TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Wednesday, November 11, 2015

Dk. Shein, Maalim Seif wateta Ikulu Z'bar. NA MWINYI SADALLAH

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amekutana na kuzungumza kwa saa sita na nusu na mgombea mwezake wa urais kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kujadili mgogoro wa uchaguzi, baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo.

Uchaguzi huo ulifanyika Oktoba 25, mwaka huu na Jecha alitangaza kuufuta Oktoba 28, kwa madai kuwa kulikuwapo na kasoro kadhaa.


Taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo vyetu mbalimbali, zimeeleza kwamba kikao hicho kati ya Rais Shein na Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, pia kilihudhuriwa na viongozi kadhaa wastaafu.

Viongozi hao ni Rais mstaafu wa Janhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Mazungumzo hayo yalifanyika Ikulu ya Zanzibar na kumalizika saa kumi jioni na ajenda kubwa ilihusu mgogoro wa uchaguzi visiwani humo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Kampeni wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, alithibitisha viongozi hao wakuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kukutana, lakini alisema hafahamu mambo yaliyojadiliwa katika kikao hicho.

“Kweli wamekutana kwa mazungumzo baada ya Zanzibar kukubwa na mgogoro wa uchaguzi, lakini mimi nipo Dar es Salaam, sifahamu kilichoendelea katika kikao hicho,” alisema Jussa, baada ya kutakiwa kueleza ajenda madhumuni ya kikao hicho pamoja na ajenda zilizojadiliwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais wa Zanzibar, Salum Maulidi Kibanzi, alisema hafahamu chochote kwa sababu yuko safari nje ya Zanzibar.

“Watafute wahusika mie nipo safari nje ya Zanzibar,” alisema Kibanzi.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Hassan Khatibu, alisema hana taarifa zozote kuhusiana na kikao hicho kwa sababu yupo nje ya ofisi na kutaka watafutwe wasaidizi wa Rais.

Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, DK Abdulhamid Yahya Mzee, hakupatikana, kutokana na simu yake ya kiganjani kuiita zaidi ya mara moja bila kupokelewa, baada ya kumalizika kwa kikao hicho.

Hata hivyo, chanzo kimoja kimeeleza kuwa hatua ya Mwenyekiti Zec kufuta matokeo ya uchaguzi na hatua ya Maalim Seif kujitangaza mshindi kabla ya Zec kutangaza matokeo ni mambo yaliyochukua nafasi kubwa kujadiliwa pamoja kasoro zilizodaiwa na Jecha wakati akitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo.

Imeelezwa kuwa viongozi hao wastaafu waliombwa kushiriki katika kikao hicho kwa lengo la kuongeza nguvu na kutumia busara katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.

Karume ndiyo alieweka msingi wa maridhiano, baada ya Zanzibar kukumbwa na mpasuko wa kisiasa wa muda mrefu tangu uchaguzi wa kwanza baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995 na kuundwa kwa SUK Novemba, 2009.
Juhudi za kutafuta maelewano zimekuja wakati vyama vya CUF na CCM vikiwa vimegawanyika kufutia uamuzi wa Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar.

Wakati CCM wanaunga mkono uamuzi wa kurudiwa uchaguzi huo, CUF inasisitiza kuwa haikubaliani na uamuzi wa kurudiwa na kwamba haitashiriki, kwa kuwa inasubiri Maalim Seif aapishwe kwa madai kuwa alishinda.

CUF inamtaka Jecha aendelee kuhakiki majimbo yaliyobakia na kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo.

Uamuzi wa Jecha umekuwa ukipingwa na waangalizi mbalimbali wa uchaguzi wa kitaifa, kimataifa pamoja na mataifa kadhaa yakiwamo Uingereza, Ireland na Marekani, wakisema hakuna kasoro zilizobainika wakati wa uchaguzi huo na kuishauri Zec kuendelea na mchakato wa kutangaza matokeo.

Wakati mgogoro huo ukiendelea, kumekuwapo na jitihada za upatanishi zinazofanywa na viongozi wa dini, Msajili wa Vyama vya Siasa na viongozi wastaafu.
www.shaabanmpalule.blogspot.com

No comments:

Post a Comment