on FEBRUARY 25, 2014 in MICHEZO
22 WAITWA TAIFA STARS KUIKABILI NAMIBIA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kikosi cha wachezaji 22 kwa ajili ya
mechi ya kirafiki ya kalenda ya FIFA dhidi ya Namibia (Brave Warriors)
itakayochezwa Machi 5 mwaka huu jijini Windhoek, Namibia.
Wachezaji walioitwa katika timu hiyo ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Sim
ba) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki wa pembeni ni Edward Charles (JKT Ruvu), Erasto Nyoni (Azam), Hassan Mwasapili (Mbeya City) na Michael Aidan (Ruvu Shooting).
Mabeki wa kati ni Aggrey Morris (Azam) na Kelvin Yondani (Yanga) wakati viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), David Luhende (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Jonas Mkude (Simba) na Mwinyi Kazimoto (Markhiya Sports Club, Qatar).
Washambuliaji ni Athanas Mdamu (Alliance Mwanza), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Yanga), Ramadhan Singano (Simba) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC).
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaingia kambini Machi 1 mwaka huu, kwenye hoteli ya Accommondia inatarajiwa kuondoka Machi 3 mwaka huu kwenda Windhoek.
Wachezaji ambao timu zao zinacheza mechi za mashindano ya kimataifa na ligi wikiendi hii wataripoti kambini mara baada ya mechi zao kumalizika.
TAARIFA YA KLABU ZOTE TANZANIA YATAKIWA TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zimewaagiza wanachama wake- vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kuwapatia orodha ya klabu zote za mpira wa miguu zilizosajiliwa katika mikoa yao.
Orodha hiyo inatakiwa kujumuisha namba ya usajili wa klabu, viongozi waliopo madarakani kwa sasa pamoja na mawasiliano yao (namba za simu na anuani za email) na eneo yalipo makao ya klabu husika.
Kwa utaratibu huo, vyama vya mikoa vitakusanya taarifa za klabu zinazocheza ligi ya mikoa, lakini wakati huo vinatakiwa kuwasiliana na wanachama wake (vyama vya wilaya) kupata taarifa za klabu zinazocheza ligi za wilaya na baadaye kuziwasilisha TFF.
Klabu ambazo taarifa zake zitakuwa hazijawasilishwa TFF hadi Agosti mwaka huu hazitaruhusiwa kushiriki ligi ya msimu wa 2014/2015 katika ngazi yoyote ile.
RAIS MALINZI KUZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atakuwa na mkutano na waandishi wa habari juu ya programu ya mpira wa miguu kwa vijana.
Mkutano huo unafanyika leo (Februari 26 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF zilizopo ghorofa ya 3 katika Jengo la PPF Tower, mtaa wa Garden na Ohio.
AZAM, ASHANTI UNITED KUKIPIGA VPL
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Februari 26 mwaka huu) kwa mechi moja itakayochezwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mechi itazikutanisha timu za Azam inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 37 dhidi ya Ashanti United iliyoko nafasi ya 12 kwa pointi zake 14.
MASHINDANO YA TAIFA YA BASEBALL YAFANYIKA KATIKA VIWANJA VYA SHULE YA SEKONDARI YA AZANIA
Mashindano ya kwanza kufanyika katika historia ya mchezo wa baseball hapa Tanzania yamefanyika na kushirikisha timu kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Ruvuma, Temeke na Ilala.
Mashindano hayo yaliandaliwa na chama cha mchezo huu wa baseball Tanzania chini ya udhamini wa “ Association for Friends of African Baseball” kutoka nchini Japan chini ya mwenyekiti wake ndugu Tomonari Shinya ambaye yupo hapa nchini kikazi na shirika la JICA.
Katika mechi zilizochezwa, timu ya Azania na Kibasila zilifanikiwa kuingia fainali na timu ya Sanya Juu ilifanikiwa kuchukua nafasi ya tatu.
Katika fainali hiyo iliyokuwa na ushindani pamoja na ufundi wa hali ya juu, timu ya Kibasila ilifanikiwa kunyakuwa ubingwa wa mchezo huu ambapo iliinyuka timu ya Azania kwa pointi 11 dhidi ya 10 walizopata Azania na kupata zawadi ya Kombe kubwa la Dhahabu pamoja na vyeti kwa kila mchezaji.
Aidha timu ya Azania ilifanikiwa kiuchukua Kombe la mshindi wa pili pamoja na vyeti kwa kila mchezaji.
Timu ya Sanya juu nayo kwa nafasi ya tatu ilipata vyeti na pia kwa timu ya Londoni liambulia vyeti.
Mashindano ya mwaka hu ni hamasa kubwa katika kuingiza mchezo huu katika shule za sekondari kwani chama cha baseball Tanzania kimedhamiria kuingiza mchezo huu hapa nchini kupitia shule za sekondari ili kupata vijana na wachezaji mahiri wa taifa letu na hatimaye tupate matokeo mazuri kwa timu yetu ya taifa katika ushiriki wa michezo ya Afrika na ile ya Dunia.
Mashindano ya mwaka hu ni hamasa kubwa katika kuingiza mchezo huu katika shule za sekondari kwani chama cha baseball Tanzania kimedhamiria kuingiza mchezo huu hapa nchini kupitia shule za sekondari ili kupata vijana na wachezaji mahiri wa taifa letu na hatimaye tupate matokeo mazuri kwa timu yetu ya taifa katika ushiriki wa michezo ya Afrika na ile ya Dunia.
Kwasasa, timu ya taifa ya baseball ipo chini ya mtaalamu wa mchezo huo ndugu Tomonari Shinya, raia wa Japan ambapo kati ya miaka ya 1997 na 1999 aliitumikia timu ya taifa ya Ghana kama meneja wa timu ya taifa na alifanikiwa kuipeleka Ghana katika michezo ya All African Games iliyofanyika Johanesburg, Afrika ya Kusini na kuipatia Ghana nafasi ya 4.
Tuna imani kwa juhudi zetu watanzania, tutafika zaidi ya Ghana ilipofika.
MAKONDA: RASIMU YA KATIBA IMEWASAHAU VIJANA.
Mimi ni Kijana, ninayoyazungumza,ninayoyafanya yana reflect uhalisia huo. Hivyo kwa wito wa Ujana najikuta nashawishika sana kuongeza umakini katika masuala yahusuyo vijana hasa kwenye Katiba.
Ni ajabu lakini kweli kuwa sehemu inayotaja juu ya Haki na Wajibu wa Vijana katika Rasimu yote ni Ibara ya 44 tu, tena inataja kwa ujumla wake bila hata kuweka ibara ndogo ama vipengele vya ufafanuzi.
Ibara hiyo inasema;
“..kila kijana ana haki na wajibu wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Jamhuri ya Muungano pamoja na jamii kwa ujumla, na kwa mantiki hiyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano, serikali za nchi washirika na jamii zitahakikisha kuwa vijana wanawekewa mazingira mazuri ya kuwa “Raia Wema” na kupatiwa fursa za kushiriki kikamilifu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni…”
Sikuwa nategemea huu unaweza ukawa ndio mwisho wa maelezo ya Rasimu kuhusu Vijana. Nilitegemea nitakuta vipengele vinavyobainisha namna vijana watakavyonufaika na rasilimali, namna ambavyo sheria ndogo na taratibu baguzi ktk upatikanaji wa ajira na fursa zitakavyobainishwa kikatiba ili kumaliza kabisa matatizo ya Vijana.
Nilidhani Rasimu itaweka bayana Uanzishwaji wa Baraza La Vijana la Taifa ili kiwe chombo cha kikatiba cha Vijana.
Nikitumia fursa na nafasi yangu kama mbunge wa bunge maalum la Katiba zipo hoja hizo kuu (3) tatu ambazo nitazisimamia ziingie kwenye Katiba kwa manufaa na mustakabal mwema wa Vijana bila kujali tofauti ya itikadi, dini ama kabila.
Na nakaribisha mawazo na michango ya fikra ktk hoja zihusuzo Vijana.
IMETOLEWA NA:
IMETOLEWA NA:
PAUL MAKONDA.
MBUNGE WA BUNGE MAALUM LA KATIBA.
CONTACTS:
MOBILE: 0684909090.
E-MAIL: makondapaul@gmail.com.
VIJANA KUANDALIWA KUWA CHACHU YA MAENDELEO YA JAMII
Mkuu wa kitengo cha kozi fupi na ushauri chuo cha Mzumbe Pro. Shiv K. Tripathi akichangia wakati wa majadiliano ya awali jinsi ya kuendeleza vijana kwa maendeleo ya jamii, kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Pro. Elisante Ole Gabriel na kushoto ni Mkuu wa Kampuni ya TATA Africa Holdings (Tanzania) Ltd Bw. Prashant Shukla.
Mkurugenzi Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi akielezea kuhusu moja ya kituo cha vijana kinachojishughulisha na ufundi makanika kilichopo Ilonga Morogoro, kulia ni Mkuu wa Kampuni ya TATA Africa Holdings (Tanzania) Ltd Bw. Prashant Shukla wakati wa majadiliano ya awali ya kuendeleza vijana kwa maendeleo ya jamii.
Na Genofeva Matemu (MAELEZO)
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na kampuni ya TATA Africa Holdings (Tanzania) Ltd imeadhimia kuanzisha programu ya kuendeleza maendeleo ya jamii kwa kutumia vijana waliopo katika ajira mbalimbali kwa kuwajengea uwezo utakaowawezesha kuleta maendeleo katika jamii yao.
Hayo yameafikiwa wakati Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Pro. Elisante Ole Gabriel alipokutana kwa ajili ya majadiliano ya awali na Mkuu wa Kampuni ya TATA Africa Holdings (Tanzania) Ltd Bw. Prashant Shukla pamoja na Mkuu wa kitengo cha kozi fupi na ushauri chuo cha Mzumbe Pro. Shiv K. Tripathi ofisini kwake leo jijini Dar es Salaam.
Lengo kuu la majadiliano hayo ni kupata ufafanuzi wa awali na kutambua maeneo ambayo Wizara itaweza kushirikiana na kampuni hiyo ili kuongeza ajira kwa vijana haswa ajira ya kujitegemea, pamoja na kuwajengea uwezo vijana katika masuala ya ujasiriamali, uongozi na ufundi makanika.
“Programu itakayoanzishwa italenga vijana hususani wale wanaojihusisha na ufundi makanika, madereva wa daladala, pamoja na waendesha pikipiki kwa maana ya usalama wao, usalama wa pikipiki na ujasiriamali utakaowawezesha kujipatia kipato na kuleta maendeleo katika jamii” amesema Pro. Gabriel.
Kwa upande wake Mkuu wa Kampuni ya TATA Africa Holdings (Tanzania) Ltd Bw. Prashant Shukla ameiahidi Wizara kushirikiana nayo bega kwa bega muda wote ili kuhakikisha kuwa tatizo la vijana mitahani linaisha na kuwa na vijana ambao wanauelewa na uwezo wa kuleta maendeleo katika jamii yao.
Naye Mkurugenzi Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi ameitaka kampuni hiyo kushirikiana na Wizara kwa kuchukua fursa ya kuboresha karakana ya Ufundi makanika iliyopo katika kituo cha vijana Ilonga Morogoro kama njia mojawapo ya kuwakomboa vijana na kuleta maendeleo.
No comments:
Post a Comment