NIKO TAYARI KUKAMATWA, MAALIM SEIF
By Hassan Ali, Mwananchi, Mwananchi Zanzibar.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema yuko tayari kukamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka, kama kitendo chake cha kujitangazia ushindi ni kosa.
Maalim Seif alikuwa akizungumza na viongozi wa majimbo, makatibu wa matawi, wajumbe wa mkutano mkuu, wajumbe wa kamati za utendaji za ngazi zote na watendaji wa chama hicho.
Alisema haoni hatua yake ya kuitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imtangaze kuwa mshindi haina matatizo kwa kuwa ana uhakika kuwa ndiye aliyeshinda kwenye uchaguzi.
“Nilichosema ni ZEC initangaze kwa kuwa nilishinda uchaguzi. Je, hapo kuna ubaya gani ati? Nishitakini basi, nasema niko tayari, nishtakini. Nitakuja mahakamani kujitetea, mnamtisha nani! Mnamtisha nani hapa?” alihoji.
Maalim Seif aliwania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akichuana vikali na mgombea wa CCM, Dk Mohamed Shein.
Hadi sasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) haijamtangaza mshindi na badala yake imefuta matokeo ya kura za nafasi hiyo pamoja na za uchaguzi wa wawakilishi, ikisema uchaguzi utarudiwa tena ndani ya siku 90.
Hata hivyo, CUF imepinga ikitaka ZEC imtangaze mshindi kwa madai kuwa chama hicho ndicho kilichoibuka na ushindi.
Maalim Seif, ambaye ameshagombea urais wa Zanzibar mara tano, alirudia wito wake wa kuitaka ZEC imtangaze kuwa mshindi ili aapishwe na kuanza kazi, ikidai anataka kuanza kuijenga upya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment