Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Peter Kakamba
Miili hiyo ya Nyanjige Mutula (70) na Grace Hayo (18) aliyekuwa mjamzito, ilizikwa katika vijiji tofauti juzi saa 12 jioni kwa hofu ya mwili wa Grace kuharibika baada ya kufanyiwa upasuaji wa kutoa kichanga cha miezi mitano kwenye Kituo cha Afya Kashishi.
Tukio hilo lililoibua hofu kwa wananchi wa vijiji na kata za Kamena, Nyakamwaga, Lwamgasa na Nyarugusu, walisema mauaji hayo yanahusiana na imani za kishirikina.
Akizungumzia mauaji hayo baada ya maziko, Afisa Mtendaji wa kijiji cha Ililika, Fabian Mugeta, alisema mikakati ya kuwapigia kura za siri watuhumiwa wa tukio hilo, ilikuwa ikiendelea.
Mugeta alisema ililazimika mwili wa Grace kufanyiwa upasuaji kabla ya kusafirishwa kwenda kijijini kwao katika kijiji cha Nyashihima na mwili wa binti huyo kuzikwa tofauti na kichanga chake.
Marehemu Mulita alizikwa katika kijiji cha Ililika kitongoji cha Mwabasabi kulikotokea mauaji hayo, na kuhudhuriwa na baadhi ya wananchi, ndugu na viongozi wa kijiji.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Peter Kakamba, alisema mpaka sasa hakuna mtuhumiwa yeyote aliyekamatwa kufuatia tukio hilo la kinyama lililotokea hivi karibuni.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment