TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Thursday, September 26, 2013

CAG KUKAGUA OFISI YA MEYA BUKOBA

 Mariam Mziwanda na Stella Aron 

   Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Ludovick Utouh, amesema ofisi yake ipo mbioni kwenda mjini Bukoba, mkoani Kagera, ili kufanya ukaguzi wa mahesabu katika Ofisi ya Meya na kutoa ripoti yenye uhakika.   Bw. Utouh aliyasema hayo Dar es Salaam  katika mafunzo yaliyoshirikisha Wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari ili kuwajengea uwezo wa kuripoti taarifa za ofisi hiyo. 

  Alisema ukaguzi wanaokwenda kuufanya mjini Bukoba, hautokani na matakwa ya Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Nape Nnauye; bali ni ombi maalumu lililotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.    Aliongeza kuwa, kumekuwa na taarifa za upotoshaji ambazo zimekuwa zikifanywa na baadhi ya makundi ambayo hayana nia njema na ofisi hiyo, hivyo ni vyema ikaeleweka kuwa, ukaguzi huo umezingatia agizo la Waziri Mkuu. 

 "Ofisi yangu inafanya kazi kikatiba si kwa matakwa ya chama chochote cha siasa, ukaguzi maalumu ambao utafanyika mjini Bukoba, utaanza wiki ijayo...ni jukumu la vyombo vya habari kuwa waangalifu wanaporipoti taarifa hizi.   "Wananchi wa Bukoba wasiwe na wasiwasi, tunakwenda huko lakini hatutaki chai ya mtu labda usafiri ambao upo kisheria kwa ajili ya ukaguzi wa miradi yenye utata iweze kufikiwa na kupatikana taarifa sahihi," alisema. 
  Bw. Utouh alisema uwajibikaji na uwazi ni mambo yasiyoweza kupatikana katika mfumo wa kuficha taarifa za utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali. 

  Alisema mahali ambapo habari inafichwa, lazima patatokea mvutano, kutoaminiana na hatimaye wananchi kuona Serikali yao ndiyo chanzo cha matatizo hivyo ni muhimu haki ya kikatiba kwa wananchi kupashwa habari ikazingatiwa.   Alitumia fursa hiyo kuvitaka vyombo vya habari nchini k u p u n g u z a u p o t o s h a j i n a kuelimisha jamii ipasavyo ili kusaidia makundi mbalimbali kuzielewa vizuri ripoti za CAG ili kuzuia machafuko yasiyo na lazima nchini. 

 "Madhara ya kuripoti taarifa za upotoshaji na mipaka ambayo inahitajika ni makubwa kwa jamii ...tunahitaji kufikiria masuala mazito yanayokwamisha kufikia malengo yetu, hivyo ni muhimu kuacha kutoa taarifa zisizo sahihi," alisema 

NCHIMBI: MSIWAHIFADHI WAHAMIAJI HARAMU

Na Penina Malundo


  Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi,amesema Serikali itahakikisha wahamiaji haramu hawarudi nchini bila kufuata taratibu za kisheria zinazostahili kufuatwa. Dkt. Nchimbi aliyasema hayo Dar es Salam jana wakatiakizungumza na waandishi wahabari na kutoa matokeo ya awali juu ya utekelezaji Operesheni Kimbunga iliyolenga kuwaondoa wahamiaji haramu nchini

  Alisema kupitia operesheni hiyo awamu ya kwanza, wahamiaji haramu 12,604 wamerejeshwa katika nchi zao kutokana na agizo la kiongozi wa nchi, Rais Jakaya Kikwete. "Kati ya wahamiaji hawa,Wanyarwanda ni 3,448, Warundi 6,125, Waganda 2,496, Wakongo 589, Wasomalia 44, raia wa Yemeni mmoja na India mmoja," alisema Dkt. Nchimbi na kuongeza;"Ni vyema wahamiaji haramu wakafuata utaratibu wa kisheria,hata Watanzania wanaokwenda nchi nyingine nao wanapaswa kufuata utaratibu na si vinginevyo,"alisema.

   Alitoa wito kwa Watanzania,kuacha utamaduni wa kuwapokea na kuwahifadhi wahamiaji haramu jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha yao na nchi kwa ujumla. Alisema Watanzania wanapaswa kuwa macho na wageni wanaoingia nchini kutoka nchi nyingine bila kufuata taratibu za kuishi nchini kwani wengi wao wanauwezo wakufanya uhalifu hasa katika kipindi hiki cha usalama wa dunia kuwa hatarini.   

   Aliongeza kuwa, katika operesheni hiyo watuhumiwa 212 wa unyang'anyi wa kutumia silaha walikamatwa pamoja na mabomu 10 ya kutupwa kwa mkono, silaha 61, risasi 662 na mitambo miwili ya kutengeza silaha aina ya magobori

PUSH MOBILE KUTOA GARI KWA MSHINDI WA FIESTA

Na Mwandishi Wetu


   Kampuni ya Push Mobile Media, itatoa zawadi ya gari aina ya Vitz kwa mshindi wa promosheni ya tamasha la Serengeti Fiesta litakalofanyika mkoani Mwanza leo    Meneja Masoko na Mauzo wa Push Mobile Media, Rugambo Rodney alisema watatoa gari aina ya Vitz kwa mpenzi wa Fiesta atakayeshiriki katika tamasha hilo kwa kutuma neno Fiesta kwenda namba 15678 na kuingia katika bahati nasibu hiyo.

Rodney alisema mbali ya kushinda gari, mshiriki pia anaweza kushinda fedha taslimu sh. 100,000 kwa siku. Pia mpenzi wa Fiesta anaweza kushinda pikipiki.Mshindi wa Mkoa wa Mwanza atakuwa wa pili kupata gari ambapo mshindi wa kwanza wa gari alikuwa Abdallah Ngagari (51) aliyeshinda kupitia tamasha la Fiesta la Kigoma.

