Wachezaji
tisa wa Kanembwa JKT pamoja na timu yao wanaolalamikiwa na Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kumpiga mwamuzi Peter Mujaya
wanatakiwa kujitetea mbele ya Kamati ya Nidhamuitakayokutana Jumapili (Februari 9 mwaka huu).
Utetezi
huo unaweza kuwa wa mdomo kwa walalamikiwa kufika wenyewe mbele ya
kamati itakayokutana saa 4 kamili asubuhi au kuuwasilisha kwa njia ya
maandishi.
Kamati
ilikutana jana Jumatano (Februari 5 mwaka huu) kusikiliza malalamiko
dhidi ya wachezaji hao na timu yao kwa tukio hilo lililotokea Novemba 2
mwaka jana kwenye mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Stand
United FC iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Wachezaji
hao ni Abdallah Mgonja, Bariki Abdul, Philipo Ndonde, Mbeke Mbeke,
Mkuba Clement, Mrisho Mussa, Nteze Raymond, Ntilakigwa Hussein na Uhuru
Mwambungu. Mlalamikiwa mwingine ambaye naye anatakiwa kujitetea ni timu
ya Kanembwa JKT.
Ikiwa
chini ya Mwenyekiti wake Tarimba Abbas, Kamati hiyo baada ya kusikiliza
malalamiko dhidi ya wahusika na kupokea ushahidi wa aina mbalimbali
kutoka kwa mlalamikaji imesema ili iweze kutenda haki katika shauri hilo
ni lazima walalamikiwa wapate fursa ya kusikilizwa.
Katika
hatua nyingine, Kamati hiyo iliyokutana kwa mara ya kwanza tangu
ilipoundwa imesema imesikitishwa na vitendo vya fujo ndani ya mpira wa
miguu, na kuwataka watu wasijihusishe na aina yoyote ya fujo.
No comments:
Post a Comment