TAN
Bayport
Kikoa
Myway entertainment
FORE PLAN CLINIC
MPINGA CUP 2016
Mashujaa Fm 89.3, Lindi
Sunday, December 13, 2015
Bilioni 10.6/- zalipwa TRA wakwepa kodi makontena
Agizo la siku saba la Rais, Dk. John Magufuli kwa wafanyabiashara waliokwepa kodi kwenda kulipa wenyewe kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), limezaa matunda ambapo bilioni 10.6 tayari zimepatikana hadi kufikia jana jioni.
Rais Magufuli alitoa siku saba ambazo ziliisha jana jioni, wakati alipozungumza na wafanyabiashara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam, Alhamisi iliyopita.
Wafanyabiashara wa kampuni 43 kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa TRA, Bandari Kavu (ICDs) na Mamlaka ya Bandari (TPA), ndio wanaotuhumiwa kutorosha makontena 329 bila kulipiwa ushuru hivyo kuikosesha serikali mabilioni ya fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Diana Masalla, alisema Mamlaka hiyo imekusanya Sh bilioni 10.6 kutoka kwa kampuni 28.
Alisema kampuni hizo zilizohusika na uondoshwaji wa makontena bandarini kinyume cha sheria na taratibu za forodha, hivyo kuikosesha serikali mapato yake.
“Kampuni sita kati ya 28 zimelipa kodi yote iliyokadiriwa pamoja na adhabu na makampuni 22 yamelipa sehemu ya kodi iliyokadiriwa pamoja na adhabu,” alisema
Alisema kampuni nyingine 15 hazijalipa kodi ambayo ni Sh. bilioni 4.7 licha ya kwamba tayari yameshakadiriwa malipo wanayopaswa kulipa.
“Leo (jana) ni siku ya mwisho iliyotolewa na Rais kwa wafanyabiashara waliokwepa kodi kwa kutorosha makontena, hivyo TRA inawaomba wote ambao hawajalipa kutekeleza agizo la Rais,” alisisitiza
Alisema kuanzia leo hatua kali zitachukuliwa kwa wale ambao hawajawasilisha mapato yao waliyotakiwa kuyalipa kufuatia agizo la Rais.
Masalla aliwaomba wananchi kuwafichua wale wote ambao wanajihusisha na ukwepaji wa kodi na kuongeza kuwa mwananchi ambaye atafanya hivyo atapatiwa asilimia tatu ya kodi iliyokuwa inapotea.
Wakati huo huo, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa 40 ambao wanaendelea kuhojiwa kwa tuhuma za kula njama na kuikosesha serikali mapato.
Alisema uchunguzi huo unafanywa kwa pamoja na maofisa wa Jeshi hilo na wale wa TRA kwa lengo la kubaini jinsi ambavyo makontena 329 na mengine 2,489 yalivyotolewa bandarini kinyume cha taratibu.
Alisema uchunguzi unaoendelea unahusisha kupitia kumbukumbu mbalimbali za forodha ili kubaini mtindo uliotumika na kuwabaini wote waliohusika katika mchakato huo.
Kamishna Kova alisema makontena 329 yaligundulika kukosekana kwenye bandari kavu ya Azam kuanzia Julai hadi Novemba mwaka huu na makontena 2,489 yaligundulika kutolewa bandarini kuanzia Machi mpaka Septemba mwaka 2014 ambayo yalikwepa kodi.
Alisema baada ya uchunguzi wao kukamilika majalada ya kesi yatapelekwa kwa mwanasheria wa serikali ili watuhumiwa watakaobainika wafikishwe mahakamani.
Aidha, Kova alisema kufuatia sakata hilo la ukwepaji wa kodi, kumejitokeza matapeli ambao wamekuwa wakiwalaghai baadhi ya wafanyabiasha kwa kujifanya wao ni maofisa wa serikali.
Alisema matapeli hao wamekuwa wakiwapigia simu wafanyabiashara na kutaka kukutana nao katika maeneo mbalimbali ya jijini kwa madai ya kufuatili watu ambao wana makosa yanayohusiana na ukwepaji wa kodi.
Hata hivyo, Kova alisema imebainika watu hao si maofisa wa serikali na lengo lao ni kujipatia fedha kwa vitisho kutokana na matukio ya msako mkali unaofanyika wa kuwatafuta waliohusika katika ukwepaji kodi ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Aliwaasa wafanyabiashara wasikubali kutishwa na watu hao na iwapo watawapigia simu waombe uthibitisho kutoka kwa uongozi wa TRA au Jeshi la Polisi kama kweli ni maofisa wa serikali. Sakata la utoroshaji wa makontena bila kulipiwa ushuru lilianza kuvuma, Novemba 27, wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea bandari ya Dar es Salaam.
Majaliwa alibaini makontena 329 yalikuwa yamepitishwa bandarini hapo bila kulipa kodi hivyo kuikosesha serikali Sh. bilioni 80.
Kufuatia sakata hilo Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade alisimamishwa kazi huku Jeshi la Polisi likiwashikilia maofisa kadhaa waandamizi wa Mamlaka hiyo.
Baadhi ya maofisa wa Mamlaka hiyo akiwamo Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki, walifikishwa mahakamani.
Katika sakata hilo, kampuni 43 ndiyo zilibainika kupitisha makontena bila kulipa ushuru.
Shehena zilizopitishwa zikiwa kwenye makontena hayo ni matairi ya magari, samani mbalimbali, betri za magari, vifaa vya ujenzi, nguo na bidhaa mchanganyiko.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
Newer Post
Older Post
Home
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment