika mji wa Shendi uliopo umbali wa Kilomita 150 kutoka Khartoum. Mechi ya Shendi na Simba itapigwa Jumapili saa mbili usiku katika Uwanja wa Shendi wenye uwezo wa kuchukua washabiki 10,000.

Kocha Mkuu wa Simba, Profesa Milovan Cirkovic alisema jana asubuhi kikosi chake hakikufanya mazoezi ya aina yoyote lakini jioni walifanya kama kawaida.

"Kuna uwezekano mkubwa wa mazoezi ya leo (jana) yakafanyika usiku muda ambao timu tutacheza ili wachezaji wazoee hali hiyo," alisema Milovan

Timu zote mbili, Simba na Shendi zinaweza kucheza kwa mara ya kwanza katika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la CAF. Simba iliweza kufika fainali ya michuano hii mwaka 1992 lakini wakati huo mfumo wa sasa wa hatua ya makundi katika hatua ya nane bora ulikuwa haujaanza kutumika.
Posted: 11 May 2012 12:02 AM PDT
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Robin Goetzsche (kulia) na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Leodgar Tenga (kushoto) wakisalimiana baada ya kusaini mkataba wa kuiwezesha TBL kuwa mdhamini mkuu wa Timu ya Taifa-Taifa Stars kwa miaka mitano ijayo kupitia Bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager. Katikati ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro premium Lager, George Kavishe. (Na Mpigapicha Wetu)
Posted: 10 May 2012 11:59 PM PDT


Na Elizabeth Mayemba

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro imeingia mkataba wa kuidhamini timu ya taifa, Taifa Stars kwa kipindi cha miaka mitano wenye thamani ya sh.bilioni 23 ambazo zitatumika katika kuimarisha timu hiyo ambayo inapeperusha bendera ya Taifa.

Uzinduzi huo ulifanyika katika hoteli ya Kempinski, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wote wakuu wa TFF, TBL na wadau mbalimbali.

Awali Stars tangu mwaka 2006 ilikuwa ikidhaminiwa na kampuni ya Serengeti (SBL).

Akizungumza katika hafla hiyo ya kutiliana saini, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Robin Goetzsche alisema udhamini huo utafungua mwanga mpya katika medani ya soka nchini Tanzania.

“Tunasaini mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya dola za Marekani milioni 10 sawa na sh.bilioni 23 za Tanzania utalifikisha soka letu Katika Kilele cha Mafanikio na kutupa kila sababu ya kujivunia kilicho chetuTuna matarajio makubwa sana na timu ya taifa kwani tunaamini kuwa ina uwezo wa kufanya maajabu, na kama nilivyosema awali, hili ni pambazuko la kuelekea mafanikio.

"Uwekezaji wetu umelenga katika kuhakikisha kambi za mazoezi zinaimarishwa, wachezaji watalala katika hoteli zenye ubora wa juu zenye zaidi ya ngazi tatu zilizo na bwawa la kuogelea na vifaa vya mazoezi, vifaa vinaboreshwa na pia vijana watapata fursa za kucheza mechi nyingi za kirafiki ili wajipime nguvu na kupata uzoefu zaidi na timu zinapata basi jipya la kisasa," alisema

Alisema udhamini wao utasaidia katika ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kisasa vya michezo, mafunzo kwa wafanyakazi wa TFF ndani na nje ya nchi, uendeshaji wa tovuti ya TFF, Semina na mikutano ya utawala bora.

Alisema wanaamini kabisa juhudi madhubuti zikiwekwa kwa kushirikiana na TFF na wadau wengine, malengo ya kuifanya Timu ya Taifa ishinde mechi zake zote yatatimia.
Goetzsche alisema TFF peke yake au mdhamini peke yake hawezi kuifanya timu ishinde lazima tujivunie kuwa na timu bora na kuimba nyimbo za ushindi kila wakati.