  "Tumepania kutoa zawadi katika mikoa yote ambayo Fiesta itafanyika, tumetenga zaidi ya sh. milioni 80 ili kufanikisha jambo hili ambapo magari aina ya Vitz yapo nane kwa ajili ya kuwapa mashabiki, tunawaomba mashabiki kushiriki kwa nguvu zote," alisema Rodney. Wakati huo huo, mkazi wa Shinyanga, Rose Mahenda amafanikiwa kushinda pikipiki baada ya kushiriki katika bahati nasibu hiyo.

WAKAZI WA DAR ES SALAAM WANUFAIKA NA TAMASHA LA WIKI YA HUDUMA ZA KIFEDHA, UWEKEZAJI NA UWEZESHAJI KWA WOTE

 Baadhi ya Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakiwa katika Mafunzo ya Biashara, na mafunzo jinsi ya kujiendeleza kiuchumi
  Baadhi ya Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakiwa katika Mafunzo ya Biashara, na mafunzo jinsi ya kujiendeleza kiuchumi
  Baadhi ya Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakiwa katika Mafunzo ya Biashara, na mafunzo jinsi ya kujiendeleza kiuchumi
  Baadhi ya Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakiwa katika Mafunzo ya Biashara, na mafunzo jinsi ya kujiendeleza kiuchumi
  Baadhi ya Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakiwa katika Mafunzo ya Biashara, na mafunzo jinsi ya kujiendeleza kiuchumi
 Semina hii ya mafunzo kwa watu wote inaendelea kwenye Viwanja vya Mnazi mmoja. Dar Es Salaam
Wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakipata Mafunzo hayo.(Picha Zote kwa Hisani ya Miss Demokrasia Tanzania)

WAKULIMA RUFIKI KUFAIDIKA NA MATREKTA KUTOKA KWA MWEKEZAJI.

Mratibu wa mradi wa kilimo cha miwa wa Kampuni ya Agro Foresty Plantation Ltd, Bw. Kiondo Mahanyu, akikabidhi funguo za Trekta kwa Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Chumbi B, Wilayani Rufiji, Bw. Abdulrahiman Ngongwe, kusaidia wakulima wa kijiji hicho kwa gharama nafuu. Kulia ni Afisa kilimo, Bi. Rose Mbezi na Bi. Mwanaidi Singano
Mratibu wa mradi wa kilimo cha miwa wa Kampuni ya Agro Foresty Plantation Ltd, Bw. Kiondo Mahanyu, akikabidhi funguo za Trekta kwa Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Chumbi B, Wilayani Rufiji, Bw. Abdulrahiman Ngongwe, kusaidia wakulima wa kijiji hicho kwa gharama nafuu. Kulia ni Afisa kilimo, Bi. Rose Mbezi na Bi. Mwanaidi Singano
Baadhi ya Matrekta ambayo wakulima hao watafaidika nayo
 WENYEVITI wa vijiji vya kata ya Chumbi Wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani wamemuomba muwekezaji ambaye amepewa aridhi kwa ridha yao kuwekeza haraka katika mashamba ya miwa ili wananchi waanze kufaidi matunda ya uwekezaji.

Matunda wanayotarajia kufaidika nayo ni pamoja na ajira kwa vijana wao kwa vile ya kulimwa miwa muwekezaji atafugua kiwanda kikubwa cha sukari na kuwa mkombozi mkubwa kwa ajira katika kata hiyo hasa kwa vijana wengi wanaomaliza darasa la saba na kulanda mitaani bila ya shghuli ya kufanya.

Wakiongea juzi mbele ya mratibu wa mradi anaesimamia shughuli zote za Agro plantation wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani, Kiondo Mahanyu ,walisema ukimia wa kuanza mradi unawatia wasiwasi wakazi wa eneo hilo kutokana na maamuzi yao ya kutoa aridhi ili baadae waje wafaidi matunda.

Wakiongea kwa pamoja katika maongenzi yaliofanyika katika ofisi za serikali Chumbi, juzi ambako wenyeviti wote wa vijiji nane katika kata hiyo walikusanyika kwa lengo la kuchukua matrekta toka kwa muwekezaji kama sehemu ya kusaidiwa kulimiwa mashamba kupitia kaya ya vijiji.

Mwaka jana muwekezaji alitoa matrekta katika kila kijiji na kufanya baadhi ya kaya kuogeza nafaka maradufu pamoja na kuwepo kwa mvua zisozoridhisha. Pamoja na kutoa matrekta pia muwekezaji anatoa misaada ya kijamii katika vijiji hivyo kitu ambacho kimefanya wanavijiji wavutiwe zaidi na muwekezaji huyo.

Wenyeviti waliokuwepo katika makabidhiano ya matrekta juzi ni pamoja na kijiji cha Nyamwage, Ibrahimi Mboweto,Said Makangu mwenyekiti wa kijiji cha Muhoro Magharibi,Rashid kisomo, mwenyekiti wa Muhoro Mashariki,Ali Nguyu mwenyekiti wa Chumbi A.

Wengine ni pamoja na Abdalahamani Ngongwe kaimu mwenyekiti wa kijiji cha Chumbi B na mwenyekiti wa kijiji cha Chumbi C. Salum Mtimbuko, wwenyeviti wa vijiji vya Roma , Tawi,Roma na Muyuyu hawakuweza kufika kutokana na udhuru, lakini trekta zao zipo kwa ajili ya kuchukua na kukodisha wananchi katika vijiji hivyo.

Akiongea wakati wa kukabidhi matrekta kwa niaba ya muwekezaji,Mratibu wa kampuni Mahanyu,alisema sehemu kubwa ya uwekezaji katika kata hiyo ni kuakikisha wananchi wananufaika na mradi huyo ikiwemo ajira kwa vijana na kwenye taaluma mbalimbali za elimu.

Amesema kuchelewa kwa kuanza mradi kumetokana na mchakato wa kupimiwa aridhi kama unavyoelekezwa na Serikali na si Muwekezaji, hatahivyo amesema hatua iliofikiwa inaridhisha na wakatai wowote wanakijiji watatagaziwa kupatikana kwa hati rasmi ya umilikaji halali wa mashamba hayo.

