Wapo wanaosema uchaguzi mdogo uliofanyika
Februari 8 mwaka huu katika kata 27 zilizopo ndani ya mikoa 15 nchini
umepeleka chereko CCM na majonzi Chadema.
Ni kicheko kwa CCM kwa sababu kimeshinda katika
kata 24, huku Chadema kikiambulia ushindi katika kata tatu na
NCCR-Mageuzi kata moja.
Wengi walidhani kuwa Chadema kingeweza kufanya
vyema, kutokana na kwamba uchaguzi ulifanyika ikiwa zimepita siku kadhaa
tangu chama hicho kikuu cha upinzani nchini kufanya Operesheni Pamoja
Daima na Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), katika mikoa mbalimbali nchini.
Wapo waliogusia helikopta tatu zilizotumiwa na
chama hicho katika operesheni hizo, hasa ile ya Pamoja Daima, pamoja na
mpasuko uliokikumba baada ya kumvua nyadhifa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu
wake, Zitto Kabwe.
Mbali na Kabwe, pia kiliwafukuza uanachama
aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Dk Kitila Mkumbo na
aliyekuwa Mwenyekiti wake mkoani Arusha, Samson Mwigamba.
Binafsi naamini kuwa zipo sababu nyingi
zilizosababisha Chadema kishindwe kufanya vyema katika uchaguzi huu,
ikilinganishwa na uchaguzi mdogo wa madiwani wa Julai mwaka jana ambapo
kilishinda katika kata zote nne za Elerai, Kaloleni, Kimandolu na Themi
mkoani Arusha.
Kata hizo zilikuwa wazi tangu mwaka 2011 baada ya
chama hicho kuwatimua wanachama wake waliokuwa madiwani Estomih
Mallah(Kimandolu), John Bayo (Elerai), Reuben Ngowi (Themi) na Charles
Mpanda (Kaloleni).
Katika uchaguzi wa Februari 8, Chadema kimepoteza
Kata ya Nyasura iliyopo mkoani Bunda na Kata ya Mkongolo iliyopo jimbo
la Kigoma Kaskazini mkoani Kigoma ambazo wameshinda CCM.
Lakini kimeibuka na ushindi katika kata mbili za
Sombetini na Njombe Mjini ambazo awali zilikuwa za CCM. Pia kiliibuka na
ushindi katika Kata ya Kiborloni ambayo hata kabla ya uchaguzi huo,
diwani wa kata hiyo alikuwa wa Chadema.
NCCR-Mageuzi chenyewe kiliweza kutetea Kata ya
Kilelema mkoani Kigoma huku CCM kikipoteza Kata ya Njombe Mjini ambayo
ilikwenda kwa Chadema.
Chadema kimeangushwa na daftari la kudumu la wapiga kura.
Tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) haijawahi kulifanyia maboresho daftari hilo jambo ambalo
naamini limeathiri uchaguzi huo na watu wengi wamepoteza haki yao ya
kikatiba ya kupiga kura. Katika kipindi hicho chote NEC imeendelea
kujificha kwenye kichaka cha Sheria iliyoianzisha (Sura ya 343). Sheria
hiyo inaeleza kwamba uboreshaji wa daftari hilo utafanyika mara mbili
kwa miaka mitano, yaani baada ya Uchaguzi Mkuu kupita na kabla ya
uchaguzi unaofuata.
No comments:
Post a Comment