Mtoto
Shangwe Mtaula (16) mkazi wa Mabatini akiwa katika chumba cha wagonjwa
mahututi katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma alikolazwa baada ya
kulipukiwa na bomu la machozi wakati wa vurugu zilizotokea mjini
Songea.Picha na Joyce Joliga
IGP MWEMA APELEKA KIKOSI CHA UCHUNGUZI, MAJERUHI HALI MBAYA
Joyce
Joliga na Kwirinus Mapunda, Songea Polisi Mkoani Ruvuma, wanawashikilia
na kuwahoji askari wake wanne kwa tuhuma za mauaji ya raia kwa kutumia
risasi za moto katika vurugu zilizotokea juzi mjini Songea.Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamhanda alisema jana kuwa askari hao
walikamatwa na wanaendelea kuhojiwa ili kujua kama kulikuwa na uzembe
katika utekelezaji wa majukumu yao.“Kwa kuwa tukio hilo limehusisha
vifo, hatuwezi kuacha hivihivi tu ni lazima tujiridhishe kuwa askari
hao hawakufyatua risasi kwa uzembe,”alisema Kamhanda.
Kamanda
huyo alisema askari hao watahojiwa baada ya kuundwa kwa tume maalumu ya
kuchunguza tukio hilo, na tume hiyo ikibaini kuwa kulikuwa na uzembe,
hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwamo kufikishwa mahakamani.
Hata
hivyo kamanda Kamhanda hakutaka kutaja majina, wala vyeo vya askari hao
kwa maelezo kwamba ni ni mapema mno, pia sababu za kiusalama.Katika
hatua nyingine Kamhanda alisema tayari watu 54 wamefikishwa mahakamani
kutokana na vurugu za juzi.
IGP Mwema achunguza
Mkuu
wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema ametuma
kikosi cha maofisa waandamizi kutoka makao makuu ya jeshi hilo,
kikiongozwa na Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo, Kamishna Paul
Chagonja kwenda mjini Songea kufanya uchunguzi wa ghasia hizo.
Chagonja
akizungumza na Mwananchi jana alisema maandamano hayo hayakuwa ya amani
bali ya kihuni kwani yalilenga kuvamia ofisi za serikali ikiwemo Ikulu
ndogo na Ofisi ya Mkuu wa mkoa. Chagonja alikuwa akijibu swali
lililotaka aeleze endapo haoni kama polisi imetumia nguvu kubwa
kutawanya raia waliokuwa wakiandamana kwa amani.
"Maandamano ya amani watu wanavamia Ikulu, maandamano ya amani watu wanazingira ofisi ya mkuu wa mkoa?"
"Sijafika
huko ndo naelekea lakini, yale si maandamano ya amani. Yaani wahuni
wanataka kuivuruga nchi waachiwe? Kuweni wazalendo, msiwe kama labda
ninyi ni waandishi wa BBC kutoka Uingereza, hii ni nchi yenu."
Alifafanua
kwamba, maandamano ya amani yanafahamika kwani watu hulazimika kuomba
kibali na kuweka wazi ajenda ya maandamano "Lakini siyo maandamano
yale, watu hayakuwa na kibali chochote, wahuni wamejiingiza wanataka
kuvuruga nchi tu."
Mkuu
huyo wa operesheni alitetea polisi akisema,"Usifikirie polisi hawana
akili. Haiwezekani watu wazima na akili zao wenye mafunzo wafyatue
hovyo risasi za moto kwa raia. Hakuna askari anapenda kuua raia...,
lakini watu wanavamia Ikulu, ofisi ya mkuu wa mkoa, magari ya polisi
hapo kuna amani kweli?"
Alitoa
angalizo kwamba ni lazima hata vyombo vya habari, viache ushabiki
badala yake viangalie maslahi ya taifa kwani nchi ikivurugika wao pia
hawatasalimika na kusisitiza, "Kuweni wazalendo bwana, msifikirie
kulishutumu jeshi la polisi tu."
Wakati
IGP akituma kikosi hicho, wanaharakati, wanasiasa na wasomi wamekosoa
matumizi makubwa ya nguvu za polisi dhidi ya raia na waandamanaji
waliokuwa wakifikisha ujumbe wao kwa mkuu wa mkoa kupinga mauaji ya
watu tisa yaliyofanywa kwa imani za ushirikina.
Juzi
wananchi waliokuwa wakiandama kupinga mauaji hayo, walipambana na
polisi ambapo watu wanne waliuawa na wengine 41 kujeruhiwa.
Hali
za majeruhi Majeruhi wanane kati ya 11 waliolazwa katika Hospitali ya
mkoa wa Ruvuma, jana waliruhusiwa. Majeruhi wengine 30 walipatiwa
matibabu juzi na kuruhusiwa kurudi nyumbani kwao.