"Nawataka wanavijiji watulie na kutafakari masuala ya mbele kutokana na mchakato kuelekea mwisho wa kufanikiwa kupata hati ili shughuli ziianze rasmi",alisema Mahanyu na kuongeza kuwa faida nyingine watakazopata wanakijiji hao ni pamoja na kushilikishwa katika kilimo cha miwa ambapo kila mwanakijiji atalima miwa na kuuzia kiwanda.

Faida zingine ni pamoja na kupewa ushauri toka kwa mabwanashamba watakaotoa elimu juu ya mashamba ya miwa na nafaka zingine zitakazolimwa katika kata hiyo.Tayari

Akiongea kwa niaba ya wenyeviti wezake nane wa vijiji hivyo katika kata hiyo ambaye pia ni mwenyekiti wa kijiji cha Chumbi A, Ali Nguyu,alisema kusuasua kwa mradi huo kumewatia wasiwasi wanavijiji wa maeneo hayo ambapo waliwakilisha suala hilo kwa Mkurungenzi wa Wilaya ambaye pia aliwasiliana na mwakilishi wa na kwa pamoja waliwekena sawa kwa ajili ya kuendelea na mradi huo.

Hatahivyo wenyeviti  walimtaka muwekezaji kupuguza ghrama za kulima kwa kutumia matrekta hayo ambapo wametaka heka moja kulimiwa kwa shilingi 35,000 badala ya 45,000/= kama ilivyokuwa mwaka jana ambapo kutokana na maombi hayo mwakilishi wa Kampuni ya Agro Forest plantation alikubali ombi hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani mama Mwantumu Mahiza alimpogeza muwekezaji huyo kwa kujitolea na kuwawezesha wakulima katika kata hiyo kulimiwa mashamba ili kuondoa hali ya njaa katika kata hiyo kutakokoenda sambamba na ukulima wa kisasa.

Akiongea kwa njia ya simu , Mahiza alisema muwekezaji huyo anatarajia kuleta mabadiliko makubwa ya kilimo na kiuchumi kwa jumla pindi atakapoaanza shughuli zake za kutayarisha mashamba ya miwa na hatimaye kufugua kiwanda cha sukari Wilayani humo.
Mwishoooo

Monday, September 23, 2013

SIMANZI nchini KENYA


Posted: 23 Sep 2013 04:04 AM PDT
  • WALIOUWAWA NA AL-SHABAAB KENYA WAFIKA 60
  • MWANADIPLOMASIA WA CANADA NAYE AUWAWA
  • MAKOMANDOO ISRAEL WATUA NAIROBI KUWASAKA
    Mmoja wa majeruhi (kushoto) akiwa na jeraha la risasi mgongoni akikimbia kuondoka eneo la tukio.
    Watu wakikimbia kuokoa maisha yao baada ya wavamizi kuanza kumiminia watu risasi.

    Majeruhi akiwa amebebwa kuondolewa eneo la tukio baada ya kushambuliwa na risasi.
    Na Goodluck Hongo
     Idadi ya watu waliokufa katika shambulio lililofanyika katika jengo la kibiashara la Westgate jijini Nairobi nchini Kenya imefikia zaidi ya watu 60 na wengine 162 kujeruhiwa baada ya kundi la watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa kundi la Al-Shabaab kuvamia na kuwamiminia risasi ovyo.

    Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha The Citizen cha nchini Kenya, kundi hilo lilivamia jengo hilo saa saba kasoro dakika 10 mchana juzi na kuanza kuwapiga risasi watu hao. Vikosi vya usalama vya nchi hiyo vikitumia mbwa na helikopta, vimeendelea kuzingira jengo hilo ambapo hadi jana mchana kundi hilo la watekaji lilikuwa bado linawashikilia watu ndani ya jengo hilo la ghorofa nne.

    Jengo hilo ambalo ni lenye maduka na migahawa mingi hutumiwa na watu wengi ambapo mara nyingi siku kama ya Jumamosi hujumuika na familia zao kufanya manunuzi ya bidhaa mbalimbali.

    Televisheni hiyo ilionesha jinsi vikosi vya usalama vya nchi hiyo vilivyokuwa vikiokoa watu ambao walikuwa ndani ya jengo, huku helikopta za kijeshi zikizunguka jengo hiloTelevisheni hiyo ilisema wanamgambo hao ambao idadi yao haijafahamika bado wamejificha ndani ya jengo hilo wakiwa wamewateka idadi ya watu wasiojulikana wakati juhudi za kuwaokoa zikiendelea.

    Mitandao ya kijamii

    Katika baadhi ya mitandao ya kijamii ilimnukuu Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, akielezea shambulizi hilo kuwa ni la kigaidi na kwamba kitendo hicho kamwe hakikubaliki.Alisema waliohusika watakumbana na mkono wa sheria. 
    Aliongeza kuwa Wakenya hawatagawanyika kutokana na shambulizi hilo na jeshi lake litaendelea kukabiliana na magaidi wa nje na ndani ya taifa hilo. Rais Kenyatta alisema baadhi ya waliofariki ni jamaa zake na miongoni mwa waliofariki ni mwanadiplomasia wa Canada na raia wawili wa Ufaransa.

    Taarifa kutoka Ikulu ya Rais wa Kenya zinasema kuwa mshukiwa mmoja aliyekamatwa alifariki kutokana na majeraha yake.

    Mashuhuda

       Walioshuhudia shambulizi hilo wanasema kuwa waliwaona watu waliokuwa wamejifunika nyuso zao wakianza kumshambulia kila mtu waliyekutana naye ndani ya jengo hilo.Inadaiwa kwamba walikuwa wakiuliza waliyekutana naye maswali na aliyeshindwa kujibu alipigwa risasi.

    Uingereza yatoa tamko

       Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague, alisema Serikali yake inashirikiana na Kenya kuhakikisha magaidi na wanamgambo hao wanapatikana.Hili ndilo shambulizi baya zaidi kuwahi kuikumba Kenya tangu shambulizi la bomu lililotokea mwaka 1998 lililotekelezwa na Al-Qaeda.

