- Tanzania imekuwa taifa la ajabu na masikitiko yetu ni kwamba mporomoko wa maadili katika jamii yetu umeziba mitima na dhamira za viongozi wetu na jamii nzima kwa jumla kiasi cha kuyaona matendo hayo kama mambo ya kawaida.
Uzoefu wetu wa muda mrefu umetuonyesha pasipo
shaka kwamba mambo mengi yanayotendeka Tanzania hayawezi kutendeka
katika nchi nyingine.
Tanzania imekuwa taifa la ajabu na masikitiko yetu
ni kwamba mporomoko wa maadili katika jamii yetu umeziba mitima na
dhamira za viongozi wetu na jamii nzima kwa jumla kiasi cha kuyaona
matendo hayo kama mambo ya kawaida.
Tunayo mifano ya matukio lukuki ya ajabu na ya kushtusha yaliyowahi kutokea hapa nchini lakini yakaonekana kama ya kawaida.
Fikiria wafanyabiashara walioiba mabilioni ya
fedha za Epa ambao muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 walikwenda
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati wa siku za mapumziko na kukwapua
mabilioni hayo kwa njia za udanganyifu. Fikiria wezi hao walivyoahidiwa
kwamba iwapo wangezirudisha wasingechukuliwa hatua yoyote.
Ebu fikiria nchi ambayo kiongozi wake anakwenda
ughaibuni na kutangaza kuwapo kwa majangili mapapa 40 na kusema kiongozi
wao yuko mikoa ya Kaskazini, badala ya kusema hayo akiwa nchini, ikiwa
ni pamoja na kuyakamata majangili hayo na kuyachukulia hatua.
Ebu fikiria matukio haya mawili ambapo Waziri Mkuu
anatamka bungeni kwamba ni sawa tu kwa Jeshi la Polisi kuwapiga
wananchi ‘wakorofi’, huku mkuu wa nchi akikiagiza chama chake cha siasa
ambacho yeye ni mwenyekiti kuwapiga wapinzani anaodai wanafanya vurugu
dhidi ya wafuasi wa chama chake. Ni nchi gani ambayo viongozi wake wakuu
wanaweza kutoa amri hizo za hatari?
Tumesema yote hayo kutokana na kitendo cha ajabu
na aibu kilichofanywa na Mwenyekiti wa Chama cha National League for
Democracy (NLD), Dk Emannuel Makaidi cha kufanya ulaghai na kujiwezesha
yeye na mkewe kuteuliwa kuingia katika Bunge la Katiba.
Katika utetezi wake, ametoa hoja za kuchefua na
kughadhabisha kuwa, kwa vile mke wake naye ni mwanachama wa chama hicho
alikuwa na haki ya kuteuliwa kama ilivyo kwa Rais Kikwete na mke wake
ambao wote ni wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.
Tunasema uteuzi huo haukubaliki hata kidogo
kutokana na kukiuka taratibu zilizowekwa kisheria kwamba vyama vya siasa
lazima viwe na sura ya Muungano katika mfumo na uendeshaji wake.
Ni ujasiri na uthubutu wa kiwango cha juu kujiteua
yeye na mkewe kama vile NLD ni mali ya kifamilia. Kudai kwamba aliteua
majina ya wanachama wanne na Rais akamchagua yeye na mkewe ni uongo wa
kupitiliza.
Hii inaonyesha kwamba zilikuwapo mbinu chafu
katika mchakato wa uteuzi huo, vinginevyo wanachama wa Zanzibar
wangenyimwa vipi uwakilishi? Hatua ya chama hicho upande wa Zanzibar ya
kumtaka Rais Kikwete atengue uteuzi wa Dk Makaidi na mkewe lazima iungwe
mkono.
Tatizo hapa ni hatua ya Serikali kuendelea
kuvibeba kwa sababu za kisiasa vyama vya siasa vilivyokufa siku nyingi.
Ukweli ni kwamba NLD na vyama vingine vingi ambavyo kwa mujibu wa sheria
ya vyama ya 1992 vinapaswa kufutiwa usajili wa kudumu bado
vinatambuliwa kiasi cha viongozi wake kuingizwa katika Bunge Maalumu la
Katiba bila kuwa na sifa stahiki.
No comments:
Post a Comment