Msanii
wa muziki wa kizazi kipya, Nassib Abdul 'Diamond' akiwa amebebwa juu na
wacheza shoo wake wakati wa uzinduzi wa Tamasha la 'Wajanja'
lililofanyika katika ufukwe wa bahari ya Coco, Dar es Salaam juzi.
Tamasha hilo lilidhaminiwa na Vodacom Tanzania. Na Mpigapicha Wetu
|
Na Zahoro Mlanzi
KLABU
ya Simba, imetangaza rasmi kusitisha mkataba wa kiungo wake, Salum
Machaku kwa ajili ya maslahi ya klabu na ya mchezaji mwenyewe. Mbali
na hilo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Milovan Cirkovic anatarajia kutua
nchini Ijumaa akitokea mapumzikoni nyumbani kwao Serbia, huku wachezaji
wa kigeni 'Maproo' nao wanatarajia kuanza kuwasili siku hiyo. Akizungumza
na gazeti hili Makamo Makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi, Dar es
Salaam jana Ofisa Habari wa klabu hiyo Ezekiel Kamwaga, alithibitisha
kuachwa kwa Machaku kwa kusema kiungo huyo sasa ni mchezaji huru. "Ni
kweli Simba imeamua kusitisha mkataba na Machaku kwa maslahi ya klabu
na yake binafsi, hivyo kuanzia hivi sasa huyo ni mchezaji huru na timu
yoyote inaweza kumsajili," alisema Kamwaga. Alipotakiwa kuanisha
zaidi sababu za kusitisha mkataba wa kiungo huyo, Kamwaga alisema ni
uamuzi wa kawaida ambao wamefanya kama walivyofanya kwa wachezaji
wengine na ndiyo maana wameangalia maslahi yake na ya klabu pia. Mbali
na hilo, Kamwaga alisema Cirkovic pamoja na wachezaji Felix Sunzu na
Emmanuel Okwi wanatarajia kutua nchini kati ya Alhamisi na Ijumaa ambapo
moja kwa moja watajiunga na wenzao walioko kambini. Akizungumzia
suala la kambi, Kamwaga alisema wana wiki ya pili tangu timu hiyo
iingie kambini ambapo walianza kwa kuingia 'gmy' na jana jioni
walitarajia kuanza mazoezi ya uwanjani kwenye viwanja vya Sigara, Dar es
Salaam.
Alisema katika mazoezi hayo ndipo watakapoonekana
wachezaji wao wapya waliowasajili msimu huu kwa ajili ya Ligi Kuu Bara
na Kombe la Kagame ambalo linatarajiwa kuanza rasmi Julai 14, mwaka huu.
|
Posted: 19 Jun 2012 12:18 AM PDT
Na Elizabeth Mayemba
WAZEE
wa Kamati ya Muafaka ya Yanga wamewajia juu baadhi ya wanachama wa
klabu hiyo ambao walikwenda kumtolea lugha chafu Seif Ahmed 'Magari',
ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa timu yao baada ya kufanikisha zoezi
zima la usajili yeye pamoja na mfanyabiashara Abdallah Binkleb, ambaye
amejitosa katika kinyang'anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo. Akizungumza
Dar es Salaam jana Katibu wa Wazee hao, Ibrahim Akilimali alisema
tayari wafanyabiashara hao walisusia kufanya usajili huo, lakini
walitumia busara zao na kuwabembeleza ili waendelee na kazi hiyo. "Kuna
wanachama watatu pamoja na kiongozi mmoja wa Kamati ya Utendaji ambao
bila aibu walikwenda kwa Seif na kumtolea lugha chafu, hali ambayo
ilisababisha asusie kazi hiyo yeye pamoja na wenzake lakini ikabidi
tuwaangukie ili waendelee na tunashukuru Mungu walituelewa wazee wao,"
alisema Akilimali. Alisema baada ya kukamilika kwa utaratibu
mzima wa uchaguzi watachukua hatua kali kwa wanachama hao wakorofi,
kwani wanalenga kuipeleka pabaya timu yao hasa katika kipindi hiki
ambacho wanakabiliwa na michuno ya Kombe la Kagame na Ligi Kuu Tanzania
Bara. Katika hatua nyingine, Wazee hao wameazimia kulifuta tawi
la Uhuru na kuwataka wanachama wake wakajisajili kwenye matawi mengine
kwani tawi hilo lipo kwa ajili ya kueneza migogoro. "Uanachama
hatuwezi kuwafuta isipokuwa wakajisajili kwenye matawi mengine,
tutalisimamia na kuhakikisha linafutwa kabisa," alisema. Katika
hatua nyingine uongozi wa klabu hiyo umemfungashia virago mshambuliaji
wake, Mzambia Davies Mwape hivyo si mchezaji wao tena. "Mwape
tumemalizana naye hivyo si mchezaji wa Yanga tena, tunaliweka wazi
hilo," alisema Katibu Mkuu wa Yanga Selestine Mwesigwa.
