Rais Dkt.Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakifariji familia
ya Marehemu Dkt. Sengodo Mvungi nyumbani kwao Kibamba Dar es Salaam
jana.
- SALAMU ZA RAMBIRAMBI ZAZIDI KUMIMINIKA
- MWILI WAKE KUWASILI KESHO,KUAGWA JUMAMOSI
Na Waandishi Wetu
Rais
Jakaya Kikwete, amesema ameshtushwa na kufadhaishwa na taarifa za kifo
cha Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi,
kilichotokea juzi kwenye Hospitali ya Milpark, Johannesburg, Afrika
Kusini.
Katika
salamu za rambirambi ambazo amemtumia Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji
Joseph Warioba, Rais Kikwete alisema amepokea kwa mshtuko mkubwa na
taarifa za kifo cha Dkt. Mvungi.
"Kwa
hakika ni taarifa iliyonisumbua na kunipa huzuni kubwa," alisema Dkt.
Kikwete. Rais Kikwete alisema hakuna shaka kuwa katika maisha yake Dkt.
Mvungi alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa namna
mbalimbali na kuwa kifo kimemfika wakati Taifa la Tanzania lilikuwa bado
linahitaji busara, hekima na mchango wake katika mchakato mzima wa
kusaka Katiba mpya.
"Kuanzia
alipokuwa mwandishi wa habari katika Magazeti ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ya Uhuru na Mzalendo, hadi uhadhiri wake katika Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, hadi uwakili katika Kampuni ya South Law Chambers, hadi
uongozi wake katika Chama cha NCCR-Mageuzi, hadi uamuzi wake wa kugombea
Urais wa Tanzania mwaka 2005 na sasa akiwa Mjumbe wa Tume ya Katiba,
Dkt. Mvungi ametoa mchango wake mkubwa sana katika maendeleo ya nchi
yetu. Na hili sitalisahau," alisema Rais Kikwete na kuongeza;
"Kwa
masikitiko makubwa, nakutumia wewe Jaji Joseph Warioba, Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu
nikiomboleza kifo cha Dkt. Mvungi.
“Nakupa
pole nyingi wewe Mwenyekiti, wajumbe wa Tume na wafanyakazi wote wa
Tume kwa kuondokewa na mwenzenu. Naungana nanyi kuombleza msiba huo
mkubwa.
“Kupitia
kwako, natuma pole nyingi kwa wana-familia, ndugu, marafiki na majirani
wa Dkt. Mvungi kwa kuondokewa na mhimili, msimamizi wa familia na
ndugu.
“Wajulishe
kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa. Wajulishe kuwa msiba wao ni
msiba wangu pia. Muhimu waelewe kuwa binafsi naelewa machungu yao katika
kipindi hiki kigumu na namwomba Mwenyezi Mungu awape subira waweze
kuvuka kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi yake.
Mbatia anena
Wakati
huo huo, mwili wa Dkt. Mvungi unatarajia kuwasili nchini kesho na
utapokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius
Nyerere na kisha kupelekwa nyumbani kwake Kibamba Msakuzi.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema baada ya mwili huo kuwasili
itafanyika misa takatifu katika Kanisa la Mt. Joseph saa nne asubuhi
Jumamosi.
Alisema
baada ya misa hiyo saa sita mchana mwili wake utapelekwa viwanja vya
Karimjee kwa ajili ya kuagwa na kisha kusafirisha kwenda Mwanga, mkoani
Kilimanjaro kwa ajili ya maziko.
Alisema katika kipindi hiki cha msiba bendera za chama hicho zitapepea nusu mlingoti kwa muda wa wiki moja.
Waziri Chikawe
Naye
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alisema msiba huo ni pigo
kwa taifa kwani marehemu alikuwa ni kiungo muhimu na alitumia ujuzi,
elimu na nafasi aliyonayo kwa jamii hasa katika kipindi hiki muhimu cha
mchakato wa katiba mpya.
Alisema
ni wananchi waelewe kuwa ikitokea kuyumba au kuwepo kwa pengo lolote
katika mchakato huo basi litakuwa limechangiwa na kutokuwepo kwake Dkt.
Mvungi.
Jaji Warioba amlilia
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph
Warioba, alisema Dkt. Mvungi ni mtu muhimu ambaye alikuwa na mchango
mkubwa kwenye Tume yake.
Alisema alitumia utaalam wake wa sheria na uzoefu katika kuhakikisha hoja zake alizokuwa akizitoa anazisimamia ipasavyo.
CUF yatuma rambirambi
Kwa upande wake Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kimepokea kwa mshituko na majonzi makubwa taarifa ya kifo
cha Dkt. Mvungi.
"Kifo cha Dkt.Mvungi kimeishtua Tanzania nzima hasa kwa vile tulitazamia kuwa angeishi kwa muda mrefu zaidi.
