(Picha zote na Benedict Liwenga)
Na Shamimu Nyaki.
Serikali kupitia Mpango wa wa Taifa wa kudhibiti Magonjwa yasiyopewa kipaumbele leo imetangaza tarehe 19 hadi 23 mwezi huu kuwa itaanza zoezi la kugawa dawa kwa makundi yanayopaswa kupata dawa za magojwa hayo.
Tamko hilo limetolewa na Katibu mkuu wa Wizara Ya Afya na Ustawi wa Jamii,Wazee,na Watoto Bw. Donald Mmbando alipokuwa anazungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kusema kuwa Magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele ni Usubi,Vikope (Trakoma), Matende, Mabusha,Ngiri maji, na Minyoo ya tumbo hivyo dawa hizo zitasaidia kupunguza tatizo.
Ameongeza kuwa zoezi hilo la ugawaji wa dawa litatekelezwa katika vituo vyote vya Afya, Zahanati,Hospitali, shule za msingi na sekondari,sokoni,vituo vya usafiri,pamoja na Ofisi za Serikali na Mashirika ya Umma na hivyo wananchi wanaombwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo ambayo haina malipo yoyote.
Katibu Mkuu huyo amesema kuwa wahusika wakuu katika kupatiwa dawa hizo ni Watu wote kuanzia miaka mitano na kuendelea,isipokuwa watoto chini ya miaka mitano,wajawazito, mama anaenyonyesha mtoto chini ya siku saba na Wagonjwa Mahututi.
“Tunataka kulinda afya zao na Uhai wao hivyo tunaomba wafuate maelekezo vizuri”.Alisema Bw Mmbando.
Aidha zoezi hilo litatekelezwa katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Singida, Dodoma,Mtwara, Lindi na Pwani kwa ajili ya kujikinga na kutibu magonjwa hayo na Mikoa mingine iliyobaki itafanya zoezi hilo katika ngazi ya jamii na shuleni mwishoni mwa mwezi Januari kuendelea hadi Februari 2016.
Naye Mratibu wa Mpango huo Dkt Edward kirumbi ameeleza kuwa takwimu zainaonyesha kuwa magonjwa yasiyopewa kipaumbele hapa nchini ni kubwa ambapo ugonjwa wa Usubi umeenea zaidi katika mikoa sita ikiongozwa na Dodoma, Ugonjwa wa Minyoo ya tumbo wagonjwa million 13, kichocho ,Matende na Mabusha tathmini za awali zinaonyesha mikoa 18 imeathirika kwa kuwa na wagonjwa million 12.
Vile vile Dkt Kirumbi ameeleza kuwa Magonjwa haya yamekuwa na athari kubwa hasa kwa kuathiri nguvu kazi ya Taifa hivyo wananchi wanapaswa kupata dawa hizo ambazo zitakuwa zinatelewa kwa mwaka mara moja ili kukinga upungufu wa Damu, kuuwa vimelea vya ugonjwa huo, kupungua kwa magonjwa ya ngozi, na kuongeza virutubisho bora mwilini.
Hata hivyo jamii inapaswa kupewa elimu zaidi kuhusu Magonjwa haya kwa vile bado haijaelewa athari za magonjwa haya kwa kiasi kikubwa hasa kwa maeneo ya vijijini ambayo ndio waathirika wakubwa.
No comments:
Post a Comment