TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Thursday, April 12, 2012

Mukama ang'aka

 *Awashukia wanaotakiwa kujivua gamba
*Adai wanatumika kumuhusisha na ufisadi
*Asema ndani ya CCM wote si Richmond


 Katibu Mkuu wa CCM Bw.Wilson Mukama.

Agnes Mwaijega na David John

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Wilson Mukama, amedai kukerwa na baadhi ya watu wanaomuhusisha na ufisadi uliofanyika kwenye miradi ya machinjio, maji na kusisitiza yeye ni msafi.

Bw. Mukama aliyasema hayo Dar es Salaam  wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya tuhuma dhidi yake ambazo zimetolewa katika vyombo vya habari vikimuhusisha na ubadhirifu wa fedha za miradi hiyo.

Alisema si kweli kwamba viongozi wote ndani ya CCM wanahusika na ubadhirifu katika miradi mbalimbali bali inawezekana tuhuma hizo zimeelekezwa kwake kwa sababu anahusika katika mapambano ya kuwavua magamba watu wanaokiuka maadili ndani ya CCM.

“Ndani ya CCM, si watendaji wote ni Richmond, inaonekana wengine wanatumia fursa hiyo kutaka kunichafua ili nionekane nashiriki ufisadi, mimi ni msafi nafanya kazi kwa kuzingatia maadili na nina wito ndiyo maana pamoja na kuwa mstaafu, bado nilionekana nafaa kuwa na wadhifa ndani chama,” alisema.

Aliongeza kuwa, taratibu za kisheria zipo hivyo kama kuna mtu ambaye mwenye hatia kwa tuhuma kama hizo kuna vyombo ambavyo vinaweza kushughulikia.

“Nashangazwa na baadhi ya watu kusema vitu ambavyo hawavijui undani wake, ni vema akaonesha uhalisia wa kitu anachokisema, miradi mingi ya maendeleo nchini inakufa kutokana na mabadiliko ya uongozi si ulaji wa fedha kama wengi wanavyodhani.

“Ieleweke wazi kuwa, miradi inakufa inapotokea yule aliyepewa nafasi ya kusimamia anapoondolewa na kuwekwa mwingine ambaye anashindwa kuuendeleza,” alisema Bw. Mukama.

Alisema kuna watu ambao hujitahidi kuonesha juhudi zao ili kuiwezesha nchi kupiga hatua lakini wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuandamwa, kusakamwa na kusemwa vibaya bila wahusika kufanya uchunguzi yakinifu.

“Katika nchi hii wanaofikiri kwa kina na kuumiza vichwa kwa ajili ya mafanikio wanaandamwa kila kukicha lakini waliokaa tu, wanaachwa na kuonekana wa maana.

“Tatizo kubwa la nchi hii wajinga ni wengi kuliko waelevu lakini haiwezekani nchi ikawa chini ya uongozi wa wajinga na wahuni ambao hawawezi kuliletea taifa manufaa.

“Watu wanaleta siasa magazetini badala ya kujikita katika kazi za msingi lakini mimi najua ninachokifanya, siwezi kuendelea kuona nchi haina mabadiliko,” alisistiza Bw. Mukama.

Aliongeza kuwa, suala la kujivua gamba katika chama litaendelea kwa wananchama wote ambao wataonekana kwenda kinyume na maadili na taratibu za chama.

Akizungumzia utendaji wa kamati za bunge, Bw. Mukama alisema kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni masuala yanayojadiliwa katika kamati hizo hayakupaswa kuwafikia wananchi kabla ya kumfikia spika na kujadiliwa bungeni.

Alisema kazi ya kamati mbalimbali si kutoa taarifa zilizojadiliwa na wabunge kwenye kamati husika bali zipo kwa kurahisisha utendaji wa wabunge.

“Mimi sioni kama ni sahihi masuala ya kamati mbalimbali za bunge kujulikana kabla ya kufika bungeni ambako ndiko yanapaswa kutolewa maamuzi,” alisema.
*Polisi kuimarisha ulinzi maeneo mengi
Na Waandishi Wetu, Arusha
MACHO na masikio ya wafuasi na wakereketwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), leo yanaelekezwa jijini Arusha ambapo Mahakama Kanda ya Arusha, itatoa hukumu ya kesi ya kupinga matokeo ya ubunge Jimbo la Arusha Mjini.

Kesi hiyo ambayo ilifunguliwa na wapiga kura watatu ni ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi mbunge wa jimbo hilo Bw. Godbless Lema (CHADEMA),  dhidi ya mpinzania wake, Dkt. Batlida Burian (CCM).

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliozungumza na Majira, walisema hukumu hiyo itatikisa jiji hilo ambapo taarifa za kuaminika kutoka vyanzo mbalimbali, zinadai ulinzi katika maeneo mbalimbali utaimarishwa ili kuhakikisha hakuna uvunjifu wa amani.

Hukumu hiyo inatolewa katika kipindi ambacho wafuasi na wapenzi wa CHADEMA wakisherehekea matokeo ya kura yaliyompa ushindi mbunge mteule wa Arumeru Mashariki, Bw. Joshua Nassari, huku CCM ikiwa inatafakari ni wapi ilijikwaa hadi mgombea wake, Bw. Sioi Sumari akabwagwa chini.

Siku ya jana katika baadhi ya maeneo, gumzo kubwa lilikuwa hukumu hiyo ambapo baadhi ya watu walisikika wakisema hukumu itakayotolewa iwe ushindi wa Bw. Lema au kutenguliwa, utatikisa jiji hilo.

Jaji ambaye atatengua kitandawili hicho ni Gabriel Rwakibarila wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga baada ya upande wa walalamikiwa kumkataa Jaji Joyce Mujulizi ambaye awali alipangiwa kusikiliza kesi hiyo kwa madai ya kutokuwa na imani naye.

Wakati wa kusikilizwa kesi hiyo, upande wa Bw. Lema uliwasilisha mashahidi wanne. Katika uchaguzi huo uliofanyika 2010, Bw. Lema aliibuka mshindi kwa kura 56,169, wakati mpinzani wake Dkt. Burian akipata 37,460.
Askari wa kikosi cha zimamoto na Uokoaji cha Halimashauri ya Jiji la Dar es salaam wakipambana kuzima moto uliolipuka na kuteketeza majiko ya soko la Samaki la kimataifa la feli jana chanzo cha moto huo ni mlipuko wa mafuta katika moja ya majiko ya kukaangia samaki.
Na Bahati Mohamed

WANACHAMA wa Chama cha Tanzanian Labour Party (TLP), wamempa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Bw. Augustino Mrema muda wa siku 40 awe amejiuzulu wadhifa wake kwa madai ya kuchangia chama hicho kishindwe katika uchaguzi wa mdogo wa ubunge Jimbo Arumeru Mashariki, mkoani Arusha.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Hamad Tao, aliyasema hayo Dar es Salaam  wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema tamko la kumtaka Bw. Mrema kujiuzulu analitoa kwa niaba ya wanachama wa chama hicho kutokana na matokeo mabaya ya kura 18 walizopata katika kata zote za jimbo hilo na kusisitiza kama atashindwa kujiuzulu ndani ya muda huo, wataitisha  maandamano nchi nzima ili kushinikiza aondoke.

“Bw. Mrema alipewa fedha za kutosha kwa ajili ya kampeni lakini hatukuona alichofanya zaidi ya kuzitumia kwa matumizi binafsi,” alisema Bw. Tao.

Aliongeza kuwa, wanachama wa TLP hawakuridhishwa na uchaguzi uliofanyika katika chama chao juu kumpata mtu ambaye atawania nafasi ya ubunge wa Afrika Mashariki.

Alisema aliyechaguliwa kugombea nafasi hiyo kwa tiketi ya TLP si mwanachama wa muda mrefu bali alipewa kadi ya uanachama akitokea CCM ili aweze kuwania nafasi hiyo.

