Na Lydia Churi- MAELEZO  
Bagamoyo –PWANI.  
WATANZANIA  wametakiwa kutowapa nafasi watu wanaopotosha mchakato wa kupata Katiba  mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bali washiriki mchakato huo kwa  amani na utulivu.  
Akizungumza  na Vijana wa Chama cha Mapinduzi wa wilaya ya Bagamoyo leo Waziri wa  Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanuel  Nchimbi  amesema kuwa Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya  Kikwete ana nia njema ya kuhakikisha kuwa watanzania wanapata katiba mpya baada ya kutimiza miaka 50 ya uhuru wa nchi yao.  
Amesema  taarifa zinazotolewa na serikali juu ya kuanza kwa mchakato wa katiba  mpya ni za dhati na serikali ina nia njema katika hili hivyo wananchi  hawana budi kuwapuuza wale wanaopotosha taarifa hizo.  
Waziri  Nchimbi  amesema hayo wakati wa  uzinduzi wa  Mnara  wa kumbukumbu ya mkutano wa kwanza wa TANU kitaifa uliofanywa na Baba  wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika harakati za  kupigania uhuru wa Tanganyika mwaka 1954.  
 Amewaasa  vijana kuwa Mnara huo usibaki kuwa kumbukumbu tu bali  wayafanyie  kazi yote yaliyofanywa na waliowatangulia.  
Amewataka  vijana kudumisha amani na utulivu uliopo nchini kwa faida ya vizazi  vijavyo na kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa Tanzania bara kwa  kutathmini kazi zilizofanywa na waanzilishi ili waweze kuwarithisha  watoto wao baadaye.   
Naye Katibu mkuu wa UVCCM Taifa, Martin Shigella akizungumza wakati wa uzinduzi huo amewataka  vijana wa CCM kuwa na moyo wa kujitolea ili waweze kuliletea taifa  maendeleo.  
No comments:
Post a Comment