Posted: 19 Mar 2013 11:41 PM PDT
Na Mwandishi Wetu, Tabora
BAADHI
ya wananchi katika Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora, wamelalamikia
kitendo cha baadhi ya askari wa vituo vya polisi Usinge na Kaliua,
kuomba rushwa kwa mtutu wa bunduki. Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wamemuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, kusikiliza kilio chao na wachukulia hatua baadhi ya askari wanaofanya vitendo hivyo ili waweze kuishi kwa uhuru na amani. Wananchi hao kutoka Vijiji vya Ugansa, Shela, Kombe, Maboha na Usinge, walitoa malalamiko hayo katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Diwani wa Kata ya Usinge, Bw. Titus Kilomba.
Mkutano
huo ulifanyika hivi karibuni kwenye Kijiji cha Ugansa, ambapo wananchi
hao walidai kuwa, mbali ya kutishiwa kwa silaha ili kutyoa rushwa pia
wamekuwa wakibambikiziwa kesi na askari. “Tunamuomba Dkt. Nchimbi
na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, atusaidie kutatua
mgogoro kati ya askari na wananchi ambao umeanza kuvunja mahusiano
wetu,” walisema. Walidai kwamba askari hao wamekuwa
wakiwanyanyasa wananchi hususani jamii ya wafugaji kwa kuwabambikia kesi
kubwa kwa lengo la kutaka wapewe rushwa. Mkazi wa Kijiji hicho,
Bw. Ngidingi Lusumisha (67), alidai yeye walimbambikia fuvu la kichwa
cha mtu na askari aliowataja katika mkutano huo (majina tunayo), ambao
walikwenda nyumbani kwake na kudai wanamtilia shaka kuwa anamiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria. “Siku hiyo ilikuwa asubuhi, askari walikuja nyumbani kwangu wakaniambia nipo chini ya ulinzi wakidai wan mashaka na mimi hivyo wanahitaji kufanya upekuzi.
“Wakati
wakiendelea kunihoji, kuna mtu ambaye nadhani alikujana na fuvu la
kichwa cha mtu na kukiweka katika zizi langu la ngo’mbe ambapo wakati
wakiendelea kunihoji, askari mmoja alitokea zizini akiwa na kichwa fuvu
hilo na kudai nimekitoa wapi,” alisema. Alisema askari hao
walianza kumtisha na kumwambia “Wewe mzee sasa utaozea jela maana adhabu
ya kukutwa na fuvu la binadamu mahakamani ni kunyongwa hivyo kama nina
sh. milioni tano, wamuachie kwani kesi yake ni nzito sana. Aliongeza
kuwa, kutokana na maelezo ya askari hao aliogopa sana hadi kulazimika
kuwalilia wakamshawishi awape sh. 200,000. ambazo alizito na kuwapa.
Hata hivyo, Bw. Lusumisha alidai kumshukuru Mwenyekiti wake wa Kijiji cha Shela, Bw. Martin Juma kwa kumshauri alifikishe suala hilo kwa Bw. Kilomba ili aweze kulifuatilia zaidi. Kwa upande wake, Bw. Kilomba alisema, amekuwa akipokea malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo askari wa Kituo cha Polisi Kata ya Usinge ambao wanadaiwa kuwanyanyasa raia na kuwalazimisha kutoa rushwa kwa mtutu wa bunduki.
Mkazi
mwingine wa Kijiji cha Kombe, wilayani humo, Bw. Ikungile Mwandu,
alidai mtoto wake Bw. John Ikungile (25), alipigwa risasi na askari wa
Kituo cha Kaliua, kwa madai ya kuchunga ng'ombe katika shamba la jirani
la kusababisha hasara ya sh. milioni 150.
Alisema baada ya askari
hao kufika nyumbani kwake, walimuweka mtoto wake chini ya ulinzi,
kumfunga pingu ambapo wakiwa njiani kumpeleka Kituo cha Polisi,
walimtaka anyooshe mikono juu na kumpiga risasi katika mkono wake wa
kulia.
