NYASI
za uwanja wa Kinesi , jijini Dar es salaam zinaendelea kuhimili daluga
za wekundu wa msimbazi, Simba SC, ambao wanajiandaa na mechi ya ufunguzi
ya michuano ya kombe la Mapinduzi januari mosi, majira ya saa 2:00
kamili usiku dhidi ya AFC Leopard kutoka Kenya, nuwanja wa Amaan,
kisiwani Unguja.
Simba
iliyopangwa kundi moja na timu za KMKM, AFC Leopard ya Kenya pamoja na
KCC kutoka Uganda inaendelea kujifua chini ya kocha msaidizi, Seleman
Matola `Veron`, huku kocha mkuu Mcroatia, Zdravko Logarusic `Loga`
akitarajia kuwasili Zanzibar januari 2 mwakani.
Kaimu
Afisa habari wa klabu hiyo, Stanley Philipo `Stan` ameuambia mtandao
huu kuwa wanatarajia kuendelea na mazoezi leo jioni, huku wakitarajia
kung`oa nanga jijini Dar es salaam kueleka Zanzibar jumanne (Desemba
31).
“Maandalizi
ni mazuri sana. Ongezeko la wachezaji wapya na kocha mpya kumeleta
mabadiliko katika kikosi, wachezaji wanajituma zaidi kutafuta namba
kwani mwalimu hawajuii”. Alisema Stanley.
Stanley
aliongeza kuwa kukosekana kwa kocha mkuu hakujaathiri chochote kwani
Matola ni kocha mzuri na ataongoza timu katika mchezo wao wa kwanza
dhidi ya miamba ya soka kutoka nchini Kenya, AFC Leopard.
“Mechi
ya ufunguzi itatupa dira halisi ya michuano ya msimu huu. Tunaheshimu
ubora wa Leopard, lakini tunajipanga vizuri kuhakikisha tunapata ushindi
wa kwanza na kuongeza imani kwa mashabiki wetu”. Alisema Stanley.
Kaimu
Afisa habari huyo alisema, kombe la Mapinduzi ni nafasi nzuri ya
kuandaa kikosi chao kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu soka
Tanzania bara, hivyo mashabiki watarajie soka zuri na la uhakika.
“Tumekuwa
wakati wa mpito kutengeneza timu, lakini sasa dawa imeanza kupatikana
kutokana na mabadiliko ya kikosi na benchi la ufundi yaliyofanywa.
Umefika wakati wa mashabiki wetu kupata burudani ya soka”. Alijisifu
Stanley.
Wakati
huo huo, kocha msaidizi wa Simba SC, Seleman Matola amejigamba kuwa
mtihani aliopewa na bosi wake ataumudu vizuri katika mchezo wa kwanza
huko Zanzibar.
Matola
alisema klabu hiyo itashusha kikosi kamili , wala haina mzaha na
mashindano hayo kutokana na umuhimu wake katika kujenga kikosi chao.
“Simba itashuka na kikosi kizima. Malengo ni kutwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi”. Alisema Matola.
Logarusic
na Matola walirithi mikoba ya makocha waliofukuzwa kazi, Abdallah
Kibadeni na Jamhuri Kiwhelo `Julio` baada ya kumalizika mzunguko wa
kwanza wa ligi kuu soka Tanzania bara, huku Simba ikiwa nafasi ya nne na
pointi 24.
Mbali
na mabadiliko ya benchi la ufundi, Simba imefanya usajili katika
dirisha dogo na kuwaongeza kikosini makipa Ivo Philip Mapunda na Yaw
Berko.
Wanandinga
wengine ni Juma Awadh Issa, Ali Badru, Donald Mosoti, na Uhuru Seleman
Mwambungu, ingawa TFF imewataka kufanya marekebisho katika usajili wao.
Zilibaki
nafasi tano, lakini wamewaombea usajili wachezaji sita (6), hivyo
wanatakiwa kupunguza, kama watashindwa kufanya hivyo, kamati Kamati ya
Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) itafanya yenyewe.
Kocha
Logarusic anatarajia kuwatumia wachezaji wote ikiwa ni mikakati yake
kuandaa kikosi cha kwanza cha ligi kuu soka Tanzania bara, ngwe ya lala
salama inayotarajia kuanza kushika kasi januari 25 mwakani.
Mbali
na Simba SC, timu nyingine za Tanzania bara zitakazoshiriki michuano
hiyo ni mabingwa watetezi, Azam fc, Dar Young Africans na Mbeya City.
No comments:
Post a Comment