*Yadhamiria kuwasaidia wazee
wasiojiweza
Na Saidi Mkabakuli
Uongozi mpya wa Jumuiya ya Watanzania
waliosoma Korea (KAAT) wamekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi mjini Zanzibar na kutoa ombi rasmi la
kuharakishwa kwa kufunguliwa kwa Ofisi za Kibalozi nchini Korea Kusini.
Wakizungumza mara baada ya
kukaribishwa na Mhe. Balozi Iddi, Rais wa KAAT, Bw. Stephen Katemba alitoa wito
kwa Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, kufikiria kufungua ubalozi
nchi Korea Kusini kwa kuzingatia umuhimu wa nchi hiyo katika uchumi wa
Tanzania.
Bw. Katemba alisema kuwa kufunguliwa
kwa ubalozi huo kutaongeza chachu ya mahusiano ya kibiashara na kindugu baina
ya nchi hizi mbili zenye urafiki wa hali ya juu.
“Tunakosa fursa nyingi za kufanya
biashara na Korea Kusini kwani wengi wa wafanyabiashara wa Korea Kusini tuliokutana
nao nchini humo wanaona usumbufu kufuata huduma za kibalozi nje ya nchi yao,”
alisema Bw. Katemba.
Kwa mujibu wa Bw. Katemba, Korea
Kusini ina soko kubwa kwa bidhaa za Tanzania ikiwemo bidhaa za vyakula na
matunda, pia Tanzania ina fursa kubwa ya kupata ujuzi hasa kwenye eneo la
kiteknolojia na ujenzi.
Kwa upande wake Balozi Iddi, alisema
kuwa Serikali inatambua umuhimu na fursa zilizopo nchini Korea, na kuahidi
kulifanyia kazi ombi hilo.
Wakati huo huo, katika kutimiza
wajibu wa kusaidia wazee na watu wasiojiweza, uongozi mpya wa Jumuiya ya
Watanzania waliosoma Korea (KAAT) upo mbioni kufanyia matengenezo nyumba za
kukaa wazee za Sebuleni, mjini Zanzibar.
Akizungumzia mpango huo, Makamu wa
Rais, KAAT (Zanzibar), Bw. Bukheti Juma amesema “KAAT inatambua mchango mkubwa
wa wazee nchini Tanzania, hivyo katika kuhakikisha wanaishi katika mazingira
safi na salama, KAAT tutafanyia matengenezo baadhi ya majengo yaliyo kwenye
hali mbaya kituoni hapo,” alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Juma zoezi hilo
linatarajiwa kufanywa katikati ya mwezi ujao.
Baadhi ya wanachama wa KAAT wakiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (Katikati). |
No comments:
Post a Comment