Akizungumzia mkasa huo, Bw. Ikungile alisema “walinipiga
risasi katika mkono wa kulia, baada ya kuanguka na kutowa damu nyingi
walinifungua pingu na kukimbia wakiwa na pikipiki.
“Baba
aliporudi alinipeleka polisi ili tukachukue PF3 ili niweze kwenda
kutibiwa hospitali lakini baada ya kufika kituoni hapo, waliniambia
tukienda hospitali nisiseme kuwa nimepigwa risasi eti, niwaambie nimechomwa na kitu chenye ncha kali,” alisema.
Mkuu wa Mkoa huo, Bi. Fatuma Mwassa, alipoulizwa kuhusu sakata
hilo alikiri kupokea malalamiko hayo na kuwa, tayari amemuagiza Kamanda
wa Polisi mkoani humo, Anthony Rutta ashughulikie suala hilo ili
wahusika waweze kukamatwa na kufunguliwa mashtaka katika mahakama ya
kijeshi.
“Taarifa hiyo ninayo...tayari nilishamwagiza RPC awachukulie hatua askari wote wanaotuhumiwa kufanya vitendo hivyo,” alisema.
Naye Kamanda Rutta alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo alidai kuwa, hana taarifa yoyote kuhusu hivyo kupingana maelezo ya Bi. Mwassa ambaye alisema tayari alishampa maagizo.
“Nani
kakuambia taarifa hizo...mimi sifahamu chochote kuhusu jambo hilo ndio
kwanza unanipa taarifa ngoja nizifanyie kazi” alisema Kamanda Rutta.
Katibu
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani humo, Bw. Iddy Amme, alisema chama
hicho hakiwezi kuvumilia vitendo vya aina hiyo vinavyofanywa na askari
wanaokiuka madili ya kazi zao.
Alisema baada ya kupata taarifa
hizo, alishituka sana na kuahidi kulifikisha suala hilo katika uongozi
wa CCM Taifa ili liweze kushughulikiwa kikamilifu.
Katibu wa CCM wilayani Kaliua, Bw. Simon Yaawo, alipendekeza iundwe tume ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo kwa wahusika.
“Mimi
nipo tayari kutoa ushahidi sehemu yoyote kama nitahitajika maana
tumechoka na matukio kama haya, mimi mwenyewe nilimuona yule kijana
aliyepigwa risasi (Ikungile).
|
Posted: 19 Mar 2013 11:35 PM PDT
ROME, Italia
KIONGOZI
Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis I, jana amesimikwa rasmi
kutumikia wadhifa huo na kutumia fursa hiyo kuwataka viongozi
mbalimbali, kuwalinda wanyonge na masikini.
Papa
Francis I, alitoa wito huo katika misa maalumu iliyofanyika kwenye
viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Petro mjini Roma ambapo katika misa
hiyo, alivalishwa pete ikiashiria sasa amekuwa Baba Mtakatifu wa 266.
Kwa
mujibu wa Kituo cha Utangazaji cha CNN, Papa Francis I, alizunguka
katika viwanja hivyo akiwa kwenye gari la wazi na baada ya kuteremka,
aliwabariki mahujaji mbalimbali.
Hata hivyo, inakadiriwa zaidi ya
watu milioni 1.6 waliudhuria sherehe hiyo huku mamilioni wakiifuatilia
kupitia vyombo vya habari wakiwemo viongozi 130 kutoka duniani kote.
Papa
huyo alichaguliwa na Mkutano wa Makadinali wiki iliyopita kuchukua
nafasi ya Papa Benedict XVI aliyetangaza kujiuzulu wadhifa huo Februari
28, mwaka huu.
Papa Benedict XVI alikuwa papa wa kwanza kujiuzulu katika miaka 600 ya historia ya kanisa hilo akidai umri wake wa miaka 85, asingeweza kutekeleza kikamilifu majukumu yake.
Katika hatua nyingine, Papa Francis I, anaonekana kuwa na mtazamo tofauti na watangulizi wake.
|
Posted: 19 Mar 2013 11:34 PM PDT
Na Jesca Kileo
RAIS
Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi,
IGP Said Mwema, kuomboleza kifo cha askari WP 2494 Koplo Elikiza ambaye
amepoteza maisha kwa kugongwa na gari juzi mchana katika eneo la
Bamaga, Dar es Salaam.
Koplo
Elikiza aligongwa wakati akimsimamisha dereva gari ambalo alijiunga na
msafara wa Rais Kikwete na kupewa amri ya kusimama badala yake akamgonga
na kusababisha kifo chake.
“Nimepokea taarifa za kifo hiki kwa
mshtuko na huzuni nyingi, nimejulishwa kuwa aligongwa na gari akiwa
kazini katika eneo la Bamaga, Dar es Salaam, wakati akiongoza msafara
rasmi.
“Ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha kwa Koplo Elikiza kupoteza maisha akiwa kazini kwenye utumishi wa jeshi lake na nchi yake wakati Taifa bado linaendelea kuhitaji sana nguvu kazi yake,” alisema Rais Kikwete.
Alimtaka IGP Mwema kumfikishia salamu zake kwa familia ya marehemu kuwa yupo pamoja nao.
Katika
hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
limesema bado linaendelea kumsaka dereva aliyesababisha kifo cha askari
huyo wa Kikosi cha Usalama Barabarani.
|
Posted: 19 Mar 2013 11:32 PM PDT
Na Rehema Mohamed
MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kesho inatarajia kutoa hukumu ya
washtakiwa wa kesi ya kufanya maandamano haramu kwenda kwa Mkurugenzi
wa Mashtaka nchini (DPP), inayowakabili wafuasi 53 wa Katibu wa Jumuiya
na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda.
Hukumu
hiyo inatarajiwa kutolewa na Hakimu Sundi Fimbo, anayesikiliza ambapo
upande wa mashtaka ulikuwa ukiwakilishwa na wakili wa Serikali, Bernad
Kongola, wakati upande wa utetezi unawakilishwa na wakili Mohamed
Tibanyendela.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na
mashahidi saba na vielelezo mbalimbali ambapo upande wa utetezi,
washtakiwa hao walijitetea wenyewe.
Washtakiwa hao wanadaiwa
kufanya maandamano haramu Februari 15 mwaka huu kwenda kwa DPP, licha ya
Jeshi la Polisi kukataza kufanyika kwa maandamano hayo.
Ilidaiwa
mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao wanadaiwa kufanya maandamano
haramu kwenda katika Ofisi ya DPP ili kumshinikiza atoe dhamana kwa
Shekhe Ponda na mwenzake Shekhe Mukadamu Swalehe.
Katika maelezo
ya awali, washtakiwa hao walidaiwa kuwa awali polisi walitoa zuio la
maandamano hayo lakini walikaidi ambapo siku ya tukio, polisi
waliwaamuru kutawanyika katika mikusanyiko waliyokuwa wakiifanya na
kukaidi ndipo wakakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Katika
maelezo hayo, mshtakiwa wa kwanza Bw. Salum Makame, alikiri kukutwa na
kisu na kipaza sauti lakini akakana kuwa hakuwa mfuasi wa Shekhe Ponda.
|
Posted: 19 Mar 2013 11:31 PM PDT
OSLO, Norway
KAMPUNI za Statoil na BG Group, zinatarajia kutumia dola za Marekani bilioni 10 kujenga kituo cha kuzalisha na kusafisha gesi ya asili nchini Tanzania ili kuiuza Asia.
Hatua hiyo inatokana na Kampuni ya Statoil kutoka nchini Norway, kugundua uwepo wa gesi nyingi Pwani mwa Tanzania.
