|
|
|
|
|
|
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Januari 18, 2016) wakati akizungumza
na baadhi ya Watanzania waishio Botswana kwenye kikao kilichofanyika kwenye
kituo cha mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.
Waziri Mkuu alikuwa nchini Botswana kwa ziara ya siku moja kumwakilisha Rais
Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa SADC Double Troika yaani kikao
maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC Summit) na Wakuu wa Nchi wanaounda
Chombo cha Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ on Politics,
Defense and Security Cooperation) uliofanyika kwenye kituo cha mikutano ya
kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.
Akizingumza na Watanzania hao, Waziri Mkuu alisema: “Tumeamua kufungua
viwanda vya kusindika ngozi kwenye mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam
(kule Pugu) ili ngozi zikishachunwa, zipelekwe moja kwa moja kiwandani,”
alisema.
Alisema Serikali imeamua kuongeza viwanda nchini kama njia mojawapo ya kukuza
uchumi, kuacha kuuza mali ghafi lakini pia ni fursa ya kuongeza ajira kwa
Watanzania.
Akijibu hoja
zilizoainishwa kwenye risala yao, Waziri Mkuu alisema Serikali bado ina nia
ya kuhamia Dodoma na kwamba itaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara nyingi
zijenge ofisi zao Dodoma. “Serikali ilikwishaamua kwamba Dodoma ni mji wa
kiserikali na Dar es Salaam ni mji wa kibiashara. Kwa sasa kuna baadhi ya
Wizara zimeshajenga ofisi Dodoma na kuna taasisi kama vile Benki Kuu nazo pia
zimejenga ofisi zake Dodoma. Tutaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara
nyingine zikamilishe ujenzi wa ofisi zao,” alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania waishio
ughaibuni (Diaspora) watafute fedha za mitaji ama zao ama kupitia kwa
marafiki zao ili waweze kuwekeza nyumbani (Tanzania).
“Nia ya Serikali sasa hivi ni kufungua milango kwa wawekezaji hasa wenye nia
ya kujenga viwanda. Njooni nyumbani muone ni eneo gani mnaweza kuwekeza, kama
mna miradi huku fungueni matawi kule nyumbani. Serikali inajivunia uwepo wenu
kwa sababu inatambua kwamba huku mliko kuna kitu mnajifunza na mnaweza
kukirudisha nyumbani kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla,” alisema.
Mapema, akisoma risala yao kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Chama cha
Watanzania waishio nchini Botswana (The Association of Tanzanians in Botswana
- ATB), Bw. Neiman Kissasi alisema chama hicho kilianzishwa mwaka 1992 kikiwa
na lengo la kuwaunganisha Watanzania waishio Botswana pamoja kujenga undugu
wao na kusaidiana.
Katika risala yao, walishauri wafugaji wa Tanzania waelimishwe na kuwezeshwa
kufuga kisasa na kuondokana na ufugaji wa kurandaranda. Pia waliiomba
Serikali iongeze kasi ya mpango wake wa kuhamisha shughuli zote za Serikali
mjini Dodoma, kwani itasaidia kupunguza matumizi ya Serikali kwa kuwa
shughuli za Serikali zitakuwa zinafanyika eneo moja.
Vilevile, waliiomba Serikali ifungue fursa za kiuchumi kwenye mikoa mingine
ya Tanga, Lindi, Mtwara, Pwani, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Arusha badala ya
kuziacha ziwe Dar es Salaam peke yake. “Hii itasaidia kuibua fursa za
kiuchumi na kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam”, ilisema
sehemu ya risala yao.
Waziri Mkuu alirejea jijini Dar es Salaam jana usiku (Jumatatu, Januari 18,
2016.)
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, JANUARI 19, 2016.
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
No comments:
Post a Comment