JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye ametuma salamu za
rambirambi kwa wanahabari wote kufuatia
kifo cha ghafla cha aliyekuwa
Mkuu wa Wilaya ya Njombe na Mtangazaji Mwandamizi wa
zamani wa Redio Tanzania(RTD), Dar es
salaam Marehemu Sara Dumba.
“Pokeeni
salamu za rambirambi zangu za dhati kwa kuondokewa na Mwanahabari mahiri Bi. Sara Dumba aliyekuwa mfano wa kuigwa”
amesema Mhe. Nape.
“Mbali
na utangazaji wake mahiri, Bi. Sara Dumba alikuwa
mzalendo wa kweli aliyetumikia tasnia hii ya Habari naSerikali
kwa uadilifu na upendo wa kweli, tutamkumbuka na tutaukosa mchango wake. Ni
wajibu wetu kumuombea mapumziko mema kwa mwenyezi Mungu na kumshukuru kwa
mchango wake alioutoa kwa moyo wa dhati”.
“Hakika
Sara tutamkumbuka, nawapa pole wananchi wote wa wilaya ya Njombe kwa kuondokewa na kiongozi wao
mpendwa mwenzao”,ameongeza Waziri Nape.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Elisante
Ole Gabriel naye ametuma salamu hizo “Salaam ziwafikie familia, ndugu
jamaa na marafiki
walioguswa na msiba huu
ambao unawagusa sana, naelewa machungu waliyonayo na huzuni, hata hivyo kwa
pamoja ni wakati wa kuzidi kumuombea Marehemu katika safari yake ya mwisho”,amesema Profesa Elisante
na kuwatakia moyo wa
subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Baadhi ya
wafanyakazi wenzake waliowahi kufanya
kazi pamoja naye ambao ni Aloisia Maneno
amesema Bi. Sara alikuwa
mwalimu wake katika masuala ya utangazaji kwa kuwa ndiye aliyemfundisha
jinsi ya kuandaa kipindi cha watoto cha Cheichei Shangazi.
Abdul Ngarawa
amesema kuwa Bi.
Sara alikuwa mchapakazi hodari, mtu mwenye kipaji cha utangazaji, mcheshi, mtu
mwenye ushirikiano na wafanyakazi wenzake na jasiri asiyeogopa kusema ukweli hata kwa wakuu wake wa kazi pale
ambapo kazi hazikufanyika
vizuri.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Hajjat Halima Kihemba akizungumzia uhusiano wake na marehemuamesema
kwamba yeye alianza kazi
RTD mwaka 1971 ambapo Bi. Sara alimkuta tayari akiwa kazini
kati ya mwaka 1974, hivyo walifanya naye kazi pamoja kwenye Idhaa ya Kiingereza ya
(External Services) marehemu
akiwa msaidizi wake.
“Alikuwa
ni mtu mwenye mchango mkubwa na yuko
tayari kufanya kazi wakati wote
unapomwihitaji usiku na mchana, mshauri hususan kwa watoto wa kike
kuacha kujidharau na kuona kwamba
hawezi kufanya kazi ya taaluma ya habari na mtu aliyependa maendeleo.
Kwa
upande wake, Bakari Msulwa ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kati Dodoma - TBC
akimzungumzia Bi.Sara Dumba amesema kuwa
alihamishiwa mkoani Morogoro mwaka 1990 akiwa mwakilishi wa RTD na baade Mkuu wa Kanda ya Kati Dodoma hadi alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya
Kilindi mwaka 2006 .Ameongeza
kwamba ni mama aliyekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za wanawake,
aliandaa vipindi mbalimbali vya biashara na alikuwa yuko
tayari kuambiwa ukweli.
“ Kwa
kweli Bi. Sara alijenga historia nzuri katika tasnia ya masuala ya habari na utumishi wa umma akiwa
katika ngazi ya ukuu wa wilaya, hivi karibuni nilionana naye mkoani Tabora miezi miwili
iliyopita alikuwa na mtazamo wa kuwaunganisha
wafanyakazi wa RTD ili waweze
kuwa na umoja utakaoweza kutupatia nafasi ya kusaidiana kwenye masuala
mbalimbali,” Amesema Msulwa.
Msulwa amebainisha kuwa Bi. Sara alisema
hayo baada ya kubaini kwamba hakuna historia ya wafanyakzi wa RTD. Hivyo
ameacha changamoto kwa hao kuacha historia zao
ili ziweze kuwa na manufaa kwa watu wengine.
Bi. Sara amefariki dunia tarehe
21 Machi, mwaka 2016 Wilayani
Njombe, baada kuugua ghafla. Alizaliwa Oktoba 19, 1956.
Bi. Sara alianza kazi katika Radio ya Taifa, Radio Tanzania Dar-es-Salaam (RTD)
na baadaye Shirika la Utangazaji Taifa (TUT) sasa TBC.
Marehemu Sara Dumba kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa
Wilaya mwaka 2006alivuma katika
kipindi cha Majira(yaani habari za hapo kwa hapo) na vipindi vingine vingi.
Kwa mujibu wa taarifa za Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Jackson Saikadau
amesema mwili wa
marehemu unatarajiwa kuagwa kesho Machi
24, mwaka huu jijini Dares Salaam na
kuzikwa nyumbani kwake eneo la Mbutu Mwembe Mdogo, Kigamboni.
Mwenyezi Mungu ailaze Roho ya Marehemu
mahali pema peponi, Amina.
IMETOLEWA NA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA
NA MICHEZO
23, MACHI, 2016.
No comments:
Post a Comment