Mkuu
wa Kitengo cha Uchimbaji wa kampuni hiyo, Bw. Tim Dodson, aliyasema
hayo juzi kutokana na utafiti waliofganya kwenye Bahari ya Hadi na
kugundua uwepo wa gesi yenye ujazo wa trilioni nne hadi sita.
“Tunafanya
kazi na BG ili kuja na makubaliano ambayo yataweka mambo sawa katika
maeneo husika, tunapaswa kukubaliana na mamlaka husika nchini Tanzania
wakati tunaingia katika hatua ya pili,” alisema Bw. Dodson wakati akizungumza na Shirika la Habari Reuters.
Aliongeza
kuwa, gesi waliyoigundua katika bahari hiyo huenda ikawa na ongezeko
kubwa kwani rasilimali hiyo inaonekana ni nyingi nchini Tanzania ambapo
kwa mujibu wa Reuters, BG imevutiwa na ushirikiano uliopo kati ya
kampuni hiyo na nyingine ya Ophir Energy.
Mwanzoni mwa wiki hii, Kampuni ya BG ilitangaza utafiti wake umefikia katika hatua nzuri za uchimbaji wa gesi Tanzania.
Katika
hatua nyingine, Wanajeolojia kutoka nchini Marekani wanadai gesi ya
asili inapatikana kwa wingi katika mwambao wa Tanzania, Kenya na
Msumbiji kuliko Nigeria ambayo ni nchi kubwa kwa uzalishaji wa nishati ya mafuta.
Reuters
liliongeza kuwa, Afrika Mashariki imeanza kuvutia watu katika sekta ya
mafuta kutokana na uhitaji mkubwa wa gesi katika Asia.
“Statoil
na BG katika ujenzi wa kiwanda hicho, tutakuwa tunapitia japo hatua
mbili, kwanza kuiandaa gesi katika kitalu namba mbili kinachosimamiwa na
Statoil na kitalu namba moja cha BG kwa nyongeza kutokana na ujazo wa
10-13 (tcf) ambao tunao.
“Kama ujazo huo utafikia 20 (tcf), wataangalia nini kifanyike ili gesi
hiyo iweze kuandaliwa vizuri, kiasi hicho cha fedha kitatumika katika
shughuli hiyo na uwekezaji utafanyika ndani ya miaka mitatu, kabla ya
mwaka 2016,” alisema Bw. Dodson.
Wakati huo huo, Mwandishi Peter
Mwenda anaripoti kuwa, Wizara ya Nishati na Madini, imeingia mkataba wa
utafiti wa gesi, mafuta na Kampuni ya JACKA Resources Ltd ya Australia.
Waziri
wa Wazara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo, aliyasema hayo Dar es Salaam
jana na kuongeza kuwa, watafiti hao wameingia mkataba wa miaka 11 ambao
umegawanyika sehemu tatu.
Alisema utafiti huo utafanyika katika eneo la Ruhuhu mkoani Ruvuma, Njombe na utakuwa wa miaka minne kwa kila awamu.
Aliongeza kuwa, awamu ya kwanza ya mradi huo kama mafuta na gesi itagundulika, kampuni hiyo itachukua asilimia 50 ya mapato na serikali ya Tanzania asilimia 50.
Alifafanua
kuwa, baada ya hapo Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania nchini (TPDC), nayo italipa kodi asilimia 30 na kampuni hiyo
italipa asilimia 30 ambazo zitatokana na mapato yao ya asilimia 50.
Awali
akizungumza katika mkataba huo, Mwenyekiti wa kampuni hiyo Bw. Scott
Spencer, alisema wao ni wazoefu katika kazi hiyo kwani waliwahi kufanya
utafiti katika Bara la Afrika na kufanikiwa kugundua mafuta ya petrol
kwenye Ziwa Albart nchini Uganda.
Alisema mradi huo utagharimu dola milioni 20 hadi 50 ambazo ni sawa na fedha za Tanzania sh. bilioni 80.
|
Posted: 19 Mar 2013 11:29 PM PDT
|
No comments:
Post a Comment