Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtaka Waziri wa
Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli kuhakikisha kuwa Sheria ya Usalama
Barabarani inasimamiwa vizuri ili kuhakikisha kuwa barabara zinazojengwa nchini
zinadumu kwa muda uliokusudiwa.
Akizungumza katika
eneo la Buziku mkoani Geita wakati akizindua ujenzi wa barabara ya Bwanga hadi
Biharamulo yenye urefu wa kilometa 67, Rais Kikwete alisema kuwa wizara ya
Ujenzi ni lazima ihakikishe inasimamia sheria zilizopo na hasa hii ya
kutoruhusu magari yenye uzito uliozidi viwango vilivyoainishwa katika Sheria Namba
30 ya Mwaka 1973.
Akisistiza umuhimu wa
kutunza barabara Rais Kikwete alibainisha kuwa “adui wakuu watatu wanao
sababisha barabara kuharibika mapema ni; magari yanayobeba mizigo zaidi ya
uzito uliowekwa kisheria, ujenzi duni usiozingatia viwango na kuachwa kwa maji
kuzagaa barabarani”.
Wakati huo huo Rais
Kikwete alielezea kufurahishwa kwa kuanza ujenzi wa mradi huo kwani wapo baadhi
ya watu waliokuwa waliokuwa wakieneza taarifa kuwa sehemu hiyo ya barabara
haiwezi kujengwa lakini sasa wameumbuka.
Awali
akitoa maelezo ya mradi huo Mtendaji Mkuu wa Tanroads Injinia Patrick Mfugale
alielezea kuwa mradi mradi wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami umegharimu
Shilingi bilioni 55 fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
“Mradi huu utajengwa kwa muda wa miezi 27 na hivyo kukamilika mwezi Februari
mwaka 2015” alisema Injinia Mfugale.
Naye Waziri wa Ujenzi
Mheshimiwa Magufuli alimhakikishia Rais Kikwete kuwa wizara yake itahakikisha
kuwa inamsimamia mjenzi wa mradi huo ambaye ni Kampuni ya Sinohydro Ltd. ya
kutoka Jamhuri ya Watu wa China ili aukamilishe kwa muda na viwango
vilivyokusudiwa na bila ya visingizio vya nyongeza ya gharama.
Akimpongeza Rais kwa kutekeleza ahadi yake, Waziri Magufuli alibainisha kuwa wananchi wa mikoa ya Geita na Kagera wamefurahishwa sana kuona kuwa hatimaye barabara hiyo muhimu inajengwa kwani hiyo ndiyo sehemu pekee iliyokuwa imebaki ikiwa haina lami kwa barabara inayounganisha mikoa hiyo ya ziwa.
No comments:
Post a Comment