       Vikosi vya usalama vikishirikiana na vikosi maalumu kutoka jeshi la nchi hiyo wameendelea kuweka ulinzi mkali ili kuwaokoa watu walioshikwa mateka na watekaji hao wenye silaha nzito kwa majibu wa mashuhuda.

       Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), lilimnukuu Waziri wa Usalama Joseph Ole Lenku, akisema watu 59 wamefariki katika shambulizi hilo lililofanywa na wanamgambo wa Al-Shabaab na wengine 175 kujeruhiwa.Waziri Ole Lenku alisema kuwa idadi ya magaidi walio ndani ya jengo hilo ni kati ya 10 na haijulikani wamejificha sehemu gani katika jumba hilo la Westgate.

    Red Cross wanena

       Shirika la Msalaba Mwekundu la nchini Kenya awali katika taarifa yake, lilisema kuwa watu 43 ndiyo waliofariki na zaidi ya 50 kujeruhiwa huku wengine wakitekwa katika shambulizi hilo.
     Habari zinaeleza kuwa hadi jana jeshi limeweza kudhibiti hali nje na ndani ya jengo hilo, magari ya kijeshi yamepelekwa katika eneo hilo, huku polisi na wanajeshi wakijaribu kuokoa mateka.

       Taarifa ambazo bado hazijathibitishwa na vyombo vya usalama vya nchi hiyo, zinasema wanamgambo hao wako ndani ya duka moja kubwa katika jengo hilo.

    Al-Shabaab watamba kuhusika

        Kwa mujibu wa BBC, ofisa mmoja mkuu wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab, aliliambia shirika hilo kuwa kundi hilo ndilo limehusika na shambulio hilo.Kwa mujibu wa ofisa huyo mashambulizi hayo yalikuwa ya kulipiza kisasi kwa Kenya kwa kujihusisha na vita ndani ya Somalia ambako wanajeshi wake wanakabiliana na kundi hilo.

      Wanamgambo wa Al Shabaab kupitia kwa mtandao wao wa Twitter , wanasema kuwa Kenya haikuchukulia kwa uzito onyo walilotoa kwa taifa hilo kwa hatua ya kuwapeleka wanajeshi wake nchini humo kupambana dhidi yao.

      Kundi hilo limesema limekuwa likitoa onyo mara kwa mara kwa Kenya kuwa ikiwa haitaondoa vikosi vyake nchini Somalia, athari zitakuwa mbaya mno.Kupitia mtandao wao wa Twitter, Al-Shabaab limesema kuwa Kenya haikusikia onyo hilo na kuendelea kuwaua Waislamu wasio na hatia nchini Somalia.

      Taarifa hiyo ya Twitter ilisema kuwa Shambulio la Westgate ni tone tu katika bahari ya mfano wa yanayowakumba Wasomali nchini Somalia.

    Makomando wa Israel wajitosa

      Katika hatua nyingine makomandoo wa Israel jana waliwazidi nguvu wanamgambo wa Somalia na kufanikiwa kuwakomboa mateka waliokuwa wakishikiliwa na manamgambo hao.Milio ya risasi ya hapa na pale ilisikika huku maofisa usalama wa Kenya wakisema walikuwa wakijaribu kuwaua au kuwateka washambuliaji waliobakia na kumaliza umwagaji damu uliodumu kwa saa 28 katika ukumbi wa soko wa Westgate.

      “Makomandoo wa Israel wamekwisha wasili na sasa w a n a w a o k o a ma t e k a n a waliojeruhiwa,” chanzo cha habari cha usalama cha Kenya kiliiambia Shirika la Habari la Ufaransa- AFP. Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ilikataa kuthibitisha au kukanusha kwamba vikosi vyake vilihusishwa 

    WAFANYAKAZI TANAPA WADAIWA KUHUSIKA KWENYE UJANGILI

    Posted: 23 Sep 2013 01:46 AM PDT

    Na Said Njuki, Arusha
      Wakati ujangili wa meno ya tembo na faru ukiinyima usingizi Serikali, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limewashtukia baadhi ya watumishi wake kutokana na kujihusisha na mtandao wa ujangili kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji wa vyombo mbalimbali vya dola.
    Kutokana na hali hiyo TANAPA inakusudia kubadili mfumo wake wa kiutendaji kutoka wa kiraia na kuwa mfumo kamili wa kijeshi kwa watumishi wote ili kujiimarisha katika kukabiliana na janga la ujangili nchini.

    Meneja Uhusiano wa TANAPA, Pascal Shelutete, aliwaambia waandishi wa habari jana mjini hapa kuwa Serikali haiwezi kuona maliasili ambazo ni urithi wa Watanzania na dunia kwa ujumla, zikiteketezwa na majangili na kuikosesha mapato Serikali.   Alisema lazima juhudi za makusudi zichukuliwe licha ya majangili hao kuwa na mtandao. Alisema ujangili hasa wa meno ya tembo na faru ni mtandao wa kimataifa unaohusisha watu wa kada mbalimbali, huku majangili hao wakitumia fedha nyingi na vifaa vya kisasa zikiwemo silaha za kivita, hali inayokwamisha jitihada za Serikali za kupambana na uhalifu huo.

      Shelutete alisema Shirika kwa kutumia vyombo vyake vya kiintelejensia vinawachunguza baadhi ya watumishi wake wanaojihusisha na mtandao huo na watakapogundulika na kujiridhisha watachukuliwa hatua kali za kisheria.  "Shirika linaendelea kuchunguza na kuchukua hatua mbalimbali za kinidhamu na kisheria kwa wafanyakazi wanaobainika kujihusisha na vitendo vya ujangili kwa kushirikiana na vyombo vya dola...uchunguzi unaendelea kufanyika kwa baadhi ya wafanyakazi na ushahidi wa kisheria utakapokamilika kwa wanaojihusisha na mtandao huo hatua za kisheria zitachukuliwa," alisema Shelutete
      "Tumepokea tuhuma dhidi ya baadhi ya watumishi wetu kujihusisha na ujangili, huo ni mwanzo mzuri kwetu katika kuchunguza tuhuma hizo kwa kutumia vyombo mbalimbali... hatukatai kuwa Shirika linaweza kuwa na watumishi wa aina hiyo, bali uchunguzi wa kina utafanyika ili tusimwonee mtu," alisema. 

