Alisema endapo utaratibu na juhudi hizo zitajengewa mipango madhubuti kizazi hicho kitachipua vyema na kuwa tayari kumpenda, kumuelewa ipasavyo pamoja na kumtukuza Muokozi wao huyo Nabii Muhammad { SAW }.
Al Hajj Ali Hassan Mwinyi alisema hayo wakati wa sherehe za Maulidi ya Kuzaliwa Mtume Muhammad {SAW }yaliyoandaliwa na Uongozi wa Kiwanda cha Nguo cha Nida {NIDA TEXTILE} na kufanyika katika Mtaa wa Indira Ghandhi Mjini Dar es salaam.
Alisema waumini wa Kiislamu wakati huu wa sasa wanapaswa kujikita zaidi katika kushughulikia Dini yao hasa katika utekelezaji wa maamrisho yote yalioagizwa katika Kitabu chao kitukufu kwa lengo la kupata mafanikio ya milele.
Rais Mstaafu wa Tanzania alieleza kwamba katika kipindi hichi cha mabadiliko ya utandawazi yaliyozikumba jamii nyingi duniani Wazazi wana kazi kubwa ya kuwafunza Watoto wao mwenendo aliokuwa nao Mtume Muhammad {SAW } hasa suala zima la uadilifu ambalo kwa sasa linaonekana kupotea kwa nguvu kubwa ndani ya Jamii.
Alisema Watoto washirikishwe ipasavyo katika kufundishwa dini itakayokuwa dira ya kuzoeshwa nyoyo zao jambo ambalo litakuwa ishara ya mazoezi ya roho ikiwa ni sehemu ya utaratibu utakaowaongoza katika maisha yao ya kila siku.
Aliupongeza na kuushukuru Uongozi wa Kiwanda cha Nguo cha Nida {NIDA TEXTILE} kwa uamauzi wake wa makusudi wa kuandaa sherehe hiyo ya Maulidi jambao ambalo huleta Baraka na kheir ndani ya maisha ya kila siku ya Jamii.
Akitoa salamu kwenye hafla hiyo ya Maulidi ya Kuzaliwa Mtume Muhammad {SAW } Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balosi Seif aliwakumbusha Waumini wa Dini ya Kiislamu juu ya wajibu wao wanaotakiwa kuutimiza wa kuzitukuza ishara na alama zote za Dini ya Kislamu ukiwemo uwepo wa utukufu wa Mtume Muhammad { SAW } ili kufikia daraja kubwa ya ucha Mungu.
Balozi Seif aliwaomba waislamu katika mikusanyiko yao ya kheir ukiwemo huu mkubwa wa hafla za maulidi ya uzawa wa Kiongozi wao wajielekeze kuhimizana zaidi juu ya umuhimu wa kutunza amani na Utulivu wa Nchi ili upendo uliopo miongoni mwa Jamii ya Watanzania uendelee kudumu.
Alisema mizozo ndani ya Mitaa inafaa kukemewa kwa nguvu zote jambo ambalo litasaidia kuwa kinga ya kujiepusha na mifarakano inayoweza kuzaa shari na hatimae kuukaribisha uadui usiokwisha.
Naye Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Moh’d Gharib Bilal alisisitiza umuhimu wa kuyaendeleza yale yote yaliyoibuka ndani ya sherehe hizo yaliyofanywa na Vijana kama usomaji wa Quran na Maulidi ili kuwajengea msingi mwema watoto hao.
Dr. Bilal alisema uendelezaji huo kwa kiasi kikubwa utakuwa dira kwa waumini hao kutekeleza wajibu wao wa kudumisha mazuri kwa kuwarithisha watoto wao mambo ambayo yamesisitizwa sana hata katika Kitabu cha Quran na Hadithi za Mtume Muhammad { SAW }.
Mapema akitoa nasaha kwa waumini waliohudhuria Sherehe hiyo ya Maulidi ya Uzawa wa Nabii Muhammad {SAW } Sheikh Juma Sadiq kutoka Kigamboni alisema kufurahia Uzawa wa Kiongozi huyo ni wajibu kwa Kila Muumini wa Dini ya Kiislamu.
Sheikh Juma Sadiq alieleza kwamba si vyema ndani ya Umma wa Kiislamu wakatokea mabaghili wa kupinga au kujiepusha na jambo hili muhimu linalotekelezwa na hata malaika wa mwenyezi Muungu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/1/2016.
========================================================================
No comments:
Post a Comment