TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Thursday, November 12, 2015

MAKABIDHIANO YA TAARIFA RASMI IKULU.





 
MAKABIDHIANO YA TAARIFA RASMI IKULU.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, leo katika Ikulu ya Dar es Salaam amepokea taarifa rasmi ya makabidhiano ya Ofisi kutoka kwa Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo mchana  na kushuhudiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue  na Maafisa wa  Ofisi Binafsi ya Rais.

Utaratibu wa kukabidhiana Ofisi katika Ofisi Kuu hapa nchini ni jambo la kawaida na hivyo imebidi  makabidhiano hayo  kati ya Rais anayeondoka na anaye ingia madarakani kufanyika.

“Umeanza vizuri, baki na msimamo huo huo utasaidia sana wananchi” .  Mhe. Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne amemueleza Mhe. Rais Magufuli wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano.

Mhe. Rais Mstaafu amekabidhi taarifa rasmi yenye kurasa 53, ambayo kwa ujumla inaelezea kazi zilizokwisha kufanyika, ambazo zinasubiri kukamilika na zile ambazo zinasubiri maamuzi ya utekelezaji. Mengine ni  hali halisi ya nchi katika nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Mhe. Rais Dkt. Magufuli amemshukuru Rais Mstaafu  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi  kwa muongozo wake siku zote .“Nikushukuru kwa kuiacha nchi salama na itaendelea kuwa salama, nikushukuru kwa muongozo wako, na  taarifa ya muelekeo na ninaahidi kuwa Hapa ni Kazi Tu”. 

 Mhe. Rais amesema na kumueleza Rais Mstaafu kuwa ametengeneza mazingira mazuri ambayo nchi nyingi zimeshindwa kufanya na hivyo basi kuahidi kuendelea kuchota hekima na busara kwa Marais wote wastaafu wakiwemo Mhe. Benjamin William Mkapa wa Awamu ya Tatu na Mzee Ally Hassan Mwinyi wa Awamu ya pili.

Wakati huo huo Mhe. Rais Magufuli ameendelea kupokea salamu za pongezi kutoka Kwa  Msimamizi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bibi Helen Clark.

“Chini ya uongozi wako, tunatarajia kuzidi kuimarisha ushirikiano baina yetu, demokrasia, kushughulikia masuala ya umaskini na ajira kwa vijana , kukuza uchumi,  na kulinda na kuhifadhi mazingira, masuala ambayo Tanzania na UNDP tumekuwatukishirikiana kuyaendeleza na kuyatimiza”  amesema Bi Clark.

Salamu zingine ni kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Uswiss, Mhe. Simonetta Sommaruga, Rais wa Jamhuri ya Italia Mhe. Sergio Mattarella, Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mhe. Joachim Gauck na pia kutoka kwa Rais wa Finland Mhe. Sauli Niinisto.

Pongezi zingine zimetoka kwa Rais wa Jamhuri ya Urusi, Mhe. Vladimir Putin, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhe. Salva Kiir Mayardit, Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe. Park Geun-hye na kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. XI Jinping.

Salamu  pia zimemfikia Mhe. Rais Dkt. Magufuli kutoka kwa Rais wa Taifa la Eritrea Mhe. Isaias Afwerki na kutoka kwa Rais wa Ufaransa Mhe. Francois Hollande.Katika ujumbe wao, viongozi hao mbali na kumpongeza Mhe. Rais Dkt.  Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  wamesisitiza kuendeleza na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi zao.

Pia wameipongeza Tanzania kwa kudumisha demokrasia imara na Watanzania kwa ujumla kwa kuimarisha amani na utulivu wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi.
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

No comments:

Post a Comment