TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Tuesday, March 10, 2015

Moruwasa kufanya upanuzi wa bwawa la Mindu

bw1
Hussein Makame-MAELEZO MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Morogoro (MORUWASA) imepanga kuongeza uwezo wa bwala la Mindu mara mbili zaidi ili liweze kukusanya maji mengi zaidi kukidhi mahitaji ya maji ya wakazi wa manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea ofisi kwake mjini Morogoro mwisho mwa wiki hii, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Mhandisi Nicholaus Angumbwike, alisema pia wamepanga kujenga mtambo mwengine wa kutibu maji ili kuongeza kiasi cha maji kutoka chanzo hicho. Alisema tayari mkandarasi ameshaandaa pendekezo la mradi (proposal) kupitia awamu ya kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) na kwamba imeshakamilika na ameiwasilisha Wizara ya Maji kwa ajili ya utekelezaji. Mhandisi Angumbwike aliongeza kuwa wanatarajia kwamba utekelezaji wa mradi huo utafanyka katika awamu ya pili ya WSDP iliyoanza Juni mwaka jana iwapo Wizara itawapatia fedha kwa ajili ya kazi hiyo. “Kuna utafiti imeshafanyika kuhusu bwawa la Mindu, kuna uwezekano kwamba uwezo wa bwala la Mindi ukaongezeka mara mbili zaidi yaani uwezo wa kukusanya maji mengi zaidi kuliko ilivyo sasa na tukajenga mtambo mwengine wa kutibu maji ili kuongeza kiasi cha maji yanayotoka chanzo cha bwawa la Mindu” alisema Mhandisi Angumbwike na kuongeza: “Hii kazi imeshafanyika katika mradi wa WSDP awamu ya kwanza, mkandarasi amefanya akaandaa proposal yake na tuna matumaini kwamba ameshakamilisha na amewasilisha Wizara ya Maji, tunatarajia katika hii awamu ya pili kama Wizara ikitufikiria tuweze kutekeleza mradi huo”

Alisema kinachotakiwa kufanyika ni kuongeza tena urefu wa tuta la bwawa hilo kwa urefu wa mita 2 na kujenga mtambo mwingine wa kutibu maji kwani mtambo ulipo una uwezo wa kutibu maji kwa siku lita milioni 27 tu. Aliongeza kuwa gharama za mradi huo wa kuongeza uwezo wa chanzo hicho cha maji cha bwawa la Mindu na mtambo wa kutibu maji, kwa mwaka 2008 ilikuwa ni shilingi Bilioni 35. Alisema mbali na juhudi hizo MORUWASA imekuwa ikitafakari vyanzo vingine vya maji kukidhi mahitaji ya wakazi 315,000 wa manispaa ya Morogoro ikiwemo kufikiria kwenda juu zaidi ya milima ya Uluguru kutafuta vyanzo hivyo. Alisema wanaangalia uwezekano wa kuchimba visima virefu lakini changamoto iliyopo ni kwamba ni shida kupata maeneo ambayo watapata maji baridi kwa sababu maeneo mengi ya Morogoro ukichimba unapata maji ya chumvi. Kwa upande wa uboreshaji wa miundombinu chakavu, Mhandisi Angumbwike alisema wamepokea fedha kiasi cha shilingi Milioni 240 kutoka Wizara ya Maji ambayo itatusaidia kubadilisha kilomita kadhaa ya miundombinu ya maji iliyochakaa ili kuboresha upatikanaji wa maji. Katika kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji vilivyopo, Mhandisi Angumbwike alisema wanashirikia na wadau wengine kama Ofisi ya Bonde la Maji, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, katika kulinda vyanzo hivyo. “Tumekuwa tukifanya kazi pamoja, tunakutana pamoja tunakwenda kwenye miradi (sites) tumeainisha maeneo ambayo yanataka kuyatunza, tumetoa elimu kwa wananchi watambue kwamba jukumu la kutunza vyanzo vya maji ni la kila Mtanzania na wao wakiwemo”alisema na kuongeza: “Wananchi wanatakiwa watambue kwamba jukumu la kutunza vyanzo vya maji ni muhimu kwa manufaa ya Watanzania wote” Kuhusu wizi wa maji, Mkurugenzi huyo alisema wana Operesheni za kukamata watu wanaojiunganishia maji kwa kupita nyumba kwa nyumba ili kuwabaini na kuwakamata watu ambao wanatumia maji bila kuyalipia. “Wapo watu ambao wanataka wapate maji bila kuyalipia, tunafanya operesheni nyumba kwa nyumba na tunapowakamata tunawatoza faini na kuwachukulia hatua lakini shida kubwa ni uunganishaji mwingine ni ngumu kuubaini” alisema Mkurugenzi huyo na kuongeza: “Wapo tuliowakamata kwa ushirikiano na wananchi na tunatoa motisha wa fedha kwa wananchi wanaotupa taarifa hizo. Pia tunacho kikosi maalum kinachopita mitaani na katika hoteli mbalimbali kuchunguza mifumo ya maji ili kubaini watu wanaoiba maji. Tumeshakamata baadhi ya hoteli zimejiunganishia maji, tukawauliza wanasema wamechimba kisima lakini baada ya kupima sampuli ya maji tunakuta kwamba ni maji ya Morowasa” Hivyo aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kuwafichua wezi wa waji au watu wanaojiunganishia maji kiholela ili kudhibiti asimilia 40 ya maji ambayo hayaipatii mapato MORUWASA.
Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) ya mwaka 2006 hadi 2025, inatekelezwa kwa awamu ya miaka mitano mitano ambapo awamu ya Kwanza ilianza mwaka 2007 na kukamilika 2014 na awamu ya Pili ilizunduliwa na Waziri wa Maji Juni mwaka jana tayari kwa utekeleaji.

No comments:

Post a Comment