Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Ufugaji, Mwigulu Nchemba akikagua mifugo waliouawa katika mapigano baina ya wakulima na wafugaji.
Mwigulu Nchemba akimjulia hali mmoja wa majeruhi katika mapigano kati ya wakulima na wafugaji.
Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Ufugaji, Mwigulu Nchemba leo amefika Kijiji cha Dihinda Kata ya Kanga wilayani Mvomero kufuatilia na kuchukua hatua dhidi ya tukio baya la mauaji na kujeruhi binadamu na wanyama lililotokea Desemba 12 mwaka huu.
Akizungumza na wananchi hao, Waziri Mwigulu Nchemba alikuwa na haya ya kusema
“Natoa rai kwa wananchi hususani wa jamii ya wafugaji na wakulima, hakuna ardhi au mnyama mwenye thamani sawa na maisha ya mwanadamu yeyote yule, njia bora na salama ya kutatua migogoro hii inayohusisha wakulima na wafugaji ni kufuata taratibu za kuonana na uongozi wa serikali wa eneo husika hatua kwa hatua”. Alisema Mh. Mwigulu
Pia Waziri Mwigulu amesema ameagiza ulinzi maeneo yote yenye migogoro, pili wahakikishe waliosababisha maafa wanakamatwa mara moja na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na Kwa waliojeruhiwa, ameagiza wapatiwe matibabu kwanza bila kuchelewa na hatua za kisheria kwa wenye hatia zifuate.
“Nawaomba wananchi waache kujichukulia sheria mikononi, tunakwenda kuunda kamati za usuluhishi wa migogoro hii kwa kila kijiji zitakazohusisha pande zote mbili ili kubaini wavamizi wa maeneo na kuwachukulia hatua za kisheria.”
CREDIT: EATV
No comments:
Post a Comment