|
Posted: 19 Jun 2012 12:17 AM PDT
|
Posted: 19 Jun 2012 12:14 AM PDT
Na Zahoro Mlanzi
TIMU
ya Yanga, imeanza rasmi mazoezi jana kwenye Uwanja wa Kaunda, Dar es
Salaam ikiwa na wachezaji tisa wakiwemo kipa Yaw Berko na Keneth Asamoah
huku kiungo wao mpya, Nizar Khalfan akiwa jukwaani akiangalia.
Gazeti
hili lilifika Makao Makuu ya klabu hiyo, Mitaa ya Twiga na Jangwani,
Dar es Salaam jana saa tatu asubuhi na kuikuta timu hiyo ikiendelea na
mazoezi huku mashabiki wachache wa timu hiyo walijitokeza kuiangalia.
Wachezaji
waliokuwepo katika mazoezi hayo yaliyokuwa chini ya Kocha Msaidizi,
Fredy Felix 'Minziro' ni Berko, Oscar Joshua, Asamoah, Jeryson Tegete,
Athuman Idd 'Chuji', Omega Seme, Ibrahim Job, Idrisa Rajab na Godfrey
Taita.
Mazoezi hayo yaliendelea mpaka saa nne na nusu ambapo
baada ya kumaliza wachezaji walisoma dua ya pamoja na kwenda kwenye
vyumba vyao, huku mashabiki wakionekana kufurahishwa na kitendo hicho.
Gumzo
lilikuwa kwa wachezaji Asamoah na Berko ambao waliripotiwa na vyombo
mbalimbali vya habari kwamba wangeachwa na kufanya kuwepo makundi ya
mashabiki kutumia muda mwingi kuwazungumzia, huku kila mmoja akishindwa
kuelewa juu ya uwepo wa wachezaji hao.
Pia Nizar naye alikuwa
kivutio licha ya kwamba hakufanya mazoezi kutokana na kuwa na udhuru,
alikuwa akizongwa na mashabiki hao na kuamua kukaa mbali na wachezaji
wenzake walipokuwa uwanjani.
Baada ya kumalizika kwa mazoezi
hayo, Minziro alizungumza na gazeti hili na kusema kwamba timu yake
imeanza mazoezi kwa ajili ya Ligi Kuu na Kombe la Kagame na kwamba
wachezaji wengine wataendelea kuwasili.
Alisema ana imani kwa
usajili walioufanya watatetea ubingwa wao wa Kagame pamoja na Ligi Kuu,
hivyo amewataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwapa ushirikiano
wachezaji wapya waliosajiliwa.
Akizungumzia kuhusu suala lake la
kulipwa mshahara, Minziro alisema ameshamalizana na uongozi wa Yanga na
kwamba kila kitu kinakwenda vizuri.
|
Posted: 19 Jun 2012 12:10 AM PDT
Na Mwandishi Maalumu, Maputo
KOCHA
wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen amesema baada ya kupoteza
mechi dhidi ya Msumbiji 'The Mambas', sasa atajipanga upya kwa ajili ya
mashindano yajayo kwani timu yake imeonesha uwezo mkubwa katika mechi
hiyo ya juzi.
Kim
aliishuhudia Taifa Stars, ambayo kwa sasa inadhaminiwa na Bia ya
Kilimanjaro Premium Lager, ikiondolewa na Msumbiji kwa penalti 6-7 baada
ya kumaliza dakika 90 kwa sare bao 1-1 kwenye mchezo huo wa kusaka
kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwakani.
Akizungumza
na vyombo vya habari, Kim alisema Stars walicheza vizuri lakini
wapinzani wao walitumia nafasi nzuri ya kuwa nyumbani na kushinda.
"Nawapongeza kwa kushinda, lakini najivunia vijana wangu kwa jinsi walivyoweza kucheza kwa umakini muda wote wa mchezo.
"Nilijua
Msumbiji wangeshambulia kwa nguvu, lakini na sisi tuliweza kucheza soka
yetu ya kawaida na kutegeneza nafasi nyingi, nashukuru tumeweza
kusawazisha lakini katika penalti lolote linaweza kutokea.
Naye kocha wa Msumbiji, Gert Engels aliwasifu Stars kwa kucheza vizuri huku akiwapongeza wachezaji wake kwa kushinda mchezo huo.
"Tanzania
ni timu nzuri inacheza kwa uwelewano mkubwa, lakini wakati wa mapumziko
niliwaambia wachezaji wangu watulie na wacheze kama nilivyoowaagiza.
Wanapaswa
kuitunza hii timu ya Taifa Stars kwa sababu ina wachezaji wengi
chipukizi wenye vipaji vya hali ya juu ni bahati mbaya tu tumewafunga
kwenye penalti.
Naye beki Erasto Nyoni, alisema wamepokea kwa
masikitiko matokeo hayo lakini aliahidi kuisaidia timu hiyo kwenye
michezo mingine.
"Tunatakiwa kujipanga upya kwa ajili ya mechi za
kusaka tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014, lazima
tukubali matokeo," alisema Nyoni.
Naye nahodha msaidizi wa Stars,
Aggrey Morris alisema hawana kingine zaidi ya kujiuliza wapi
walipokosea, ili kurekebisha makosa hayo.
Watanzania wengi
waliojitokeza kushuhudia mchezo huo walioneshwa kufurahhishwa na kiwango
cha Stars na kusema hata kama wameondolewa, walicheza kwa kujituma.
Anuary
Aziz, ambaye anafanya kazi Maputo alisema hajawahi kuona Watanzania
wanaoishi nchini hapa wakijitokeza hivyo kushangilia timu yao na
kuongeza kuwa walishapata taarifa kuwa Taifa Stars imeboreshwa.
“Kwa
kweli timu imebadilika na kocha huyu asisumbuliwe aachwe afanye kazi
yake, tumeshindwa lakini vijana wamecheza hadi dakika ya mwisho kwa
kweli tumefurahi na tumeshangilia sana. “Tanzania tutafika mbali
sana tuwe na subira tu kwani wachezaji wetu wanatupa matumaini
sana…mchezo huu ulikuwa wa kwetu lakini tumeshindwa kwa penalti
tumekubali matokeo na tunajua tutafika mbali,” alisema Mohamed Ali
ambaye ni Mtanzania mwingine anayeishi Maputo. Stars inategemewa kuwasili leo usiku ikitokea Maputo kupitia Nairobi.
|
Posted: 19 Jun 2012 12:06 AM PDT
Mashabiki
wa Taifa Stars wanaoishi nchi Msumbiji wakiishangilia timu yao wakati
wa mechi ya kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika
iliyochezwa juzi jijini Maputo. Stars ilifungwa kwa mikwaju ya penalti
7-6. Na Mpigapicha Wetu
|
Posted: 19 Jun 2012 12:03 AM PDT
MSANII
wa muziki wa kizazi kipya nchini, Nassib Adbdul ‘Diamond’ anatarajia
kupamba mashindano ya kumsaka Redd's Miss Dar Intercollege 2012,
yaliyopangwa kufanyika Juni 22 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Makumbusho ya
Taifa , uliopo mkabala na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM). Akizungumza
Dar es Salaam jana Mratibu wa mashindano hayo Dina Ismail alisema mbali
na Diamond, onesho hilo pia litapambwa na burudani kutoka bendi ya
Skylight ambayo ipo chini ya mshiriki wa Tusker Project Fame mwaka juzi,
Anneth Kushaba. Alisema maandalizi yanakwenda vyema ambapo
warembo 14, watakaosghiriki wanaendelea na mazoezi katika hoteli ya The
Grand Villa iliyopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam. “Mwaka huu
tumejipanga vyema kuhakikisha mmoja ya warembo kutoka Miss Dar
Intercollege anafanya vizuri katika fainali za Miss Tanzania,” alisema
Dina. Warembo watakaoshiriki mashindano hayo wanatoka vyuo vya
Biashara (CBE), Uandishi wa Habari (DSJ) na Time, Ustawi wa Jamii,
Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo Kikuu Huria (OUT ambapo taji hilo
linashikiliwa na Rose Msuya kutoka IFM. Dina aliwataja wanyange
watakaopanda jukwaani kuwa ni Veronica Ngota, Rose Muchunguzi, Nancy
Maganga, Hilda Edward, Diana Nyakisinda, Neema Michael, Veronica
Yollla, Jacquiline Cliff, Sharifa Ibrahim, Natasha Deo, Saada Suleiman,
Rose Masanja na Jamila Hassan.
