Na Baraka Mpenja
KIPIGO cha bao 1-0 walichopokea Simba sc kutoka kwa Wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga jana uwanja wa Taifa katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara kimezidi kuwavuruga na kuwafanya wawe wanyonge ngwe hii ya lala salama.
Wagosi wa Kaya wakiwa katika morali ya ushindi , waliandika bao la ushindi dakika ya 45 kipindi cha kwanza kupitia kwa mlinzi wake wa pembeni, Hamadi Juma kufuatia mabeki wa Simba kujikoroga.
Matokeo hayo yamepokewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa klabu hiyo ambao wanaona kama ligi kuu inawaonea msimu huu.
Hata hivyo Uongozi wa Simba sc kupitia kwa Afisa habari wake, Asha Muhaji umewataka mashabiki na wanachama wao kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu kwao.
“Matokeo ya jana hatukuyatarajia hata kidogo. Tumeshitushwa mno na kipigo hicho. Lakini hayo ndio mambo ya uwanjani. Mpira umechezwa vizuri na tumepoteza. Hatuna budi kuukubali ukweli japo unauma”. Alisema Asha.
Mwamuzi vipi?: Kocha wa Simba sc, Dravko Logarusic (wa kwanza kulia) akiwa hailewi cha kufanya na kuonesha kuwa muda bado wakati mwamuzi anapuliza kipenga cha mwishoShughuli ilikuwa pevu mno jana uwanja wa Taifa
Afisa habari huyo aliongeza kuwa kutokana na matokeo wanayozidi kuyapata, yanawapa watu cha kusema, lakini soka huwa lina tabia ya kupanda na kushuka.
“Siku za nyuma mashabiki wetu walikuwa wanatoka na furaha uwanjani. Kwa sasa mambo yamebadilika. Huo ndio Mpira, ukiupenda lazima uwe na moyo wa kukubaliana na kile kinachotokeo”. Alisema Asha.
Asha alisisitiza kuwa bado wamebakiwa na mechi nne, hivyo mashabiki waendelee kuiunga mkono klabu yao ili iweze kufanya vizuri.
No comments:
Post a Comment