OFISA mfawidhi kituo cha kulelea
watoto yatima Kurasini, Ramadhani Yahaya ameiomba serikali kufanya
jitihada za kuwaondoa vijana wanaoendelea kuishi katika kituo hicho,
licha ya kupoteza sifa ya kuishi katika kituo hicho kwa kuwa wamevuka
miaka 18.
Ofisa huyo aliyaeleza hayo jijini Dar es
Salaam jana, wakati Mkurugenzi wa Rahabu Ulcers Clinic, Dk Rahabu Rubago
alipokuwa akitoa zawadi mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea mwaka mpya
ikiwemo chakula, vinywaji na vifaa vya shule kwa watoto wa kituo hicho
waliokuwa wamechanganyika na watoto wa kituo cha wasabato.
Ramadhani alisema kituo hicho
kwa sasa kinakumbwa na changamoto kubwa ya kuwa na vijana wengi wenye
umri zaidi ya miaka 18 hivyo wanashindwa kufuata masharti ya kituo hicho
ikiwemo kuwa ndani ya uzio ifikapo saa 12 jioni.
“Changamoto kubwa ni vijana
wenye umri mkubwa kuendelea kuishi katika kituo hiki naiomba serikali
iwatengenezee vijana hawa mazingira ya kuwaondoa katika maeneo haya ili
nao wakawe na maisha yao na kuachana na utegemezi wa hapa” alisema
Ramadhani
Naye Dk Rahabu aliwataka vijana
na watoto hao kutokukata tamaa katika maisha yao huku akiwataka kusoma
kwa bidii ili waweze kukamilisha ndoto zao na malengo waliyojiwekea.
“Mimi niliishi hapa nimekuja
kufurahi nanyi na kuwatia moyo msijione kama mpo peke yenu tupo pamoja
na kutokana na kujibidiisha tumefanikiwa hivyo nanyi nawahasa
mjibidiishe kwa bidii zote ili muweze kufanikiwa na kufikia malengo
yenu,” alisema Dk Rahabu”alisema Rahabu
Naye mwanafunzi anayesoma chuo
cha uhasibu, ambaye anaishi katika kituo hicho, Robert Bernard ameiomba
serikali kutowaondoa vijana waliozidi miaka 18 bila kuwatengenezea
mazingira mazuri ya kwenda kuishi.
“Kuondoka hapa si tatizo
tunachoomba kama serikali inataka kutuondoa hapa kwa kuwa umri wetu
mkubwa hatukaidi bali tunachoomba watuwekee mazingira mazuri huko
wanakotaka twende lakini bila hivyo watakuwa hawajatusaidia” alisema
Bernard.
No comments:
Post a Comment