FUNDI BAJAJ MADAI YA ASKARI Gemini kudhamini mchezo wa Judo Waislaamu watakiwa kupuuza wanapinga sensa IFNA yashauri Taifa Queens icheze Kombe la Dunia TOZI Good Hope kuibua makocha, Waamuzi Songea Ngoma NCCR-Mageuzi wapata pigo, Athanasi ajivua kundini KATUNI Magereza ziwe vyuo cha maadili kwa wafungwa Mama Tunu Pinda awajaza 'manoti' Taifa Queens TIC Vijana Yanga wamuangukia Manji


Posted: 14 May 2012 12:22 AM PDT
Mbunge wa jimbo la Kisesa (CCM) Bw.Luhaga Mpina akihutubia mkutano wa kuhamasisha maendeleo jimboni mwake
Posted: 14 May 2012 12:16 AM PDT

Fundi wa kutengeneza pikipiki za gurudumu tatu (Bajaj) jina (halikufahamika) akining'inia kwenye chombo hicho wakati akikifanyia majaribio bila kujali usalama wake, kama alivyokutwa Magomeni Mikumi, Dar es Salaam jana. (Picha na Charles Lucas)
Posted: 14 May 2012 12:13 AM PDT

Posted: 13 May 2012 11:50 PM PDT

Na Mwali Ibrahim

KAMPUNI ya Gemini  Corporation imejitokeza kudhamini mashindano ya taifa ya mchezo wa Judo yanayotarajiwa kufanyika Mei 26 hadi 27 Landmark Ubungo  Dar es Salaam.
Mashindano hayo yanatarajiwa kushirikisha wachezaji kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watakaochuana kuwania ubingwa huo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Yuil Tarverdyan alisema kutokana na mapenzi ya mchezo huo kampuni yake imejitokeza kugharamia mashindano hayo kwa mara ya pili ikiwa ni katika kugharamia gharama zote za mashindano.
Alisema, gharama hizo zitahusisha mahali pa kufanyia mashindano zawadi ambazo nifedha kwa washindi wa mashindano hayo.
Alisema, kutokana na chama cha Judo nchini (JATA) kwa sasa kuwa na viongozi wapya, anatarajia kufanya kikao cha pamoja na viongozi hao ambao tayari wameshawasiliana kuhusu udhamini huo, ambapo gharama za mashindano pamoja na zawadi atazitaja katika kikao hicho.
Alisema licha ya kuwa na mahusiano mazuri na uongozi uliopita hakusita kuacha kudhamini mchezo huo kutokana na mapenzi yake katika mchezo huo ambao pia huchezwa nchini kwao Ujerumani.
Kwa mujibu wa  aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Kashinde Shaaban aliyezungumza kwa simu alisema wanaitambua kampuni hiyo kutokana na kujitokeza kuwadhamini wakati wa uongozi wao, ambapo kwa sasa kiongozi huyo amefungiwa maisha.
"Alinipigia kutaka kudhamini kutokana na kufahamiana na uongozi wetu kipindi hicho, lakini nilimfahamisha kuwa sipo tena madarakani na kumtaka kuendeleza udhamini huo kwa viongozi waliokuwepo madarakani sasa," alisema Kashinde.
Posted: 13 May 2012 11:32 PM PDT

Na Anneth Kagenda

MKURUGENZI wa Taasisi ya Kiislam ya  Peace Foundation Tanzania (TIPF), Bw. Sadiki Godigodi, amewataka Watanzania kupuuza ushawishi unaotolewa na baadhi ya watu wa dini hiyo wa kuwataka wasishiriki kwenye sensa kwani hakuna nchi ambayo inaweza kukaa bila kujua idadi ya wananchi wake.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema kuwa ni muda muafaka kwa waumini wa dini hiyo kutosikiliza ushawishi unaotolewa na baadhi ya watu badala yake wakubali kushiriki vyema kwenye sensa hiyo.
"Tunawaomba waislam, wakristo na Watanzania wote kwa ujumla kujitokeza kutoa ushirikiano wa zoezi la kuhesabu watu na makazi linalotarajia kuanza hivi karibuni na wapuuze kauli za watu wachache wenye malengo ya kujipatia maslahi binafsi," alisema.
Alisema watu hao ambao wamekuwa wakishawishi wenzao kutoshiriki Sensa ni kikuzwa, kwani hii ni fursa muhimu.Katika hatua nyingine (TIPF) ilimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa hatua yake ya kusikiliza mawazo ya wabunge na badaye kuchukua hatua mbadala ya kuwawajibisha wale wote walioonekana kuwa si waadilifu kwenye Baraza la Mawaziri.
"Kwanza kabisa taasisi yetu inapenda kumpongeza Rais Kikwete kwa uamuzi wake wa kusikia kilio cha wabunge hatimae kuwawajibisha mawaziri wenye kashfa za ufisadi.
Posted: 13 May 2012 11:31 PM PDT
Na Amina Athumani

