UCHAGUZI
mdogo wa udiwani Kata ya Sombetini umeanza kwa vurugu baada ya wanachama
watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kujeruhiwa na
kundi la vijana walinzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Green Guard.
Aidha,
mgombea wa CCM kwenye kata hiyo, David Lesikari, akiwa na watu wengine
anadaiwa kuwashambulia na kitu chenye ncha kali wanachama wawili wa
CHADEMA na kumjeruhi mwingine kichwani na mgongoni.
Mwenyekiti
wa CHADEMA wilayani Arusha, Ephata Nanyaro, aliwaeleza waandishi wa
habari jana kuwa vurugu hizo zilitokea Januari 20 mwaka huu na kwamba
licha ya wanachama wao kuumizwa, Jeshi la Polisi liliwakamata na
kuwageuzia kesi kuwa wao ndio waliofanya vurugu.
Alisema siku
hiyo saa nane mchana mwanachama wao, Vitalis Bernad, alipigwa shoka la
kichwa na kijana aliyedai kuwa kiongozi wa CCM wakati akipita kwenye
kona ya Mbauda akiwa kwenye pikipiki yenye bendera ya CHADEMA wakielekea
kwenye mkutano wa mgombea wa chama chao, Ally Bananga.
“Kwa bahati
Bernard alikuwa amevaa kofia ngumu za waendesha pikipiki hivyo hakuumia
sana lakini watu waliokuwa pale walijaribu kumkimbiza mhusika lakini
hawakufanikiwa, kwani alikimbilia kwenye ofisi ya CCM ambapo walitokea
kundi la watu wenye mapanga kutoka ndani ya ofisi hizo jambo
lililowafanya wananchi kutawanyika kwa hofu,” alisema Nanyaro.
Alisema
Bernard akiwa na viongozi wa CHADEMA walienda polisi kufungua taarifa
namba Ar/RB/982/2014 kwenye kituo kidogo cha Mbauda karibu na ofisi hizo
za CCM ambapo waliwaeleza polisi kuwa mtuhumiwa yuko ndani ya ofisi
hizo lakini hawakutaka kwenda kumkamata.
Mwenyekiti
huyo wa wilaya alisema siku hiyo hiyo saa 12 jioni Wanachadema wawili,
Loserian Laisi na Mozec Joseph wakitokea kwenye mkutano wa kampeni
wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki walivamiwa na kundi la watu
wakiongozwa na mgombea wa CCM ambapo waliwashambulia kwa mapanga na
silaha za jadi.
Nanyaro
alisema katika tukio hilo Loserian alikatwa kichwani na kiunoni kwa kitu
chenye ncha kisha kutelekezwa migombani kabla ya kusaidiwa na wasamaria
wema waliompeleka Kituo cha Polisi cha Sombetini kupata fomu ya
matibabu (PF3) na kwenda hospitali.
“Polisi bila
weledi walichukua maelezo kwa saa mbili huku Loserian akiwa kwenye
maumivu na damu zikimtoka hata hivyo alipatiwa matibabu katika hospitali
ya Kaloleni, akiwa anaendelea na matibabu polisi walifika hospitalini
na kumchukua hadi Kituo Kikuu cha Polisi na kumweka rumande,”
alilalamika Mwenyekiti huyo wa CHADEMA.
Kwa upande
wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alikiri ofisi
yake kupokea taarifa za vurugu za jioni huku akibainisha kwamba taarifa
za tukio la mchana hakuzipata.
Akizungumza
na Tanzania Daima, Kamanda Sabas alisema kwenye tukio hilo la jioni
vijana wa CHADEMA wakiwa kwenye pikipiki mmoja alishuka na kumpiga vibao
mgombea wa CCM, Lesikari, ambapo wananchi walioona walipandwa na hasira
hivyo kuwashambulia na kukiri kwamba vijana wa CHADEMA kuhojiwa na
polisi kuhusu tukio hilo.
“Unaweza
kupigwa karibu ya kituo cha polisi haimaanishi waliokupiga ni polisi,
hivyo huyo inawezekana kabisa alipigwa hapo kona ya Mbauda karibu na
ofisi za CCM lakini wahusika si Wana CCM, kwenye kesi kinachotafutwa ni
ushahidi si hisia,” alisema kamanda huyo.
No comments:
Post a Comment