Mwakilishi
mteule wa Chama cha Alliance for Development Change (ADC) Hamad Rashid
Mohammed, amemuomba Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, atakapounda
serikali achague watendaji wenye utaalamu wanaoweza kuisaidia serikali
kuinua uchumi wake.
Akichangia
hotuba ya Rais baada ya kuapishwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi,
Rashid amesema kupewa nafasi kwa wataalamu kutaisaidia serikali kufikia
malengo inayojipangia kwa kuwaletea maendeleo wananchi.
Mwakilishi
huyo aliyegombea urais wa Zanzibar kupitia ADC katika uchaguzi mkuu
uliopita, amesema katika kipindi cha pili cha awamu ya saba, Dk. Shein
anahitaji wataalamu wachumi na watakaotumikia nchi kwa uadilifu.
Aidha,
alisisitiza vyombo vya sheria vitumie nafasi yao dhidi ya watendaji na
viongozi watakaokiuka sheria na kujaribu kuikwamisha serikali kutimiza
malengo yake.Aliiomba serikali iache muhali kwa kulea watendaji
wasiotimiza majukunmu yao ipasavyo, akisema ni lazima watu kama hao
wachukuliwe hatua madhubuti vyenginvyo nchi itarudi nyuma kimaendeleo.
Rashid
alieleza kuwa, kinachokwamisha nchi kupata maendeleo ni watendaji na
viongozi wengi kutojali wakati na kupoteza muda mwingi kwa mambo
yasiyokuwa ya msingi badala ya kufanya kazi.“Tumeshuhudia watu wengi
wakkinyimwa au kucheleweshewa huduma wakiwemo wawekezaji wanaoomba
miongozo. Hili ni tatizo na lazima tufike wakati likomeshwe,”
alisisitiza.
Aliitaka
serikali kuiga mfano wa Tanzania Bara, ambapo amesema mtu anayeomba
huduma hupangiwa mtendaji maalumu wa kumsaidia, na pia hujulishwa mapema
tarehe atakayomaliziwa mchakato wake na kupewa majibu au kutumiwa
kokote aliko.
Kwa
upande mwengine, aliitaka serikali iwe makini katika kusimamia
ukusanyaji wa mapato kwani kodi ndio msukumo wa kuharakisha
maendeleo.Rashid aliwataka wananchi waondokane na fikra za kutegemea
misaada kutoka nchi za nje, na badala yake wakaze buti katika kufanya
kazi za uzalishaji na huduma kwa kutumia rasilimali zilizomo nchini.
Kwa
upande wake, Mohammed Aboud Mohammed ambaye pia ni mwakilishi wa
kuteuliwa na Rais, amewaomba wajumbe wenzake waache siasa kwani
uchaguzi umekwisha na kilichobaki sasa ni kujenga nchi.Amefahamisha kuwa
katika suala la maendeleo, si vyema kuingiza itikadi za kisiasa, dini,
ukabila au maeneo watu wanakotoka kwani Zanzibar ni nchi ya Wazanzibari
wote.
Aidha
aliwataka wananchi wawe watulivu, wavumilie na kushirikiana katika
shughuli za maendeleo na kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwao.
No comments:
Post a Comment