SHIRIKISHO la Kimataifa la Mchezo wa Netiboli (IFNA), limekipa Changamoto Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kuiingiza timu ya Taifa ya Netiboli (Taifa Queens) kwenye michezo ya Dunia.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Mwakilishi wa IFNA,  Joan Smith alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika mchezo huo hususani kikosi cha Taifa Quens kilichoshiriki michuano ya Afrika kimeimarika tofauti na alichokiona mwaka 2009 katika  mashindano kama hayo.
Alisema pia maandalizi yaliyofanywa na CHANETA kwa mwaka huu yamekuwa ni mazuri zaidi na kwamba chama hicho kina uwezo pia wakuandaa mashindano ya Dunia endapo watafanikiwa kuwa na Uwanja wa Ndani wa kisasa.
Alisema kutokana na maandalizi waliyofanya CHANETA, IFNA inao uwezo wa kuipa kibali Tanzania kuandaa mashindano ya Dunia na kwamba cha msingi ni Serikali ya Tanzania kukisaidia chama hicho katika kuhakikisha kinapata kiwanja cha ndani chenye hadhi ya kisasa.
Tanzania ni mara ya pili kuandaa michezo ya Afrika ambapo mara ya kwanza iliandaa michezo hiyo mwaka 2009 na iliiwezesha Tanzania kupanda viwango vya kimataifa vya mchezo huo vinavyotambulika na IFA.
Kwa sasa Tanzania ipo nafasi ya 20 katika viwango vya mchezo huo na  ipo nafasi ya tatu kwa viwango vya Netiboli Afrika (AN) ambapo kupitia mashindano yaliyomalizika juzi huenda Tanzania ikapanda viwango vya Afrika.
Posted: 13 May 2012 11:30 PM PDT

Posted: 13 May 2012 11:28 PM PDT
Na Mhaiki Andrew, Songea

SHIRIKA lisilokuwa la Kiserikali la Klabu ya michezo ya Good Hope la mkoani Ruvuma, lina mpango na mikakati ya kutoa mafunzo ya ukocha na waamuzi kwa wanafunzi wa shule za Sekondari ikiwa na lengo la kuibua na kuendeleza taaluma ya michezo mkoani hapa.
Akizungumza mjini hapa juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Joseph Mapunda alisema mafunzo hayo yatalenga wanafunzi wa shule hizo za Sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tatu katika kuwapa taaluma ya michezo badala ya kutegemea makocha kutoka nje ya mkoa kuja kufundisha.

Alisema Shirika hilo limejiwekea malengo endelevu katika kusaidia kuinua michezo hiyo kitaaluma ambapo alidai baada ya kukamilika zoezi hilo kwa shule za Sekondari pia mafunzo hayo yatatolewa kwa vijana wa shule za msingi kwa kuanzia darasa la tano.
Alisema kabla ya kuanza kwa utoaji wa mafunzo ya ukocha kwa wanafunzi hao, alidai bodi ya Shirika hilo limekutana na kuweka mikakati itakayowezesha  kufanikisha zoezi hilo.
Alisema katika mapendekezo yao wamedai wataanzia na shule za Sekondari katika wilaya mbili  za Songea na Namtumbo na baadaye Nyasa, Mbinga na Tunduru.
Aliongeza mafunzo hayo yatatolewa kwa michezo 10 ambayo baadhi ni soka, netiboli, ngumi, riadha  na mpira wa wavu.
Posted: 13 May 2012 11:27 PM PDT

Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mkoani Simiyu (CCM),  Luhaga Mpina (mwenye vazi la chama) akishiriki kucheza ngoma za utamaduni wakati alipofanya ziara katika Kata ya Kisesa kwa ajili ya kutoa zawadi kwa vikundi vya ngoma za Wagika na Wagalu na kuimarisha utamaduni jimboni humo. (Picha na Suleiman Abeid)
Posted: 13 May 2012 11:23 PM PDT

Na Anneth Kagenda

ALIYEKUWA mgombea Ubunge Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi Bw. Mawazo Athanasi amejiondoa kwenye chama hicho kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kukosa imani na Mwenyekiti wake Bw. James Mbatia.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam mara baada ya kufika jijini hapa akitokea Kigoma, alisema kuwa amechukua maamuzi hayo magumu kutokana na mwenyekiti wake kuwa mwanachama wa CCM kutokana na kwamba kama angekuwa ni mwanachama wa NCCR- Mageuzi asingekubali kupewa cheo cha wanawake wa CCM (Viti Maalum).
"Awali tulikuwa tunajiuliza maswali mengi kwamba Bw. Mbatia ni wa chama chetu au CCM...sasa ukweli tumeupata kwamba ni wa CCM, pia ninajiuliza kama angekuwa na nia ya dhati na chama basi angekataa cheo hicho ambacho ni cha wanawake wa viti maalum CCM, lakini ninajiuliza je? Huko bungeni anaenda kufanya nini na anakitetea chama gani.
"Niko katika chama hiki tangu mwaka 2003, lakini nilikuwa nashangazwa na mwenendo wa chama changu, baada ya kuona mambo yanazidi kuharibika ngoja nikae pembeni kwani chama hiki hiki kilishindwa kunitetea hata nilipokuwa nashughulikia kesi yangu ambapo nilishindwa kutimiza masharti ya kupeleka sh. milioni tano mahakamani wakati milioni mbili zilikuwa zimepatikana, lakini nikakosa milioni tatu," alisema.
Aidha, alisema kuwa awali Bw. Mbatia alimwambia (Bw. Athanasi) kwamba aachane na kesi hiyo ambayo aliamini kwamba angeshinda kutokana na kwamba aliibuka kidedea cha mshindi wa pili na kwamba kura zake ziliibiwa na Bw. Christopher Chiza wa CCM ambapo alisema kuwa kitendo hicho cha kuhujumiwa na chama chake hakukifurahia.
Alisema, pia anakubali uteuzi wa Rais wakati akijua kuwa tayari alimteua mwizi wa kura zake (Chiza) kuwa Waziri na kusema kuwa iweje ampende Bw. Mbatia wakati anajua kuwa aliwaibia kura katika Jimbo la Buyungu na kusema kuwa kilichoendelea kumuudhi ni viongozi wa NCCR-Mageuzi kuunga mkono uteuzi wa Bw. Mbatia.
Hata hivyo aliwataka vijana wote wa mkoani Kigoma ambao wako kwenye chama alichokihama kuondoka mara moja kwa madai kuwa chama hicho kinakufa na kuwa CCM kwani viongozi wake wataendelea kuongopewa kwa kupewa vyeo na Rais Jakaya Kikwete.
Posted: 13 May 2012 11:20 PM PDT

Posted: 13 May 2012 11:19 PM PDT
Na Darlin Said

KWA nyakati tofauti Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imekuwa ikitoa taarifa juu ya mlundikano wa wafungwa na hali mbaya ya magereza nchini.
Mfungwa ni mtu aliyeadhibiwa kwenda Gerezani baada ya kutenda makosa au uhalifu katika jamii ili kujifunza na kutorudia kosa hilo.

Adhabu hutolewa kisheria na mahakama ambapo hutumikia adhabu hiyo huku akisimamiwa na kurekebishwa tabia zao.Mfungwa hupokea mafunzo mbalimbali na kupelekea kupata ujuzi katika ufundi, ukulima, ufugaji na fani nyingine nyingi.Ni tegemeo la serikali na jamii kuwa, mfungwa anamaliza kutumikia kifungo chake awe amebadilika kitabia na kuwa raia mwema anayeweza kushiriki katika kuleta maendeleo ya jamii inayomzunguka.Kwa kulitambua hilo Chama cha kurekebisha mwenendo wa watu waliomaliza kifungo Tanzania (E.R.S.T) kilianzishwa mwaka 2009 chini ya mwenyekiti  Bw.Shafii Kondo ili kuwapatia mafunzo.