Mganga
mfawidhi wa hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Benedicto Ngaiza alisema
tayari wagonjwa wanane kati ya kumi na moja waliolazwa katika hospitali
hiyo wameruhusiwa na kwamba ni wagonjwa watutu ndio waliobaki.
Mmoja
wa wagonjwa hao, Shangwe Mtaula (16) mkazi wa Mabatini hadi jana
alikuwa hajitambui kutokana na kipigo cha polisi kilichosababisha
kuumia vibaya katika paji lake la uso.
Muuguzi
wa wodi alimolazwa mgonjwa huyo, Hildetha Mhonyo alisema binti huyo
alifikishwa hospitalini hapo juzi saa tano asubuhi akiwa hajitambui na
hivyo alilazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi.
Muuguzi
huyo alisema, bado hali ya Shangwe si nzuri ingawa jana alianza
kuzungumza kwa taabu na kwamba anaonekana kuwa na maumivu makali kwenye
paji lake la uso, huku macho yake yaonekana kuvimba.Mgonjwa mwingine ni
Esta Mbali (29) mkazi wa Mshangano, ambaye amelazwa wodi namba tano
baada ya kupigwa risasi katika bega lake la kushoto na kuumizwa vibaya.
Mgonjwa
huyo anasema, hali yake inaendelea vizuri kwa sasa baada ya kupata
matibabu. Alisema, katu hatasahau tukio hilo kwani alikuwa akitoka
hospiatali kumsalimia binamu yake ambaye alikuwa amejifungua na wakati
akiwa njiani alikutana na kundi kubwa la watu wakiandamana na baadaye
polisi walianza kuwatawanya kwa mabomu ya machozi, ambapo alifanikiwa
kukimbia na kujificha kwenye nguzo ya umeme, lakini ghafla alisikia
kitu cha moto kikimuumiza begani mwake . Alisema alipatwa na kiwewe na
kuanza kukimbia ovyo, hali iliyosababisha mwili mzima kulowa kwa damu
ambayo wakati huo hakuweza kufahamu chanzo chake.
Esther
aliendelea kusimulia kuwa baada ya kutokwa damu nyingi, aliishiwa nguvu
na kuanguka, hadi aliposaidiwa na wasamaria wema ambao walimpakia
kwenye gari na kumkimbiza hospitalini.
Mwingine
ni Sinje Mchompa (29) mkazi wa Bombambili, ambaye alijeruhiwa katika
tukio hilo na kuumizwa vibaya na kipande cha bomu mdomoni eneo la
SODECO, wakati alipokuwa akielekea Mabatini.
Sinje
alisema alipokuwa katika eneo hilo ndipo vurugu zilianza na kwamba
alishtukia akipigwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni kipande cha bomu
mdomoni na kutoboka mdomo hali iliyosababisha meno kuuma sana.
Mgonjwa huyo ameomba msaada wa kupatiwa matibabu zaidi ili hali yake iweze kurejea kama awali.
Kwa
upande wake Matroni wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma Helta Soko, ametoa
ushauri kwa wananchi kuacha tabia ya kufanya vurugu katika maeneo ya
hospitalini kwani hali hiyo inasababisha usumbufu kwa wagonjwa
waliolazwa.
Kauli
ya Helta inatokana na baadhi ya wananchi kupiga kelele wakati
walipokuwa wakiwarushia mawe wauguzi na askari waliokuwa wakipeleka
mwili wa mmoja wa waliokufa katika tukio hilo katika chumba cha maiti.
Habari
tulizozipata wakati tukienda mitamboni zinasema, kwa mara nyingine,
jana saa 12 jioni, polisi mjini Songea walilazimika kutumia mabomu ya
machozi kuwaokoa watu wawili waliokuwa wakipigwa na wananchi
wakiwatuhumu kwamba ni majambazi wanaojihusisha na vitendo vya mauaji
ya wananchi.
Watu
hao ambao walijeruhiwa vibaya walikamatwa na wananchi katika eneo la
Mkuzo nje kidogo ya Manispaa ya Songea baada ya kujitambulisha kwa
wenyeji kwamba wao walikuwa wakitatafuta shamba la kununua, huku mmoja
wao ambaye ni mwanamke akitoroka na kukimbilia kusikojulikana.
Kutokana
na kuwatilia mashaka, wananchi hao waliwazingira na kuwaweka chini ya
ulinzi kisha kuwafikisha nyumbani kwa kiongozi wa Serikali ya mtaa wa
Mkuzo, John Moyo na baadaye walianza kuwapiga baada ya kutokea utata
katika maelezo yao.Soma zaidi www.baloziwademokrasia.blogspot.com
No comments:
Post a Comment