TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Monday, December 30, 2013

Katiba: Mwelekeo mpya kujulikana

katibaWajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakitia saini Rasimu ya Pili ya Katiba juzi. Rasimu hiyo itakabidhiwa leo kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais Ali Mohamed Shein, Karimjee, Dar es Salaam. Picha ya mtandao. 
………………………………………………………………………………………………
Dar es Salaam. Swali la nini kilichomo katika Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya litajibiwa leo wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapokabidhi rasimu hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Rasimu inayosubiriwa kwa hamu na wananchi wa kada zote itatolewa ikiwa imepita miezi saba tangu tume hiyo ilipotoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba ambayo ilijadiliwa na kuboreshwa katika Mabaraza ya Katiba yaliyoketi kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2, mwaka huu.
Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 3, 2012 kwa kukusanya maoni ya wananchi, iliandaa rasimu ya kwanza iliyotangazwa Juni 4, mwaka huu.
Hafla ya kukabidhi rasimu hiyo itafanyika leo saa 6.00 mchana katika Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na asasi mbalimbali.
Baada ya kukabidhi rasimu hiyo ya Katiba, Tume ya Mabadiliko ya Katiba itavunjwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Warioba ndiye atakayesoma rasimu hiyo kwenye Bunge Maalumu la Katiba linalotazamiwa kuanza vikao vyake Februari, mwakani.
Alipoulizwa nini kilichoongezwa au kupunguzwa katika rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema: “Siwezi kueleza kama kuna kilichoondolewa au kurekebishwa… kesho (leo), Watanzania watapata fursa ya kujua mapendekezo ya tume, wasubiri.”
Baadhi ya mambo yanayosubiriwa kwa hamu kujua kama yamefanyiwa marekebisho au la kwenye Rasimu Mpya ni pamoja na mfumo na muundo wa Muungano, umri wa kugombea urais, wabunge kutokana na mikoa, umri wa kugombea urais na mengine.
Serikali Tatu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupitia Rasimu ya Kwanza ilipendekeza kuundwa kwa Serikali Tatu na alipokuwa akizungumzia hilo wakati akitangaza Rasimu ya Kwanza, Jaji Warioba alisema uamuzi huo ulifikiwa kwa kuwa yalikuwa ni maoni ya wananchi walio wengi.
Hata hivyo, pendekezo hilo lilizua mjadala mkubwa kwani chama tawala, CCM, kilipinga na kuweka bayana kwamba kinataka muundo wa Muungano uendelee kuwa wa Serikali mbili.
Vyama vya upinzani kwa upande wake, viliunga mkono pendekezo hilo la muundo wa Serikali Tatu huku CUF kikienda mbali zaidi kwa kutaka Zanzibar ipewe mamlaka ya kuwa na dola kamili.
Katika Rasimu ya Kwanza ilipendekezwa mambo saba tu ndiyo yabakie kwenye mamlaka ya Muungano.
Mambo hayo ni pamoja na Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa na Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Mambo hayo, ilipendekezwa na Tume hiyo kuwa chini ya wizara ambazo zitaongozwa na mawaziri wakazi ambao hawatatokana na wabunge kwani watatakiwa kuchaguliwa nje ya taasisi hiyo.
Kurejeshwa kwa jina la Tanganyika
Baada ya kutolewa kwa Rasimu ya Kwanza, mjadala mwingine ulioibuka hasa baada ya kupendekezwa kwa muundo wa Muungano kuwa wa Serikali Tatu ni hatua ya Tume kuendelea kutumia jina la Tanzania Bara.
Baadhi ya wadau walikosoa pendekezo hilo wakitaka jina la Tanganyika litajwe katika Katiba badala ya Tanzania Bara.
Katika Rasimu ya Kwanza, Tanzania Bara na Zanzibar zilihesabiwa kuwa washirika wa Muungano.
Ikiwa Serikali tatu zitarudishwa swali linakuja kama Tanzania Bara itatumia jina la Tanganyika ambalo ililitumia kuanzia mwaka 1961  hadi 1964 ilipoungana na Zanzibar.
Kufutwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu
Rasimu ya kwanza ilipendekezwa kufutwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu kwenye Serikali ya Muungano na badala yake kupendekeza kuwapo kwa Rais na Makamu wake.
Baadhi ya wadau walihoji juu ya usimamizi wa kazi za kila siku za Serikali jukumu ambalo kwa sasa lipo kwa Waziri Mkuu.
Umri wa kugombea urais
Suala hilo nalo lilizusha mjadala mkali wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya.
Mapendekezo ya Rasimu ya Kwanza yalitaka moja ya sifa za mgombea urais kuwa miaka 40 lakini baadhi ya wanasiasa, hasa vijana, wametaka umri huo ushushwe hadi miaka 35.
Wagombea binafsi
Jambo jingine lililopendekezwa katika Rasimu ya Kwanza ni kuwapo kwa mgombea binafsi kuanzia ubunge hadi urais.
Hilo halikuwa na mjadala mkubwa miongoni mwa wadau mbalimbali kutokana na ukweli kwamba ni jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele kwa muda mrefu na wananchi.
Muundo wa Bunge la Muungano
Rasimu ya Kwanza ilipendekeza kuwa wabunge watakuwa 75.
Kwa maana ya 50 kutoka Tanzania Bara, 20 kutoka Zanzibar na watano kutoka kundi maalumu ambao watateuliwa na Rais kwa ajili ya kuwatetea watu wenye ulemavu.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya Rasimu ya Kwanza, wabunge wa kuchaguliwa watagombea kupitia mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Rasimu ya kwanza ilipendekeza kuwa kila mkoa utachagua mbunge mmoja wa kike na wa kiume ili kuleta uwiano na kupendekeza kufutwa kwa viti maalumu suala ambalo lilizua mjadala.
Haki za Binadamu
Moja ya mambo ambayo yaliibuka mjadala ni haki za binadamu. Katika Rasimu ya Kwanza, ilipendekezwa kuundwa kwa Tume ya Haki za Binadamu itakayokuwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wasiozidi saba.
Lakini wadau wengi waliotoa maoni yao walitaka sheria kandamizi 40 za Tume ya Nyalali zisiwepo katika Katiba Mpya.
Mambo mengine
Kuhusu madaraka ya Rais, Tume hiyo ilipendekeza katika Rasimu yake ya Kwanza kwamba yabaki kama yalivyo hasa kwa uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu, pia ashirikiane na taasisi na vyombo vingine katika uteuzi.
Katika Rasimu hiyo ya Kwanza, pia ilipendekezwa kusiwepo na uchaguzi mdogo, isipokuwa kama nafasi hiyo itaachwa na mgombea binafsi lakini kama ni wa kutoka katika chama cha siasa, ijazwe na mtu kutoka chama chake.
Kuhusu Tume ya Uchaguzi, Tume hiyo ilipendekeza katika Rasimu ya Kwanza kwamba jina la Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), libadilishwe na iitwe Tume Huru ya Uchaguzi.
Rasimu hiyo, ilipendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court), majaji wa Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani watateuliwa na Rais, baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment