Mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’ ameweka rekodi mpya ya mabao wakati sare zikitawala kwenye viwanja vinne, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) ilipoingia raundi ya 11.
Nahodha huyo wa Azam FC, alifunga mabao mawili wakati timu yake ikishikwa sare ya 2-2 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku mabingwa watetezi Yanga nao wakilazimishwa suluhu dhidi ya Mgambo Shooting jijini Tanga.
Bocco alifunga goli la kwanza sekunde ya 54, lilikiwa ni bao la pili la mapema tangu kuanza kwa msimu huu Septemba 12. Bao la mapema zaidi lilifungwa sekunde ya 40 na Salum Kipanga wa Mgambo Shooting katika mechi yao waliyoshinda 1-0 dhidi ya African Sports Septemba 30.
Goli la kwanza la Azam jana lilimfanya Bocco amfikie mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi ambaye kabla ya mechi ya jana alikuwa na idadi kubwa zaidi ya mabao (matano) katika mechi za VPL kati ya timu hizo tangu kikosi cha Wanalambalamba kipande Ligi Kuu msimu wa 2008/09.
Matokeo ya mechi za jana yaliiongeza Azam pointi moja kileleni mwa msimamo ikifikisha 26 huku Simba ikiendelea kukaa nafasi ya nne ikiwa na mtaji wa pointi 22 baada ya timu zote kucheza mechi 10.
Yanga imeendelea kukaa nafasi ya pili ikiwa na mtaji wa pointi 24, mbili mbele ya Mtibwa Sugar walioko nafasi ya tatu.
Hadi mapumziko kwenye Uwanja wa Taifa, matokeo yalikuwa 1-1, Azam, Simba wakisawazisha kupitia kwa mshambuliaji Ibrahim Ajibu aliyemalizia kwa shuti la mguu wa kulia pasi murua ya kiungo Said Ndemla iliyopenyezwa ndani ya boksi dakika ya 25 ya mchezo.
Bocco alifunga goli hilo la mapema akimchambua kwa shuti la mguu wa kulia kipa wa Simba, Muivory Coast Vincent Angban baada ya kupenyezewa pasi safi ya kuparaza na winga Farid Mussa Malik, aliyempokonya mpira beki Mrundi Emery Nimubona.
Ajibu ambaye kabla ya mechi ya jana alipiga ‘hat-trick’ katika ushindi wao wa 6-1 nyumbani dhidi ya Majimaji, aliipatia Simba bao la pili dakika ya 68 kwa shuti kali baada ya kumlamba chenga beki Said Morad ndani kisha kupiga shuti la mguu wa kulia ndani ya sita na kumwacha kipa Aishi Manula akiwa anatupa lawama kwa beki wake.
Baada ya bao hilo, Azam walipiga kambi kwa dakika tano kwenye lango la Simba na kufanikiwa kusawazisha kupitia kwa Bocco akipiga shuti kali la mguu wa kushoto ndani ya boksi baada ya kusetiwa mpira na Kipre Tchetche.
Goli hilo limfanya afikishe mabao sita na kuwa kinara wa mabao katika mechi kati ya timu hizo akifuatwa na Okwi (5) na Tchetche (4), Mussa Mgosi (3), Ramadhani Singano ‘Messi’ (2) na Mike Barasa (2).
MKWAKWANI
Yanga ilishindwa kutumia fursa ya Azam kubanwa na Simba baada ya wachezaji wake Juma Abdul, Simon Msuva na Thaban Kamusoko kushindwa kutumia vyema nafasi nyingi za magoli walizopata na kujikuta wakilazimishwa suluhu ugenini dhidi ya Mgambo.
“Kama timu inatengeneza nafasi na unashindwa kuzitumiaa ni wazi huwezi kushinda, kikubwa tumeshindwa kuzitumia nafasi tulizozipata na ndiyo maana matokeo yamekuwa hivi,” alisema kocha mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm baada ya mechi.
Matokeo mengine ya mechi za jana yalikuwa:
Mbeya City 2-2 Mtibwa
Stand United 0-2 Mwadui FC
Kagera Sugar 1-1 Ndanda FC
Majimaji 0-4 Toto Africans
No comments:
Post a Comment