Pia, ni kuwaunganisha wafungwa waliomaliza vifungo vyao na kuwarekebisha
tabia zao ili wasiweze kufanya tena uhalifu ambao utawasabishia kurudi tena gerezani.Lengo lengine ni kutoa elimu katika jamii ili waweze kuwapokea na kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kutumia ujuzi walioupata gerezani.Vilevile kuhakikisha wanasimamia vema haki za wafungwa zilizosaulika  mfano haki ya kupiga kura na ya kukutana na wanandoa wenzao.

Pia kuhakikisha kwamba wanatoa  msaada wa kifedha, vifaa na rasilimali ardhi ili iwe changamoto kwa waliomaliza vifungo kujiunga  na Taasisi za aina  hii ili waweze kujiepusha  kujiingiza katika vitendo vya uhalifu.Ili waweze kufanikisha malengo yao chama kimeanzisha miradi mbalimbali ikiwemo shughuli za kuchana mbao, karakana, ukulima na ufugaji.

Kwa uhalisia tunaona kwamba, katika magereza nchini kuna matatizo  ya kisheria yanayopelekea wafungwa kukosa uhuru wao ambayo ni kinyume na haki za binaadamu.Kwa mfano katika sheria zetu wafungwa hawana haki ya kupiga kura kumchagua kiongozi anayemtaka na pia hawana haki ya kukutana na wanandoa wao ambapo ni kinyume na haki za kibinaadamu.Serikai inatakiwa kubadili mfumo wa sheria ya magereza kutoka mfumo wa kikoloni  ambazo zinaonekana kandamizi kwa wafungwa na kuwanyima haki zao za msingi.

Sheria ziliopo ni za kikoloni wakati wafungwa ni wa kisasa, pia washirikishwe kutoa mawazo  yao katika mchakato wa kubadilisha katiba kwani ni haki yao ya msingi. Katika magereza bado sheria hazijaboreshwa ukilinganisha na sehemu nyingine hali inayopelekea kuwa na matatizo mbalimbali ikiwemo msongamano wa wafungwa.Magereza mengi yamefurika wafungwa na mahabusu kupita kiasi, huduma za chakula, matibabu na haki nyingine za wafungwa zimekuwa ama haziheshimiwi kabisa au pale zinapoheshimwa ni kwa kiwango cha chini kabisa.

Nionavyo gerezani kuna matatizo mengi ambayo wafungwa wanakumbana nayo ambao aidha yanasabashwa na sheria zilizopo ambayo wafungwa ndio wanayoyafahamu vema kuliko mtu yeyote.
Mfano wafungwa kutoruhusiwa kuwa karibu na waume/wake zao ni tatizo kubwa ambalo linaweza ikapelekea tatito la ushoga gerezani.Lakini kama kungekuwa na sheria inayoruhusu wafungwa kukutana na wake zao ingesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hilo na maambukizi ya VVU.

Aidha upande wa serikali itilie mkazo kwa kufanya magereza yawe ni vyuo vya mafunzo ya kuwafanya wafungwa wapate ujuzi mbalimbali na siyo sehemu ya kupata adhabu na unyanyaji .Tunafahamu na kutambua kuwa magereza siyo hoteli ya kitalii kwa maana hiyo iwe na huduma za kiwango cha juu sana, lakini pia siyo sehemu ya kuwatesa wafungwa na kukataa walau kutambua haki zao za msingi.

Tujifunze kutoka kwa ngugu zetu wa visiwani badala ya kuita magereza wanaita vyuo vya mafunzo hii inasaidia jamii kuwaona wafungwa ni wenzetu ambao wapo mafunzoni.Kwa upande wa magereza ya watoto, serikali ihakikishe kuwa inawapatia watoto hao elimu bora na wasiwape adhabu kubwa zisizo endana na umri wao. wa kufanya hivyo tunaweza kujenga taifa linalowajali wafungwa  ingawaje  wametenda makosa au uhalifu katika jamii.