Kifo
hicho kinazidi kusikitisha kwa vile kimetokana na kushambuliwa kikatili
na watu wasiojulikana wanaodaiwa kuwa ni majambazi," ilieleza taarifa
ya CUF.
Mwenyekiti
wa Taifa wa Chama cha Wananchi CUF, mimi mwenyewe na viongozi
waandamizi wa CUF walimjua vizuri sana Marehemu Dkt. Mvungi kwani
tulifanya kazi naye kwa karibu," alieleza taarifa ya CUF iliyotolewa na
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Maalim
Seif, alisema Dkt. Mvungi alikuwa mpambanaji jasiri asiyeyumba katika
mapambano ya kuiletea Tanzania mfumo wa kidemokrasia halisi unaolenga
kulinda haki za kila Mtanzania bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile.
Alisema Dkt. Mvungi alichukia uonevu, manyanyaso, ukandamizaji na dhuluma dhidi ya binadamu yoyote.
"Tulishirikiana
naye kwa karibu katika mchakato wa kudai Katiba mpya ya Tanzania na
pale vyama vya siasa vilipounda kamati ya kufanya rasimu ya Katiba mpya
Marehemu Dkt. Mvungi ndiye aliyekuwa Mwanasheria wa Kamati hiyo.
Alitoa mchango mkubwa katika kuandaa na kukamilisha rasimu hiyo," alisema Maalim Seif na kuongeza;
"Wengi tulifarijika pale alipoteuliwa kuwa miongoni mwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.
Tulijua
uwezo wake, umahiri wake, utendaji kazi makini wake na dhamira yake ya
kuona Tanzania inapata Katiba nzuri kwa masilahi ya wananchi wote bila
kujali itikadi za vyama."
Alisema Dkt. Mvungi alikuwa ni wakili mahiri, msomi makini na kiongozi shupavu.
Alisema
alikuwa jasiri hasa katika kuwatetea wanyonge na katika kutoa mawazo
yake. Alikuwa ni mchambuzi hodari wa mambo ya kisheria, hasa sheria
inayoambatana na masuala ya Katiba.
Hali
kadhalika alikuwa mchambuzi aliyebobea katika masuala ya kijamii na ya
kisiasa na aliguswa sana na umuhimu wa kuendeleza elimu bora nchini
Tanzania.
Maalim
Seif alisema kifo chake ni pigo zito kwa familia yake, Chama cha
NCCR-Mageuzi, Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
kwa jamii nzima ya Watanzania.
"Kwa
niaba ya Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, Wajumbe wa Baraza Kuu la
Uongozi la CUF na Wanachama wote wa CUF na kwa niaba yangu mwenyewe,
tunatoa mkono wa tanzia kwa familia ya Marehemu, Mwenyekiti wa Taifa wa
NCCR-Mageuzi, Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na wafiwa wote,"
alisema.
CCM yatoa pole
Umoja
wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesikitishwa na kifo cha Dkt.
Mvungi na umeonya kuwa umaskini usifanye Watanzania kuwa chanzo cha
kuua watu wengine.
Akizungumza
Dar es Salaam jana Mkuu wa Idara ya Hamasa na Chipukizi wa UVCCM Taifa,
Paul Makonda, alisema wamepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba huo.
"Umaskini
wetu wa kipato, akili na mawazo, usiwe sababu ya kuumizana na kugharimu
maisha ya mtu kwani hata wale waliomvamia na kumjeruhi huenda
wamesukumwa na tamaa zao za kimaisha," alisema.
Polisi yanasa mwingine
Jeshi
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia mtu mmoja
anayetuhuniwa kuhusika katika tukio la mauaji ya marehemu Dkt.Sengondo
Mvungi.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Kamishna wa Polisi
Kanda, Maalum Suleiman Kova alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi
katika maeneo ya Twiga Jangwani.
Kamishina
Kova alisema kuwa; "mtuhumiwa alitambuliwa na kukamatwa kisha kuhojiwa
na Polisi na alikubali kuhusika katika tukio hilo na askari waliongozana
naye hadi nyumbani kwake Kiwalani Migombani ambapo alikutwa na silaha
ambayo ni bastola aina ya REVOLVER No.BDN 6111 pamoja na risasi 21 za
bastola hiyo ikiwa ni mali ya Dkt.Mvungi,"alisema Kova.
Pia
katika upekuzi uliofanywa na Jeshi la Polisi katika chumba cha
mtuhumiwa vilipatikana baadhi ya vifaa vya mlipuko vya aina tofauti
vikiwemo,baruti aina ya Explgel, Tambi mbili ambazo ni viwashio vya
baruti pamoja na mlipuko.
Aliongeza
kuwa mtuhumiwa alipohojiwa kuhusu umiliki wa silaha hiyo alikiri kuwa
hana kibali cha kumiliki silaha. Alisema silaha hiyo ni miongoni mwa
vitu vilivyoibwa kwa Dkt. Mvungi.
No comments:
Post a Comment