Bw. Tao aliipongeza CHADEMA kwa kupata ushindi katika uchaguzi uliofanyika Arumeru Mashariki.
TATIZO la rushwa nchini lipo katika sekta mbalimbali lakini hali hiyo haina maana kuwa inakubalika katika jamii.
Ukweli ni kwamba, rushwa haikubaliki kutokana na madhara yake ndio maana Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa.

Rushwa inaathiri maendeleo ya mtu binafsi, familia, Taifa na kushusha hadhi ya mtoaji na mpokeaji. Rushwa inachangia kupindisha kanuni za maadili wakati wa kutekeleza majukumu kwa maslahi ya umma, mtu au kikundi fulani.

Vitendo hivyo vinajumuisha matumizi mabaya ya madaraka na kusababisha baadhi ya viongozi wa umma na sekta binafsi, kutumia madaraka waliyonayo kinyume cha sheria ili kujinufaisha.

Rushwa 'imebatizwa' majina mengi, wengine huiita mlungula, kitu kidogo, shati la mikono mirefu au zawadi.

Watu wanaojihusisha na vitendo hivyo, wanawanyima wananchi mategemeo ya kuwa na maisha bora, kuwakosesha elimu, huduma bora za afya, chakula, maji na mahitaji mengine ya kibinadamu.

Sisi tunasema kuwa, rushwa ni wizi dhidi ya Taifa na wananchi ambao wanategemea maisha bora, inachochea makosa ya jinai yanayovuka mipaka, kuvunja amani na utulivu.

Rushwa ina madhara makubwa kiuchumi kwa lugha nyepesi ni uovu unaowavunja moyo Watanzania na wafanyabiashara ambao wangependa kuwekeza nchini.

Inaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wakati mwingine husababisha kupungua ubora wa bidhaa ambazo huzalishwa viwandani.

Imani yetu ni kwamba, rushwa husababisha mapato ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kupungua hivyo kupuguza uwezo wa kutoa huduma kwa wananchi kutekeleza malengo ya kuboresha maisha yao na miundombinu ya nchi.

Uovu wa rushwa unachangia kuongeza umaskini katika jamii, kuathiri ubora wa elimu na sekta nyingine nchini. Rushwa inaweza kusababisha mgonjwa asipone haraka au kupoteza maisha kama atakataa au kukosa kile alichodaiwa kukitoa.

Tukifikia kiwango cha kuibubali rushwa kama sehemu ya utamaduni wetu katika vyombo vya sheria, waathiriwa wataamua kujilinda wenyewe kwa kuchukua sheria mkononi hivyo kuharibu sifa ya amani na utulivu tulionao.
Na Godwin Msalichuma, Kilwa
WAKULIMA wa korosho wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi, wamekitaka chama
kikuu cha ushirika mkoani humo, Ilulu kutenga korosho kwa ajili ya
kubangulia  ili kuziongezea thamani ya zao hilo na zingine kuzitafutia soko nje ya nchi.
Hali hiyo itasaidia kuacha  kutegemea wanunuzi wa kati ambao wengi wao ni wababaishaji  na wanachangia soko la zao hilo na hivyo kusababisha mkulima kukosa malipo kwa wakati na kuendelea kulima kilimo kisicho na tija.

Mwito huo ulitolewa hivi karibuni na wakulima hao waliokutana katika
mkutano wa wadau wa kilimo ulioitishwa na shirika lisilo la kiserikali
la kimataifa la Action Aid Internainal Tanzania (AAIT) ikiwa ni sehemu
ya utekelezaji wa mradi wa kuimarisha na kukuza kilimo cha zao hilo
wilayani humo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha
maendeleo ya wananchi mjini Kilwa masoko.

Walisema ili kuondokana na ubabaishaji unaofanywa na wanunuzi wa kati
ni vyema Ilulu ikatafuta soko la zao hilo nje ya nchi na kuuza ,moja
kwa moja kwa wanunuzi wakubwa mara baada ya kukusanya korosho kutoka
kwa wakulima na kuachana na utaratibu wa sasa ambapo chama hicho
kinawauzia wanunuzi wa kati ambao nao wanaenda kuuza kwa wanunuzi
wakubwa wanauza nje ya nchi.
“Mfumo wa ununuzi unaotumika ni mzuri lakini linapokuja suala la soko
ndio tatizo linapoanzia hapo…tunadhani ili kuondokana na tatizo hili
ni vyema chama chetu kikuu kikatafuta soko nje ya nchi…lakini pia kiwe
na mipango madhubuti ya kubangua angalau kiasi kidogo ili kuongeza
thamani korosho zetu”, alisema Bw.Yusufu Mcheni Mwenyekiti wa Chama
cha Msingi cha TAPWA.

Naye Bw. Athumani Kingolopi wa Chama cha  Msingi Ujirani Mwema ,
alisema kuwa ununuzi  ulikwenda  vizuri mwaka jana chini ya mfumo wa
stakabadhi ghalani na kuwa  mfamo mzuri wa kuigwa, lakini mwaka huu
wanunuzi waligoma kununua kwa bei nzuri mnadani na hivyo kuyumbisha
wakulima ambao wengi wao hadi leo hawajalipwa malipo yao ya pili.

“Kwa maoni yangu naona ni bora tutenge kiasi fulani kwaajili ya
kubangua na zinazobaki zikuzanywe na kuuzwa moja kwa moja nje ya nchi
ili kuondokana na tatizo hili na kumuongezea mkulima kipato…hawa
wanunuzi wa kati wanatuyumbisha”, alisema Bw. Kingolopi.

Awali Mkuu wa Idara ya Kilimo na Usalama wa Chakula kutoka Action aid
Makao Makuu, Bw. Elias Mtinda, alisema kuwa shirika hilo lipo tayari
kuwadhamini wakulima hao ili kupata mkopo kutoka vyombo vya fedha
kwa ajili ya kununulia mashine za kubangulia korosho zao.
Na Said Hauni, Lindi

WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamevamia makazi ya viongozi wa dini ya Kikristo Parokia ya Nyangao Wilaya na Mkoa wa Lindi huku wakipora fedha taslimu sh. milioni tano.

Pia inadaiwa licha ya kupora fedha hizo viongozi hao, ilidaiwa walijeruhiwa watu wanne wakiwemo viongozi wawili na walinzi wao wawili kwa kuwacharanga mapanga sehemu mbalimbali ya miili yao.

Habari kutoka Kata ya Nyangao ambazo zilithibitishwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa zilieleza kuwa tukio hilo lilifanyika Machi 30, mwaka huu majira ya saa 6:45 za usiku.

Kaimu Kamanda wa Polisi, Bw. George Mwakajinga alisema katika tukio hilo watu watatu kati ya hao walishambuliwa kwa kupigwa mapanga sehemu mbalimbali za miili yao wakati mmoja alifungwa kamba na kutupiwa kwenye shimo la taka.

Bw. Mwakajinga aliwataja walioshambuliwa kuwa ni ni, Paroko Housiager Hugo (74) na Padri Michael Mrope (75), Bw. Victor Hanga (58) na Joseph Mathias (45) ambao ni walinzi wa nyumba za viongozi hao.

Alisema, Bw.Hugo ambaye kwa sasa amelazwa Hospitali ya Mision ya Ndanda iliyopo Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara alipigwa mapanga kichwani na mbavuni ambapo, Bw. Hanga ambaye ni mlinzi pia alijeruhiwa na panga kichwani na kulazwa Hospitali Teule ya Nyangao.

Pia aliongeza kuwa Padri Mrope alishambuliwa kwa kupigwa huku mlinzi wake, Bw. Michael akifungwa kamba na kutupiwa kwenye shimo la taka hadi majambazi hayo yalipoondoka na kuokolewa na askari polisi waliofika kwenye eneo hilo.

Alisema, majambazi hayo ambayo yanasadikiwa kufikia zaidi ya 10 walikuwa na silaa mbalimbali yakiwemo mapanga, marungu na bunduki na walivamia makazi ya viongozi hao na kufanikiwa kupora fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni tano na kutokomea nazo kusikojulikana.

“Kabla hawajazichukuwa fedha hizo walipambana na walinzi waliokuwa wakiwalinda, lakini walizidiwa nguvu na ndipo majambazi hayo yalimfunga kamba mlinzi mmoja na mwingine kumjeruhi kwa panga kichwani,” alisema Bw. Mwakajinga.

Kaimu Kamanda huyo alisema katika tukio hilo hakuna mtu ambaye amekamatwa hadi sasa na kwamba askari wanaendelea na kazi ya kuyasaka majambazi hayo ili yaweze kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

Baadhi ya wananchi wanaodai waliweza kushuhudia sakata hilo lakini walishindwa kujitokeza kutoa msaada kutokana na majambazi hayo kufyatua risasi mbili hewani ambapo yalielekea kwenye makazi ya viongozi hao wakiwa kwenye gari moja aina ya Toyota 'Pick Up'.
Radhia Ramadhani na Joyce Kambota

WATU wanne raia wa Nigeria wamekamatwa na madawa ya kulevya aina ya HEROINE yenye thamani ya shilingi bilioni 1 .4 za kitanzania jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar e Salaam, Kamanda wa Polisi  kanda maalum mkoa wa Dar es Salaam Bw. Suleiman Kova alisema watuhumiwa wa kesi hiyo sio watanzania ni  wanaigeria waishio maeneo ya Tabata kinyerezi kibaga.

" Tukio hilo limekuwa la ajabu sana kwani hatujawahi kukamata dawa za aina hiyo zilizokuja kwa dizaini ya pakti za chumvi tena zimekaushwa" alisema Kamanda Kova.

Watuhumiwa hao waliotambulika kama Bw.Ifeanyi     Oko(33),Bw.Uchendu Jerry(35),Bw.Ugwu Valentine(31) na Bi. Ani Lawretta(27)mbali na kukamatwa na paketi nne pia wamekutwa na kete 12 za madawa zilizokuwa tayari kwa kumezwa.

Kamanda Kova aliongeza kuwa hadi sasa nchini kumekuwa na mtandao wa madawa ya kulevya kutoka nchi za nje hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuwafichua watu ambao wana mashaka nao.

Wakati huohuo Kamanda Kova alisema walifanikiwa kuwakamata waalifu Sugu (84) kwa tuhuma mbalimbali kufuatia misako inayoendelea ili kuhakikisha hali ya jiji la Dar es Salaam ni tulivu.

"Miongoni mwa vitu ambavyo tunaweza kujivunia jeshi la polisi ni pamoja na juhudi zilizofanywa na kikosi maalum wakishirikiana na ulinzi shirikishi kwa kufanya dolia na kuwakamata waarifu hao"alisema Kova.

Baadhi ya watuhumiwa hao ni Bw.Rashid Seif(25),Bi.Habiba Juma(22),Bw.Ramadhan Suleiman(30),Bw.Shaban Adam(33),Bw.Salehe Omary(17)na wengine79.
MA D I WA N I w a Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya wamesema kupungua kwa ukusanyaji wa mapato ya halmashauri hiyo ni dalili inayotokana na uvujaji wa fedha unaofanywa na baadhi ya watumishi.Pia walidai hali hiyo imekuwa ikichangia baadhi ya watumishi  kuvujisha na hata kughushi stakabadhi za kukusanyia mapato.
Imeelezwa kuwa watumishi hao wamekuwa wakiigeuza halmashauri hiyo kama shamba la bibi kwa kuchota fedha watakavyo na hivyo kusababisha kushuka kwa mapato kutoka sh. milioni 600 zilizokusanywa mwaka jana hadi kufikia sh. milioni 300 mwaka huu.
Hayo yalisemwa juzi wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani  kilichofanyika katika Ukumbi wa John Mwankenja ambapo walisema kama vitendo vya ufujaji fedha vinavyofanywa na baadhi ya watendaji vitaendelea itabidi Mkurugenzi wa wilaya hiyo Bw. Noel Mahyenga pamoja na Mweka  Hazina wa halmashauri Bw. John Shirima wawajibike.
Akizungumza katika kikao hicho Diwani wa Kata ya Masukulu, Bw. Rephson Mwaisupule alisema,  miezi mitatu iliyopita katika  kipindi cha mwaka jana fedha  zilizokuwa zimekusanywa katika  vyanzo vya ndani vya mapato  zilikuwa sh. milioni 600 lakini  katika hali ya kushangaza mwaka  huu zilizokusanywa ni sh. milioni  300 tu.
Naye Diwani wa Kata ya Kawetele  Bw. Anyimike Mwasakilali alisema tatizo la ufujaji wa fedha za mapato katika halmasahauri hiyo  ni aibu hivyo inatakiwa watendaji wote waliofanya ubadhirifu huo kuchukuliwa hatua za kisheria wakiwemo watendaji wa kata na vijiji wanakusanya fedha katika  kata zao na vijiji.
Naye Diwani wa Kata ya  Lwangwa Bw. Robart Mwaibata alisema baadhi ya watumishi wamekuwa   wakiandika ushuru ma l i p o ma k u bwa ka t i k a stakabadhi za malipo lakini fedha zinazofikishwa halmashauri ni kidogo hali ambayo imekuwa ikisababisha halmashauri kujikuta haina mapato ya  kutosha.
Akizungumzia malalamiko hayo ya madiwani Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Bw. Meckison Mwakipunga alisemna kuwa halmashauri tayari imeanza kuchukua hatua dhidi ya watendaji
wanaofuja fedha ambapo hadi sasa watumishi 11 wa halmashauri hiyo wamesimamishwa kazi.
Alisema kuwa, tayari watumishi hao hawapo kazini baada ya kubainika kufuja fedha hizo na uchunguzi zaidi unaendelea  kuhusiana na ufujaji huo ili kujua kama kuna watumishi wengine waliofanya ubadhirifu huo nao waweze kuchukuliwa hatua kama walivyochukuliwa hawa wengine.
Tunachoomba ni ushirikiano kwa nyie madiwani kwenye kamati ya fedha ambayo tayari ipo, kazini
kushughulikia ubadhirifu huo, tunajua tutawabaini wengine ambao wamejificha kwani fedha hizo zimefunjwa na wengi, alisema Mwenyekiti huyo.

Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. JakayaKikwete ajuwa na mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa kamuni ya UnileverGlobal, Bw. Paul Polman, Ikulu jijini Dar es Salaam jana. (Picha na Ikulu)
Anneth Kagenda na Flora Amon

HALMASHAURI y a Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara imepewa siku 14 kuwa imepeleka mchanganuo mpya ambao pamoja na mambo mengine uwe unaainisha vizuri matumizi ya sh. milioni 77 ambazo inadaiwa kuwalipa wafanyakazi hewa. Agizo hili lilitolewa Dar es Salaam jana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Bw. Idd Azzan.
Alisema  halmashauri hiyo imetumia fedha hizo kuwalipa wafanyakazi hewa  na watu waliostaafu, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Alisema watu waliolipwa fedha hizo watatakiwa kuzirudisha na ikiwa watakaidi sheria itachukua
mkondo wake. Alisema kuwa halmashauri hiyo inatakiwa kuwabana ili wazirudishe pamoja  na kutoa mchanganuo unaoeleweka juu ya fedha sh. milioni 119 ambazo zilikuwa ni za ujenzi wa zahanati.
"Tunaomba maagizo yote tuliyotoa yatekelezwe kwa muda muafaka, lakini pia ikumbukwe kwamba kamati imesikitishwa kuona hoja zingine zimeshindwa kupatiwa majibu yanayoeleweka," alisema.
Mwenyekiti huyo aliitaka halmashauri hiyo kuwa makini mara tu zinapotakiwa kuwasilisha michanganuo inayoonesha utendaji wao, kutoa ushirikiano kati ya halmashauri ya Babati Mjini na Vijijini.
Naye Mwenyekiti wa LAAT Bw. Augustino Mrema, alitoa onyo kali kwa halmashauri hiyo na kusema;
"Lazima makosa yao yatafutiwe adhabu ya onyo la mdomo ili kuleta tija" alisema.
Wakati huo huo,Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetakiwa kupunguza matumizi ya fedha kwenye semina, maonsho.
Hayo yalibainisha Dar es Salaam  na Makamu Mwenyekiti wa Hesabu za Serikali Bi.Zainabu Vullu,wakati wakupitia hesabu za wizara hiyo. Bi.Vullu alisema, sh. Bilion 1.9 zimetumika kinyume na bajeti ikiwemo sh. milion 729 kutumika kwenye sherehe za nane nane mjini Dodoma. Alisema mbali na fedha hizo pia Wizara ilichangisha kwa Taasis mabalimbali sh. miloni 86.kwa ajili ya sherehe ya nane                          
Watoto wakicheza kwa kuning'inia katika gari lilokuwa Mtaa wa Braziri eneo la Kinondoni,Dar es salaam.bila kujua kuwa wanahatarisha usalama wao.