|
Posted: 19 Jun 2012 12:01 AM PDT
Mchezaji
wa timu ya soka ya NBC, Hussein Shabani (kulia), akiwania mpira na
Henry Justin wa Barclays wakati wa mchezo wa kirafiki uliofanyika Dar es
Salaam juzi. NBC ilishinda kwa penalti 4-3. (Na Mpigapicha Wetu)
|
Posted: 19 Jun 2012 12:00 AM PDT
Na Amina Athumani
CHAMA
cha Kuogelea Tanzania (TSA), kimewataka wanachama wake 13 kuandaa
mafunzo ya kuogelea na uokoaji kama yaliyofanywa na Klabu ya Tanzania
Marine Swiming Clab (TMSC), ili kuwasaidia Watanzania wengi kupata mbinu
ya kujiokoa. Akizungumza
Dar es Salaam juzi wakati wa kuhitimisha mafunzo ya kuogelea na uokoaji
yaliyofanywa na TMSC Katibu Mkuu wa TSA, Noel Kiunsi alisema hii ni mara
ya kwanza klwa mwanachama wa TSA kuandaa mafunzo hayo ambayo kwa kiasi
kikubwa pia yanasaidia kuutangaza mchezo huo. Alisema TSA
imeanzisha programu ya kuendeleza mafunzo ya uokoaji chini ya Baraza la
Michezo la Taifa (BMT), ambapo kwa sasa wapo katika mchakato wa kupata
fedha kwa ajili ya kuanza programu hiyo ambayo itakuwa ikiendeshwa na
TSA pamoja na wanachama wake, ambao ni klabu kwa nchi nzima. Kiunsi
alisema msukumo wa kuanzisha programu hiyo umetokana na matukio
endelevu yanayotokea majini, hasa katika vyombo vya usafiri huku
akizitaja ajali za majini ambazo ziliwahi kupoteza maisha ya watu wengi
kama ajali ya Meli ya MV Bukoba na ile ya MV Spice Islander. Alisema
endapo Watanzania wengi watapatiwa mafunzo hayo kutaepusha wimbi la
watu kuzama majini, hasa yanapotokea majanga katika vyombo vya usafiri
na hata vile vya angani ambavyo hukimbilia baharini kwa kunusuru maisha
yao. Kiunsi aliwataja wanachama TSA ambao watashirikiana
kuendesha programu hiyo kuwa ni Talis, Hopac, UDSM, TMSC, Dar swim,
Stringleis, Isamilo, Agakhan, JKT na klabu za Zanzibar.
|
Posted: 18 Jun 2012 11:58 PM PDT
Na Zourha Malisa
SIKU
chache baada ya serikali kuwasilisha bajeti ya mwaka wa fedha
2012/2013, bungeni mjini Dodoma, baadhi ya wasanii wameipongeza kwa
kuweza kutambua mchango wa kazi zao kwa kuwaingiza katika mfumo rasmi
utakaolinda kazi zao. Wasanii
hao wameipongeza serikali kwa jitihada za kuinua uchumi wa nchi na
kipato cha msanii kwa kulinda kazi za wasanii kupitia mapato
yatakayopatikana. Akizungumza Dar es Salaam jana Rais wa
Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba alisema mfumo wa
sekta rasmi utapunguza wizi wa kazi za wasanii pamoja na kulinda haki
ya msanii. “Kutakuwa na takwimu sahihi za mauzo ya kazi za
wasanii na mapato ya wasanii, pia yataeleweka na mwisho wa mwaka unaweza
kujua nani ameuza kwa kiwango gani,” alisema. Alisema watakuwa
na kila sababu ya kudai serikalini kwani kila kitu kitakuwa kipo wazi
hivyo serikali itoe elimu kwa jamii, ili kujua kazi ipi ni sahihi
kununua kwa ajili ya kuongezea pato la taifa. Aliongezea kwamba
wanyonyaji wanauchukia mfumo huo, kwani walishazoea kuwakandamiza
wasanii hivyo mfumo huu ni tiba kwa wale wote waliozoea kujinufaisha kwa
kupitia nguvu za wasanii.