       Alisema shirika linajua ukubwa wa tatizo, hivyo linajiandaa kwa mikakati mbalimbali ili kukabiliana na ujangili na tayari uimarishaji wa doria za magari, miguu na matumizi ya mbwa hifadhini kote nchini hali inayodhihirisha kupunguza kwa kiwango cha vitendo hivyo.  Alitoa mfano wa hifadhi za Tarangire na Ziwa Manyara akieleza kuwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita ujangili ulikuwa umeshika kasi umedhibitiwa kwa asilimia 100 kwa maana hakuna tembo hata mmoja aliyeuawa.

      Alitaja mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa kikosi maalumu cha kupambana na ujangili na matukio ya dharura, kutoa mafunzo maalumu ya awali kwa askari 100 ambao wataingia katika mafunzo ya awamu ya pili hivi karibuni.  Aliyataja baadhi ya mafanikio kuwa ni pamoja na kunasa majangili 1,116 ndani ya hifadhi za taifa nchini, wakiwemo majangili 248 walioshikwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti pekee katika kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu, kukamata silaha za moto 85 na waya zinazotumika kutega wanyama 25,422, mbao 3,275' mbao 1030 na mifugo 6,650.

    MOTO WA MSWADA WA KATIBA WAHAMIA VISIWANI ZANZIBAR

    Posted: 23 Sep 2013 01:58 AM PDT

    Na Mwajuma Juma, Zanzibar


      Chama cha Wananchi (CUF) kimemtaka Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, kujiuzulu wadhifa huo kwa kushindwa kusimamia maslahi ya Zanzibar.  Kauli hiyo ilitolewa mjini Zanzibar jana na Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Ismail Chusa Razu, wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kibanda Maiti. Alisema Balozi Seif amegeuka dalali wa kuiuza Zanzibar baada ya kukiri kuwa Zanzibar ilishirikishwa katika Mswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Muungano katika kipengele kinachohusu Zanzibar, jambo ambalo sio kweli. 

    Aliongeza kuwa, Balozi Seif akiwa kiongozi alistahili kuzungumza na Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na Mwanasheria Mkuu ndipo apate cha kuzungumza."Namtaka Balozi Seif ajiuzulu nafasi yake kwa kushindwa kusimamia maslahi ya Zanzibar, ikiwa ana uchungu wa Zanzibar hakustahili kusema hivyo," alisema na kuongeza kuwa kuanzia sasa watakuwa wakimuita Balozi Mkazi wa Tanganyika na Zanzibar.Kwa upande wa kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru,kusema anashangaa wazee wenzake kuleta rasimu ya Serikali tatu wakati Serikali mbili zilizopo kila moja ina mipaka yake na Zanzibar na bara zilikufa mwaka 1964 wakati nchi mbili zilipoungana,Chusa alisema Zanzibar bado ipo hai na itaendelea kuwa hai hadi kiama.

      Alisema iliyokufa ni Tanganyika hivyo kama lengo ni kuizika Zanzibar bado hawajafanikiwa kwani Wazanzibari wapo macho."Zanzibar ipo hai na itaendelea kuwa hai hadi kiama, nchi hii haijazikwa," alisisitiza.  Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad, alimtaka Rais Jakaya Kikwete, asisaini mswada huo, kwani ana nia nzuri, lakini wenzake wanataka kumpeleka kubaya. "Rais Kikwete ana nia nzuri lakini wenzako wanakupotosha, usisaini mswada huu tunajua una nia nzuri,"alisema Maalim Seif na kuongeza kuwa iwapo atakubali kusaini mswada huo atazuia wajumbe wa chama hicho wasishiriki Bunge la Katiba.

      Alishauri mswada huo urejeshwe Zanzibar ili kupata Katiba Bora. Kuhusu Balozi Seif, Maalim Seif alisema anamuonea huruma makamu mwenzake huyo kwa sababu hakujua ni mswada upi aliuona.
    Alisema Mei 6, mwaka huu aliitwa Dodoma na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kuambiwa kuwa wanataka kufanya marekebisho kwenye vipengele sita ambapo walifanya marekebisho, lakini waliporudi Tanzania Bara walifanya marekebisho kwenye vipengele nane.
    Alisema makamu wake hakujua hilo na anashangaa ni kwa nini wana-CCM wenzake wamemtosa. Alisema bila shaka walikuwa wamepanga jambo hilo.Alisema Waziri wa Sheria na Katiba Zanzibar, Mwanasheria Mkuu, Rais wa Zanzibar na yeye mwenyewe hawakubaliani na hilo.

    MAMA AUA MWANAYE MCHANGA

    Posted: 23 Sep 2013 02:11 AM PDT


     Na Elizabeth Joseph, Dodoma

       Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Cecilia Laurent (28) mkazi wa Uhindini mkoani Dodoma ambaye ni mhudumu wa baa na nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kama CDA Club mkoani hapa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mtoto wake mchanga.     Akielezea tukio hilo jana Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Mary Motto alisema kuwa mwanamke huyo alipokelewa majira ya saa 8 usiku ambapo pia hakuwa na kadi ya kliniki jambo ambalo lilidhihirisha kuwa hajahudhuria kliniki tangu kushika ujauzito huo, lakini walimpokea.  

       “Cecilia alifika hapa saa 8 usiku, bila ya kadi ya kliniki na ilipofika majira ya saa 9 usiku alienda chooni na kujifungua mtoto wa kiume, bila kutoa taarifa kwa wauguzi na baada ya kujifungua akamsukumiza mtoto katika tundu la choo kisha akafungua bomba la maji ili kukisukuma kiumbe (kuflash) jambo ambalo lilishindikana kutokana na tundu la choo hicho kuwa dogo kupitisha kiumbe hicho," alidai Muuguzi huyo.   