Anneth Kagenda na Frola Amon

ADHA y a k u k a t i k a umeme mara kwa mara imewawakumba wabunge  waliokuwa wakihudhuria vikao vya kamati za bunge kwenye Ofisi Ndogo ya Bunge, hatua iliyowalazimu kuahirisha vikao hivyo. Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) Mwenyekiti wake, Bw. John Cheyo, alisema kutokana na adha hiyo, walilazimika kusitisha vikao vyao baada ya kusubiri umeme urudi bila
mafanikio.
"Waheshimiwa wajumbe naahirisha kamati hadi (kesho) kwani leo, hatuwezi kuendelea bila umeme," alisema Bw. Cheyo. Wakati akiahirisha kikao hicho tayari watendaji wa Idara ya Mwasibu Mkuu wa serikali walikuwa wamefika ofisi za bunge kuwasilisha taarifa za matumizi ya fedha. Kwa upande wak e
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Bw. Augustino Mrema, yeye alisitisha
kusikiliza mchanganuo wa ripoti ya mkoa wa Singida kutokana na matatizo hayo ya umeme. Wa k i z u n g u m z a n a waandishi wa habari baadhi ya wabunge walisema kukatika kwa umeme kunaathiri shughuli nyingi nchini.
Mbunge wa Mufindi Kusini Bw. Mendrad Kigola alisema "Kukatika kwa umeme kumetuadhiri kwani mambo mengi yameshindwa

Na Charles Mwakipesile, Mbeya

MKUU wa Mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro, amesema mafisadi wanaoiba dawa za Serikali, kuzipeleka kwenye maduka ya watu binafsi na kusababisha uhaba mkubwa wa dawa katika Bohari Kuu (MSD), hawawezi kuvumiliwa.
Bw. Kandoro aliyasema hayo jana mjini Mbeya wakati akifungua warsha ya siku moja iliyoshirikisha wadau wa MSD kutoka mikoa ya Singida, Dodoma, Iringa na Njombe.

Alisema Serikali imekuwa ikishuhudia uhaba mkubwa wa dawa uliopo MSD wakati maduka binafsi yanauza dawa za Serikali ambazo haziruhusiwi kuuzwa katika maduka hayo.

“Kimsingi Serikali inatumia mabilioni ya fedha kuhakikisha MSD inakuwa na dawa za kutosha ambazo zitasambazwa katika hospitali ili ziweze kuwasaidia Watanzania,” alisema.

Aliongeza kuwa, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapaswa kufanya uchunguzi katika maduka binafsi kubaini mafisadi wa dawa ili wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo.

Bw. Kandoro alisema tabia ya wizi wa dawa unafanywa na watu wasio na nia njema na uchumi wa nchi ambao unategemea watu wenye nguvu na afya bora hivyo kinachotakiwa kufanya uchunguzi ili kuwabaini watu wanaofanya ufisadi wa kuiba dawa MSD.

“Nawaonya wauzaji dawa katika maduka binafsi kuacha tabia ya kuuza dawa zilizopita muda wake, kitendo hiki ni sawa na uuaji kwani matumizi yake ni sawa na sumu mwilini hivyo kusababisha madhara makubwa kwa mtumiaji kiafya,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kanda, Bw. Cosmas Mwaifwani, alisema MSD imejipanga kuhakikisha inawahudumia Watanzania kwa kiwango stahiki na kukidhi mahitaji yao.

Alisema katika mpango wa muda mfupi, wamejipanga kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa kufikisha dawa hadi vituo vya afya kwa ajili ya kumaliza tatizo la upungufu na upatikanaji wa dawa.

Aliongeza kuwa, mawakala wamekuwa wakichelewa kupeleka maombi ya dawa MSD hivyo kusababisha zisipatikane kwa wakati.
Na Zahoro Mlanzi

KIKAO cha Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kimeshindwa kumalizika juzi kama ilivyotarajiwa kutokana na wajumbe waliohudhuria kikao hicho, baada ya kutokea mvutano katika kufikia muafaka wa rufani zilizowasilishwa na Klabu ya Yanga.
Kikao hicho kilianza juzi jioni na kuendelea tena jana chini ya Mwenyekiti wake Kamanda Mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana akiwa na baadhi ya wajumbe wake pamoja na viongozi wa Yanga, wajumbe wa Kamati ya Ligi na wawakilishi wa TFF.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana baada ya kuulizwa kilichofikiwa katika kikao cha kamati hiyo iliyokutana juzi, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema kikao kilishindwa kumalizika na kwamba kilitarajiwa kumalizika jana usiku.

"Kwa kweli hatutaweza kutoa taarifa juu ya kilichoamuliwa katika kikao hicho kama nilivyoahidi kutokana na kuwa hakikumalizika, hivyo kinaendelea leo (jana) jioni na kwamba watakalofikia lolote kesho (leo) au keshokutwa tutatoa taarifa," alisema Wambura.

Kikubwa katika rufani hiyo, Yanga walipinga adhabu iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya kuwafungia wachezaji wao watano, pamoja na kupinga maamuzi yaliyotolewa na mwamuzi Israel Nkongo, katika mechi yao hiyo dhidi ya Azam FC.

Wachezaji waliofungiwa ni Stephano Mwasika aliyefungiwa mwaka mmoja na faini ya sh. milioni moja, Jerry Tegete kifungo cha miezi sita na faini ya sh. 500,000, Nadir Haroub 'Cannavaro' alifungiwa mechi sita na faini ya sh. 500,000, Omega Seme na Nurdin Bakari wao walifungiwa mechi tatu kila mmoja.

Kutokana na adhabu hiyo, Yanga ilikata rufani kwa Kamati ya Tibaigana ambapo baada ya kamati hiyo kuomba vielelezo kwa kamati husika na kukosekana iliamua kuzisimamisha kwa siku 14 kutoa nafasi ili kupata ushahidi wa kutosha isipokuwa kwa zile zilizotolewa ndani ya dakika 90 ya mchezo.

Wakati hilo, likiwa bado halijapatiwa ufumbuzi kamati ya ligi ikaipoka Yanga pointi tatu na kuipa Coastal Union ya Tanga, pamoja na mabao mawili kutokana na kumchezesha Canavaro ikidaiwa hajamaliza adhabu aliyotakiwa kuitumikia ya kukosa mechi tatu kitu ambacho kimeibua mjadala mwingine upya.

Katika hatua nyingine, alipotafutwa Ofisa habari wa Yanga, Louis Sendeu kuthibitisha kwamba wamekata rufani juu ya kupokwa pointi, alisema wanasubiri kwanza maamuzi ya Kamati ya Nidhani, ndipo watajua la kufanya.

Hata hivyo wakati gazeti hili linakwenda mitamboni, zilipatikana taarifa kwamba katika hicho cha Kamati ya Nidhamu kulikuwa na mvutano mkubwa huku Kamati ya Ligi ikionekana kuzidiwa hoja na wajumbe wengine juu ya adhabu walizotoa kwa wachezaji wa Yanga.

Maskini Lulu, ombi lake latupwa

                                  
Na: Elizabeth Michael
 Suleiman Mbuguni

MSANII wa filamu nchini, Elizabeth Michael 'Lulu' jjuzi ameshindwa kutoa salamu za mwisho kwa msanii mwenzake katika tasnia hiyo, Steven Kanumba ambaye anadaiwa kabla ya kifo chake walikuwa pamoja nyumbani kwa marehemu Sinza Vatcan jijini Dar es Salaam.
Lulu ambaye anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Osterbay, Kinondoni jijini Dar es Salaam inadaiwa kwamba aliomba kwenda kutoa salamu za mwisho kwa msanii huyo nguli wa filamu ambaye alifariki Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam.

Hata hivyo msanii huyo alishindwa kutokea katika shughuli za kumuaga Kanumba, kutokana na habari zilizodai kwamba ni za kiusalama.

Juzi Kamanda wa Mkoa wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyela alinukuliwa katika vituo vya televisheni nchini akisema kwamba Lulu anashikiliwa katika cha Oysterbay, lakini kwa kuwa suala hilo lipo kisheria alikuwa anasubiri matokeo ya daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Kanumba.

"Ni kweli tunamshikilia Lulu, lakini hata hivyo hatuwezi kulizungumzia lolote kwa kuwa suala hili lipo kisheria na bado mwili wa marehemu unafanyiwa uchunguzi hospitalini," alisema Kenyela.

Hata hivyo katika shughuli za kuuga mwili wa Kanumba yaliyofanyika katika viwanja Leaders Klabu, Dar es Salaam maelfu waliojitokeza kutoa salamu za mwisho kwa nyota huyo wa filamu nchini walishindwa kufanya hivyo kutokana na wingi wa watu waliojitokeza.

Ilikuwa ni simanzi, majonzi na vilio katika viwanja hivyo baada ya mwili wa Kanumba kuwasili sehemu iliyotayarishwa, huku baadhi ya wanawake wakidondoka na kupoteza fahamu.

Hatua hiyo iliwafanya watoa huduma ya kwanza kutoka Msalaba Mwekundu kuwa na shughuli pevu ya kuwapeleka katika magari yao kwa ajili ya kuwahudumia.

Kutokana na tafrani hiyo MC alilazimika kutangaza kusitisha shughuli ya kumuaga Kanumba, kitu ambacho watu waliofika katika viwanja hivyo kuanza kupiga kelele za kutoridhishwa.

Hata hivyo kabla ya kutangaza kusitisha viongozi wa serikali walioongozwa na Makamu wa Rais, Mohamed Ghalib Bilal kupewa nafasi ya kuuga mwili huo pamoja na baadhi ya ndugu wa karibu.

Viongozi wengine waliopata nafasi ya kutoa salamu za mwisho kwa marehemu Kanumba, alikuwa mke wa Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete, Mke wa Makamu wa Rais Mama Bilal, Waziri Ardhi Anna Tibaiujka, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe.

Viongozi wengine ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Dkt. Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecky Sadiq, Mbunge wa Kinondoni Idd Azzan, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana na Meya wa Manispaa hiyo, Yusuf Mwenda.

Tuesday, March 13, 2012

Lipumba arejea kuinusuru CUF



*Apata mapokezi ya kihistoria akitokea Marekani
*Adai Tanzania hakuna utawala wa kidemokrasia
*Wanafunzi 808 Dodoma wakihama chama hicho


Na Peter Mwenda
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amewasili jana akitokea nchini Marekani na kupata mapokezi ya kihistoria.

Wachambuzi wa mambo ya siasa wanasema kuwa, kurejea kwa kiongozi huyo kutasaidia kukinusuru chama hicho ambacho hivi sasa kimekubwa na jinamizi la kuondokewa na wanachama wake.

Profesa Lipumba aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere saa 9:20 alasiri ambapo viongozi mbalimbali wa chama hicho walijitokeza kumpokea wakiwemo wabunge na wanachama wakiongozwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad.

Baada ya kushuka kwenye ndege, Prof. Lipumba alifanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa CUF katika chumba maalumu cha mapumziko.

Baada ya kumaliza mazungumzo, Prof. Lipumba alitoka nje na kuvalishwa shada la maua huku vigelegele na nderemo zikitawala katika maeneo mbalimbali ya uwanja huo.

Eneo la uwaja lilijaa wafuasi wa CUF waliokuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kumpongeza Prof. Lipumba kwa kuwa mwafrika pekee kuchaguliwa kwenye kamati ya kuchunguza chanzo cha mdororo wa uchumi duniani.

Kutokana na wingi wa watu walijitokeza kumpokea, Maofisa Usalama walimzuia Prof. Lipumba na Maalim Seif, kuhutubia wananchi katika uwanja huo.

Maofisa hao walishauri viongozi hao waondoke ndipo Prof. Lipumba aliamua kuzungumza na waadishi wa habari na kusema kuwa, kazi anyoifanya nchini Marekani angeweza kuifanya Tanzania kama mchumi aliyebobea lakini hapati ushirikiano.

“Nipo tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania kuhusu masuala ya uchumi, hii itatokana na utawala na demokrasia ambao kwa sasa haupo nchini Tanzania,” alisema.

Aliwashukuru Watanzania na wafuasi wa CUF kwa kujitokeza kumpokea na kudhihilisha kuwa, wananchi wana imani na chama hicho.

Kwa upande wake, Shekhe Issa Ponda, akiongoza mashekhe wenzake 20 kutoka misikiti mbalimbali jijini Dar es Salaam, alisema mchango wa Prof. Lipumba ni heshima kubwa kwa Tanzania.

Ofisa Mawasiliano wa CUF, Bw. Salium Biman, alisema chama hicho kitachukua dola mwaka 2015 kutokana na umati mkubwa wa watu waliojitokeza uwanjani wenye imani na Prof. Lipumba.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar, Bw. Ismail Jussa Ladhu, alisema umati uliojitokeza kumlaki Mwenyekiti huyo ni salamu tosha kwa mbunge wa Wawi, Bw. Hamad Rashid Mohammed kuwa chama hicho bado kina nguvu.

“CUF imeanza kazi rasmi ya kuimarisha chama ili 2015 tuchukue dola kwa kishindo,” alisema, Bw. Jussa.

Baada ya kuzungumza na waandishi wa habari, Prof. Lipumba aliondoka na msafari wa watu walifika kumpokea ukiongozwa na pikipiki, magari na watembea kwa miguu hadi Uwanja wa Karume.

Awali mapokezi hayo yaliingia dosari baada ya gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 854 AMN, lililokuwa limejaza wafuasi wa chama hicho, kupinduka na kusababisha watu 10 kuumia.

Taarifa nyingine zinasema kuwa, gari lingine ambalo lilikuwa likitokea Rufiji mkoani Pwani kupeleka wafuasi wa chama hicho uwanjani hapo, lilimgonga mtembea kwa miguu na kufa papo hapo.

Wakati huo huo, Mwandishi wetu kutoka Dodoma anaripoti kuwa, zaidi ya wanafunzi 808 wa Vyuo Vikuu mkoani hapa ambao ni wananchama wa CUF, wametoa tamko la kujitoa na kurudisha kadi kwa uongozi wa chama hicho kwenye matawi ya vyuo vyao.

Wanafunzi hao walidai kuwa, wamelazimika kujiondoa katika chama hicho kutokana na kitendo cha viongozi wa ngazi ya juu kujali zaidi maslahi binafsi na kukidumaza chama.

Tamko la kujitoa katika chama limetolewa na Mwenyekiti wa Tawi la St. John  Bw. Muhamed Abdullha kwa niaba ya wanafunzi wezake katika kikao kifupi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano chuoni hapo.

Bw. Abdullah alisema wanachama waliojitoa ni wasomi wa elimu ya juu katika vyuo vyote mkoani haapa ambao wamerudisha kadi za chama hicho na kila mmoja atachagua chama cha kwenda ambacho kina mtazamo wa kuleta maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

“Uongozi wa CUF kimsingi umetuchosha, hatujui unajali maslahi ya nani, inaonesha wazi kuwa viongozi wachache wa juu wanalinda maslahi binafsi na ndiyo maana chama hakikui.

“Kutokana na hali hiyo, wanafunzi ambao ni wanachana wa CUF tumelazimika kurudisha kadi, kila mmoja atachagua cham cha kwenda chenye mwelekeo wa kusaidia wananchi,” alisema.

Walisema Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Bw. Ismail Jussa Ladhu, amekuwa akitumia madaraka yake vibaya na kukiuka katiba ya chama hicho jambo ambalo limekuwa kilichangia kuwepo matakaba kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika tamko lao, wanafunzi hao walidai kuchoshwa na tabia za viongozi wa chama kuingiza udini kwa kuwabagua Wakristo na Waislamu na kujenga ukuta kati ya Wazanzibari na wenzao wa bara jambo ambalo ni kinyume na katiba yao.
Posted: 11 Mar 2012 11:49 PM PDT
Maelfu ya wanachama na wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) wakiwa wamejaa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) kumpokea Mwenyekiti wao Profesa Ibrahim Lipumba aliyewasili jana alasiri akitokea Marekani, picha ndogo ni Profesa Lipumba na Katibu Mkuu  wake, Maalim Seif Sharif Hamad wakisalimia wananchi. (Picha na Peter Mwenda)
Posted: 11 Mar 2012 11:30 PM PDT
*Ataka mafisadi watoswe katika chaguzi za chama hicho
Na Mwandishi Wetu, Mwanza

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Samuel Sitta, amewapa mtihani mzito wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Mwanza na mikoa mingine nchini kuweka historia katika chaguzi mbalimbali ndani ya chama hicho kwa kukisaficha chama na kuwatosa wagombea wanaotaka uongozi kwa maslahi binafsi kwani wanachangia kukishushia hadhi chama hicho.

Alisema kama mafisadi na makundi yao yatapewa nafasi za uongozi ndani ya chama, watajuta kupoteza nafasi muhimu ambazo zinapaswa kufanyiwa mabadiliko ya kihistoria na watakuwa wameshiriki kuisaliti CCM na kuiweka pabaya chaguzi zijazo.

Bw. Sitta aliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara ambao ulihudhuriwa na maelfu ya wana CCM pamoja na waananchi katika Uwanja wa Magomeni, uliopo Kata ya Kilumba, jijini Mwanza.

Alisema njia pekee ya kuinusuru CCM ni wanachama kuhakikisha wanachagua viongozi waadilifu kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa.

Aliongeza kuwa, wananchi wengi bado wana imani na chama hicho lakini wanalalamikia mwenendo wa baadhi ya viongozi hivyo uchaguzi wa mwaka huu lazima uwe wa kihistoria.

“Hii ndio fursa ya kukinga’risha chama chaetu, wana CCM tumieni uchaguzi huu kuchagua viongozi wanaopinga aina zote za ubaguzi ukiwemo wa kipato, tuchague viongzoi wenye huruma na wanaotetea wanyonge ambao ndio wengi.

“Tusipofanya hivyo na kuwaachia wenye uchu na matajiri, tutakuwa hatujaitendea haki imani yetu, itikadi yetu na misingi yetu, tuweke historia katika uchaguzi huu kwa kuwaenzi waasisi wetu wa Taifa.

“Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alituachia msingi wa CCM kutetea wanyonge na huu umedhihirika, tumekuwa wakombozi hadi nje ya nchi, ukombozi huo ndio aliomnfanya Mzee wetu Karume kuwajengea maghorofa wanyonge hivyo lazima turudi katika misingi hiyo,” alisema Bw. Sitta.

Bw. Sitta ambaye alialikwa na Kamati ya Siasa Wilaya ya Ilemela na Kata ya Kirumba kuzindua kampeni za kumnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, alisema CCM imekuwa ikilaumiwa na Watanzania kwa kupoteza uelekeo, kushindwa kuendeleza sera na itikadi iliyomo ndani ya katiba yake.

“Imani yetu rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa, huu ndio wakati wa kurudisha chama chetu katika njia yake na kusafisha vumbi la kila aina ili CCM ing'ae mbele ya jamii, tusipofanya hivyo, tutakua hatukitakii mema,” alisema.

Akimnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, Bw. Jackson Robert, maarufu kama 'Masamaki', Bw. Sitta alisema mgombea huyo anastahili kuchaguliwa kutokana na uadilifu na msimamo wake thabiti katika kusimamia sera za CCM.

Alisema ushindi alioupata wa asilimia 70 ndani ya chama hicho ni dalili ya ushindi wake katika uchaguzi huo.

Bw. Robert atachuana wagombea wengine wa vyama mbalimbali huku mpinzani wake mkuu akitarajiwa kutoka chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Posted: 11 Mar 2012 11:28 PM PDT
Pamela Mollel na Queen Lema, Arusha

RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa, leo anatarajia kuzindua kampeni za mgombea ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, kwa tiketi Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Sioi Sumari.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa CCM mkoani hapa, Bi. Mary Chatanda, alisema kampeni hizo zitahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.

Alisema uzinduzi huo utakuwa tofauti na vyama vingine vya siasa ambavyo vinakodisha watu kutoka nje ya jimbo hilo.

“Tutazindua kampeni kwa kishindo ili kuwapa wananchi fursa ya kuona jinsi tulivyojipanga kushinda, kampeni zetu zitafunguliwa na Rais mstaafu, Bw. Benjamin Mkapa na viongozi wengine wa kitaifa watakuwepo ila tumeojipanga kupambana,” alisema Bi. Chatanda.

Katika hatua nyingine, Bi. Chatanda alisema wananchi wanapaswa kutokubali kudanganywa na aina yoyote ya propaganda kuhusu madai ya mgawanyiko wa wanachama ndani ya CCM.

Alisema wanachama wote wapo katika kundi moja jambo ambalo linawapa matumaini ya ushindi. Akizungumzia pingamizi lilowekwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), dhidi ya mgombea wao, Bi. Chatanda alisema pingamizi hilo limefutwa.

Bw. Sumari alikuwa amewekewa pingamizi na CHADEMA kwa madai kuwa hajawahi kukana uraia wa nje.
Posted: 11 Mar 2012 11:24 PM PDT
FEBRUARI 2009, Rais Jakaya Kikwete alimvua madaraka na kumfukuza kazi aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera, Bw. Albert Mnali, kutokana na kitendo cha kuwacharaza bakora walimu wa shule za msingi wilayani humo.

Hatua hiyo ilitokana na Bw. Mnali kufanya kitendo cha udhalilishaji kisichokubalika katika jamii na kuwavunja moyo walimu.

Bw. Mnali aliamrisha polisi kuwacharaza viboko walimu ambao aliamini wao ndio wamechangia wanafunzi wa shule za msingi wilayani humo kufeli mitihani.

Tukiachana na hilo, wachambuzi wa mambo ya uchumi wanasema ufadhili unaotolewa na wahisani kutoka mataifa mbalimbali duniani una faida na madhara yake.

Mwishoni mwa wiki, gazeti moja linalotoka kila siku liliandika habari inayosema “Mholanzi amchapa vibao Mwalimu Mkuu”. Tukio hili lilitokea katika Shule ya Msingi Marera, iliyopo Kata ya Rhotia, Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha.

Mashuhuda wa tukio hilo wanadai kuwa, raia wa Uholanzi, Bi. Marise Koch, ambaye ndiye mfadhili wa shule hiyo kwa kukarabati majengo ya shule, ofisi, nyumba ya walimu na kutoa kompyuta ndogo 'Laptop', alimdhalilisha Mwalimu Mkuu Bw. Emmanuel Ginwe kwa kumpiga vibao mbele ya wanafunzi, walimu wenzake.

Tukio hilo limeripotiwa katika Kituo cha Polisi Karatu na kufunguliwa jalada namba KRT/RB/835/2012. Bi. Koch aliwakuta walimu wa shule hiyo wakipanga ratiba ya shule na kuhoji kwanini hawajaingia darasani.

Walimu hao walijibu tayari wanafunzi wamepewa kazi za kufanya lakini majibu hayo hayakumridhisha. Aliamua kwenda ofisini kwa Bw. Ginwe na kudai yeye anafadhili vitu vingi lakini walimu hawafundishi, kuanza kukusanya kopyuta alizotoa kama msaada shuleni hapo lakini Mwalimu Mkuu alimsihi asifanye hivyo.

