Na Mwandishi wetu
SWEDEN
imeyapatia mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo hapa nchini jumla ya
shilingi bilioni 42/- ili kusaidia katika miradi yake ya maendeleo
inayofanya nchiini Tanzania.
Makubaliano
ya fedha hizo yametiwa saini jana kati ya Balozi wa Sweden Lennarth
Hjelmaker na Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania
Alvaro Rodriguez.
Fedha
hizo ambazo ni sawa na dola milioni 24, zitaelekezwa kwenye miradi ya
UNDAP inayoendana na sera za Sweden za kuwezesha masuala ya utawala
bora, ustawi wa jamii, wanawake na watoto na usawa wa kijinsia.
Kwa
mujibu wa Balozi wa Sweden, fedha hizo zitasaidia utekelezaji wa
Mkukuta, Mkuza na Matokeo makubwa sasa (BRN) mipango inayofadhiliwa na
mashirika ya Umoja wa Mataifa .
Alisema
ni matumaini yake kuwa fedha hizo zitaboresha hali ya kufanya biashara,
kuwekeza kwa lengo la kutoa ajira zaidi,kuwezesha uchaguzi huru,
kuimarisha huduma za jamii, kuimarisha mipango, uwajibikaji na
kuimarisha mawasiliano ya radio kwa ajili ya upashanaji habari vijijini
ili kusaidia maamuzi yenye mtazamo mpana zaidi miongoni mwa watu wa
vijijini.
Katika
hafla hiyo Balozi wa Sweden alisema pamoja na kutoa fedha hizo kwa
mashirika ya Umoja wa Mataifa, nchi yake itaendelea na makubaliano
yaliyofikiwa na serikali ya Tanzania na kuendelea kutoa misaada yake ya
kimaendeleo.
Akijibu
swali la kwanini wanatoa fedha kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa pekee,
na kama wameacha kutoa misaada ya moja kwa moja serikalini, Balozi huyo
alisema misaada ya taifa hilo imelenga kupata matokeo yanayotakiwa na
kwamba itaendelea kusaidia pia taasisi nyingine zisizo za kiserikali na
serikali yenyewe.
Aidha
Balozi Lennarth HjelmÄker alisema kwamba Tanzania imekuwa mfano bora
kabisa wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kuwezesha ufanisi mkubwa wa
miradi ya maendeleo yaliyolenga kuwawezesha watanzania kupiga hatua
mbele na kuhakikisha kuwapo kwa amani.
Alisema
wanafurahia kusaidia masuala ya utawala bora, kazi kwa vijana, usawa wa
kijinsia na kuwapo kwa uchaguzi huru na wenye amani.
Sweden
imesema itaendelea kusaidia Umoja wa Mataifa nchini hasa inapotekeleza
mradi wake wa misaada kwa Tanzania (UNDAP) kama mashirika hayo
yalivyokubaliana na serikali ya Tanzania.
Naye Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Alvaro Rodriguez, ameishukuru Sweden kwa kuendelea kuwa mdau wa maendeleo.
Tanzania
na Umoja wa Mataifa wanatekeleza mradi wa miaka mitano wa UNDAP ambapo
mashirika ya UN yaliyopo nchini yanatoa kwa umoja wake huduma stahiki
ili kupata Matokeo Makubwa.
No comments:
Post a Comment