         Mmoja kati ya mashuhuda waliokuwa wodini hapo aliyejitambulisha kwa jina la Nyamizi Muhosi alisema kuwa, wakati akiwa bafuni anafua alimuona mwanamke huyo akianza kuzaa akiwa kachuchumaa kwenye tundu la choo, ndipo alipomkataza na kumwambia awaite wauguzi jambo ambalo hakulisikiliza.  “Nilikuwa bafuni nafua. huyo Cecilia alikuja chooni nikaona mtoto kashaanza kutoka nikamwambia awaite wauguzi wa zamu, lakini alikataa na kuendelea kuzaa mwenyewe bila kusaidiwa kisha akakisukumiza kichwa cha mtoto wake katika tundu la choo na kufungulia maji (kuflash) ili kuzidi kumsukuma, halafu akaanza kupiga kelele akidai mtoto wake kadumbukia chooni kwa bahati mbaya, jambo ambalo si la kweli,”alisema Muhosi. 

       Shuhuda mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mary Chihuma alidai kuwa, mwanamke huyo alidhamiria kuua mtoto wake, kwani tangu alipofika wodini hapo alikuwa akijigonga kwa makusudi katika vitanda vya wagonjwa wengine, lakini walipomuhoji kwa nini anafanya hivyo hakuwajibu kitu.Mtu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Juma Alikanda alikemea kitendo hicho na kusema kuwa si cha kiungwana na kama hali ya maisha yake ni ngumu haikumpasa kuchukua maamuzi hayo na kuitaka serikali kuchukua hatua za kisheria ili kukomesha tatizo hilo.
       Kwa mujibu wa mfanyakazi mwezake na mtuhumiwa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa, mtuhumiwa huyo alikuwa akiongopa kuhusu miezi ya mimba yake kwa kutaja miezi tofauti tofauti ambapo hata shangazi yake alikuja hivi karibuni kwa ajili ya kumuangalia, lakini mtuhumiwa huyo alimjibu mimba ni ya miezi minne jambo lililomfanya shangazi huyo kurudi kijijini kwao Usandawe Kondoa mkoani hapa. 

    Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Upelelezi mkoani humo, ASP Damas Nyanda alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mwili wa kichanga hicho umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Rufaa mkoani hapa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

    AZAM FC 'YAINYUNYIZIA LAMBALAMBA

    • '
     Na Elizabeth Mayemba

       Azam FC  waliifunga Yanga mabao 3-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.     Mpira ulianza kwa kasi ambapo Azam walipata bao la kwanza dakika ya kwanza lililowekwa kimiani na John Bocco kwa kichwa akiunganisha krosi iliyochongwa na Brian Umony. Azam walifuata tena lango la Yanga dakika ya tano, Humphrey Mieno akiwa na kipa Ally Mustafa 'Berthez' alipiga shuti lililotoka nje ya lango. Yanga ilizinduka dakika ya tisa ambapo, Didier Kavumbagu alipata nafasi nzuri ya kufunga lakini shuti lake likatoka nje ya lango.  Dakika ya kumi, Jerry Tegete aliachia shuti kali lililogonga mwamba na kurudi uwanjani ambapo mabeki wa Azam wakaokoa.

      Yanga waliendelea kulibana lango la Azam na kulitia kashikashi ambapo dakika ya 12, Mbuyu Twite alipiga shuti kali mpira wa faulo lakini kipa akapangua na kumkuta Kavumbagu alipiga nje ya lango.  Twite nusura angeipatia Yanga bao dakika ya 43, baada ya kuachia shuti kali akiwa nje ya 18 lakini mpira ukagonga mwamba na kutoka nje.  Yanga waliibana Azam kwa kiasi kikubwa na kuwafanya kurudi nyuma kulinda lango lao na kuwapa nafasi wapinzani wao kufanya mashambulizi kila mara.Kipindi cha pili dakika ya 49, Kavumbagu aliipatia Yanga bao baada ya kupewa pasi ndefu na Haruna Niyonzima na kuukwamisha mpira wavuni.

    Dakika ya 59, Hamis Kiiza aliyechukua nafasi ya Tegete akiwa na kipa, alipiga shuti kali lililookolewa na kipa.Kiiza alirekebisha makosa yake dakika ya 65 baada ya kuipatia Yanga bao la pili baada ya kupokea pasi ya Simon Msuva.Dakika ya 69, Kipre Tchetche aliisawazishia Azam bao la pili kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Yanga Kelvin Yondan kuunawa mpira katika eneo la hatari.Azam ilipata bao la tatu dakika ya 90 kupitia kwa Joseph Kimwaga baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa Tchetche.













    KIVUMBI

    Posted: 22 Sep 2013 11:14 PM PDT .

    Wafuasi wa vyama mbalimbali vya siasa vya upinzani, wakinyoosha mikono ikiwa ni ishara ya kukubaliana na matamko ya viongozi wa vyama hivyo, wakati wa mkutano wa kupinga kupitishwa kwa mswada wa Katiba Mpya katika mkutano uliofanyika kwenyeViwanja vya Jangwani Dar es Salaam jana.

    • Wapinzani wampa JK mtihani ndani ya wiki mbili
    • Askofu Kakobe nae amtaka asisaini mswada
    • Maandamano nchi nzima yanukia iwapo utapita
     Anneth Kagenda na Salim Nyomolelo
       Viongozi wa Vyama vya Siasa vya upinzani wamempa Rais Jakaya Kikwete, muda wa wiki mbili na nusu awe ametoa majibu kwa wananchi kama atasaini au hatasaini Mswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, vinginevyo wataitisha maandamano nchi nzima ikiwa ni pamoja na kususia kuingia kwenye Bunge la Katiba    Msimamo huo ulitolewa Dar es Salaam jana kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Jangwani na kuudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na madhehebu ya dini. 

    Akihutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema Rais Kikwete, anatakiwa awe amejibu madai yao ndani ya muda huo vinginevyo yatafanyika maandamano hayo.Mbowe alisema wataitisha maandamano hayo Oktoba 10, mwaka huu na hawataenda Polisi kuomba kibali isipokuwa watatoa taarifa kwani IGP Said Mwema ameelezwa jambo hilo.
    Alisema safari hii hawatakuwa tayari kuitwa kwenda Ikulu kuzungumzia suala hilo kwa sababu hata madai yao ya awali waliyokubaliana na Rais Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam hakuna kilichofanyiwa kazi.

    “Hatutakuwa tayari kwenda Ikulu kunywa chai wala juisi kwani hata makubaliano ya awali kuhusu mswada huo hakuna kilichofanyika,” alisema Mbowe. Alisema madai yao yote Rais Kikwete anayafahamu hivyo hawarudi kujadili suala hilo badala yake wanataka majibu ya madai yao.Alisema kwa sasa hatua ambazo tayari wamechukua ni kwenda kuona makundi mbalimbali ya kijamii nje ya wanasiasa ili kutafuta ufumbuzi wa suala hilo kwa kuamini kuwa wananchi ndiyo msingi wa katiba.

    Mbowe alisema migogoro ya ardhi inayoendelea nchini inachangiwa na Katiba, hivyo lazima ipatikane katiba ambayo itakuwa suluhisho la matatizo hayo. “Kosa kubwa kati ya makosa yote ni woga wa kudai haki, kinachotakiwa kwa sasa ni ujasiri,” alisema na kuongeza kwamba, kuwa na watu wenye woga ndiyo chanzo cha kuwa na katiba mbovu.

    Mbatia
    Kwa upande wake Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia, alisema katiba ni kitendo cha maridhiano na wala si cha kibabe kama CCM inavyotaka kufanya, hivyo watahakikisha inapatikana kwa gharama yoyote.Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar zinakinzana kwenye suala la madaraka ya rais. Alitoa mfano kuwa Katiba ya Zanzibar inamnyang’anya Rais wa Jamhuri ya Muungano madaraka katika suala la kuigawa nchi na hiyo inaonesha wazi kuwa kuna mgogoro wa kikatiba.

    “Inabidi ieleweke kuwa, Tanzania kwanza vyama baadaye...ieleweke kuwa CCM itayeyuka lakini Tanzania itabaki,” alisema na kuongeza kwamba ieleweke wazi kwamba, nchi sasa tayari ipo kwenye mgogoro wa kikatibaAlisema katiba inatakiwa itokane na wananchi wenyewe na si kuhodhiwa na chama kimoja cha CCM na wananchi kupoteza haki ili kupata katiba bora kwa ajili ya miaka 100 ijayo.

    Prof. Lipumba
    Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema CCM inatumia ubabe hadi ndani ya Bunge kiasi cha kufikia hatua ya wabunge wanapigwa. “Hiki ni kielelezo kuwa umefika wakati wa kuanza kufanya mazoezi ya viungo,” alisema na kuongeza kuwa tunahitaji kupata katiba inayohakikisha rasilimali za Tanzania zinatumika kwa manufaa ya wananchi wote.

    Aliongeza kuwa mswada uliopelekwa bungeni hauna ridhaa ya wananchi na umepitishwa kwa kuvunja katiba ya sasa ambayo inaeleza kuwa unatakiwa upitishwe na wabunge zaidi ya theluthi mbili, lakini idadi hiyo haikufika mswada ukapitishwa.Prof. Lipumba alisisitiza kuwa wananchi wa Zanzibar hawakushirikishwa kutoa maoni yao.

    “Makamu wa pili wa Rais Zanzibar alidhalilishwa kwani alipigiwa simu na waziri Mkuu Mizengo Pinda, ili aende Dodoma na baada ya kufika mswada wenye vipengele 11 vimepitishwa na vitano vimeongezwa ambavyo hajawahi kuviona,” alisema Prof. Lipumba na kusisitiza kuwa; “CCM wabaya! Wanamdhalilisha hata mwana-CCM mwenzao?”

    Askofu Kakobe
    Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe, alimtaka Rais Kikwete asisaini mswada huo; na akifanya hivyo atakuwa ameshindwa mtihani mkubwa wa kitaifa kwani suala hilo lipo mikononi mwake.Alisema mwanzo alionesha njia nzuri kwa kukubali mchakato wa Katiba mpya na iwapo atasaini wataona ilikuwa danganya toto. Alisisitiza kuwa makundi ya jamii hayajashirikishwa.“Katiba ya kweli inaanza na sisi wananchi ambao ndio chimbuko la viongozi wote na 
      
    Shekhe Kitimba
    Naye msemaji wa Shiah ya Maimamu Shekhe Rajabu Kitimba ; “Hili la katiba ni letu, haki haiombwi na sisi tunaunga mkono viongozi wote kwa asilimia 100.”Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa pamoja na wale wa dini ambapo walitoa matamko ya kumtaka Rais Kikwete asisaini mswada huo.

    SHAMBULIO LAUA WATU 22 NCHINI KENYA Posted: 22 Sep 2013 11:05 PM PDT



     NAIROBI, Kenya
      Watu 22 wanahofiwa kufariki baada ya watu wenye silaha kufyatua risasi mjini Nairobi, Kenya, kwenye eneo la maduka katika mtaa wa Westlands.Walioshuhudia tukio hilo, wanasema kuwa maguruneti pia yalitumika katika shambulio hilo.

      Kwa mujibu wa Mwandishi wa BBC mjini Nairobi washambuliaji inaarifiwa walivaa vilemba kama vya al-Shabaab, lakini haikuthibitishwa kama wapiganaji hao wamehusika. Taarifa za awali za BBC zilieleza kuwa watu sita waliuawa kwenye shambulio hilo.

      Polisi waliokuwa na silaha walizingira jengo la maduka liitwalo Westgate, katika mtaa wa Westlands na kuna taarifa ya watu waliojeruhiwa walikuwa wakitolewa hapo kwa machela.Ilielezwa kuwa watu wengi walikuwa wamenasa ndani ya jengo.