Baada ya Bi. Koch kuona anazuiwa, alimpiga Bw. Ginwe vibao na kuendelea kuzikusanya kitendo ambacho kiliwashtua walimu na wanafunzi walioshuhudia tukio hilo.

Sisi tunasema kuwa, tukio hili halikubaliki kwani dhana ya ufadhili si kunyanyasa watu wanaopewa misaada na kuingiza mambo yao katika mitaala ya elimu nchini.

Kimsingi, kilichofanywa na Bi. Koch ni kosa kisheria hivyo tunaliomba Jeshi la Polisi wilayani Karatu, lichukue hatua stahiki za kuhakikisha mfadhili huyo anafikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Matatizo yaliyopo katika sekta ya elimu na nyinginezo si kigezo cha kuwafanya Watanzania wanyanyasike na kudhalilishwa ndani ya nchi yao. Tumechoka na manyanyaso ya aina hii, tunataka sheria imuadhibu Bi. Koch kama ilivyofanya kwa Bw. Mnari ambaye alifukuzwa kazi kwa kosa la kudharirisha walimu.

Kama Serikali itashindwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya mfadhili huyu, upo uwezekano wa kukwamisha maendeleo ya elimu shuleni hapo kutokana na ukweli kwamba, walimu katika shule husika hawatakuwa na imani na serikali yao kwa sababu haijawali.
Posted: 11 Mar 2012 11:22 PM PDT
Na Pendo Mtibuche, Dodoma
SERIKALI mkoani Dodoma imesema suala la upandaji holela huduma za matibabu ya afya chini ya mifuko ya  afya ya jamii NHIF na CHF limekuwa likiathiri utendaji wa mifuko hiyo.

Hali hiyo imedaiwa kutokana na wauzaji wa dawa na watoa huduma kubadilisha
bei ya dawa wanavyotaka na kwa wakati wowote.

Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt.Rehema Nchimbi wakati akifungua kongamano la siku moja la wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Dodoma.

Alisema, sekta hiyo ya afya imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ambazo ambazo zimekuwa kuongeza malalamiko mengi kuhusu ukosefu wa dawa katika vituo vingi vya Serikali na hasa vilivyopo ndani ya Manispaa ya Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.

Alisema, kutokana na suala hilo kuwa nyeti basi ipo haja ya Serikali
kulitazama kwa makini suala hilo na kulitafutia ufumbuzi.

Mbali na changamoto hiyo ya kupanda kwa bei ya matibabu, lakini pia Mkuu huyo wa mkoa alibainisha kuwa  pia kumekuwepo na vituo vya afya ambavyo  vina uhaba wa watoa huduma wenye sifa hasa vijijini, hivyo suala hilo linasababisha utoaji huduma hafifu zisizokidhi kiwango kinachotakiwa kwa wanachama.

Alisema, hali ya afya katika Mkoa wa Dodoma inahitaji kufanyiwa tathimini ya uhakika ili kuona ni njia zipi zitakazoinua mifuko hiyo miwili ya afya ya jamii yaani NHIF na CHF ili iweze kufanya vizuri.
Posted: 11 Mar 2012 10:59 PM PDT
Na Mkwasi Issa, Pemba
ZAIDI ya miche 15,000 ya mikarafuu inatarajiwa kutolewa kwa wakulima kisiwani Pemba katika kipindi cha mvua za msimu wa masika ambazo zinatarajiwa kuanza kunyesha visiwani humo mwaka huu.

Ofisa wa Mashamba ya Serikali kisiwani Pemba, Bi.Asha Saleh Mbarouk aliyaeleza hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kuhusiana na mikakati ya Serikali ya kuimarisha zao la karafuu katika msimu huu.

Alisema kuwa, ni vema wakulima kuanza kuyatayarisha mashamba yao mapema kabla ya mvua za masika hazijaanza ili kujiweka tayari kwa ajili ya kupanda mikarafuu mipya.

Bi. Mbarouk alisema, kila mkulima anayehitaji kupatiwa miche ya mikarafuu anatakiwa kujaza fomu ambazo zinapatikana kwa maofisa wa kilimo kwa kila shehia, fomu amabazo zitamuwezesha kupatiwa miche hiyo.

Aidha, alisema miche hiyo inapatikana vitalu vilivyoko Weni katika Wilaya  ya Wete, Kicha kwa wilaya ya Micheweni, Kigope Wilaya ya Mkoani pamoja na Kitalu Wilaya ya Chake.

Hata hivyo Ofisa huyo aliwataka wakulima kuwa tayari kwenda kuchukuwa na kujaza fomu ambapo kwa sasa watendaji wa kilimo wameanza kukagua na kupima mashamba operesheni ambayo kwa sasa inaendelea katika shehia ya Mtambwe Kaskazini.
Posted: 11 Mar 2012 10:57 PM PDT
Na Theresia Victor, Dodoma
MHANDISI Deogratius Assey ambaye amejitokeza katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya ubunge, Bunge la Afrika Mashariki (EAC) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema tayari amerejesha fomu katika ofisi ya chama hicho mkoani Dodoma kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo.

Akizumgumza na Majira baada ya kurudisha fomu hiyo jana, Bw. Assey alisema, alilazimika kuingia katika ushindani huo kwa ajili ya kutaka kutetea maslahi ya vijana kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Bw. Assey alisema, pamoja na kuwepo kwa sera za kuwepo kwa jumuiya hiyo lakini bado haijapata mtu madhubuti ambaye yupo tayari kwa ajili ya kuwatetea na kuwapiagania vijana kuingia katika ushindani wa ajira kupitia EAC.

Alisema, alilazimika kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kwani alikuwa hajiamini kuwa kama angeweza kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi kwa kumuunga mkono kama ambavyo kwa sasa mambo yamekuwa mazuri kwa kupata ushirikianao wa kutosha.

“Lakini cha kushangaza nimeungwa mkono na wanacha wote wa Chadema na hata wale wasiyo kuwa wanachama, hata hivyo wamenichangia hata gharama za kulipia fomu ambayo ilikuwa inagharimu shilingi laki moja...lakini wamenichangia,”alisema Bw.Assey.

Aliongeza kuwa, ikiwa atafanikiwa kuipata nafasi hiyo atahakikisha kuwa vijana wanatetewa zaidi katika masuala ya ajira tofauti na ilivyo sasa ambapo Watanzania bado hawajaweza kunufaika na suala zima la ajira kwa vijana katika jumuiya.

Aidha, kwa upande wake Katibu wa Mkoa wa Dodoma CHADEMA, Bw. Stivine Masawe alisema, ameipokea fomu ya mgombea huyo na kusema kuwa haina makosa yoyote na hivyo iko sawa na ataiwasilisha Makao Makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo jijini Dar es Salaam.

Bw. Masawe alisema, kujitokeza kwa Mhandisi Assey ambaye ni kijana na mwanachama hai katika chama hicho ni fursa pekee kwa vijana kutatuliwa matatizo yao kama atapata nafasi ya kuchukua nafasi hiyo ya ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Posted: 11 Mar 2012 10:50 PM PDT
Kiungo wa timu ya Simba, Patrick Mafisango (kulia) akijaribu kuwatoka mabeki wa Toto African ya Mwanza wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.(Picha na Michael Machellah)
Posted: 11 Mar 2012 10:49 PM PDT
*Wadaiwa kumpiga mtoto, mechi yao yaingiza mil. 73/-
Na Zahoro Mlanzi
WACHEZAJI wa Yanga Nurdin Bakari, Athuman Idd 'Chuji' na Jerryson Tegete, wanadaiwa kumpiga mtoto anayeishi Mtaa wa Faru na Swahili, Kariakoo, Dar es Salaam na kumsababishia maumivu.
Tukio hilo lilitokea juzi usiku baada ya mtoto huyo kuwazomea kutokana na kipigo cha bao 3-1 dhidi ya Azam FC ambapo gari la Yanga lililokuwa limebeba wachezaji,  lilisimama na wachezaji hao kwenda kumpiga mtoto huyo ngumi na mateka.

Kwa mujibu wa shuhuda aliyekuwepo eneo la tukio (jina tunalo),  alisema “ Baada ya mtoto huyu kuwazomea, Chuji, Nurdin na Tegete walishuka kwenye gari la kumuadhibu, walipomaliza kiu yao walirudi katika basi lao na kuondoka,” alidai mtoa habari huyo.
Alidai kuwa, walipokwenda kumuangalia mtoto huyo walimkuta katika hali mbaya huku mwili wake ukiwa na majeraha.

Vyanzo mbalimbali vya kuaminika vilidai kuwa, mtoto huyo alikimbizwa hospitali kutokana na hali yake kuwa mbaya.

Alipotafutwa kwa njia ya simu ili aweze kuzungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda Mkoa wa Kipolisi Ilala, Saada Juma, alisema hana  taarifa zozote kwani hadi anaondoka ofisini juzi saa 1:30 usiku, hakuna mtu aliyetoa taarifa ya tukio hilo.

“Leo (jana) Ma-OCD wangu walikuwa wakinipa taarifa za mara kwa mara kuhusiana na tukio la kuwasili kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Ibrahim Lipumba lakini taarifa za kupigwa mtoto hadi akafariki dunia au kukamatwa kwa wachezaji wa Yanga hilo sijalipata,” alisema Kamanda Juma.

“Kama lipo nadhani nitapata taarifa ila kinachonishangaza, tutaanzaje kupaata taarifa za kifo kabla ya kuumizwa mtoto husika kwani hizo ndio zingesaidia kupata majibu ya uhakika kwa hicho unachonieleza lakini siwezi kusema uongo ila ukweli ni kwamba sina taarifa na hilo,” alisema.

Majira halikuishia hapo pia lilimtafuta Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llody Nchunga ambaye alisema hana taarifa za wachezaji wake kufanya fujo, kukamatwa au kufa kwa mtoto huyo.

“Sijui kama hilo tukio lina ukweli, ninachokiamini mimi ni kwamba, wachezaji wote walirudi klabuni na leo (jana) asubuhi, nilikwenda kuzungumza nao tukaamua kuwapa siku moja ya mapumziko hivyo wamekwenda majumbani kwao,” alisema Nchunga.

Alisema kama tukio hilo lilifanyika, labda ni baada ya kurudi klabuni na baadhi yao kutoka tena kwenda mitaani kufanya fujo lakini walipotoka uwanjani, warurudi klabuni.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu timu hiyo, Kostadin Papic atawachukulia hatua wachezaji wote waliomfanyia fujo mwamuzi  Israel Mujuni kutoka Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Papic alisema kitendo kilichofanywa na wachezaji wake hakikuwa kizuri na utovu wa nidhamu hivyo atahakikisha anawachukulia hatua.
Wakati huo huo, mchezo kati ya Yanga na Azam umeingiza sh. milioni 72,731,000.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari Dar es Salaam na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema watazamaji 19,339 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 3,000 viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B wakati kwa VIP A ilikuwa sh. 15,000.

Sunday, March 11, 2012

RC awashukia watendaji wenye majungu ofisini

Posted: 08 Mar 2012 10:51 PM PST
Na Charles Mwakipesile, Mbarali
MKUU wa Mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro, amewataka watumishi wenye tabia ya kuwasema wenzao ofisini 'majungu', kuacha mara moja ambapo watakaobainika kuwa na tabia hiyo, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Bw. Kandoro aliyasema hayo juzi katika hafla ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri Wilaya ya Mbaarali, mkoani hapa Bw. George Kagomba.

Hafla hiyo ilifanuyika katika Makao Makuu ya halmashauri hiyo baada ya kustaafu utumishi wa umma na kuongeza kuwa, siri ya mafanikio kwa mtendaji yeyote wa Serikali ni kuchapa kazi kwa bidii, kuepuka majungu.

Alisema kitendo cha kuwagawa wafanyakazi kinakwamisha maendeleo ya wannchi na utekelezaji wa shughuli za Serikali.

“Kiongozi ambaye leo tunamuaga, amefanya kazi kwa bidii na kufanikiwa kuleta mabadiliko makubwa, kufyeka kichaka porini na kujenga Makao Makuu ya Halmashauri.

“Bw. Kagomba ni kielelezo cha watendaji bora wa serikali wasio na majungu  ambaye amewaunganisha wafanyakazi kuwa kitu kimoja na kuharakisha maendeleo,” alisema.


Alisema watendaji wa Serikali ambao wanaendeleza majungu badala ya kufanya kazi, huambulia kufukuzwa na kutokumbukwa kwa lolote walilofanya wakati wa utumishi wao serikalini.

“Sipendi kusikia Mkoa wetu unakosa maendeleo kwa sababu watumishi hutumia muda mwingi kuzungumza habari za majungu badala ya kufanya kazi kwa bidii,” alisema.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bw. Keneth Ndingo, alisema Bw. Kagomba atakumbukwa kwa mambo mengi pamoja na kujenga Makuu Makuu ya halmashauri hiyo ambayo ina majengo ya kisasa yaliyozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete.

Mbali ya kufanikisha ujenzi wa majengo hayo pia ameweza kukuza pato la halmashauri na ujenzi wa majengo ya sekondari za kata hivyo aliiomba Serikali iangalie uwezekano wa kumuongezea muda wa utumishi kwa mkataba maalumu.

Kwa upande wake, Bw. Kagomba alisema bila kupata ushirikiano kutoka kwa watumishi wengine, asingeweza kufanikisha majukumu aliyopewa ambayo yamezaa matunda.
Posted: 08 Mar 2012 10:45 PM PST
Na Zahoro Mlanzi
SERIKALI imesema mpaka kufikia mwishoni mwa Aprili mwaka huu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam utakuwa tayari umekamilika kwa asilimia 75 na utaanza kutumika kwa shughuli mbalimbali rasmi Juni, mwaka huu.

Uwanja huo awali ulitakiwa kukamilika kabla ya sherehe za miaka 50 ya Uhuru lakini mpaka kufikia Desemba 9, mwaka jana ulikuwa haujakamilika, hivyo sherehe hizo kulazimika kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Serikali ulisimamisha shughuli za uwanja huo, tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2010/2011.

Akijibu swali kuhusu uwanja huo utakamilika lini, baada ya kushindwa kukamilika kabla ya kuanza kwa sherehe za Uhuru wa miaka 50 Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Leonard Thadeo alisema ni kweli ulitakiwa kukamilika kabla ya sherehe za Uhuru, lakini kikubwa kilichokwamisha ni mkandarasi alichelewesha baadhi ya mambo muhimu.

“Hivi sasa ujenzi unaendelea kama kawaida na ninakuhakikishia mpaka kufikia mwishoni mwa Aprili, mwaka huu utakuwa umekamilika kwa asilimia 75, kwani kazi kubwa iliyobaki ni kuweka viti katika jukwaa mbalimbali zilizojengwa,” alisema Thadeo.

Alisema wakati maboresho hayo yakiendelea kwa kuhakikisha viti vinawekwa na mambo mengine, mpaka kufikia Juni mwaka huu ana imani kila kitu kitakuwa kimekamilika na shughuli mbalimbali zilizokuwa zikifanyika katika uwanja zitaendelea kama kawaida.

Thadeo alisema kukamilika kwa uwanja huo kutapunguza matumizi ya Uwanja wa Taifa, kwani mechi zitakazokuwa si za lazima kuchezewa kwenye uwanja huo, zitafanyika Uwanja wa Uhuru kama ilivyokuwa hapo awali.

Pia alitoa wito kwa mashabiki na wanamichezo kwa ujumla kuhakikisha kuutumia vizuri uwanja huo, pindi utakapokamilika ili kuepusha madhara yatakayoweza kujitokeza kama ilivyokuwa katika mechi ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba na Kiyovu ya Rwanda.

Katika mechi hiyo ya Simba, viti 152 viliharibiwa na 11 vilivunjwa kutokana na mashabiki hao kuvunja na kurushiana wakati mechi hiyo ikiwa mapumziko.