|
Posted: 18 Jun 2012 11:53 PM PDT
Na Amina Athumani
MWANAMUZIKI
wa kizazi kipya nchini Mh. Temba kesho anatarajia kutoka na wimbo wake
wa kwanza wa taarab utakayojulikana kama 'Usisemwe kwani wewe nani'. Akizungumza
Dar es Salaam jana, mtayarishaji wa wimbo huo Haji Ndanda kutoka studio
ya HVP iliyopo Kigamboni, alisema wimbo huo wa taarabu ni wa kwanza
kuutoa na kwamba ana imani italiteka soko la muziki huo. Alisema Temba amezoeleka kuimba muziki wa kizazi kipya na kwamba kwa mara ya kwanza ameamua kuja na staili mpya ya taarabu. Mtayarishaji
huyo alisema wimbo huo utaanza kuonekana na kusikika katika vyombo
mbalimbali vya habari kesho na kwamba ipo katika video na audio. Alisema
wimbo huo ameamua kumshirikisha msanii mwenzake wa muziki wa kizazi
kipya, Z-Anto ili kuongeza vionjo na kwamba ana imani mashabiki wengi wa
taarabu wataupokea vizuri hasa kutokana na uhodari wa Temba aliouonesha
katika video ya wimbo huo.
|
Posted: 18 Jun 2012 11:51 PM PDT
Na Amina Athumani
MWAKILISHI
wa Tanzania katika michezo ya Olimpiki bondia wa ngumi za ridhaa
Selemani Kidunda, amesema ingawa amekosa mapambano ya kimataifa bado ana
nafasi ya kufanya vyema katika michezo hiyo. Michuano ya
Olimpiki inatarajia kufanyika London, Uingereza Julai 27 mwaka huu
ambapo Tanzania itawakilishwa na wanamichezo sita akiwemo Kidunda na
wanariadha Zakia Mrisho, Samson Ramadhan, Dickson Marwa na Faustin Musa
pamoja na muogeleaji Magdalena Mushi. Akizungumza
Dar es Salaam jana, Kindunda alisema mechi za kirafiki alizocheza
makocha wake wamepata nafasi ya kurekebisha makosa yaliyojitokeza na
kwamba bado anayo nafasi nzuri ya kufanya vyema kwenye michezo ya
Olimpiki. Alisema hakupata mapambano mengi ya kimataifa kama kama
ilivyoshindikana kwenda Botswana na yale yanayoendelea nchini Kenya
kutokana na Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) kukumbwa na
ukosefu wa fedha. Kidunda ambaye kwa sasa yupo Kibaha, Pwani
katika kambi iliyopo Shule ya Sekondari ya Filbert Bayi, ananolewa na
kocha Zakaria Gwandu pamoja na bondia mmoja kwa ajili ya kumpa sapoti. Wawakilishi hao wa Tanzania katika michezo Olimpiki wanatarajia kuondoka nchini Julai 8, mwaka huu kwenda kwenye michuano hiyo.
|
Posted: 18 Jun 2012 11:45 PM PDT
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
PAZIA
la mashindano ya Epiq Bongo Star Search (EBSS) kwa Mkoa wa Dodoma,
limefungwa rasmi jana huku vipaji vingi vikiwa vimejitokeza na kuwavutia
majaji. Kilichovutia zaidi ni washiriki wa miaka 16, ambao
walionekana kuimba vyema na kuwafurahisha hata kwa washiriki wenzao
waliofurika katika Ukumbi wa Royal Village. Akizungumzia
mshindano hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Benchmark Production
inayoandaa EBSS, Ritha Paulsen alisema amevutiwa na wingi wa washiriki
mkoani hapa, hasa idadi ya washiriki ya wasichana. Alisema ikiwa
ni mara ya kwanza kuruhusu washiriki wa miaka 16 kuingia katika usaili
wa EBSS 2012, ameshuhudia hazina kubwa ya vipaji vya washiriki wa umri
huo. Katika usaili huo kulikuwa na washiriki wa aina mbalimbali
wakiwemo wanafunzi, wafanyabiashara ndogondogo, vijana wa mitaani na
wadau wengine wa muziki. Kwa kuthamini umuhimu wa akina mama na
watoto mshiriki aliyefika kuonesha kipaji chake katika ukumbi huo
alipewa nafasi ya kuimba, ili aweze kuwahi kuondoka. Naye Mkuu wa
Kitengo cha Mawasiliano wa Kampuni ya Mawasiliano ya Zantel ambao ni
wadhamini wakuu wa EBSS 2012 Awaichi Mawalla, mbali na kuvutiwa na
ushiriki wa vijana waliojitokeza, pia alihamasisha upimaji wa damu kwa
kuchangia damu kwa kituo cha damu mkoani Dodoma. “Kwa kupitia
EBSS 2012, tunataka kuwafikia vijana si tu katika muziki bali hata
katika kuhamasisha masuala mbalimbali yahusuyo jamii kama vile hili la
kuchangia damu na mengineo,” alisema Awaichi. Washindi
watakaopatikana watatangazwa baadaye katika vyombo vya habari. Baada ya
Dodoma kwa sasa inafuata Zanzibar Ijumaa ijayo katika eneo la Ngome
Kongwe.
