*Ni Toleo Maalum la Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania
*Linatumika kuitangaza Tanzania kwa watu mashuhuri
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
amezindua jarida la kimataifa la FIRST ambalo limesheheni taarifa za
kuitangaza Tanzania kwa wadau wa nchi mbalimbali duniani huku likielezea
hatua mbalimbali za ustawi kwa miaka 50 tangu nchi ipate uhuru.
Uzindusi huo ulifanyika kwenye
ofisi za ubalozi wa Tanzania jijini London, Uingereza ambako pia Waziri
Mkuu alikabidhiwa nakala ya kwanza ya toleo la sasa ambayo iliwekwa
kwenye jalada jekundu la ngozi (leather bound red cover).
Akizungumza katika uzinduzi huo,
Waziri Mkuu alisema Serikali ya Tanzania imepata fursa nzuri ya kujinadi
kwa watu maarufu na wafanyabiashara wa kimataifa duniani kupitia jarida
hilo na akataka uwekwe utaratibu wa kujinadi kisekta.
Alimtaka Balozi wa Uingereza, Bw.
Peter Kallaghe aweke mkazo na kusimamia suala hilo ili kuhakikisha
matoleo yanayofuata yanakuwa ya kisekta zaidi. “Balozi hapa umefanya
kazi nzuri sana ya kuinadi nchi yetu, wala usichoke. Tujitahidi sasa
kila mwaka waandike kuhusu fursa za uwekezaji kwa miradi ya kisekta kama
utalii, nishati, madini na kadhalika,” alisema.
Waziri Mkuu alimshukuru Mwenyekiti
wa taasisi ya First, Bw. Rupert Goodman kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa
ajili ya Taifa la Tanzania. “Kazi uliyoifanya ni nzuri lakini katika
tolea lijalo tuangalie jinsi ya kuitangaza miradi ya uwekezaji ambayo
inauzika na iende sekta kwa sekta. Ukisirikiana na Balozo wetu hapa,
lazima utapata kitu kizuri,” alisema.
Mapema, akielezea kuhusu jarida
hilo la FIRST, Balozi Kallaghe alisema jarida hilo linasambazwa kwenye
mashirika mbalimbali ya ndege kama vile British Airways, Air Astana, Lufthansa, United Airlines, Gulf Air, American Airlines, South African Airways, Korean Airways, Etihad Airways, Qatar Airways na Continental Airlines.
“Siyo tu kwamba linasambazwa katika mashirika haya ya ndege, bali pia linawekwa kwenye vyumba vya kupumzikia (First Class and Business Class Lounges) abiria wa daraja la kwanza na la pili wa mashirika haya kwenye viwanja vingi vya ndege,” alisema.
Alisema hili ni toleo la sita
ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano na ofisi yake (Ubalozi wa Uingereza)
ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania lakini
pia ikilenga kutangaza fursa za uwekezaji lakini pia ikitangaza hatua
mbalimbali za maendeleo ambazo nchi hii imepitia.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na
Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Maalim na Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Bw. Charles Kitwanga. Wengine ni Naibu Waziri wa
Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Said
Mwambungu ambao pia wamefuatana na Waziri Mkuu.
No comments:
Post a Comment