TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Monday, September 8, 2014

MWANAHARAKATI KHADIJA LIGANGA ATOA SEMINA YA UNYANYASAJI WA KIJINSIA NA UKATILI DHIDI YA WATOTO KWA VIJANA ZAIDI YA 100 JIJINI MWANZA

Mwanaharakati toka Shirika la Kutetea Haki za Wanawake la KIVULINI la jijini Mwanza, Bi. Khadija Liganga ametoa mafunzo ya siku moja kuhusu Unyanyasaji wa kijinsia na ukatili Dhidi ya watoto kwa vijana takribani 100 wa jiji la Mwanza ikiwa ni hatua za kuwajenga vijana katika misingi ya kuachana na mila, tamaduni na dhana potofu zinazowakandamiza wanawake na watoto katika jamii.

Semina hiyo iliyoandaliwa na Teen Club Mwanza, ililenga Kujenga uwezo wa kutambua ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, kuelewesha na kutoa njia za namna ya kuripoti unyanyasaji na ukatili na kuwasihi vijana kutoendeleza tabia za unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Akizungumza mara baada ya kutoa mafunzo hayo Bi. Khadija Liganga alisema ni lazima jamii ichukue jukumu la makusudi kukomesha vitendo vyote vinavyowakandamiza na kuwanyanyasa wanawake na watoto kwani ni moja ya sehemu inayochangia kwa kiasi kikubwa kuleta umasikini na kurudisha nyuma gurudumu la maendeleo kwa haraka sana.

“Mwanamke akipigwa au kutukanwa hatoweza kufanyakazi zake, mtoto akiteswa na kunyanyaswa hatoweza kusoma vizuri shuleni, huwezi pata maendeleo. Ili vijana waweze kupeleka ujumbe sahihi wa masuala ya ukatili wa kijinsia wanatakiwa kujua na kufahamu masuala yanayohusiana na tofauti za kijinsia, kulingana na suala la ukatili wa kijinsia (GBV) na namna ya kuzikemea tabia hizo” alisema Bi. Khadija.

Kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF ‘Watoto na Wanawake Tanzania’ ya mwaka 2010 inasema kuwa kuwekeza kwa watoto na wanawake ni moja ya njia bora kabisa kwa maendeleo ya Tanzania. Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012 inaonesha Zaidi ya asilimia 50 ni watoto, ubunifu wao na umahiri wao katika kuzalisha ndio msingi mkubwa wa kufikia malengo ya Tanzania 2025.

Bi. Khadija aliendelea kusema kuwa bado katika jamii nyingi watoto hukatazwa kusema hadharani kwamba wananyanyaswa, mila nyengine watoto hawastahili kuzizungumzia, hivyo hivyo mwanamke anaona aibu au anaogopa kuzungumzia suala la ukatili wakati mwanaume anaweza kufanya kisema mbele za watu na wakati mwingine kwa kujidai /kujigamba amempiga mkewe. Hivyo basi ushiriki wa wa vijana ni muhimu sana kuelimishwa ili kujenga familia na jamii salama isiyo na ukatili Dhidi ya wanawake na watoto.

“Ni swali la kujiuliza kama sisi watu wazima tumeshindwa kujenga miji iliyo salama, kwanini tusiwekeza nguvu nyingi kwa hawa vijana, waswahili husema ‘ashakum si matusi’ni ngumu kumfundisha mbwa mzee mbinu mpya, hivyo naomba serikali, vyombo vya habari, mashirika ya kijamii, wazazi, pamoja na wanaharakati kuwekeza katika kuwapa kundi hili la vijana elimu ya ukatili wa kijinsia na haki za watoto ili kujenga kizazi bora” alimalizia kwa kusema Bi. Khadija.

Ripoti ya “Ukatili Dhidi ya Watoto Tanzania” ya UNICEF 2011, inasema kuwa karibu wasichana 3 kati ya 10 na mvulana 1 kati ya 7 wameripoti kutendewa walau tukio moja la ukatiliwa kijinsia kabla ya kutimiza umri wa miaka 18. Huku karibu asilimia 6 ya wasichana wamelazimishwa kujamiiana kabla hawajatimiza miaka 18. Marafiki, majirani, na watu wasiowafahamu walitajwa na wasichana na wavulana kama wakosaji wa ukatili wa kijinsia.
Kundi la vijana Zaidi ya 100 toka katika klabu ya Vijana (Teen Club) jijini Mwanza wakisikiliza kwa makini mafunzo toka kwa Bi. Khadija Liganga ya jinsi gani wanaweza kukabiliana na Unyanyasaji na Ukatili wa kijinsia lakini pia jinsi ya kuripoti matukio mbalimbali ya ukatili katika vyombo husika.
Bi. Khadija Liganga, Mwanaharakati wa kupigania Haki za Wanawake wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake KIVULINI akitoa semina ya siku moja kuhusu unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto kwa vijana Zaidi ya 100 kutoka klabu ya vijana (Teen Club) ya jijini Mwanza.

No comments:

Post a Comment