|
Posted: 18 Jun 2012 11:44 PM PDT
Madam Ritha akipokea mtoto kutoka mshiriki huyu aliyekuja nae katika shindano hilo kabla ya kuanza ya kuanza kuimba.
|
Posted: 18 Jun 2012 11:37 PM PDT
Na Victor Mkumbo
BONANZA
la michezo mbalimbali la Vyuo vya Elimu ya Juu vya Dar es Salaam
lililofanyika juzi lilikuwa kivutio kwa wadau waliojitokeza. Bonanza
hilo lililoshirikisha vyuo saba ambalo lake lilikuwa kuibua vipaji
lilifanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Salaam. Vyuo
vilivyoshiriki bonanza hilo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo
cha Usimamizi wa Fedha(IFM), Chuo Cha Ustawi wa Jamii, Chuo Kikuu cha
Biashara (CBE), Chuo cha Ualimu (DUCE) na Chuo Kikuu cha Kampala (KIU). Katika
bonanza hilo ambalo lilifanyika kwa mwezi mmoja lildhaminiwa na Kampuni
ya Bia ya Tanzania Breweries (TBL) kupitia kinywaji chake cha Grand
Malt, ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni
Bernad Marcelline, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Akizungumza
mara baada ya kumalizika bonanza hilo, Marcelline alisema michezo hiyo
imefanikiwa kuimeibua vipaji vya wanafunzi wa vyuo hivyo katika michezo
mbalimbali. Alisema vijana hao hawana budi kujikita katika fani mbalimbali za michezo, kutokana na kuwa michezo ni ajira. Marcelline
alisema washindi walioshinda kwenye michezo mbalimbali wanatakiwa wawe
changamoto kwa kuwashawishi wenzao kuingia katika fani ya michezo. Naye
Meneja wa Grand Malt Consolata Adam, alisema wanatarajia kuendelea
kudhamini bonanza hilo katika mikoa yote yenye vyuo vikuu.
|
Posted: 18 Jun 2012 11:37 PM PDT
Na Victor Mkumbo
MNYANGE
Lisa Jensen, ndiye atakayewakilisha Tanzania katika mashindano ya
urembo ya Miss World 2012, yatakayofanyika Inner Mongolia nchini China
mwaka huu. Lisa aliibuka kidedea katika mashindano madogo ya Redd's Miss Tanzania, yaliyofanyika juzi katika Ukumbi wa 327 Dar es Salaam. Mrembo
huyo aliibuka mshindi baada ya kuwashinda wenzake tisa, ambapo
mashindano yalishirikisha warembo 10 ambao waliwahi kushiriki fainali za
Miss Tanzania zilizopita.
Katika mashindano hayo ya Redd's Miss
Tanzania, yalikuwa tofauti na ilivyozoeleka ambapo warembo hawakuulizwa
maswali ila walikuwa wanatoa mada tofauti tofauti kuhusu upeo wao na
jinsi ya kuisaidia jamii. Baada ya kuibuka mshindi Lisa
alizawadiwa sh. milioni 2, kugharamiwa gharama zote za safari pamoja na
kambi ya mwezi mmoja ambayo itakuwa Dar es Salaam, kabla ya kwenda China
katika mashindano ya Miss World 2012 na gharama zote zitalipwa na
Kampuni ya Lino Agency ambayo ndiyo inayoandaa Miss Tanzania. Warembo
walioshiriki katika mashindano hayo ni Gloryblaca Mayowa, Hamisa
Hassan, Queen Saleh, Christine Willium, Pendo Laizer, Lisa Jensen,
Mwajabu Juma, Neema Saleh, Jenifer Kakolaki na Stella Mbuge. Nafasi ya pili ilichukuliwa na Hamisa Hassan huku Pendo Laiser akishika nafasi ya tatu. Katika
mashindano hayo kulikuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa kikundi cha
ngoma za asili cha Wanne Stars pamoja na Saluti Dancers.