Serikali imetakiwa kuwashirikisha wafungwa katika mchakato mzima wa kupiga kura, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kupata haki ya kukutana na wenzi wao hasa wanapokuwa  kifungoni.
Posted: 13 May 2012 11:17 PM PDT

Na Zahoro Mlanzi

BAADA ya kuwa wa pili katika michuano ya netiboli ya Afrika kwa kuifunga Botswana mabao 32-23,Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda ametimiza ahadi aliyoitoa kwa timu ya Taifa ya Netiboli (Taifa Queens) kwa kutoa jumla ya sh. milioni 20.8.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Irene Bwire, ilieleza kwamba Mama Pianda alitoa sh. milioni moja kwa kila mchezaji endapo wangetwaa ubingwa wa kombe hilo ambayo mashindano yake yalimalizika juzi na Malawi kutwaa ubingwa.
Ilieleza Mama Pinda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kuisaidia timu hiyo, alitimiza ahadi hiyo juzi katika hafla fupi ya kukabidhi mfano wa cheki iliyofanyika juzi usiku, Dar es Salaam.

"Wachezaji 16 walipewa sh. milioni moja kila mmoja, na maofisa sita wa timu walipewa sh. 800,000 kila mmoja, hivyo kufanya jumla ya sh. milioni 20.8," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Akizungumza na wachezaji hao, viongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), na baadhi ya Wake wa Viongozi ambao ni wanachama wa New Millenium Women Group, Mama Pinda aliwapongeza wachezaji hao kwa jinsi walivyojituma na kufanikiwa kushika nafasi ya pili.

Aliwataka wachezaji hao kuzidi kujituma zaidi hata katika mashindano yatakayofanyika mwakani nchini Malawi na kwamba walifanya kazi kubwa kuifunga timu ngumu kama Botswana.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wachezaji wenzake, nahodha wa timu hiyo, Lilian Sylidion alisema ahadi ya Mama Pinda ambayo aliitoa wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo iliwapa hamasa na kuchochea kupatikana kwa ushindi huo.
TIC
Posted: 13 May 2012 11:11 PM PDT

Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bi. Beatrice Chonjo (kushoto) na Mkurugenzi wa Program ya kusaidia wajasiriamali wa nchi zinazoendelea ya Finnpartnership ya Finland, Bi.Siv Ahlberg, wakizungumza na wadau wakati wa mkutano huo ulitayarishwa na ubalozi wa Finland na TIC, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. (Na Mpigapicha Wetu)
Posted: 13 May 2012 11:08 PM PDT

Na Elizabeth Mayemba

VIJANA wa Klabu ya Yanga, wamemuangukia aliyekuwa Mfadhili wa timu hiyo, Yusuph Manji aje kuinusuru hasa katika kipindi hiki kigumu walichonacho.
Klabu hiyo hivi sasa ipo katika mvutano mkubwa kati ya uongozi uliopo madarakani chini ya Llody Nchunga ambaye Baraza la Muafaka la Wazee pamoja na vijana wa klabu hiyo wanashinikiza kiongozi huyo kujiuzulu kutokana na kudai ameshindwa kuiongoza timu.

Wakizungumza kwa niaba ya vijana wenzao katika kikao cha vijana kilichofanyika jana Dar es Salaam ambacho kilihudhuriwa na zaidi ya wanachama 200, Omari Chambuso (003850), Hussein Mfaume (00607) na Waziri Jitu (001732), walisema wanataka Mkutano Mkuu ufanyike Mei 20, mwaka huu badala ya Julai 15 kama alivyotangaza Nchunga.

Walisema tarehe hiyo waliyopanga ndiyo tarehe ambayo Nchunga atakutana na Wazee wote wa Yanga na kwamba kama ana uwezo wa kukutana na wazee wote ni bora uwe mkutano mkuu kabisa.
"Nchunga amepanga Mkutano Mkuu ufanyike Julai lakini ni mbali sana, hivyo sisi tunataka ufanyike Mei 20 na pili tunataka ajiuzulu yeye pamoja na uongozi mzima," walisikika wakisema kwa nyakati tofauti.

Pia walimuomba Manji arudi kuisaidia klabu hiyo kwani uongozi uliopo madarakani wamedai umeshindwa kuiongoza timu hiyo kutokana na kukabiliwa na madeni mengi.Waliongeza watajihidi vijana kwa umoja wao kuhakikisha wanajipanga kusaidia katika suala zima la usajili hususani katika kipindi hiki ambacho timu yao inakabiliwa na mashindano ya Kombe la Kagame.