      Magari yaliyoegeshwa nje ya maduka yaliharibika. Shirika la Habari la Reuters liliarifu kuwa mpiga picha mmoja aliona watu wamelala chini.Hadi sasa hakuna taarifa rasmi kama kuna watu waliokamatwa kwa kuhusishwa na tukio hilo

    MAGEUZI YA KILIMO YAMPAISHA KIKWETE

     Na Mwandishi Maalum

    Rais Jakaya Kikwete, ametunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Udaktari wa Sheria na Chuo Kikuu cha Guelph cha Toronto, Canada, kutokana na mchango wake mkubwa wa kuleta mageuzi ya kilimo nchini na Afrika kwa ujumla . Rais Kikwete alitunukiwa shahada hiyo juzi katika sherehe ya kufana iliyohudhuriwa na mamia ya wasomi wa chuo hicho wakiwemo wanafunzi na wahadhiri na Wana-jumuya ya Watanzania waishio Canada.  

    Rais Kikwete ameitunuku Shahada hiyo kwa niaba ya wananchi wote wa Tanzania na hasa wakulima wadogo ambao wanapigana kufa kupona kuboresha maisha yao kupitia kilimo. Hiyo ni heshima ya juu kabisa ambayo Chuo Kikuu kinaweza kutoa; na Rais Kikwete anakuwa Mtanzania wa kwanza kutunukiwa Shahada hiyo katika historia ya zaidi ya miaka 100 ya Chuo hicho, maarufu kwa utafiti wa kilimo na magonjwa ya wanyama. Makamu Mkuu wa chuo hicho na Kaimu Rais wa chuo hicho, Dkt. Maureen Mancuso, alifungua rasmi Baraza la Kutunuku Shahada. 

    Akieleza sababu ya kumtunuku shahada hiyo Rais Kikwete, Profesa Dkt. Kevin Hall, alisema chuo hicho kimeamua kutoa Shahada hiyo kwa kutambua mchango wake katika kuendeleza, kuboresha na kuleta mageuzi katika kilimo cha Tanzania na Afrika. “Tumeshuhudia kwa namna isiyokuwa ya kawaida kabisa jinsi gani Rais Kikwete amekuwa sauti isiyochoka ya kusemea kilimo cha Afrika na kuishawishi dunia katika kusaidia kuleta mageuzi na mapinduzi ya kijani katika Bara hili muhimu sana kwa kukabiliana na changamoto zinazokabili kilimo katika Bara la Afrika,” alisema Dkt. Hall ambaye ni Makamu wa Rais wa Chuo hicho anayesimamia shughuli za utafiti.

    Aliongeza kuwa kwa miongo mingi hawajashuhudia kiongozi mmoja wa Afrika akijitokeza kwa namna isiyofichika kabisa kukabiliana na changamoto zinazokabili shughuli inayoajiri watu wengi sana na ambayo ni tegemeo kubwa la maisha ya mamilioni ya watu. “Rais Kikwete tunakushukuru kwa mchango wako mkubwa katika kuleta mapinduzi ya kilimo katika Afrika kupitia progamu zako kama vile Kilimo Kwanza na SACGOT,” alisema.Rais Kikwete, kama kawaida yake anapozungumzia shughuli za kilimo, ametoa hotuba ya kusisimua ambayo ilizungumzia hali ya kilimo katika Tanzania na Afrika, changamoto kuu za kilimo na hatua ambazo zinachukuliwa kukabiliana na hali hiyo.

       Akizungumzia umuhimu wa kilimo katika Tanzania, alisema kuwa asilimia 75 ya Watanzania wanaishi maeneo ya mashambani na kutegemea kilimo kwa maisha yao na kuwa hata wale wanaoishi mijini uhai wao unategemea kilimo kwa njia nyingi.  “Kilimo kinatupa chakula tunachokula, mali ghafi ya viwanda vyetu, mapato yetu ya fedha za kigeni na ajira kwa ajili ya watu wetu. Kilimo kinaingiza asilimia 25 ya Pato la Taifa, asilimia 34 ya mapato yetu ya fedha za kigeni, asilimia 95 ya chakula chetu na kinaajiri asilimia 75 ya watu wetu. Kwa ufupi basi, maendeleo ya uchumi na ustawi wetu unategemea kilimo,” alisema.

       Rais alisema pamoja na umuhimu huo wa kilimo kwa Tanzania na Afrika, bado kilimo cha Bara hilo kinabakia cha jadi, kilicho duni na chenye sifa ya uzalishaji mdogo.Niruhusuni nitoe takwimu kufafanua hoja hii. Katika Tanzania hekta moja ya mahindi inazalisha tani 1.3, wastani wa Afrika ni tani 1.9, katika China ni tani 5.7 na hapa Canada naambiwa ni tani 10. Vivyo hivyo, kwa uzalishaji wa mpunga na pamba.    Akizungumzia umuhimu wa kilimo katika Tanzania, alisema kuwa asilimia 75 ya Watanzania wanaishi maeneo ya mashambani na kutegemea kilimo kwa maisha yao na kuwa hata wale wanaoishi mijini uhai wao unategemea kilimo kwa njia nyingi.

      “Kilimo kinatupa chakula tunachokula, malighafi ya viwanda vyetu, mapato yetu ya fedha za kigeni na ajira kwa ajili ya watu wetu. Kilimo kinaingiza asilimia 25 ya Pato la Taifa, asilimia 34 ya mapato yetu ya fedha za kigeni, asilimia 95 ya chakula chetu na kinaajiri asilimia 75 ya watu wetu.    Kwa ufupi basi, maendeleo ya uchumi na ustawi wa wetu unategemea kilimo,” alisema.Rais alisema pamoja na umuhimu huo wa kilimo kwa Tanzania na Afrika, bado kilimo cha Bara hilo kinabakia cha jadi, kilicho duni na chenye sifa ya uzalishaji mdogo.