|
Posted: 18 Jun 2012 11:36 PM PDT
Miss tz Mwakilishi
wa Tanzania katika mashindano ya Miss World, Lisa Jensen (wa pili
kulia), akivishwa taji na Miss Tanzania Salha Israel,baada ya kutangazwa
mshindi katika shindano la Redd's Miss Tanzania lililofanyika juzi,
kushoto ni mshindi wa pili Hamisa Hassan na kulia ni mshindi wa tatu
Pendo Laiser(Picha na Victor Mkumbo)
|
Posted: 18 Jun 2012 11:32 PM PDT
Na Amina Athumani
KLABU
a kuogelea ya Tanzania Marine Swimming Club (TMSC), jana ilimaliza
mafunzo ya kuogelea na kujiokoa kwa watu zaidi ya 50 yaliyofanyika
katika fukwe za chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni. Mafunzo hayo
ya siku mbili yaliandaliwa na TMSC na kudhaminiwa na Kampuni ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) yakilenga kutoa mbinu za uokoaji, kuogelea
na jinsi ya kujiweka katika hali ya kusubiri kuokolewa pindi maafa
yanapotokea. Akizungumza wakati
wa kufunga semina hiyo ambayo iliendeshwa kwa nadharia na vitendo
Mratibu wa mafunzo hayo, Geofrey Kimimba alisema programu hiyo itakuwa
endelevu kwa kuwa ni moja ya malengo ya klabu yake. Alisema
wameamua kuandaa semina hiyo kutokana na ukweli kwamba majanga ya majini
yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara, lakini Watanzania wanashindwa
jinsi ya kujisaidia pindi majanga hayo yanapotokea. Kimimba
alisema kwa kufanya hivyo itasaidia idadi ya watu wengi kujiokoa ama
kuokoa wenzao, pale watakapopatwa na janga la kuzama kwa chombo cha
majini ama mafuriko kama yaliyowahi kutokea jijini Dar es Salaam Desemba
mwaka jana. Alisema mikakati ya klabu yake ni kuhakikisha
wanatoa mafunzo hayo mara kwa mara, ingawa muitikio wa Watanzania
unahitaji zaidi kusukumwa kutokana na watu wengi kushindwa kujitoa hata
pale wanapoamua kuendesha mafunzo hayo bila kiingilio. Mratibu
huyo alisema semina hayo ililenga zaidi kuwafundisha Watanzania ambao
hawajawahi kuogelea na hawajui jinsi ya kujiokoa na kwamba mafunzo hayo
yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, kutokana na washiriki wote kuelewa kwa
vitendo walichofunzwa. TMSC kwa sasa ina waogeleaji 55 tangu
kuanzishwa mwaka 2009 ambapo mpaka sasa klabu hiyo imeshiriki michezo
mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. "Tumefanya hivi ili kusaidia
kizazi chetu cha Tanzania, ambacho kisingekuwa na uwezo wa kulipia
gharama kubwa katika klabu nyingine ambazo zinaonekana asilimia kubwa ya
washiriki wake ni wazungu," alisema Kimimba. Alisema klabu hiyo
inatumia bahari katika kutoa mafunzo kwa waogeleaji wake, tofauti na
klabu nyingine ambazo zinatumia mabwawa na kwamba waogeleaji wake,
ingawa wanatumia bahari wamekuwa wakitoa upinzani mkubwa katika michezo
ya ndani na nje ya nchi.
|
Posted: 18 Jun 2012 11:31 PM PDT
Na Amina Athumani
WAANDAAJI
wa tamasha la filamu la Zanzibar International Film Festrival (ZIFF),
wameandaa warsha na kongamano kwa waandaaji na watayarishaji wa filamu. Warsha
hiyo itaanza Julai 9, mwaka huu na kushirikisha watayarishaji na
waandaaji kutoka nchi mbalimbali, zitakazoshiriki tamasha hilo
linalofanyika kila mwaka Ngome Kongwe, Zanzibar. Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa tamasha hilo, Martine Mhando alisema warsha hizo zitasaidia kuongeza ujuzi katika kupiga picha na kuhariri filamu. Alisema
pia kutakuwa na warsha maalumu ya uongozaji itakayotolewa na Mario Van
Pleebles, ambaye ni muongozaji wa filamu wa kimataifa ambapo itawasaidia
zaidi waongozaji wa filamu wa hapa nchini. Mhando alisema
tamasha hilo kwa mwaka huu litawavutia zaidi washiriki kutokana na ZIFF
kujipanga na kufanya mabadiliko makubwa mwaka hadi mwaka. Mbali
na warsha hizo, tamasha hilo pia linatoa nafasi kwa wasanii wa filamu
kutoka nchi mbalimbali kwa kazi zao kuingia kwenye tuzo za ZIFF, ambazo
zinatolewa kwa msanii aliyefanya vizuri katika ikiwemo tuzo ya filamu
bora, msanii bora na tuzo nyingine.
|
Posted: 18 Jun 2012 11:30 PM PDT
Mshambuliaji
wa Taifa Stars, Thomas Ulimwengu akiwatoka mabeki wa timu ya Msumbiji
katika mechi ya kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika
mwakani iliyochezwa jana jijini Maputo. Stars ilifungwa kwa penalti 7-6.
