Posted: 08 Mar 2012 10:51 PM PST
Na Charles Mwakipesile, Mbarali MKUU
wa Mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro, amewataka watumishi wenye tabia ya
kuwasema wenzao ofisini 'majungu', kuacha mara moja ambapo
watakaobainika kuwa na tabia hiyo, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa
sheria.
Bw. Kandoro aliyasema
hayo juzi katika hafla ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri
Wilaya ya Mbaarali, mkoani hapa Bw. George Kagomba.
Hafla hiyo
ilifanuyika katika Makao Makuu ya halmashauri hiyo baada ya kustaafu
utumishi wa umma na kuongeza kuwa, siri ya mafanikio kwa mtendaji yeyote
wa Serikali ni kuchapa kazi kwa bidii, kuepuka majungu.
Alisema kitendo cha kuwagawa wafanyakazi kinakwamisha maendeleo ya wannchi na utekelezaji wa shughuli za Serikali.
“Kiongozi
ambaye leo tunamuaga, amefanya kazi kwa bidii na kufanikiwa kuleta
mabadiliko makubwa, kufyeka kichaka porini na kujenga Makao Makuu ya
Halmashauri.
“Bw. Kagomba ni kielelezo cha watendaji bora wa
serikali wasio na majungu ambaye amewaunganisha wafanyakazi kuwa kitu
kimoja na kuharakisha maendeleo,” alisema.
Alisema watendaji
wa Serikali ambao wanaendeleza majungu badala ya kufanya kazi, huambulia
kufukuzwa na kutokumbukwa kwa lolote walilofanya wakati wa utumishi wao
serikalini.
“Sipendi kusikia Mkoa wetu unakosa maendeleo kwa
sababu watumishi hutumia muda mwingi kuzungumza habari za majungu badala
ya kufanya kazi kwa bidii,” alisema.
Mwenyekiti wa Halmashauri
hiyo, Bw. Keneth Ndingo, alisema Bw. Kagomba atakumbukwa kwa mambo mengi
pamoja na kujenga Makuu Makuu ya halmashauri hiyo ambayo ina majengo ya
kisasa yaliyozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete.
Mbali ya
kufanikisha ujenzi wa majengo hayo pia ameweza kukuza pato la
halmashauri na ujenzi wa majengo ya sekondari za kata hivyo aliiomba
Serikali iangalie uwezekano wa kumuongezea muda wa utumishi kwa mkataba
maalumu.
Kwa upande wake, Bw. Kagomba alisema bila kupata
ushirikiano kutoka kwa watumishi wengine, asingeweza kufanikisha
majukumu aliyopewa ambayo yamezaa matunda.
|
Posted: 08 Mar 2012 10:45 PM PST
Na Zahoro Mlanzi SERIKALI
imesema mpaka kufikia mwishoni mwa Aprili mwaka huu Uwanja wa Uhuru,
Dar es Salaam utakuwa tayari umekamilika kwa asilimia 75 na utaanza
kutumika kwa shughuli mbalimbali rasmi Juni, mwaka huu.
Uwanja
huo awali ulitakiwa kukamilika kabla ya sherehe za miaka 50 ya Uhuru
lakini mpaka kufikia Desemba 9, mwaka jana ulikuwa haujakamilika, hivyo
sherehe hizo kulazimika kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Serikali ulisimamisha shughuli za uwanja huo, tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2010/2011.
Akijibu
swali kuhusu uwanja huo utakamilika lini, baada ya kushindwa kukamilika
kabla ya kuanza kwa sherehe za Uhuru wa miaka 50 Dar es Salaam jana,
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Leonard Thadeo alisema ni
kweli ulitakiwa kukamilika kabla ya sherehe za Uhuru, lakini kikubwa
kilichokwamisha ni mkandarasi alichelewesha baadhi ya mambo muhimu.
“Hivi
sasa ujenzi unaendelea kama kawaida na ninakuhakikishia mpaka kufikia
mwishoni mwa Aprili, mwaka huu utakuwa umekamilika kwa asilimia 75,
kwani kazi kubwa iliyobaki ni kuweka viti katika jukwaa mbalimbali
zilizojengwa,” alisema Thadeo.
Alisema wakati maboresho hayo
yakiendelea kwa kuhakikisha viti vinawekwa na mambo mengine, mpaka
kufikia Juni mwaka huu ana imani kila kitu kitakuwa kimekamilika na
shughuli mbalimbali zilizokuwa zikifanyika katika uwanja zitaendelea
kama kawaida.
Thadeo alisema kukamilika kwa uwanja huo
kutapunguza matumizi ya Uwanja wa Taifa, kwani mechi zitakazokuwa si za
lazima kuchezewa kwenye uwanja huo, zitafanyika Uwanja wa Uhuru kama
ilivyokuwa hapo awali.
Pia alitoa wito kwa mashabiki na
wanamichezo kwa ujumla kuhakikisha kuutumia vizuri uwanja huo, pindi
utakapokamilika ili kuepusha madhara yatakayoweza kujitokeza kama
ilivyokuwa katika mechi ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba na Kiyovu
ya Rwanda.
Katika mechi hiyo ya Simba, viti 152 viliharibiwa na
11 vilivunjwa kutokana na mashabiki hao kuvunja na kurushiana wakati
mechi hiyo ikiwa mapumziko.
|
No comments:
Post a Comment