MAKAMU WA RAIS ASISITIZA KUSHIRIKISHA WANAUME KATIKA AJENDA YA MTOTO WA KIKE
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
akihutubia kwenye Tamasha Fadhili Mtoto Asome pamoja na Binti Clubs
iliyoandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Binti Foundation ambapo
aliahidi kuwasomesha watoto 100 na aliwasihi Wanawake wanapoweka
mipango ya kimaendeleo kuwashirikisha pia wanaume.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan (kulia) akiwa pamoja na mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa
mara baada ya uzinduzi wa Binti Clubs jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya watu waliojitokeza kwenye Tamasha Fadhili Mtoto Asome pamoja
na Binti Clubs iliyoandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Binti
Foundation ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia
Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan akipitia
kitabu cha Binti Foundation wakati wa Tamasha Fadhili Mtoto Asome.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia)
akitazama jambo liliokuwa linaendelea (halionekani pichani) pamoja na
Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa Binti Foundation Johari Sadiq .
Sehemu ya watoto walioshiriki kuonyesha mitindo mbali mbali ya Mavazi pamoja na Wabunifu wao.
Makamu
wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameyataka Mashirika yasiyo ya
Kiserikali nchini (NGOs) yanayoshughulikia masuala ya wanawake na watoto
kujenga utamaduni wa kushirikisha wanaume katika kampeni za kumwinua
mtoto wa kike kwa lengo la kuleta mabadiliko yanayokusudiwa.
Mheshimiwa
Samia ametoa kauli hiyo jana kwenye hafla ya uzinduzi wa Binti club
iliyofanyika sambamba na harambee ya fadhili mtoto asome ya kuchangisha
fedha kwa ajili ya watoto 500 wa wilaya ya Kinondoni iliyoandaliwa na
Shirika lisislo la Kiserikali la Binti Foundation katika ukumbi wa
PSPF jijini Dar es salaam
Alisema wanaume kama wakala wa
mabadiliko wanapaswa kushirikishwa na wajue ajenda ili wawe mabalozi
wazuri katika kuzungumzia umuhimu wa kumwinua mtoto wa kike kielimu,
kiafya na kwenye masuala ya ujasiriamali.
"Tuwaingize wanaume
kama wakala wa mabadiliko, tuwashirikishe, wajue ajenda zetu katika
mapambano hayo. wanaume wanashikilia sehemu nyingi, watumie nafasi hizo
tulete mabadiliko," alisema Makamu wa Rais na kuongeza."Penye mkusanyiko
wa watu 100, ukiingiza wanaume 20, na wakajua madhumuni ya mkusanyiko
wetu, wataenda kushawishi wenzao 20,000 huko nje."
Aliipongeza
Taasisi hiyo ya Binti Foundation kwa kuunga mkono jitihada za serikali
katika suala la elimu kwani safari ya mtoto wa kike ya kupata elimu
inakuwa na ugumu zaidi kuliko wanaume kutokana na kukabiliwa na
changamoto mbalimbali zikiwemo za mila potofu, hali ya uchumi katika
familia na jinsi jamii inavyomwangalia kutokana na ujanajike wake.
"Tuna kazi kubwa ya kumtayarisha mtoto wa kike aweze kupambana na changamoto zinazomzunguka," alidokeza.
Mheshimiwa
Samia alitumia fursa hiyo kuelezea hatua mbalimbali zinazochukuliwa na
serikali katika kukabiliana na changamoto za elimu ikiwa ni pamoja na
kuondoa ada katika shule za msingi na sekondari, kuboresha ajira za
walimu pamoja na maslahi yao, kujenga mabweni kwa wasichana na kuondoa
tatizo la madawati ambapo amewashukuru Watanzania kwa kuchangia
madawati.Aliwataka wazazi kuwatunza watoto wao kwani ni zawadi kutoka
kwa Mungu na kuhakikisha wanapata elimu zote ya dini na ya dunia ili
kuwajenga kimaadili waweze kuwa raia wema.
Mtendaji Mkuu wa
Binti Foundation Johari Sadik alimweleza Makamu wa Rais kuwa shirika
hilo liliamua kuunga mkono jitihada za serikali ili kuwawezesha watoto
kumudu masomo yao na hatimaye kufikia malengo yao."Kwa hiyo ukiwa na
fedha taslimu, ama vifaa kama vile kalamu, madaftari, pedi, vyote
tunapokea kwa ajili ya kusaidia watoto ambao malengo yao yanaweza
yasitimie kutokana na changamoto hizo,"
Kampeni hiyo ya fadhili
mtoto asome imeanzia kwa watoto 500 wanaoishi kwenye mazingira magumu wa
shule za msingi Mwananyamala, Hananasif, Kumbukumbu na Msasani zilizoko
katika wilaya ya Kinondoni, mkoa wa Dar es salaam.Katika hafla hiyo
iliyopambwa na onesho la mavazi la watoto Makamu wa Rais ambaye
alikubali kuwa mlezi wa Binti Foundation aliahidi kusomesha watoto 100
wakati mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa alitoa ahadi pia ya kusomesha
watoto 50.
No comments:
Post a Comment