(Na Mpigapicha Wetu)
|
Posted: 18 Jun 2012 11:28 PM PDT
Na Mwandishi Wetu, Maputo
TIMU
ya Taifa (Kili Taifa Stars), jana imetolewa kiume na Msumbiji 'Mambas'
katika mechi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika
(AFCON), zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini. Katika
mechi hiyo Taifa Stars ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 7-6, baada ya
kutoka sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida. Katika hatua hiyo
ililazimika kupigiana penalti zaidi ya tano baada ya kila timu kufunga
mikwaju yote. Mechi hiyo ilipigwa katika Uwanja wa Taifa wa Zampeto jijini Maputo. Katika
mechi hiyo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 dakika 90 za kawaida na
kulazimika kutumika sheria za kupigia penalti ambapo washindi waliibuka
na mabao 7-6. Awali timu hizo ambazo zilikutana jijini Dar es Salaam, mwanzoni mwa mwaka huu zilitoka sare sare ya bao 1-1. Katika
mechi hiyo Stars ndiyo iliyoanza kufungwa kipindi cha kwanza kwa bao
lililofungwa na Jeremies Saito aliyeunganisha krosi ya Helder Pelembe. Kipindi
cha pili Stars iliingia kwa nguvu na kutandaza soka la uhakika kwa
lengo la kutafuta mabao, lakini ukuta wa wapinzani wao ulikuwa mgumu
kupitika kutokana na mabeki wake kuwa imara. Juhudi za vijana hao
wa Poulsen zilizaa matunda dakika ya 90, baada ya kupata bao
lililofungwa na Agrey Morris baada ya kuunganisha kona iliyochongwa na
Amir Maftah. Baada ya dakika 90 kumalizika ndipo sheria za
mikwaju ya penalti ikatumika ambapo wachezaji wa Stars Mbwana Samatta,
Morris na Kelvin Yondani walikosa na kuifanya Msumbiji kusonga mbele.
|
Posted: 18 Jun 2012 11:27 PM PDT
Na Mwandishi Wetu
UCHAGUZI
wa Yanga, uliopangwa kufanyika Julai 15 mwaka huu umeingia 'gundu'
baada ya aliyewahi kuwa Mhazini wa klabu hiyo Ahmed Falcon kuwawekea
pingamizi wagombea wote. Akizungumza Dar es Salaam jana Falcon
alisema ameamua kuweka pingamizi kutokana na kwamba uchaguzi unafanyika
na katiba ambayo haijasajiliwa na Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo. "Nimeamua
kuwawekea pingamizi wanaowania uongozi Yanga kwa kuwa wanafanya
uchaguzi usio halali kuwa katiba wanayotumia bado haijasajiliwa na
msajili," alisema. Alisema yeye kama mwanachama halali wa Yanga, hawezi kuona taratibu zinakiukwa baadhi ya watu kutokana na maslahi yao binafsi. Falcon
ambaye alijiuzulu Yanga, wakati wa uongozi wa Imani Madega alisema huu
si wakati wa kufumbia macho madudu yanayotaka kufanywa na wasioitakia
klabu hiyo mema. Alisema atahakikisha anafuatilia maslahi ya Yanga hadi kieleweke kwa kuwa kukaa kimya ni kuitakia mabaya klabu hiyo kongwe. "Ni
lazima tuwe na uchungu na klabu yetu, hatuwezi kuona kanuni na taratibu
zinavunjwa makusudi kwa kuwa ilitakiwa kuisajili katiba kama ilivyo kwa
vyama vingine," alisema. Baadhi ya wanachama waliojitokeza
kuwania uongozi wa klabu hiyo ni pamoja na aliyewahi kuwa mdhamini Yusuf
Manji, John Jambele na Sarah Ramadhan wanaowania nafasi ya Mwenyekiti. Wagombea wengine waliojitokeza ni Yono Kevela, Ayoub Nyenzi, Ally Mayay na Clement Sanga wanaowania nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
|
No comments:
Post a Comment