“Waziri
hana mamlaka ya kumwondoa mkurugenzi wa halmashauri, taasisi, shirika
na katibu wa wizara yake kutokana na kubanwa na mfumo.” Makamba.
…………………………………………………………………………….
Mwanza. Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema
ipo haja ya kubadili mfumo wa watendaji serikalini ili wanapoboronga nao
wajibishwe na mawaziri.
Akizungumza katika mahojiano
yaliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini hapa, Makamba alisema mfumo uliopo
sasa, hauwapi nguvu mawaziri ili kuwawajibisha watendaji pale
wanapokosea na badala yake unawabana wenyewe hivyo kuendelea kuwa
kitanzi kwao.
“Mimi ni waziri, akikosea katibu
nawajibishwa huyu anabaki, mimi siwezi kumwajibisha hivyo wanafanya
lolote na sisi tunalazimishwa kuwajibishwa kisiasa kwa makosa ya
watendaji,” alisema.
“Baada ya Kamati ya Maliasili
Ardhi na Mazingira iliyo chini ya Mwenyekiti wake, James Lembeli kuomba
kwa Spika kutumia ushahidi kwa kuweka kanda za video ili kuonyesha
kilichotokea kwenye Operesheni Tokomeza Ujangili, hali ilichafuka ndani
ya kikao cha Bunge na kila mmoja akawa na hisia na wengine kuanza
kububujikwa na machozi na wabunge kuchangia hoja za kutaka mawaziri
kuachia ngazi, hawakuangalia kiini cha tatizo, waliwabana mawaziri tu,”
alisema.
Alisema
Serikali kupitia mamlaka za juu, inapaswa kuangalia mfumo uliopo kwa
lengo la kuubadilisha na kuingiza mapendekezo na mfumo mpya kwenye
Katiba Mpya kuhusu uwajibikaji wa mawaziri na watendaji wakuu kwenye
wizara, taasisi, idara, halmashauri na mashirika ya umma ambao ni
wataalamu mbalimbali kuwajibishwa na mawaziri husika endapo kutaonekana
utendaji wao haukidhi ama kwenda kinyume na maadili na sheria zilizopo.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment